Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Prof. Shukrani Elisha Manya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. PROF. SHUKRANI E. MANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi ya kuchangia hoja za Kamati ya Maji na Mazingira. Natangulia kusema kwamba naunga mkono hoja, maoni na mapendekezo yote ya Kamati yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura ya 191 inabainisha hitaji la kuwepo maeneo yanayoitwa “maeneo lindwa.” Tulipokuwa tukijadili jambo hili katika Kamati, ilionekana kwamba kanuni za kusimamia utekelezaji wake bado hazijakamilishwa na hivyo limekuwa ni pendekezo la Kamati kwamba kanuni hizi pamoja na miongozo ya kutambua maeneo lindwa, basi ziandaliwe haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika haya maeneo lindwa kuna fursa muhimu ambayo imeachwa na isipoangaliwa vyema tutakuja kugundua kwamba uharibifu wa mazingira unaotokana na kutoyalinda na kuyahifadhi maeneo haya, basi utaleta athari kubwa kwenye maeneo haya. Fursa hii napenda niitambulishe katika dhana inayoitwa Geoparks. Sasa ili niweze kuiweka vizuri naomba uniruhusu niweze kuizungumza kwa lugha ifuatayo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, what are the Geoparks? Geoparks are places where outstanding geological heritage (naomba uchukue hilo neno) ‘outstanding geological heritage’; is used to support sustainable development through conservation, education, community engagement and sustainable tourism. Kwamba ni maeneo yenye umuhimu wa kipekee kijiolojia ambayo yanapaswa kulindwa na kuhifadhiwa ili kuzuia uharibifu unaoweza kutokana na shughuli za kibinadamu. Pia kuwa sehemu ya kutoa elimu na mafunzo kwa vijana wa Taifa hili, na pia kuwa urithi kwa vizazi vijavyo kwa sababu ni maeneo yenye umuhimu wa kipekee, na zaidi sana kuwa sehemu ya kukuza utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi ukakuza utalii katika maeneo ya geoparks mpaka vitu vifuatavyo viweze kufanyika: Lazima uweze kutengeneza historia yake vizuri, lazima uweze kuandikia maeneo kama haya maelezo ambayo ni yakinifu na baada ya hapo yanapaswa yawe katika maandishi na ikiwezekana hata katika video clips. Sasa haya maeneo ni fursa ambayo katika Sheria yetu ya Mazingira yapo, kanuni hazipo, lakini tumekuwa tukipoteza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niruhusu nitoe mifano michache. Mfano wa kwanza ni Oldonyo Lengai ambao Kimasai wanaita Mlima wa Mungu. Sasa umuhimu wa Oldonyo Lengai ndiyo mlima pekee ambao unatoa active volcano, lakini tabia ya pili ya Oldonyo Lengai, the only active nitro carbonatite volcanic in the world. Dunia nzima, mlima unaotoa volcano yenye madini ya nitro carbonatite. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaongelea kitu ambacho dunia nzima inatambua hivyo na wengine wote wanaokuja hapa nchini, atakwambia baada ya mambo yote I want to do Oldonyo Lengai. Ataenda ku-hike pale, lakini Taifa halipati mapato yoyote kutokana na Lengai, badala yake, wale watu wanaitwa porters wanawapandisha mlimani lakini haukuhifadhiwa kwa njia yoyote ile. Kwa hiyo, wabeba mizigo pekee ndio wanaofaidika kupata mapato kwa kuwapeleka watu pale mlimani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupe uzoefu. Wakati fulani jopo la wataalam tukiwa pale mlimani, ilikuja helicopter kutoka nchi Jirani, ikawa inakuja ku-shoot picha wakati volcano ilipokuwa imelipuka bure, wakati sisi hatutambui. Kwa hiyo, lengo la kutamani kwamba geoparks zitambuliwe na zilindwe, ni kuhifadhi maeneo kama haya ambayo yana urithi mkubwa wa kijiologia lakini pia yanaweza yakaliingizia Taifa pato la kutokana na utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mwingine, wote mnao-drive kwenda Dar es Salaam, mnapomaliza Mbuga ya Kongwa, upande wa kulia ukipenyeza macho tu dirishani kwa gari yako utaona mlima una miamba myeupe, white sheets za mlima mmoja unaitwa Mautia. Huu ni mlima pekee ambao madini aina ya Yoderite yaligunduliwa kwa mara ya kwanza duniani, lakini leo ukienda unakuta watu wanachimba kokoto. Kwa hiyo, maana yake ni kwamba tusipohifadhi, next time utakuta kale kamlima ketu kameondoka na wale watu wanaosoma literature ya kwamba Yoderite kwa mara ya kwanza imegunduliwa Tanzania, watakuta mlima haupo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu, tumekuwa tukiongelea Tendaguru site kama site ambayo ilikuwa na Dinosauria mkubwa kabisa aliyeko baharini Ujerumani. Leo nenda pale Tendaguru uone panafanyika nini? Hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pendekezo langu ni kwamba, watu wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), watakapotunga kanuni hizi, washirikishe wataalam wa kijiolijia kwa sababu tunazo geoparks zaidi ya 20 nchi hii ambazo zote hazitambuliwi umuhimu wake, lakini pia zimeachwa tu na wakati mwingine fedha iliyopaswa kuingia, utalii ambao tungeweza kuupata haufanyiki. Naomba sana hilo liweze kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongee hoja ya mwisho nadhani muda wangu utakuwa unaniruhusu kuongea hoja moja kwamba, tumeshuhudia maji mengi ya mvua zilizotokea miezi hii ya karibuni, lakini maji haya hayaelekezwi kuingia kwenye mabwawa yetu. So, hili linapaswa lifanyiwe kazi kwamba ni kwa nini unapo-drive kutoka Mtwara mpaka Mwanza maji yamejaa, lakini kwa nini hayaingii kwenye mabwawa? Ni tatizo la kimazingira, lazima tulifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yetu katika mapendekezo yake tumesema, tunatamani kuona mwongozo wa kitaifa wa uvunaji maji kuanzia kwenye kaya na familia. Yaani kwa maana ya kwamba, mtu unapokuwa umejenga nyumba yako, weka gata basi tuvune maji ili kupunguza surface run off ambayo ndiyo inapelekea kuleta mafuriko baadaye. Pia katika hii hoja ya kutoharibu mazingira kwa sababu ya maji ya mvua, ujenzi wetu umeendelea kuwa wa kale. Unajua kabisa hili ni daraja, ili uweze kuepuka yale mafuriko na kuvunja madaraja, kwa nini hatujengi kingo katika madaraja kuanzia mbali kidogo ili maji yasipate nguvu ya kubomoa madaraja? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona unaangalia muda wako. Naomba uniruhusu kumalizia kwamba tunaweza tukafanya jambo la msingi sana iwapo tutazingatia uvunaji maji, mwongozo wa kuanzia kaya na taasisi za Serikali. Miaka mitatu iliyopita, tumejenga shule ngapi? Vituo vingapi vya afya? Ni habari gani kama tungekuwa na gata za kutunza maji katika nyumba za taasisi za Serikali peke yake, tungepunguza surface run off, lakini pia tungekuwa na hifadhi ya maji ya kutosha kwa ajili ya matumizi ambayo tungeyahitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa nafasi. Naunga mkono hoja. (Makofi)