Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Regina Ndege Qwaray

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia Taarifa ya Kamati iliyoko mbele yetu. Mchango wangu utajikita kwenye Taarifa ya Kamati ya Maji na Mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanza, nampongeza sana Mheshimiwa Rais ambaye ni mwana mazingira namba moja, kwani amekuwa akisisitiza suala la mazingira toka akiwa Makamu wa Rais na hivi juzi tuliona wakati wa kumbukumbu ya kuzaliwa kwake aliadhimisha kwa kwenda kuotesha miti katika maeneo mbalimbali. Kwa hiyo, hii inadhihirisha kwamba Mheshimiwa Rais ana dhamira ya dhati ya kuhakikisha kwamba mazingira yetu yanatunzwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mazingira siyo suala la mtu mmoja, wala siyo la Serikali peke yake, ni suala la kila binadamu na kila Mtanzania. Mazingira yanaanzia kutoka katika familia zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Taarifa ya Kamati ya Maji na Mazingira, uchambuzi wa Kamati umeeleza kwamba shughuli za binadamu ndiyo chanzo kikuu cha uharibifu wa mazingira. Mfano shughuli za kilimo, ufugaji pamoja na ukataji hovyo wa miti katika misitu yetu. Shughuli hizi za kibinadamu zimeendelea kuathiri maendeleo yetu siku hadi siku, kwa sababu watu wanaongezeka lakini maeneo hayaongezeki. Shughuli za binadamu zimekuwa nyingi pia kulingana na mahitaji ya kibinadamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, humu ndani kila mmoja ni shahidi, katika maeneo yetu tunakotoka tunajua ni namna gani mazingira yameharibiwa hasa mazingira ya misitu. Leo ukipita katika maeneo ya misitu, utakuta watu wamekata miti hali inayohatarisha sana mazingira yetu. Hata maeneo ya milima, watu wamelima mpaka milimani, watu wamejenga mpaka milimani. Maeneo mengi yameharibiwa kwa kukata miti sana. Jambo hili linafanyika wakati mamlaka zinaona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mamlaka za Serikali za Kijiji, Mamlaka ya Serikali za Mitaa, lakini mtu anaenda anajenga mlimani, anaachwa pale kwa muda mrefu na wengine wanaendelea kuongezeka na mwisho wa siku eneo lile linakuwa ni makazi ya watu, jambo ambalo linasababisha mvua kubwa inapokuja, kunakuwa na mmomonyoko wa ardhi katika maeneo yale na kusababisha mafuriko katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi hiki cha mvua ya mwaka huu tumeona ni namna gani maeneo mengi yameathirika kulingana na kwamba kuna uharibifu mkubwa wa mazingira katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kuna suala zima la taka ngumu na plastic. Katika maeneo yetu, Serikali imeshindwa kusimamia suala zima la ukusanyaji wa taka ngumu. Taka ngumu bado zinatupwa ovyo ovyo na kuzagaa katika maeneo mbalimbali hasa maeneo ya mijini yenye population kubwa. Unakuta eneo kubwa kama Mji wa Dar es Salaam hakuna ma-damp-o ya kutosha. Kwa hiyo, inasababisha watu kutupa takataka hata kwenye mifereji ya maji. Mwisho wa siku mvua kubwa inaponyesha tu, tayari mifereji inaziba na madaraja yanasombwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, angalia Wilaya ya Ubungo, kwa population iliyopo, kuna dampo moja tu. Hivi ukizingatia eneo lile na ukubwa wake, kuwa na damp moja maana yake ni nini? Maana yake watu wanatupa taka sehemu zisizotakiwa taka ngumu. Ni kwa nini Serikali isiweke…

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Regina kuna taarifa kutoka kwa Neema Gelard Mwandabila.

TAARIFA

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka nimpe taarifa mzungumzaji kwamba hizo taka ngumu siyo mijini tu, hata maporini. Tumeona mabasi mengi yanayosafiri yanatupa takataka katika mapori yetu. Kwa hiyo, taka zinapatikana huko mijini, vilevile mapori yetu yanaendelea kuchafuliwa, ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Regina Ndege Qwaray, taarifa hiyo unaipokea?

MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni taarifa nzuri, naomba niipokee kwa mikono miwili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kusema kwamba Serikali inatakiwa ikasimamie kanuni na miongozo iliyojiwekea ya kwamba mazingira lazima yatunzwe. Tukiacha utaratibu huu wa kutokukusanya taka ngumu, mwisho wa siku lazima tutaendelea kupata athari kubwa za mmomonyoko wa ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tuko hapa katika Mji wa Dodoma, maeneo tunayotoka, mitaa yetu tunayokaa haina utaratibu unaoeleweka katika kukusanya taka ngumu. Katika mitaa yetu, hata taka zile zinazopatikana majumbani, watu wanakusanya taka na baada ya kukusanya hawana pa kuzipeleka, na mwisho wa siku wanazitupa kwenye mitaro, jambo ambalo linakwenda kusababisha uharibifu wa mazingira katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukija kwenye vifaa vya plastic. Naipongeza sana Serikali kwamba iliweka katazo la kutengenezwa kwa mifuko ya plastic, imepiga hatua kubwa. Leo hii huwezi kukuta mifuko ya plastic inasambaa kila mahali, lakini bado inahitajika jitihada ya pekee, Serikali ikaweke msisitizo na mkazo zaidi katika matumizi ya mifuko ya plastic kwa sababu mifuko hiyo bado inatumika sokoni. Ukiangalia, inatoka wapi hiyo mifuko? Ni lazima tuangalie, yawezekana bado kuna viwanda bubu vinatengeneza hiyo mifuko. Inawezekana mifuko inatoka nchi za jirani. Serikali ikakae na nchi zetu za jirani hasa nchi za SADC kuona namna gani wanaweza kushirikiana kukomesha hii biashara na uingizaji wa mifuko ya plastic.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kuna suala lile la chupa za plastic. Kuna viwanda vinatengeneza vinywaji na kuhifadhi katika chupa za plastic ambazo haziwezi kufanyiwa recycling. Tunapongeza vile viwanda vinavyotengeneza chupa za maji ambazo zinaweza kufanyiwa recycling, lakini hizi chupa za plastic ambazo hazifanyiwi recycling. Serikali ione ni kwa namna gani wale wanaotengeneza chupa za plastic ambazo hazifanyiwi recycling, viwanda hivyo vipewe miongozo. Aidha, kuacha kabisa kutengeneza hizo chupa au watengeneze chupa ambazo zinaweza kufanyiwa recycling. Pia kuona namna gani viwanda hivyo kama hawawezi kufanyiwa recycling na viwanda vingine, wenyewe kama wenyewe watumie zile chupa kwa ajili ya baadaye kuhifadhia vinywaji vingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba, bado kuna jitihada zifanyike. Maeneo mengi kuna suala la uchimbaji wa michanga na uchimbaji wa kokoto. Ule uchimbaji wa mchanga na kokoto unafanyika kiholela, watu wanachimba kokoto, watu wanachimba mchanga maeneo ambayo hata ni makazi ya watu lakini mwisho wa siku baada ya kuchimba kokoto na maji, kinachotokea ni kwamba yanatokea makorongo na mvua kubwa ikinyesha, yale maeneo tayari yanakuwa ni makorongo na kusababisha mmomonyoko wa ardhi na mafuriko katika makazi ya watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)