Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Jackson Gedion Kiswaga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalenga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. JACKSON G. KISWAGA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MAJI NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii sasa kuja kihitimisha hoja yangu ya Kamati ya Maji, ambayo leo asubuhi tulikuwa tumeisoma mbele ya Bunge lako Tukufu. Niwashukuru sana Wabunge wenzangu, Wajumbe wa Kamati lakini na Wabunge wengine waliochangia. Kwa kweli tumepata jumla ya wachangiaji 16 katika watu waliochangia leo ambayo inaonesha kwamba hoja hii ya maji ni hoja nzito ambayo imeungwa mkono na kuchangiwa na Wajumbe wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kuiomba Serikali kwamba michango na ushauri mbalimbalii ambao umetolewa na Wajumbe na Wabunge unapelekea kuisaidia Serikali ili kuweka mipango yake ya baadaye vizuri hasa sasa tunavyoelekea kwenye bajeti ili kuweza kuleta maendeleo katika Taifa hili na kuboresha maisha ya Watanzania na ustawi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kuchangia katika eneo ambalo limechangiwa pia na watu wengi naona hata Mawaziri wangu wakati wanahitimisha wamezungumza suala la uhuishaji wa sheria zinazoendana na mabadiliko ya sasa. Sheria ya Mazingira ya Sura Na. 191 pia ile Sheria ya Maji ya mwaka 2002, sheria hizi ni muhimu tukizingatia kwamba mabadiliko ya tabianchi ya sasa yanahitaji hayo mabadiliko ili kuendana na mazingira halisi ya sasa. Tunaiomba Serikali ilichukulie jambo hili kwa umuhimu na liende kwa kasi zaidi ili matarajio ya Wabunge na Bunge hili basi yaweze kutimia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamezungumzia uharibifu wa mazingira lakini nikizingatia namna hata Askofu Gwajima alivyozungumza kwa msisitizo, ni kweli kwa mfano Dar es Salaam kila mwaka mvua nyingi zinavyonyesha zimekuwa zikiharibu sana miundombinu hasa mito na hii kuifanya Serikali wakati mwingine ipate hasara kubwa kwa sababu inakuwa inatumia fedha nyingi kukodi mitambo kuweza kutoa mchanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiongozi mmoja wa kuaminika sana wakati fulani alinipigia simu akaniambia Kiswaga unajua kwenye mitambo hii ambayo tunakodi kuondoa mchanga kwa siku tulipa fedha nyingi sana akanitajia kiasi fulani na mimi nikashtuka sana. Kwa hiyo, ninapende kuishauri Serikali katika eneo hili la mito ya Dar es Salaam sisi viongozi mbalimbali tumetembea nchi nyingi na tumeona nini wenzetu wanafanya. Ukiangalia sehemu nyingi za mito duniani wamejengea, sasa na sisi Tanzania ningependa kutoa ushauri kwamba hii mito ya Dar es Salaam na sehemu nyingine ambayo kila mwaka inaharibika basi Serikali iendelee kutenga fedha kidogo kidogo. Tunaweza kuanza kujenga mto mmoja baadae mwingine, badala ya kuendelea kila mwaka kukodi mitambo kutoa michanga na tunatumia fedha nyingi za walipa kodi, kwa hiyo Serikali ijipange kwa ajili ya hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia uharibifu wa mazingira ambao umeendelea sana katika nchi hii nasi kama Kamati tumeshauri na tupende kuielekeza Serikali kwamba izingatie upangaji wa miji. Miji yetu mingi ambayo tunaijenga imeendelea kujengwa kiholela, hivyo unakuta kwamba miundombinu mingine kwa mfano, tumezungumzia miundombinu ya maji taka unakuta kwamba haina, sasa ujengaji holela tukiendelea nao utaigharimu Serikali mambo mengi zaidi. Kwa hiyo tuombe kwamba miundombinu hii inavyojengwa tuzingatie sana athari za mazingira kwa maana kwamba tuhakikishe kwamba mifumo ya majitaka inawekwa kila Mji unaojengwa hii itasaidia sana Serikali kuweza kujipanga kuwa na miji misafi lakini kuboresha mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo tuhakikishe kwamba madampo yanajengwa katika miji yetu mingi. Unakuta kwamba Jiji Kubwa kama la Dar es Salaam lina madampo pengine mawili au matatu kwa ukubwa ule hiyo siyo sawa. Kwa hiyo, Serikali ijipange kuhakikisha kwamba tunaongeza madampo pia tunakuwa na usimamizi mzuri wa mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, limezungumzwa pia suala la taka ngumu. Suala la taka ngumu wote mtashuhudia hata mkizunguka huko nje wakati mwingine ukitembea kwenye mitaro utaona chupa za aina fulani zipo kwenye mitaro. Sasa sheria zipo lakini bado mazingira yanaendelea kuchafuliwa. Tuiombe sana Serikali kwenye suala la usimamizi wa sheria isiwe na kigugumizi. Sheria za Tanzania ni nzuri sana tatizo liko kwenye usimamizi, kwa hiyo unakuta kwamba hawezi kuwa mfanyabiashara fulani tu yeye anatupatupa tu takataka na Serikali ipo, Serikali ni kubwa kuliko jambo lolote. Kwa hiyo, tunaitaka Serikali suala hilo liisimamie kwa ukamilifu kama hawawezi kufanya recycling basi viwanda wavifunge. Kiwanda kimoja au viwili kuvifunga ili kuzuia uchafu haiwezi sisi kutupunguzia chochote, Serikali ilichukulie jambo hili kwa u-serious mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo lingine la mazingira tumezungumzia maeneo lindwa. Mheshimiwa Profesa Manya wakati anachangia hoja yake alizungumzia maeneo muhimu yenye upekee sana wa kijiolojia katika nchi ya Tanzania. Akazungumzia Oldonyo Lengai akazungumzia na maeneo mengine. Tanzania inaweza kunufaika sana na maeneo haya ya kipekee mengi ambayo tunayo katika nchi hii, kuna vimondo na kadhalika. Haya maeneo kama yanaweza kulindwa yakawekewa sheria, yakatengenezewa historia nzuri, Serikali ya Tanzania inaweza kuendelea kupata fedha nyingi inayotokana na haya maeneo ya kipekee. Kwa hiyo, niombe Serikali kwa kushirikiana na Wajiolojia mahiri mbalimbali tulionao katika nchi hii waliopo katika Vyuo Vikuu, waweze kuyatambua haya maeneo kwa haraka lakini na hizi kanuni za haya maeneo lindwa zikishakamilika itakuwa ni vizuri zaidi, kwa hiyo Tanzania inaweza kunufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo nchi unakuta tu watu wengi walikufa wameshatengeneza memorial hapo watu wanapeleka dola lakini sisi Tanzania tuna maeneo mazuri ambayo Mungu ametupatia tunaweza kutengeneza pesa kwenye utalii kwa kuyalinda maeneo yetu na kuyawekea historia nzuri. Kwa hiyo, Serikali ione namna gani inafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na mabadiliko ya tabianchi kama wenzangu walivyozungumza ziko fedha zinazotolewa na mifuko ya dunia, GCF na mingine mingi ambayo ipo ambayo inatoa fedha za kigeni. Kweli Tanzania imekuwa hainufaiki sana na hizo fedha. Changamoto ambayo ninaiona hata mimi nilihudhuria COP 28 pale Dubai mtu mmoja akasema kwamba alikuja pale kwenye banda letu akasema kwa nini msitumie washauri wa kimataifa? Ni afadhali tutumie hao washauri wa kimataifa kama fedha tutapata ili kama mshauri na yeye anapata kidogo na sisi tupate kuna hasara gani? Kwa hiyo suala la kutumia washauri wa ndani na washauri wa kimataifa katika kutengeneza maandiko yetu ili fedha hizi za dunia ziweze kuja hili suala lizingatiwe ili nchi nayo iweze kunufaika na hizo fedha ambazo tunaweza kuzipata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na kuongezewa fedha hasa kwenye Wizara hii ya Mazingira. Ni kweli tunashukuru fedha nyingi zinatoka nje lakini kwa sababu suala la mabadiliko ya tabianchi sasa hivi ni kubwa na limekuwa ni mtambuka, Serikali ijipange vizuri kuona namna gani yenyewe katika vyanzo vyake inaiongezea Wizara fedha za ndani ili sisi wenyewe tuendelee kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi wakati tunasubiri hawa wajomba watuletee fedha. Serikali inaweza kufanya, Serikali ijipange hii ni nchi kubwa na inaweza kupata fedha kutoka vyanzo mbalimbali, kwa hiyo hili Serikali ilizingatie na ione namna gani inatekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda kwenye maji imezungumzwa habari ya wakandarasi kutokulipwa kwa wakati. Ukiona watu wanalalamika maana yake tatizo lipo, kwa sababu wasingelalamika kama tatizo halipo. Tunamshukuru Waziri ametueleza hapa alivyokuwa anahitimisha pia akichangia hoja amesema wameshapokea fedha. Sisi kama kamati na Wabunge haturidhiki sana na mtiririko wa fedha ambao unatolewa kwa wakandarasi wetu kwa sababu unakuta kwamba certificate zipo nyingi ni zaidi ya bilioni 100 kwa taarifa ambazo tunazisikia lakini fedha zinazotoka; okay niseme Serikali inajitahidi lakini tunataka ifanye zaidi, zile certificate ambazo zimekaa kuanzia miezi labda mitatu na kuendelea zilipwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la maji kwa kweli halina mjadala. Unaweza ukakaa bila umeme siku tatu lakini huwezi kukaa bila maji kwa siku tatu, nne mpaka tano. Zamani kule vijijini tulikuwa tunakunywa maji na ng’ombe lakini ukiangalia uchafuzi wa mazingira ambao unaendelea sasa haiwezekani watu kunywa yale maji ambayo wanakunywa na ng’ombe wakawa salama. Kwa hiyo, Serikali ijitahidi kuhakikisha kwamba hizi fedha zinapatikana lakini sambamba na hilo kwamba tuna vijiji zaidi ya 2,300 ambavyo inaonekana bado haviko katika mpango wa kupelekewa maji. Kutokana na umuhimu wa maji tunaiomba Serikali itafute fedha kokote inapoweza kutafuta tunapokwenda 2025 kuelekea kwenye uchaguzi angalau tupunguze vijiji vingi zaidi, kama tukiweza kumaliza ni jambo zuri, Serikali inaweza kuwa na namna ya kupata fedha, itakuwa ni jambo zuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusiana na Serikali kudaiwa, Serikali itafute fedha kokote ilipe mamlaka za maji hizi fedha wanazodaiwa ili Serikali iweze kutekeleza majukumu yake. Hili jambo muhimu ili hizi mamlaka ziendelee kuwa na nguvu. Kwa mfano, RUWASA ni taasisi bado changa ina miaka miwili, mitano inahitaji kuendelea kukua na kuwa na nguvu, kwa hiyo sasa kama tukikaa na pesa zake maana yake hatuitendei haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine hapo hapo ni kuendelea kuimarisha uwezo wa wataalam wetu, building institution capacity kwamba tuendelee kujenga uwezo wa taasisi, kujenga uwezo wa wataalam hii itasaidia hizi mamlaka kutekeleza wajibu wake vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, limezungumzwa suala la mita za malipo kabla. Hili ni jambo muhimu sana, unakuta kwamba ukusanyaji wa madeni kwa wateja wengi ni changamoto. Kwa hiyo, ninachokiomba ni kwamba, kwa mfano tuchukulie DAWASA; nilikuwa nawauliza DAWASA, ninyi kwa nini hamjaanza kufunga mita za malipo kabla? Wakasema bwana uwezo wetu pia wa kifedha siyo mkubwa sana. Hawajaongezewa bili za maji kwa karibu miaka nane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo Taasisi za Serikali, kwa mfano NSSF na PSSSF, hawa wamekuwa wakiwekeza kwenye miradi mbalimbali ya majengo na wakati mwingine hawapati return kwa wakati. Serikali ione namna gani hizi Wizara zinaweza kushirikiana. Hawa NSSF na PSSSF wana fedha nyingi, wanaweza kuipa DAWASA kwa mfano fedha nyingi kwa mara moja shilingi milioni 100 kwa mfano wanayohitaji. Wana wateja karibu laki nne na nusu pale, kama wakifunga zile mita kwa mara moja, wataweza kurudisha fedha haraka NSSF na PSSSF watapata fedha zao, lakini pia na hawa Wizara ya Maji watakuwa wametatua hii changamoto ya ukusanyaji wa madeni. Kwa hiyo, hilo Serikali ilifikilie ione itafanyaje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, gridi ya Taifa ni muhimu sana. Kwa ufupi naiomba Serikali izingatie michango yote ambayo imetolewa na Wabunge pamoja na maoni na mapendekezo ambayo yameletwa na Kamati. Inapokwenda kuandaa hizi bajeti, iende kuyazingatia haya ili isaidie kuboresha maisha ya Watanzania ili sekta zetu ziwe endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja. (Makofi)

MHE. HAJI MAKAME MLENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.