Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Eng. Hamad Yussuf Masauni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kikwajuni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ya Kamati. Nachukua nafasi hii kwanza kuishukuru na kuipongeza Kamati yetu ya NUU chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Vita Kawawa. Kwa kweli imekuwa ikitupa ushirikiano mkubwa katika kutekeleza majukumu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namhakikishia Mheshimiwa Mwenyekiti, maelekezo yaliyotolewa kwenye taarifa ya Kamati tumeyapokea na tutayafanyia kazi, pamoja na yale ambayo yamechangiwa na Waheshimiwa Wabunge mbalimbali waliopata nafasi ya kuweza kuzungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako ambayo tutaweza kuyatolea ufafanuzi hapa sasa hivi na yako ambayo tutayachukua, tutayafanyia kazi na kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wake. Jambo linalonipa faraja kupitia taarifa ya Kamati yetu ni kuona jinsi ambavyo Kamati kwa kiasi kikubwa inaridhika sana na mafanikio ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara yetu ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Hili jambo linatia faraja kubwa sana kama ambavyo tulisikia ripoti ya Kamati ilivyoeleza, mambo mengi ya pongezi na mafanikio yaliyopatikana katika kipindi hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafanikio haya ambayo hata Waheshimiwa Wabunge waliochangia wengi wao wameyagusia, yanatokana na kazi kubwa ya Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ushahidi wa hilo ni maamuzi yake thabiti ya kuunda Tume ya Haki Jinai. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume ya Haki Jinai imetoa maelekezo ya mambo mengi. Kuna mambo yalikuwa yanahusu maboresho mbalimbali, yawe maboresho ya kitaasisi, maboresho ya kisheria, maboresho ya kisera, yako masuala ya kiutendanji, ya kioperesheni zaidi yanayohitaji uimarishaji wa vitendea kazi, bajeti na mifumo na TEHAMA, yako masuala yanayohusu welfare za Askari, haki zao stahiki, mafunzo na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote ambayo yametolewa kama taarifa ya utekelezaji, ni mapendekezo ya Tume hii ambayo utekelezaji wake umeshaanza. Kwa kiasi kikubwa yamesaidia sana Wizara yetu kuweza kufikia mafanikio haya ambayo tunajivunia. Nitoe mfano mmoja, maana mafanikio hayawezi kukosa changamoto. Wako Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumzia changamoto ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na vifaa. Leo nimesimama hapa nikiwa na faraja kubwa sana kwamba nazungumza hapa nikiwa najiamini kwamba sasa hivi changamoto hii ambayo inawagusa Waheshimiwa Wabunge karibu katika majimbo yao mengi nchi nzima, inaenda kufika mwisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunavyozungumza tayari tumeshapokea magari mapya 12, yameingia juzi. Magari mengine 150, boti 23 na helikopta moja ziko njiani. Kuanzia mwisho wa mwaka huu tutaanza kupokea mpaka mwakani vifaa vyote hivi tunatarajia vitakuwa vimekamilika, kufikia mwaka 2025. Kwa hiyo, kilio cha Waheshimiwa Wabunge kuhusiana na changamoto ya vitendea kazi ya ukweli kabisa katika Jeshi la Zimamoto na Uokoaji sasa inakwenda kuwa historia, chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutamwalika Mwenyekiti wa Kamati ya NUU kesho kutwa, tumemwomba Mheshimiwa Rais ratiba yake itakapokuwa inamruhusu, si tu aje kupokea magari ya Zimamoto na Uokoaji, lakini magari kwa ajili ya Jeshi la Polisi kwa Wilaya zote nchini na yenyewe tutayapokea kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ni la kujivunia ni suala la msongamano wa mahabusu Magerezani. Kamati na Waheshimiwa Wabunge wengi walipongeza juu ya mafanikio hayo. Takwimu za leo zinaonesha tuna wafungwa 18,037 wakati mahabusu ni 9,061. Hili jambo siyo la kawaida. Halijawahi kutokea katika miaka ya hivi karibuni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka yote tunavyosoma takwimu za wafungwa na mahabusu, tunakuta ongezeko la mahabusu zaidi ya 2,000. Leo imekuwa kinyume chake. Maana yake ni kazi kubwa imefanyika katika dhana ile ile ya utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai ya kupunguza idadi ya mahabusu isiyokuwa na sababu katika Magereza yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua imegusa maeneo mengi. Kuna kazi imefanyika katika taasisi mbalimbali. Kwa mfano, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashataka imefanya kazi kubwa, Mahakama imefanya kazi kubwa, Mama Samia Legal Aid Campaign nayo imefanya kazi kubwa, lakini kwa upande wa Jeshi la Polisi, halikadhalika tumefanya kazi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tumetoa maelekezo na tunafuatilia utekelezaji wake kwamba hakuna kumkamata mtu na kumweka mahabusu kwa kisingizio kwamba upelelezi haujakamilika kwa makosa ya kawaida, labda kwa makosa yale ambayo yapo kwa mujibu wa sheria. Hii imesaidia sana kupunguza msongamano wa mahabusu katika Magereza. Tumefanya hivyo kwa kuweza kuandaa utaratibu mzuri wa elimu kwa Askari wetu na wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile jambo hili litaweza kuwa endelevu kwa sababu tumeweka utaratibu mzuri wa kufuatilia. Binafsi nimekuwa mara kadhaa nikipita katika vituo vya Polisi na Magerezani kushuhudia jinsi utekelezaji wa jambo hili unavyoendelea. Kama hiyo haitoshi, hata eneo la kuimarisha mifumo, sasa hivi tuna mifumo ambayo inasaidia. Kwa mfano, katika vituo takriban 20 mpaka 30 vya Polisi, sasa hivi tuna mwelekeo wa kufunga mifumo ya kisasa ambayo inasomana na taasisi nyingine za Haki Jinai, hivyo kuepusha shutuma mbalimbali zilizokuwa zinaangukia baadhi ya Askari za kubambikia watu kesi au kuonea wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo ni mengi na muda ni mdogo, lakini jambo lingine ambalo nilikuwa nataka nieleze kabla sijazungumzia hoja muhimu sana ya Mheshimiwa Gwajima na muda kabla haujaisha, hili litahitaji muda kidogo nilifafanue vizuri, lakini nimalizie kusema kitu kimoja cha muhimu sana katika hii hoja ambayo nataka niikamilishe hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala siyo tu la upelelezi ukamilike, lakini upelelezi ufanyike inavyotakiwa. Upelelezi uwe umeshiba. Katika hilo, nitaunganisha na hoja za Waheshimiwa Wabunge kwamba kazi kubwa ya kuimarisha mifumo yetu ya TEHAMA katika kubaini na kuzuia uhalifu, katika bajeti ya mwaka jana 2023 nilisoma hapa, tuliahidi kwamba katika mwaka huu wa fedha kuna miradi mikubwa kadhaa ambayo tutaisimamia iweze kutekelezwa katika mwaka huu wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya mradi huo ni mradi ambao utasaidia sana katika eneo la kufanya upelelezi wetu uwe wa uhakika zaidi kwa kutumia mifumo ya kisasa, wanaita Automated Biometric and Identification System. Hivi tunavyozungumza, jambo hili lipo katika hatua ya mbali kabisa kukamilika. Tunafanya mazungumzo na Mheshimiwa Waziri wa Fedha kukamilisha kupata fedha za kuanza utekelezaji wa mradi huu wakati wowote kuanzia sasa. Hatua nyingine zote za maandalizi zimeshakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi mwingine umezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge vile vile unagusa tatizo la usalama barabarani. Wako Waheshimiwa Wabunge hususan walioko katika majiji makubwa wanalalamika kuhusiana na changamoto ya waendesha pikipiki au bodaboda kwamba labda zimeshindwa kudhibitiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, majiji yote makubwa duniani yaliweza kudhibiti siyo tu ajali hata changamoto ya bodaboda. Wameweka mifumo hii ya miji salama na mifumo ya kufunga mitambo ya kamera katika majiji makubwa. Hivi tunavyozungumza, mchakato wa ufungaji wa mifumo hii katika majiji manne kwa kuanzia, Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza na Arusha upo katika hatua za mwisho. Hali kadhalika, kupitia utaratibu wa PPP wa kuunganisha mifumo kutoka mji mmoja mwenda mji mwingine na wenyewe upo katika hatua za mwisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumalizia hoja muhimu ya Mheshimiwa Gwajima, najua dakika zimebaki chache. Hii ni hoja ya muhimu sana na nisingemtendea haki yeye wala Wabunge wala wananchi kama nisingelitolea ufafanuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na hoja ambayo inazungumzwa sasa ya utekaji, kwamba wananchi wanatekwa, hawaonekani wako wapi; na ukiangalia kauli hizi zinazotolewa inaweza kukupa taswira kama labda kuna crisis kubwa sana ikazua taharuki kubwa katika jamii. Nimefarijika Mheshimiwa Gwajima amezungumza hiyo, pengine nitakapotoa ufafanuzi sasa inaweza ikasaidia kuliweka hili jambo kwa ukweli zaidi na uelewa mpana zaidi kwa jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka kueleza kitu kimoja cha msingi, madhumuni ya kuwa na vyombo vya usalama; vya dola likiwemo Jeshi la Polisi ni kuzuia uhalifu. Kama hakuna uhalifu, hatuna haja ya kuwa na hivi vyombo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tuna bahati ya kuwa na vyombo imara sana vya usalama katika dunia na vinaheshimika na kusikika. Ndiyo maana mawimbi yoyote ya uhalifu yanayotokea katika nchi hii, na ninyi ni mashahidi, kuna kipindi lilitokea wimbi la uhalifu wa ndugu zetu wenye ualbino, ikaleta taharuki kubwa katika nchi hii. Jeshi letu la Polisi hili hili lilidhibiti, hali ikatulia. Kuna kipindi yakatokea mambo ya Mkuranga kule na Rufiji, Jeshi letu la Polisi hili hili lilidhibiti na hali leo imetulia na vyombo vyetu vya usalama hivi hivi. Juzi juzi hapa mmesikia mambo ya panya road, Jeshi la Polisi hili hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mifano iko mingi. Kwa hiyo, ninachotaka kusema, jambo la kwanza tuwe na imani na vyombo vyetu vya usalama hasa jeshi letu la Polisi. Ni makosa na dhambi kubwa sana kutengeneza taswira ya kuiondoa imani chombo cha usalama kama Jeshi la Polisi ambalo linafanya kazi kubwa ndani ya jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, watu wote ambao wanazungumzia haki za wananchi ambazo ni za msingi, lazima tuwe makini ya namna ya ku-portray image ya Jeshi letu la Polisi mbele ya jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyozungumza Mheshimiwa Gwajima, sasa tuna wimbi la utekeji. Sasa sijui wimbi hili ni kubwa kiasi gani nikilinganisha na mawimbi ambayo tumevuka salama, hili nasema ni wimbi dogo. Kwanini nasema hivyo? Kwa takwimu ambazo ninazo mimi hapa, kuanzia Januari mpaka Desemba mwaka 2023, kati ya matukio ambayo hayo yanayozungumzwa na kusema kwamba watu wamepotea, haijulikani wameenda wapi au haijulikani kimefanyika nini, asilimia 72.5 ya matukio yote, hao waliopotea wameshapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, siyo kwamba labda watu wamepotea halafu hakuna kinachofanyika, Polisi hawawapati hao wahalifu, hawawapati wahanga, siyo sahihi. Kuna kazi kubwa imefanyika na matunda yake ndiyo hayo ambayo nimeyazungumza kwamba katika matukio 20, matukio 21 Polisi imebaini waliohusika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vyanzo vilivyobainika ni nini? Vyanzo vilivyobainika ni wivu wa mapenzi, ushirikina, kugombania ardhi, urithi, mpaka kujiteka ipo, visasi na utapeli. Asilimia kubwa ya vyanzo ni mambo haya. Kwa hiyo, kwanza ni lazima Watanzania tujiangalie, na ndiyo maana tumefanya kazi kubwa sana ya kuimarisha utaratibu wa Polisi Jamii na ulinzi shirikishi ili kuteremsha elimu kwa jamii kuanzia ngazi ya Kata. Malengo ya Serikali kuimarisha mifumo ya Polisi kwenye ngazi ya Kata ni kwa lengo la kujenga elimu ya wananchi, kwa sababu haya mambo yote yanahitaji elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana kuna baadhi ya wananchi wakawa hawajaridhika, wala siyo kosa. Ndiyo maana hata mimi nilieleza wakati nilivyoitisha kikao cha Wakuu wa Jeshi la Polisi na Makamanda wote wa mikoa kwa ajili ya kutathimini hali ya usalama hususan katika eneo hili. Niliwaeleza waandishi wa habari kwamba kama kuna mtu yeyote ambaye anadhani hajaridhika na uchunguzi wowote, awasilishe malalamiko yake Wizarani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepokea malalamiko manne na nimeyaundia Tume inayojitegemea kabisa kutoka katika taasisi mbalimbali za Umma kwa ajili ya kufanya uchunguzi. Kwa hiyo, milango iko wazi, lakini kama mtu anadhani kwamba kila jambo litafanyika kwa haraka haraka anavyotaka, masuala ya uchunguzi wakati mwingine yanahitaji muda. Ndiyo maana anavyozungumza kwamba kuna hoja baadhi ya wananchi wanalamika katika mikutano ya siasa, mtu yeyote hata ingekuwa ni wewe, kama unadhani kwamba kuna tatizo ambalo halijapatiwa ufumbuzi, utasema. Ukisema haina maana kwamba kazi haifanyiki. Kazi inafanyika na tunaendelea kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumalizia kwa kumwomba Mheshimiwa Gwajima na Waheshimiwa Wabunge wengine na wananchi wote kwa ujumla popote walipo, tushughulike na matukio haya ya kihalifu, tukio kwa tukio, tusijumuishe tukazua taharuki katika jamii isiyokuwa na sababu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu ya matukio haya yote yapo na mimi nataka kuwahakikishia, kwa usimamzi na dhamira ya thabiti ya Amiri Jeshi Mkuu, ambaye anataka kuhakikisha kwamba nchi hii inaongozwa kwa misingi ya haki bila kumuonea mtu. Ndiyo maana akaunda Timu ya Haki Jinai, kwamba kila mmoja avune alichokipanda. Hakuna mtu yeyote ambaye atafanya tendo la kihalifu, iwe raia wa kawaida, hata iwe Askari Polisi kama atahusika. Wapo baadhi ya Askari Polisi, wachache, ambao Jeshi la Polisi limekuwa likiwachukulia hatua, hata Serikali, kwa matukio mbalimbali, wala si jambo geni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hapa nimezungumzia hoja ile ya kwenye vituo vile vya Polisi kuharakisha upepelezi. Ni zaidi ya Askari 865 ambao wameshindwa kutekeleza maelekezo ya kuwazuia watu kwenye vituo vya mahabusu kwa muda mrefu; tumewachukulia hatua, zaidi ya miaka sitini na kitu. Ni jambo la kawaida kabisa, ni jambo la kawaida kabisa; hivyo hakuna hoja ya kusema kwamba kuna tukio la kihalifu litafanywa na mtu yeyote, litafungiwa macho. Lazima mfahamu kazi ya Jeshi letu la Polisi inayofanywa ni kubwa sana. Tuwape moyo na tuwaunge mkono; na pale ambapo yanatokea mapungufu tushirikiane kuyatatua. Nakushukuru sana. (Makofi)