Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Desderius John Mipata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Na mimi niungane na wenzangu kuchangia hotuba ya Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima, lakini vilevile nawashukuru wana Nkasi Kusini kwa namna ambavyo wananipa ushirikiano wakiwepo viongozi wangu wa Chama cha Mapinduzi, Mkurugenzi wangu Kaondo, DC wangu Kimantra na wananchi kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana mkono na watu wote wanaosema kazi ya Wizara hii ni nzuri na Mheshimiwa Muhongo pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Kalemani wana uwezo wa kutosha na wanafanya kazi vizuri sana. Mimi bahati nzuri niko kwenye Wizara hii, naona uongozi wanaoutoa kwetu sisi ushirikiano kama wana Kamati, lakini pia kwa Wizara nzima. Kwa hiyo, tunawatia moyo na kuwapa big up, waendelee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la muhimu ni kwamba katika kazi ya kupeleka umeme vijijini, yapo maeneo yamebaki nyuma. Kwa mfano, tunaposema umeme mkubwa Gridi ya Taifa, Mikoa kama ya uzalishaji ya kilimo kama vile Rukwa na Katavi wamechelewa na Kigoma pia hawajapata. Tunaomba Wizara ifanye juhudi kuhakikisha kwamba tunapata umeme mkubwa ili tuweze kusisimua maendeleo katika maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya Mkoa wa Rukwa yako hodari kwa kilimo, namna pekee ya ku-attract wawekezaji katika kuongeza thamani ya mazao yetu ya kilimo ni kupatikana kwa nishati ya uhakika. Vilevile katika maeneo ya Namwele, Komolo II pale kwenye Jimbo langu, kuna deposit ya kutosha ya makaa ya mawe, muichunguze, ambapo inaweza ikasaidia kuongeza umeme katika Gridi ya Taifa kama inapita sehemu hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengine ambayo tunahitaji kupata umeme ni vijijini kwa kupitia REA. Kusema ukweli utekelezaji wa REA Awamu ya Kwanza na ya Pili kwa Wilaya yangu na Jimbo langu, umetia moyo sana wananchi kwa utekelezaji wa Serikali hii. Kwa hakika ni kitu ambacho tumejivunia hata kurudi hapa Bungeni. Nawapongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kosa tu ninaloliona ni kwa Serikali kutopeleka pesa ya kutosha inayotengwa kwa REA. Hiki kimekuwa kikwazo kikubwa ambacho kinarudisha juhudi kubwa zinazofanya na watendaji wakuu hawa wa Wizara huko vijijini. Umeme unakuwa hauendi kwa wakati. Sasa tunaweza tukajidanganya tena, leo tumetenga hela za kutosha, lakini kama mtindo ni huu wa kutowapa pesa, bado tutarudi nyuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, azma ya kupeleka umeme vijijini, wenzangu wamesema, ni ya muhimu sana, inatusaidia hata kuokoa suala la mazingira. Umeme utakapofika vijijini kote, tutaokoa tatizo la uharibifu wa mazingira kwa sababu litapeleka nishati, ukiachilia mbali ajira na mambo mengine ambayo yametajwa na wenzangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwangu, mwaka 2015 tulitarajia kupeleka umeme katika Makao Makuu ya Jimbo, Kate, kupitia vijiji vya Kalundi, Miula, Komolo II, Katani, Chonga lakini mpaka sasa umeme haujawaka. Bado vijiji ambavyo vimeorodheshwa tena katika awamu hii, naomba na vyenyewe vifikiliwe, navyo viko katika vijiji vya Tuchi, Kitosi, Sintali, Nkana Mkomanchindo, Kasapa na Kata tatu za Mwambao wa Ziwa Tanganyika. Mheshimiwa Waziri kata tatu za mwambao wa Ziwa Tanganyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kata tatu za mwambao mwa Ziwa Tanganyika naomba uziwekee umuhimu wa mbele sana, ni maeneo ambayo hayana barabara na kila mara huduma tunawafikishia kwa kuchelewa na wakati mwingine hawapati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi ninavyozungumza, Kata hizi hazina mawasiliano ya simu, hazina barabara nzuri, lakini juhudi na uthubutu wa Wizara hii nafikiri mnaweza mkawahi ninyi. Nawaomba kwa heshima niko chini ya miguu yenu, naomba mwapelekee wananchi hawa ili waweze kuonja neema ya nchi yao. Wananchi hawa wa Kata hizi wamekuwa wakizalisha samaki, wanavuna sana samaki, lakini wanazipeleka Zambia kufuata soko, kwa sababu hatuna uwezo wa kuchakata minofu. Utakapopeleka umeme utatusaidia sana kuhakikisha kwamba sasa wanaweza wakapata wawekezaji ambao wanavutiwa na nishati hii muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni geological survey. Mkoa wa Rukwa, una miamba na mazingira yanayofanana na sehemu nyingine nchini, lakini hatuna bahati ya kupata aina yoyote ya madini tunayoshughulika nayo kule.
Kwa hiyo, inaonesha kwamba utafutaji wa madini katika maeneo yale, kazi hiyo haijafanywa kwa juhudu ya kutosha; na tunaona mahali ambapo juhudi zimefanywa watu wanapata ajira, mzunguko wa pesa umekuwa mwingi na wawekezaji wamepatikana katika maeneo ambayo tumeona madini yamepatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawaomba kitengo kinachoshughulika na kazi hiyo, kijaribu kutafuta kwa nini Mkoa wa Rukwa tu pasipatikane madini yoyote ambayo tunashughulika nayo kwa sasa? Hebu tujaribu kuona katika nchi yote, ni eneo gani tunaweza tukanufanika? Ni aina gani ya madini yanaweza yapatikana katika maeneo hayo? Zipo traces na watu wengi wamekuwa wakija wanazunguka zunguka, siyo maalum sana, lakini wanapata na wanasafiri wanarudi. Kwa hiyo, inaonekana kama juhudi ikifanyika ya kutafuta madini, tunaweza tukapata madini ambayo yanaweza kutusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wamesema hapa jiografia inatueleza kwamba maumbile ya miamba yaliyoko Rukwa na yale ambayo yako kwenye eneo la Ziwa Albert kule Uganda ambako kulipatikana mafuta, yana asili moja. Sasa kama yana asili moja, maana yake, juhudi ikifanyika zaidi tunaweza tukanufaika na jambo hilo la kupata mafuta katika Bonde la Rukwa. Kwa hiyo, tufanye hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana kama siyo mwaka juzi, Wizara ilitueleza kwamba kuna leseni ya kutafuta mafuta katika maeneo ya Ziwa Tanganyika, hasa katika Jimbo langu au kule juu; na nimeona juhudi ya hawa watu waliokuwa wanatafuta, lakini sijaona kama imeripotiwa humu kwenye hotuba yako na ningependa kupata maelezo hawa watu hoja yao imeishia wapi? Walisema mnataka leseni msizitoe ili watu waweze kuanza kutafuta mafuta katika maeneo hayo. Sasa ni kitu kimekaa kimya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nikizunguka kwenye ziara yangu, wananchi wananiuliza, nitakosa kupata majibu, kwa sababu wameona ambavyo watu wameenda, wamezunguka sana, lakini sasa nimeona kwenye bajeti hii hakuna kitu kilichotajwa kama hicho.
Mheshimiwa Waziri, naamini udhubutu wako unaweza, tuhakikishe kwamba ziwa lile Tanganyika nalo tukilifanyia kazi vizuri tunaweza tukafanikiwa kupata aina fulani ya madini, kama siyo mafuta na tukanufaika kama hao wengine wenzetu ambao sasa hivi Mtwara wameonesha kabisa matumaini kwamba pamoja na kwamba walikuwa wamebaki nyuma kidogo, sasa hivi wanakuja juu na uchumi wao utapanda kwa haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nawashukuru sana, naomba umeme ufike katika Jimbo langu la Nkasi Kusini uwashwe, waya umeshafika lakini bado kuwasha na pengine mnawapa wakandarasi goigoi. Huyu Mchina ambaye anajenga huu umeme kupeleka kwenye Jimbo langu, hata kwa Mheshimiwa Malocha amezungumza hapa, ni mtu nadhani hana uwezo wa kutosha. Mjaribu ku-recruit watu ambao ni wenyeji wetu. Muwatafute wazawa ambao watakuwa na uchungu pia wa uzalendo. Hawa wenzetu, hata mimi nina wasiwasi na vifaa vyenyewe havina specification ya kutosha, wanakuja vina-bounce, vinakuwa haviwezi kufanya kazi vizuri...
MWENYEKITI: Ahsante, tunaendelea.