Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Donge
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia taarifa za Kamati zetu mbili hizi ya Maji na Mazingira na ile Kamati ya Ulinzi na Usalama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niwapongeze Wenyeviti wote pamoja na Wajumbe wa Kamati hizi, wamezitendea haki hizi taarifa, wamezitayarisha vizuri na wameziwasilisha vizuri vilevile. Pia, nawapongeza Waheshimiwa Mawaziri wote pamoja na timu nzima za Mawizara, kwa kweli wanafanya kazi vizuri, lakini changamoto haziwezi kuacha hasa ukilinganisha kwamba uwezo wa kibajeti umekuwa ni mgumu na inashusha morali na ufanisi wa kazi katika baadhi ya maeneo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba mchango wangu niuelekeze zaidi katika Kamati ya Maji na Mazingira na zaidi sekta ya mazingira na nianzie pale mwenzangu alipomailizia Mheshimiwa Kavejuru; biashara ya hewaukaa au biashara ya carbon. Kwa kweli biashara ya carbon ni biashara ambayo Umoja wa Mataifa imeipendekeza au imeianzisha ili kusaidia kama ni incentive au motisha katika shughuli za uhifadhi. Sasa wenzetu kwa kweli katika baadhi ya nchi nyingi watumia sana fursa, na kwa kweli wamepata faida kubwa ya kipindi kirefu, lakini sisi tumechelewa kidogo. Kwa hiyo mimi nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri sasa hivi kwa kasi anayokuja na nimuombe kasi hii iendelee ili twende tukapate faida ambayo wenzetu wameshaipata kwa kipindi kirefu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hapa suala la uratibu ni suala muhimu zaidi hapa kwa sababu tunazungumzia suala la hewaukaa. Biashara ya hewaukaa misitu ipo TFS, uratibu upo Idara ya Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais na kituo cha hewa ukaa kipo SUA (Chuo Kikuu cha Sokoine Morogoro). Sasa uratibu hapa ni muhimu ili kufanya hii biashara ya hewa ukaa iwe na tija na iweze kufaidisha wanajamii kwa haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije haraka haraka kwenye suala zima la uhuishaji wa sheria ambalo wenzangu vile vile wameligusia. Mheshimiwa Waziri anajitahidi sana kwenye suala hili lakini inaonekana kuna sehemu kidogo anahitaji kusaidiwa. Kwa hiyo mimi nimuombe sana Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri Mkuu akaweke kidogo nguvu katika uhuishaji wa Sheria ya Mazingira sura 191 kwa sababu hii imebeba mambo mawili makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza kuipandisha hadhi NEMC ili iweze kuwa mamlaka. Jambo hili tukifanikiwa tunakwenda kuongeza thamani (value) ya uhifadhi na udhibiti wa mazingira yetu. Pia kuna kitu kingine ambacho ni muhimu pia ambacho kimebebwa katika Sheria hii kwenda kuandaa Mamlaka ya Kitaifa ya hewaukaa au ya uratibu wa hewaukaa (carbon).
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunazungumzia kuhusu biashara ya hewaukaa, lakini ni muhimu kuwa na Kituo cha Taifa cha Uratibu katika suala zima hili ambalo haliwezi kufanyika bila kuipitisha hii Sheria ya Mazingira. Kwa hiyo ningeliomba tu ili kuongeza tija katika biashara ya hewaukaa Mheshimiwa Waziri jikaze na uwaombe viongozi hasa Mwanasheria Mkuu na Mheshimiwa Waziri Mkuu hili jambo lisukumwe liende haraka kwenye Baraza la Mawaziri ili sheria ipitishwe na hivi vyombo viwili ambavyo ni muhimu viweze kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nije kwenye suala la zima la ushirikiano baina ya Zanzibar na Tanzania Bara katika masuala mazima ya mazingira. Kama tunavyojua kwamba masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi si masuala ya Muungano lakini masuala ya mikataba ya kimataifa na ya kikanda inayohusiana na mazingira ya mabadiliko ya tabianchi ni masuala ya Muungano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ningeliomba hili tukalizingatia vizuri kwa sababu tulishazungumza mara nyingi hapa na kwenye Kamati pia kwamba lazima tusiende kirafiki zaidi, twende tukatengeneze formal system, yaani tuwe na MOU (Memorandum of Understanding) baina ya taasisi ambayo inashughulikia masuala ya mazingira ya bara pamoja na ile taasisi ya Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sijui kwa nini Mheshimiwa Waziri na timu yake wanakigeugeu au wana kama kigugumizi katika hili. Kwa sababu ni suala dogo, ni kukaa tu, either kuamua; tunajua mnafanya kazi na ZEMA, mnafanya kazi na DoE Zanzibar, mnafanya kazi na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais lakini hii haitoshi kwa sababu ipo kirafiki zaidi. Twende tukatayarishe maandishi na dunia ndiyo ilivyo hivi sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiandaa maandishi, tukiwa na MOU, tukawa na agreements inajulikana kwamba huyu anafanya kazi hii na ushirikiano anashirikiana na nani inaenda vyema. Hii ndiyo imepelekea ile miradi ya kule Micheweni na Mradi ule wa Kaskazini ‘A’ Unguja kuwa imechelewa kwa sababu hakuna uratibu mzuri wa hii miradi kwa sababu hakuna chombo ambacho unaweza ukakikamata Zanzibar haraka zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nije kwenye suala zima la matayarisho ya mkakati wa mabadiliko ya tabianchi pamoja na hali ya mazingira ya Tanzania. Haya ni maeneo mawili muhimu kwa udhibiti wa mazingira yetu Tanzania. Sasa mkakati wetu wa mabadiliko ya tabianchi ambao ulitayarishwa mwaka 2012 hivi sasa inabidi umeshafika muda ufanyiwe mapitio ili uweze kuendana na hali ya sasa ilivyo. Sasa katika hili uratibu nao unahitajika kwa sababu Sekta ya Mazingira peke yao hawawezi kukaa wakatayarisha maandiko haya mawili makubwa. Lazima wapate takwimu na data kutoka katika sekta nyingine za misitu, maji, nishati na kadhalika… (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni vyema kwanza tukatenga bajeti nzuri lakini pia tukaziwezesha hizi sekta ziweze kuratibika na kuweza kuchangia data ambazo ni authenticated. Zile data ziwe makini kwa sababu mara nyingi hata ukiangalia ripoti zilizopita za kipindi kilichopita huzioni kwamba ziko…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa unga mkono hoja muda umeisha.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naomba niunge mkono hoja na nimpongeze Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa kazi nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)