Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Amber. Mbarouk Nassor Mbarouk

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ya kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu. Kwanza, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mtukufu mwingi wa rehema kwa kuturuzuku uhai na uzima na kutuwezesha kuwepo hapa kwa siku hii ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue fursa kuzipongeza Kamati zetu zote za Bunge kwa taarifa nzuri ambazo wamekuwa wakiziwasilisha toka wiki iliyopita. Kipekee niipongeze Kamati yetu ya NUU inayoongozwa na Mwenyekiti mahiri Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa na Wajumbe wote wa Kamati hii kwa ushirikiano mkubwa ambao wamekuwa wakitupatia pia kwa michango yao, miongozo yao na ushauri wao ambao umetuwezesha kutekeleza majukumu yetu kwa ufanisi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee zaidi nichukue fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ndiye mwanadiplomasia namba moja, pamoja na Wasaidizi wake, Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Waziri Mkuu na Naibu Waziri Mkuu kwa maono na maelekezo yao katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara yetu na katika kuipaisha diplomasia ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepokea michango mingi kutoka kwenye Kamati pia kwa Wajumbe mbalimbali ambao wamechangia hoja hii. Jumla ya Wajumbe Sita wamechangia hoja ambazo zinahusu Wizara yetu, naomba niwashukuru wote na niwahakikishie kwamba michango yao ni muhimu sana na tunaahidi kuifanyia kazi ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nichangie hoja kwa kutoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja kwa kadri ya muda utakavyoruhusu. Katika michango yote hii iliyochangiwa kwa Wizara yetu yote iligawanyika sehemu tatu; kwanza, ni suala la uendelezaji wa viwanja vya balozi lakini pili ni suala la Kituo cha AICC Arusha na tatu ni issue iliyoongelewa hapa ya hadhi maalum kwa wana-diaspora wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na hoja ya Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha AICC. Imeelezwa hapa kwamba hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya watumishi waliohusika na Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha AICC ambao watabainika kwa ushiriki wa uuzaji wa viwanja na mali za kituo kinyume cha utaratibu wachukuliwe hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi ya Wakurugenzi ya AICC ilimuomba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya uchunguzi wa kina kuhusu viwanja vilivyouzwa au kubadilishwa na ambavyo havionekani katika umiliki wa AICC ambavyo vipo katika sheria iliyoanzisha kituo. Taarifa ya uchunguzi itawasilishwa katika kikao cha bodi ifikapo tarehe 04 Machi, mwaka huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kulikuwa kuna hoja ya kwamba hatua stahiki zichukuliwe kwa wale watu ambao wamevamia maeneo ya kituo. Kituo cha AICC kilifungua kesi mbili za ardhi, Kesi Namba 12 na Na. 16 ya mwaka 2015 dhidi ya watu ambao walivamia hivi viwanja. Kufuatia hatua hiyo kituo kiliiomba Mahakama pamoja na mambo mengine kutangaza umiliki wa halali wa eneo hilo kwa AICC pia na kutoa amri ya kuwaondoa na kuweka zuio dhidi ya wavamizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shauri hilo lilisikilizwa na kutolewa hukumu tarehe 29 Septemba, 2017 ambapo Kituo cha AICC kilitangazwa kuwa mmiliki halali wa ardhi iliyovamiwa na kupewa amri ya kuwaondoa wavamizi na kubomoa majengo ambayo yaliwekewa uzio. Kituo kilifungua maombi ya kutekeleza hukumu hiyo tarehe 29 Oktoba, 2019 na sasa shauri la kutekeleza hukumu hiyo limepangwa kusikilizwa tarehe 19 Februari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na issue ya madai ambayo kituo hiki kinazidai taasisi mbalimbali za umma, ushauri huu umepokelewa. Aidha, napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba hadi kufikia tarehe 31 Januari mwaka huu Kituo cha AICC kimekusanya jumla ya shilingi bilioni 1.7 kutoka kwenye deni la tarehe 30 Juni, ambalo lilikuwa na shilingi bilioni tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala ambalo liliongelewa kwa hisia kidogo ni kuhusu umiliki wa viwanja vyetu vya ubalozi uliopo Ethiopia. Ubalozi wetu wa Addis unamiliki viwanja viwili vyenye ukubwa wa mita 2,000 na cha pili chenye ukubwa wa mita 1,414, hiki kiwanaja ambacho kina ukubwa wa mita 2,000 tulipewa na Serikali ya Ethiopia, kiwanja hiki cha pili ambacho kina mita 1,414 kilinunuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2007 kwa gharama ya dola za Kimarekeni 63,000 na kwa sasa kiwanja hicho kina thamani ya milioni 2.5.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Ethiopia ni kweli kwamba ilitunyang’anya hivi viwanja mwaka 2018 kwa sababu ya kutokuendelezwa. Hata hivyo, baada ya majadiliano marefu, ikiwa ni pamoja na juhudi za Kamati yetu ya NUU kufuatiia ziara yao iliyofanyika nchini huko mwaka 2022, viwanja hivyo vilirejeshwa chini ya umiliki wa Ubalozi mwezi Februari, 2023 kwa masharti ya kuuendelezwa ndani ya miezi tisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kupokea hati za viwanja hivyo, Ubalozi ulielekezwa kuomba kwa mamlaka za Addis Ababa ruhusa ya kuunganisha viwanja hivi viwili ili kiwe kiwanja kimoja. Wakati wa mchakato huo, Ubalozi ulitakiwa kurejesha kiwanja hiki ambacho tulinunua chenye ukubwa wa mita za mraba 1,400 ili mamlaka za Ethiopia zijiridhishe na uhalali wa umiliki wa kiwanja hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo Ubalozi uliwasilisha hizo nyaraka zote za kuthibitisha ununuzi halali wa viwanja hivyo. Hata hivyo, mamlaka hiyo bado inaendelea na mchakato wa ndani na kwamba hivi karibuni Ubalozi wetu utapewa umiliki wa kiwanja hicho kimoja kilichobakia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia kulifahamisha Bunge kwamba mkandarasi tayari ameshapatikana kwa ajili ya kujenga uzio ambao utazunguka viwanja hivi vyote. Kwa sasa Wizara inaendelea na hatua za ndani kwa ajili ya kuweka saini mkataba kwa mkandarasi aliyeshinda zabuni hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna suala la diaspora. Serikali bado ina nia ya dhati ya kutoa hadhi maalum kwa diaspora ambao ni raia wa nchi nyingine na wana asili ya Tanzania. Hawa ni Tanzania Non-citizen Diaspora kwa kuzingatia baadhi ya maombi yao ambayo wameyaeleza. Utekelezaji wa azma hii unahusisha marekebisho ya Sheria ya Uhamiaji Sura Na. 54 ili kuwezesha diaspora hao kuingia nchini bila kuhitaji visa na kuweza kukaa nchini hapa bila ya ukomo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna hitaji la kubadilisha Sheria ya Ardhi Sura Na.113 ili kuwezesha diaspora hao kumiliki ardhi kwa utaratibu maalum na vigezo ambavyo vitawekwa na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sera yetu pamoja na wadau wengine ndani ya Serikali tunaendelea kukamilisha masuala muhimu yakiwemo maandalizi ya Muswada wa Mabadiliko ya Sheria hizo na kuwasilishwa hapa Bungeni ili iweze kujadiliwa na kupata ridhaa ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na muda, tutazijibu hizi hoja nyingine kwa maandishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Nakushukuru sana. (Makofi)