Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na mimi kunipa nafasi ili niweze kuchangia jioni hii ya leo. Nami naomba nimtangulize Mungu katika mchango wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na pongezi kuwapongeza Wenyeviti wote wawili, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Mwenyekiti wa Kamati ya Maji na Mazingira na Wajumbe wote wa Kamati hizo, naomba pia nichukue nafasi hii kumpongeza sana Waziri wetu wa Maji, Mheshimiwa Jumaa Aweso, Naibu wake Maryprisca Mahundi pamoja na Waziri wa Mazingira Mheshimiwa Jafo na Naibu wake Mheshimiwa Khamis Hamza Khamis na Watendaji wote wa Wizara zote hizo mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa sijajitendea haki, niungane na wenzangu wote waliompongeza Mheshimiwa Rais wetu ama Samia Suluhu Hassan, ambaye kwa kweli sera yake ilikuwa ni kumtua mwanamke ndoo kichwani, tunaona kwa kweli amejitahidi kutafuta pesa popote kuhakikisha kwamba anamtua ndoo kichwani mwanamke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kupongeza hii Wizara ya Maji, kwa sababu tumefanya ziara kwenye miradi, kati ya miradi mingi tuliyoitembelea ni mizuri sana. Bahati nzuri tulikwenda hata Babati kwenye mradi wako ule wa maji ambao ni mradi mkubwa sana tumeona umetekelezwa na Wahandisi wa Ndani, katika ule mradi tulichojifunza kwamba Wahandisi wa Maji pia wanafanya vizuri sana, kwa sababu waliokoa karibu bilioni kumi ambazo hizo zingeweza kwenda kwenye miradi mingine. Kwa hiyo, tunaomba Serikali iendelee kuwatumia pia Wahandisi wa ndani ambao wamekuwa wakitekeleza pia miradi mikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasema kwamba haki inatakiwa iendane na wajibu, ukipata huduma ya maji, basi na wewe una wajibu wa kulipa bili za maji. Leo hii mimi ninasikitika sana kuona Taasisi zetu za Serikali ndiyo zenyewe zina deni kubwa sana la maji. Taasisi hizi zinadaiwa takribani zaidi ya bilioni 26, hizi ni pesa nyingi sana, tungeamua hizi pesa tuende tukachimbe visima vya maji nafikiri Majimbo mengi sana yangeguswa na Kata nyingi sana zingeguswa na vijiji vingi sana vingeguswa. Kwa hiyo, kutolipa madeni haya kunapelekea sasa hizi mamlaka zetu kutofanya vizuri sana. Sasa mimi ninajiuliza OC mnazipeleka wapi hizi ambazo huwa tunazipitishwa kwa ajili ya kutumia? Kwa nini hampeleki kwenda kulipa madeni ya maji? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sasa uwepo mpango maalum, Mheshimiwa Jenista tunaomba utusaidie na Waziri Mkuu, kwamba hizi taasisi zinazodaiwa haya madeni zilipe uwepo mpango maalum ikiwezekana basi Hazina yenyewe moja kwa moja ipeleke kwenye Mamlaka ya Maji. Kwa sababu haiwezekani Taasisi za Serikali zinaongoza kwa kutolipa madeni, kwa kutolipa bili na sasa hivi basi wawekewe hata mita za LUKU zile ili wasiendelee kujilimbikizia madeni. (Makofi)

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ritta kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Chumi.

TAARIFA

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Ritta Kabati, dada yangu kwamba hata kule AICC kama ambavyo imeonesha taarifa yetu ambao wanaongoza kwa kutolipa madeni na kutolipa bili ni taasisi za umma.

Kwa hiyo, hicho kinachojitokeza huko kwenye maji yawezekana kiko kwenye TANESCO kama ambavyo ilivyo kwenye AICC, kwa hiyo hatua kali zinatakiwa kwa kweli zichukuliwe na utaratibu mzuri ufanyike taasisi za umma zilipe bili ili hizi taasisi ziweze kujiendesha na ziweze kutoa huduma kwa ufanisi. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Ritta taarifa unaipokea?

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea hii taarifa kwa mikono miwili kwa sababu kwa kweli siyo vizuri OC tunazipitisha kwa nini hawalipi hizi bili? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee na hoja yangu nyingine ni upotevu wa maji nchini. Kumekuwepo na upotevu mkubwa sana katika hii miradi ya maji, tunajenga miradi ya maji mikubwa lakini pia upotevu wake ni mkubwa sana. Sasa ziko sababu, sababu ni uchakavu wa miundombinu ya mabomba lakini pia na hii miradi inakuwa muda mrefu sana haifanyiwi ukarabati, tunaomba hili liangaliwe ili miundombinu ikarabatiwe kwa wakati ili kusiwepo na upotevu wa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kumekuwepo na kupasukapasuka kwa mabomba hasa yanayopita katikati ya barabara lakini tunaona kuna uzembe unafanyika kwa hawa watendaji wetu kwamba, maji yanatoka usiku na mchana unaweza ikatolewa taarifa lakini unaona taarifa ile haizingatiwi maji yanaendelea kupotea na pesa nyingi tumezipoteza katika hiyo miradi tunaomba kwa kweli hili liangaliwe na ikiwezekana kama kuna upungufu wa watumishi wawepo watumishi ili waweze kufanya hiyo kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nimejipanga kuzungumia kuhusu Bwawa la Mtera kwa sababu na sisi tulifanya pale ziara na mbaya sana tuliambiwa kwamba lile bwawa lina maji mengi mpaka walitutaka tulete maji kuja kuleta huku Dodoma kwa ajili ya kutumia, lakini sasa tunashangaa kuona kwamba lile bwawa halijazi maji. Mheshimiwa Manyanya ameongea sana, sasa naomba jamani hili jambo lisichukuliwe poa ni jambo zito sana la nchi hii lakini kuna vyombo mbalimbali viende vikafanye tafiti kabisa kuona ni kwa nini jambo hili linatokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nizungumzie kuhusu hali ya upatikanaji wa maji vijijini. Mpaka sasa hivi tumeona kwamba maji vijijini kuna karibu vijiji 9,670 vimepatiwa maji lakini kumekukuwepo na vijiji karibu 12,318, nilikuwa naomba Serikali sasa ijipange na iwe na mkakati haswa wa kuhakikisha kwamba vijiji 2,300 vinapatiwa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niwapongeze sana REA wana mpango mzuri sana kuhakikisha umeme unapatikana katika vijiji. Sasa mimi ninaomba hata hawa RUWASA pamoja kuwa na Mtendaji wao mzuri sana naomba wajipange kuhakikisha vijiji vinapatiwa maji, kwa sababu Serikali iliweka hiyo Wakala na Wakala inafanya vizuri sana ikiendeshwa na Engineer Kivejaro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa ambayo ipo hapo sasa ziko changamoto zinazosababisha wasifanye vizuri sana, kwanza upatikanaji wa fedha za Mfuko wa Taifa wa Maji, hii ni changamoto kubwa sana kwamba Hazina na yenyewe inakuwa hailipi fedha za certificate na advance payment na kusababisha sasa miradi mingi kutokwisha kwa wakati na miradi mingi ikicheleweshwa maana yake pia gharama ya mradi inaongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba hili jambo liangaliwe sana hii changamoto itatuliwe ili kusiwepo na matatizo makubwa kama hayo, lakini tumeona kwamba kuna miradi inakamilika lakini pesa ya usambazaji maji inakuwa haitolewi kwa wakati. Sasa tunafanya hii miradi ya nini? Kama maji hayasambazwi je, nia ya kumtua mwanamke ndoo kichwani iko wapi? Mimi ninaomba hili jambo pia liangaliwe sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kitu kikubwa ambacho kinanisikitisha imenunuliwa mitambo ile ya maji ya kuchimba visima vya maji, kila Mkoa ipo lakini ile miradi imekaa imelala tu, changamoto nini? Hakuna bajeti, hili jambo naomba jamani tuweke mkakati halisi. Kuna kata nyingine hazina miradi ya maji, hazina visima lakini gari limekaa hapo tatizo ni pesa na hapo hapo madeni kibao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba Serikali iwe na mkakati kuhakikisha kwamba haya magari kama ambavyo yametumia pesa nyingi basi yanatumika na maji kweli kumtua mwanamke ndoo kichwani itimie kwa sababu hii ndiyo sera kubwa ya Mama yetu na sera kubwa ya kuhakikisha kwamba sisi wanawake wote tunamuunga Mama mkono na taasisi zote kuhakikisha kwamba mwanamke anatuliwa ndoo kichwani. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Ritta Kabati, unga mkono hoja.

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa kuna changamoto ya upandaji wa bei za maji kutofautiana katika maeneo mbalimbali hili na lenyewe ni muhimu sana, unakuta vijijini bili za maji zinakuwa kubwa kuliko hata mijini sasa uwekwe mkakati wa kuhakikisha kwamba bili angalau zinakuwa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja, nakushukuru sana. (Makofi)