Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kondoa Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
3
Ministries
nil
MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu lakini pili nizipongeze Kamati zote zilizoleta hoja mezani. Na nianze kwa kuunga mkono hoja zilizowekwa mezani na Kamati zote mbili zilizowasilishwa hapa Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru Serikali inafanya kazi kubwa na mambo mengi ambayo kwa kweli kila mmoja wetu anaona. Sasa tunachangia; na mimi nitachangia kwenye maeneo mawili nikipata muda nitaongeza la tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza eneo la maji. Kiukweli Serikali imefanya kazi kubwa sana hasa katika hii miaka mitatu katika kufanya miradi ya maji. Kwa hiyo tunawapongeza, tunampongeza Mheshimiwa Waziri. Ni mtu makini sana, mnyenyekevu na mfuatiliaji wa mambo kiasi kwamba kwa kweli sisi tunakuwa huru kumfuata katika kila hoja inayohusiana na maji na huwa anatusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, iko haja ya kumsaidia Mheshimiwa Aweso na Wizara yake kuhakikisha miradi tuliyoanza nayo hii miaka mitatu inakamilika. Kiukweli iko hali ambayo inatutatanisha sisi. Ukizungumzia Wizara nyingine, Wizara za Afya tunaweza tusilalamike sana kwa sababu tumejenga sana vituo vya afya na fedha zimekuja, tumejenga zahanati, hospitali za wilaya wala hakuna shida. Ukiangalia sehemu za barabara TARURA, TANROADS wamefanya vizuri sana na miradi yao imekamilika na imekabidhiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia vilevile kwenye elimu tumejenga sekondari, tumejenga shule za msingi, tumejenga madarasa na vifaa kila kitu; Wizara nyingine zimefanya vizuri sana. Sasa sisi nadhani tunahisi Wizara hii ya Maji bado haikutendewa haki sana. Kwa hiyo nilikuwa naomba kushauri kwamba Baraza la Mawaziri wamshauri Mheshimiwa Rais atusaidie Wizara hii ni muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ikiwezekana ule mkakati maalum wa kuhakikisha ile miradi ambayo imeanzwa inakamilika kabla ya Bajeti ambayo tunakwenda kuianza; bajeti ya mwaka mpya unaofuata kwa sababu miradi mingi imeanzishwa, mingi imeishia katikati. Bila kuikamilisha ile miradi maana yake tutakuja na miradi mingine ambayo pia nayo haitokamilika. Kwa hiyo natarajia bajeti ijayo ihakikishe inakamilisha miradi yote ambayo ilianzishwa na imeishia njiani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, iko miradi ambayo imefika asilimia 70 lakini leo wakandarasi hawapo, hawafanyi kazi. Iko miradi asilimia 30, iko miradi mingine asilimia 10 lakini na ukiangalia mwaka wa bajeti umeisha. Baraza la Mawaziri lisaidie kuisaidia Wizara hii ifanye vizuri kama Wizara nyingine kwa sababu Wizara ya Maji inashika maeneo mengi, inakamata maeneo mengi. Ukiangalia hata hoja za CAG katika miradi ya force account utakuta gharama kubwa zinakwenda kwenye maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi mingi inajengwa maeneo ambayo hayana maji, maji yanatafutwa. Wilaya nyingine wanatumia mpaka shilingi laki tatu kununua boza la maji, na utaona kwamba ni namna gani variation ya miradi inakuwa kubwa kwa sababu ya ukosefu wa maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kwenye Jimbo la Kondoa kuna mradi wa shilingi bilioni nne uko asilimia zaidi ya sabini. Kama ule mradi utakamilika utasaidia sana kuliko kuanzisha mradi mwingine mpya kabla hatujamaliza ule mradi mwingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mradi kwenye mitaa ya Hachwi pamoja na Mluwa ni miradi ya shilingi milioni 800 lakini leo ni mwaka wa tatu hata sura ya mkandarasi hatuioni. Watu wanatamani watumie maji; tumechimba visima nane kwenye maeneo tofauti tofauti. Tumechimba Hurumbi, Chora, Usia, Mluwa, Msui, Chemchem na Kwamtwara. Visima hivi leo vinakwenda mwaka wa pili wananchi wanaangalia mashimo lakini visima haviwasaidii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ili tupate tija tuhakikishe Wizara ya Maji inawezeshwa ili hivi visima tulivyovichimba; na ndiyo maana mimi siongelei hata hilo gari lililonunuliwa kwa sababu gari litakuja kuchimba visima wananchi wanakuta mashimo lakini hawajatatua bado changamoto ya maji. Ni vyema sasa bajeti ijayo Wizara ya Maji iangaliwe kama vile mkakati maalum wa kuhakikisha tunakwenda kutekeleza ile azma ya Mheshimiwa Rais ya kumtua mama ndoo kichwani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye masuala ya mazingira. Kwenye suala la mazingira, hasa mimi kama mwakilishi wa Wananchi Jimbo la Kondoa Mjini sijui ni nani hasa mahususi anashughulika na suala la mazingira katika Halmashauri yetu. Kwa sababu tunaona mambo ni makubwa yanazungumzwa lakini hali ilivyo kiuhalisia hatuoni utekelezaji wa zile ahadi na mipango ambayo tunaipanga katika kunusuru mazingira yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mipango na mikakati hatujui kabisa; hasa fedha hizo za Mfuko wa Mazingira tunanufaika nazo vipi? Tulikuwa na eneo moja uharibifu wa mazingira umefanyika kutokana na tabia hali ya nchi. Kingo za mto zimelika, mto umehama njia yake ya asili umehama kwenye mto mdogo, tendo ambalo linaweza likaleta hasara kubwa. Miundombinu ya umeme iko hatarini, miundombinu ya barabara ipo hatarini; leo tunatumia gharama kubwa kuanzisha barabara mpya kwa sababu tumeshindwa kuzuia ule ambao nilikwenda NEMC, nilishaongea na Mheshimiwa Waziri lakini sijaona reaction yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sasa kama sisi kama Tanzania tutakuwa tunategemea misaada kutoka nje maana yake suala la utunzaji wa mazingira kwetu inakuwa kama siyo kipaumbele, jambo ambalo baadaye tutakuja kujutia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie kwenye Zimamoto. Zimamoto nimeona ajabu sana. Mpaka kufikia mwezi Machi tunaambiwa bajeti ya miradi ya maendeleo walitengewa shilingi bilioni 9.9, lakini mpaka inafikia kipindi cha mwezi Machi hawakupelekewa hata shilingi moja. Tunapata mashaka hawa Zimamoto wanawezaje kutekeleza miradi yao kama mpaka leo Wizara ya Fedha haijawapelekea fedha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi pale Kondoa tunajambo letu tumekwishawakabidhi Zimamoto eneo kubwa kwa ajili ya kufanya mambo yao ya miradi ya maendeleo. Sasa kwa hali hii nina mashaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba; hili Jeshi ni muhimu sana; na ukiangalia kutoka Dodoma mpaka Babati hapa katikati majanga mengi yanatokea, lakini tunashindwa kuweza kukabiliana nayo. Kama gari inaungua itaungua mpaka itaisha, kama nyumba inaungua itaungua mpaka inaisha; ni kwa sababu watu hawa hawana vifaa vya kusaidia kazi yao ili iweze kuwa rahisi. Waangaliwe sana na utaona mapungufu yalivyo makubwa ambayo yapo katika ripoti ambayo imesomwa na Mwenyekiti wa Kamati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo ninaunga mkono hoja na ninakushukuru kwa nafasi. (Makofi)