Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Eng. Stella Martin Manyanya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nyasa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa hii nafasi. Nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa rehema zake, lakini pia nikushukuru wewe mwenyewe kwa namna ambavyo unaongoza Bunge letu vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli hatuwezi kuchangia kabla hatujamsemea Mheshimiwa Rais na wanaomsaidia. Kimsingi Mheshimiwa Rais pamoja na timu yake inayomsaidia, tukianza na Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Naibu Waziri Mkuu lakini na sisi tukirudi kwenye Bunge letu, Mheshimiwa Spika, tuko vizuri na ninaona tunakwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuwapongeza Waheshimiwa Wenyeviti wetu wote ambao wamewasilisha taarifa zao hapa. Mwenyekiti wetu wa Kamati ya Maji na Mazingira pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama. Nawapongeza sana kwa taarifa zenu zote ambazo zinalenga kuisaidia nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo niwapongeze Waheshimiwa Mawaziri ambao wnasimamia sekta ya maji pamoja na mazingira kwa ujumla wake kwa kweli wanajitahidi. Wanajitahidi sana pamoja na wale wote wanaowasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo naomba nirudi kwenye suala linalohusiana na Sheria Na. 11 ya mwaka 2009, kifungu namba 23 ambacho kinahusisha Sheria ya Usimamizi wa Matumizi ya Rasilimali Maji. Pia, hapo naomba kwa kweli nirudie kusema ambayo pengine wengine walisema. Hata hivyo, kwa unyeti wa suala hili inabidi lazima nirudie tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kufahamu mimi kama Mbunge ninayesimamia sekta ya maji, lakini kama Mhandisi wa umeme; nataka kufahamu kwa nini Bwawa la Mtera halina maji? Tunahitaji majibu ya uhakika kwa nini Bwawa la Mtera halina maji? Nikizungumzia Bwawa la Mtera inamaana ni Mtera itaambatana na Kidatu, itaambatana na Kihansi, kwa sababu wote hawa wako kwenye mstari mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni suala muhimu sana kulitafakari. Ni muhimu sana kwa sababu gani? Nchi yetu tumekwishapitia changamoto nyingi za kupatikana kwa umeme, na chanzo chake ni ukosefu wa maji kwa sababu tumekuwa tukitegemea sana umeme wa maji. Kwa bahati nzuri Mwenyezi Mungu ametupatia maji kwa kiasi cha kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inashangaza, inashangaza sana. Mara ya mwisho nimepita pale Mtera tarehe 9, ilibidi nisimame nipige picha. Niliomba kama Mjumbe wa Kamati japo hawaruhusu. Niliomba, nikasema kwamba hivi ni kitu gani? Maana mpaka sasa magugu yameanza kuota yanaingia mle kwenye bwawa. Ni kitu gani hiki? Mvua zinanyesha kote kabisa na zinanyesha kila siku. Hivi kweli ukame uko Mtera tu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hatuwezi kuendelea kupeana majibu rahisi rahisi, haiwezekani. Tunategemea sasa hivi nchi nzima iwashe umeme kupitia vijiji vyetu tunavyovisambazia umeme. Vile vile tunawahamasisha wawekezaji wa aina mbalimbali waje kuwekeza Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu umeme tunaouzungumzia wa Bwawa la Mwalimu Nyerere megawatt 2,100 haziingii leo kwa mara moja. Zitaingia awamu kwa awamu. Tumeambiwa hapo kwamba, zitaanza megawatt 235, zitafuatia megawatt 235, jumla yake 470 na kadhalika. Sasa, wakati huo unapofanya hiyo kazi, unaingiza megawatt 470 lakini una-phase-out (unazitoa kwenye system megawatt 473), yaani ukijumlisha 80 ya Mtera, 204 Kidatu, 189 ya kule Kihansi unazitoa kutokana na upungufu wa maji halafu unasema unaingiza nyingine. Hii hesabu ya kutoa na kujumlisha inatupatia kitu gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naifikiria nchi hii kuna watu wanatuchezea. Hata hawa watu ambao wanaokuja kutusaidia kwa mfano kwenye suala la utafiti au uandaaji wa miradi lazima tuwe nao makini. Mbona tunao wasomi wengi kwa nini kila siku tunarudi kwenye tatizo hilo hilo? Tutasema haya tusubiri Malagalasi nayo tunaijenga, sawa tunajenga labda megawatt kama 70 mpaka 80, Rusumo imeingia, lakini kwa sababu ya kutokutunza hivi vyanzo vya maji, kutokuwa na mawasiliano katika utekelezaji wa miradi yetu ya maendeleo, matokeo yake hata hiyo itakauka hivyo hivyo. Ni nani huyu aliyeamua kutuangamiza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naongea haya kwa uchungu. Nimesema hili na nilisema siku ile nisichangie siku ya Kamati ya Nishati kwa sababu niliona kwanza nisimuonee Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, ameingia juzi japo ni sekta anaendelea nayo. Nimesema nianzie na hawa watu wa maji tunaowasimamia, kwa nini hawasimamii matumizi bora ya maji? Kwa nini wanaleta hii changamoto?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunafurahia hapa. Wizara ya Kilimo na yenyewe inasema nitachimba mabwawa, nitapeleka umwagiliaji na nini inatoka, wa mifugo anasema vya kwake vinatoka. Kwa nini hakuna usimamizi wa pamoja tukajua wewe wa kilimo utachukua maji kiasi fulani na utachukulia eneo fulani, huyu hapa anayehusika na mifugo atachukulia eneo fulani lakini sasa tumekuwa tunakwenda na kila mtu anapambana kwenda kivyake. Hii hatuiweki vizuri nchi yetu katika hali inayostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni namna ambavyo tunavilinda hivi vyanzo. Kwa mfano, Dar es salaam kila mwaka mafuriko, mara sijui mafuriko, mara sijui madaraja yamebomoka. Hivi nyie mnataka hela yote iwe inakwenda kujenga Dar es salaam tu? Sisi huku tunasubiri mpaka lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ukiangalia mahali kama mle Vigunguti kwenye mabonde hapakuwa na nyumba, zinajengwa tu, kwenye mabonde; usimamizi ni mdogo, matokeo yake kila mwaka sisi ni watu wa kulia sijui nyumba zimechukuliwa. Watu kwa akili zao wanakwenda kujenga kwenye mifereji ya mito halafu wanalia maji yanawaondoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nadhani, wizara inayohusika na Mazingira na tena bahati nzuri iko chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais, ichukue nafasi yake katika kuongoza mapambano katika kuhifadhi mazingira yetu. Si hivyo tu, tunashauri kwamba, iwe sasa ndiyo msimamo. Wizara hiyo ipewe meno ya kutosha katika kuhakikisha kwamba Wizara zote zinawajibika na kutoa taarifa maalum kabla haijafanya mradi wowote ule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo nikirudi upande wa maji. Tunasema kwamba, maji vijijini karibu tunafika asilimia 75, mjini asilimia 85. Hata hivyo, hizi taarifa za ujumla zinaumiza baadhi ya maeneo. Juzi jumamosi iliyopita tulikuwa Tabora. Nilipata huzuni kujua kwamba Wilaya ya Urambo pale Urambo Mjini mpaka sasa asimia ya maji ni 24.5 tu. Watu wa Nyasa wanisamehe, mimi ni Mbunge wa Nyasa na wa kitaifa, lazima pale tunapoona kuna mapungufu tuwasaidie wenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Urambo ina hali mbaya, Sikonge ina hali mbaya. Pamoja na kuwa na huu Mradi tunaoutegemea wa kutoa maji Ziwa Victoria kupeleka huku, Mradi huu uharakishwe na usaidiwe. Hata kama pesa zinakuwa hazitoshi, basi hawa wapewe jicho la kipekee ili waweze kupata maji. Yako maeneo kama hayo katika nchi yetu yafikiriwe na yapewe Kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda kwa ujumla ujumla kweli kuna watu wanaumia lakini tunafikiria kwamba tuko nao kumbe wenzetu wana hali mbaya sana. Mimi binafsi siku ile nilitaka kutoa machozi niliposikia kwamba kule walipoanzia machifu, kwa akina Mama Sitta, akina Mzee Sitta aliyesimamia Bunge hili, Jimbo lile halina maji kabisa, maana yake nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi ninaomba sana, nafahamu Wizara inajitahidi sana lakini kusema kweli katika hili sisi tutakuwa mstari wa mbele kuanza sasa kufuatilia kwa karibu, kuona kwamba maeneo yale ambayo yana changamoto kubwa yaweze kusaidiwa. Jambo lingine tunasema kwamba katika ulinzi huo basi ni vyema ushirikishwaji uwe mpana zaidi hata kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno yangu haya nakushukuru sana naunga mkono hoja ya Kamati ya Maji na Mazingira. (Makofi)