Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chwaka
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. HAJI MAKAME MLENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi jioni hii, nami niweze kuchangia katika Kamati hizi ambazo zimeleta taarifa mbele yako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kutupa nguvu na uhai wake kuweza kufika Bungeni jioni hii. Aidha, nampongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi zake ambazo anazifanya na kupata sifa kubwa ndani na nje ya nchi. Hapa kwetu ndani ya nchi ameonesha ukomavu mkubwa. Juzi tu wenzetu walipokuwa wanadai maandamano, walitegemea sana kwamba watazuiwa ili iwe kama ndiyo kigezo cha silaha yao ya mazungumzo, lakini Mheshimiwa Dkt. Samia aliwahurusu na kuwapa ulinzi wa kutosha ili waweze kufanya maandamano yao na pia kukosa neno la kuzungumza kwa sababu hawakuzuiliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Wizara ya Maji na leo ndiyo nitakayochangia, japo mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Maji na Mazingira, lakini kwa leo nitachangia Wizara ya Maji. Nitachangia mafanikio na pia changamoto ambazo zinapatikana katika Kamati na katika Wizara ya Maji. Nianze na kuipongeza Wizara ya Maji kupitia Waziri wake, kaka yangu Mheshimiwa Aweso pamoja na watendaji wake wote kwa utendaji mkubwa ambao anaufanya. Ameonesha umahiri mkubwa kwa sababu Wizara yake ina jukumu kubwa la kusambaza maji katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020/2025 imeiagiza Serikali ikifika mwaka 2025 iwe imeshafikisha asilimia 95 ya upatikanaji wa maji mijini na asilimia 85 ya upatikanaji wa maji vijijini. Wizara hii imeshafanya kazi na kufikia asilimia 88 mijini na asilimia 77 vijijini. Aidha, kwa kupitia miundombinu, mijini wameshafikisha asilimia 91 na vijijini 80. Kwa hiyo, hii ni juhudi kubwa ambayo wanaifanya Wizara ya Maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia bajeti ya mwaka 2023/2024 Wizara ya Maji ilikuwa na plan ya kutengeneza miradi 244. Kati ya miradi 244 miradi 70 tayari wameshatekeleza, maana yake wameshatimiza na miradi 174 ipo katika hatua mbalimbali na tunategemea kabla ya kumaliza Juni, miradi hii itakuwa imeshakamilika zaidi wakiwa wamewezeshwa katika yale maeneo ambayo yanawategemea watu wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kidogo kwenye changamoto. Kamati imebaini kuna changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa vikwazo kwa Wizara ya Maji kuweza kufikia hatua ambazo wanazikusudia au kufanya mwendo kuwa wa kasi ili kufikia kutatua upatikanaji wa maji safi na salama. Unajua kwamba maji yanapatikana katika maeneo mengi, lakini mengine siyo maji safi na salama na wananchi wanahitaji maji safi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwenye changamoto hizo Wizara ya Maji kulingana na mwonekano wake au kulingana na kwamba inafanya kazi katika maeneo yote ya Tanzania, kwa hiyo, inahitaji fedha nyingi sana ili kuweza kutengeneza miradi mbalimbali ya kuweza kufikisha maji safi na salama katika maeneo mbalimbali ya nchi. Hili ni tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kwamba mbali ya kuwa Wizara hii imeongezewa bajeti lakini bajeti bado haitoshi kulingana na uasilia wa Wizara hii. Nashauri kwamba bajeti inayokuja ya mwaka 2024/2025 basi Wizara ya Maji iangaliwe sana kwa kuongezewa bajeti ili iweze kufanya kazi kwa urahisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye changamoto ya pili kuhusu mashirikiano. Ninaposema ‘mashirikiano,’ hasa nakusudia kwenye taasisi za Serikali au kupitia Wizara na Wizara. Kama kutakuwa hakuna ushirikiano mzuri, maana yake Wizara inaweza ikapata vikwazo vya kuweza kufikia zile idadi ambazo zinatakiwa; asilimia 95 mijini na asilimia 85 vijijini kutokana na kukosa ushirikiano na taasisi nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nitoe mfano. Mwenzangu amesema kwamba Serikali inadaiwa shilingi bilioni 26.9 ambazo hawajalipa mpaka leo. Sasa tuone Serikali kama hawajalipa vipi tutatoa huduma ya maji safi na salama? Kwa sababu huduma ili iweze kupatikana vizuri, hata wale wote wanaopatikana ndani ya huduma, nao wahudumiwe vizuri. Wakikosa kuhudumiwa vizuri, siyo rahisi kutoa huduma nzuri. Hivi vitu vinaenda pamoja. Kwa hiyo wahudumiwe vizuri nao watoe huduma nzuri, nasi tunategemea tupate maji safi na salama. Kwa hiyo, naiomba Serikali kuweza kuangalia suala hili liweze kufanyiwa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba katika ushirikiano, mwenzangu alizungumza kuhusu Bwawa la Mtera. Kamati yetu ilitembelea eneo lile, na tukaambiwa changamoto zinazopatikana katika bwawa lile. Moja kati ya changamoto ambayo tuliambiwa, kuna matajiri au kuna watu wenye nguvu na uwezo wanajenga maeneo kwa ajili ya kuzingia maji yasije katika lile bwawa, bali yaende katika mashamba yao, kwa ajli ya kufanya kazi zao. Changamoto hizo tayari zimeshajitokeza, japokuwa kwa wakati huo waliweza kuzitatua. Maana yake kama kitu ulikiona leo kimefanyika, kinaweza kufanyika tena. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Bwawa la Mtera halina maji na bwawa lile linategemewa kwa kazi nyingine ili kuweza kupatikana umeme. Kwa hiyo, ushirikiano ukiwa mdogo, maana yake Wizara inaweza kushindwa kufikia hatua ya kutupa huduma nzuri ya kupata maji safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine ni ujenzi wa makazi usiozingatia taratibu za mipango miji. Hili jambo unaweza ukaliona ni dogo, lakini ni kubwa ambalo linaweza kusababisha vikwazo vya kutokufikia kutoa huduma ya kupata maji safi na salama. Kwa mfano, tulikwenda kutembelea mji mmoja ili kuangalia miradi. Mradi leo unautengeneza na unaamini katika kijiji kile umeshafikia asilimia labda 90 au 100, lakini baada ya muda mchache kuna wananchi wanaenda katika maeneo mengine ambayo yanakuja kufanya mradi ule usifikie katika kile kiwango ambacho kimetakiwa. Kwa hiyo, ushirikiano hapa unapokosekana huwa hakuna mipango mizuri ambayo inapangwa au kukaa pamoja baina ya taasisi na wahusika na huku na huku ili kuona namna gani tutatatua matatizo yetu na kuweza kwenda pamoja ili kufikia malengo yetu, kwa sababu sote tunajenga nyumba moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu naona umeshawasha, niseme tu kwamba naunga mkono hoja zote ambazo zimetolewa na Kamati. Ahsante sana. (Makofi)