Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Vita Rashid Kawawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Namtumbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. VITA R. KAWAWA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MAMBO YA NJE, ULINZI NA USALAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ili niweze kuhitimisha hoja ya Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama. Kwanza nawashukuru wote waliochangia hoja hii. Kulikuwa na wachangiaji 11 waliochangia hoja hii na nitaomba kidogo nitoe ufafanuzi mdogo kwa waliochangia, halafu nimalizie kwa kutoa mapendekezo ya Kamati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza kabisa lilisemwa kuhusu usafirishaji haramu wa binadamu. Hoja hii ilichangiwa na Mheshimiwa Fakharia ambaye alizungumzia usafirishaji wa vijana wetu nje na kufanyishwa kazi zisizo na maadili ya utamaduni wa nchi yetu. Pia aliongezewa kwenye taarifa na Mheshimiwa Njau kuwa, hakuna ukaguzi wa kina kwa vijana wetu wanaokwenda nje kujua wanaenda kufanya nini; na inawezekana kuwa kuna mahusiano baina ya watumishi wasio waaminifu wanashirikiana na wasafirishaji haramu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa naomba niliseme hili kwamba sasa hivi dimbwi hili ni kubwa sana. Biashara hii imezungumzwa hapa pia na Mheshimiwa Tendega kwamba ni biashara haramu ambayo ni ya tatu duniani kwa upatikanaji wa fedha. Biashara haramu ya kwanza ni ya silaha haramu, ya pili ni ya madawa ya kulevya na sasa hivi ya tatu ni hii ya usafirishaji haramu wa binadamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie fursa hii kuwaambia wananchi wote na Bunge lako Tukufu kwamba sasa hivi kuna biashara hii, yaani naweza nikarudi nikasema, “a modern slave trade.” Hii ni biashara ya usafirishaji wa binadamu wa kisasa. Wakati wa ukoloni tulikuwa tunasafirishwa, kwamba tunakamatwa kwa pamoja, tunafungwa minyororo, tunapelekwa kuuzwa bila ridhaa yetu, lakini sasa hivi biashara hii haramu mtu unauzwa kwa ridhaa yako mwenyewe, lakini bila kufahamu kama unafanyiwa biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara hii kubwa kuna Mawakala ndani ya nchi yetu hapa na kuna Mawakala nje ya nchi yetu. Nitawapa mfano mmoja ambapo walioathirika na biashara hii walikuja ku-confess katika Kamati yetu kwamba, msichana mmoja alikuwa anafanya biashara yake hapa ya kuuza nguo katika duka dogo, lakini alishawishiwa na mtu kwamba wewe kuna biashara ukija kwenye nchi hii, kuna kazi ambazo utakuwa unalipwa Dola 700 kwa wiki. Hiyo ni biashara gani unaifanya?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, akapiga hesabu akaona ni sahihi, akaambiwa basi utaletewa mtu, atakuja kushughulikia masuala ya Visa na kuhakikisha kwamba unasafiri. Yule akapata tamaa, akakubali kufanya kazi hiyo. Akamfuata huyo mtu na wakamtengenezea utaratibu wote na Visa. Siku wanakwenda airport wakajikuta wapo wasichana tisa na wakaenda wakapitishwa immigration pale bila kuulizwa unakwenda kufanya nini? Wakasafiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, walipofika huko, yeye alipofika kuona mazingira yale ni tofauti na walichoendea, kufika kwanza walinyang’anywa passport zote, halafu wakawekwa kwenye chumba ambacho wanaletewa watu kuwatizama kwamba huyu anafaa au huyu hafai. Sasa hili ni jambo ambalo ni baya sana, lipo duniani sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka Watanzania wote wafahamu kwamba kuna biashara hii ambayo wewe mwenyewe unauzwa kwa kuridhika mwenyewe. Kwa hiyo, ilikuwa ni kazi sana, walipata shida sana wadada hao mpaka huyo mmojawapo ambaye aliyekuwa anafanya biashara hiyo ambayo haikuitegemea, ilibidi lazima aridhike aifanye ili apate mawasiliano. Aliweza kuridhika na akapata mawasiliano na kuwasiliana na nchini hapa na kufanya Serikali yetu kumsadia mpaka kurudi huku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, modern slave trade imeshamiri ndani ya nchi yetu. Pia kuna watu ambao wanashirikiana na hawa wahalifu, wasafirishaji binadamu. Kamati inaiomba Serikali ifuatilie kwa kina wale watumishi ambao siyo waaminifu kuwashughulikia. Serikali yetu ina macho makali, ina pua ndefu na ina masikio marefu, tunaiomba Serikali yetu isimamie suala hili na ilifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Tendega yeye alizungumzia kuhusiana na kuchelewa kwa kupelekwa na fedha za maendeleo katika Wizara ambazo tunazisimamia na mafungu ya Wizara ambayo tunayasimamia. Ameiomba Wizara ya Fedha ipeleke fedha pia kwa Jeshi la Zimamoto ambalo ni fungu halijapata fedha za maendeleo mpaka Desemba. Kwa hiyo, tunaomba, nami nasisiza kwamba Serikali iweze kupeleka fedha katika Jeshi letu hili la Zimamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Neema alizungumza katika mchango wake kuhusiana na teknolojia ya sasa na lazima Serikali iangalie kuwekeza kwenye electronic warfare. Namshukuru sana pia Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi amejibu vizuri hapa, ametolea ufafanuzi kwamba nchi yetu inakwenda na teknolojia ya sasa na tunaiomba iendelee hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaomba lazima tuangalie teknolojia hii ya sasa. Leo hii tuna matumizi mazuri ya teknolojia ya sasa. Leo tuna drones ambayo zinasaidia kwenye Habari, lakini tunasikia kwamba zitasaidia kwenye maeneo ya kusambaza vifaa tiba au dawa vijijini kwetu na kwenye Kilimo. Sasa lazima tuangalie pia drones hizi kiusalama pia. Hizi drones tunaziona tu, zinaruka kwenye mikutano zinachukua Habari. Tunashukuru sana, zinatuhabarisha, lakini lazima Serikali iangalie sana teknolojia hii kwenye Mambo ya Ulinzi na Usalama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii teknolojia hii pia inatumika katika vita mbalimbali. Kwa hiyo, nasi pia tutambue teknolojia hii inatumika kwenye udukuzi mbalimbali, na vile vile inatumika kushambulia. Kwa hiyo, lazima tuangalie pia kwa msisitizo kabisa teknolojia hii inapotumika kwenye jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mkundi alizungumzia mpango wa ujenzi wa Balozi zetu. Nashukuru sana Mheshimiwa Waziri ameeleza hapa vizuri, lakini Kamati inasisitiza kwamba ujenzi uanze kule. Kama tulivyosisitiza katika mapendekezo ya Kamati kwamba lazima tutunze heshima yetu ya diplomasia ya nchi yetu, tusiachie viwanja vyetu vikanyang’anywa. Imetolewa miezi tisa pale Addis Ababa mpaka Desemba tulikuwa hatujafanya kazi yeyote. Tumepewa miezi mitatu Abuja na imekwisha, bado hatujafanya kazi yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali tusije kunyang’anywa tena viwanja Addis Ababa, tusije kunyang’anywa kiwanja tena Abuja. Tunaomba Serikali ipeleke fedha ya ujenzi. Tumesikia na kwenye Kamati tuliambiwa kwamba Mkandarasi amepatikana Addis Ababa. Tunaomba akaanze kazi, tusicheleweshe tusije tukanyang’anywa viwanja hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Ngassa alizungumzia utalii wa mikutano na alishauri kuwe na convention center yenye facilities zote katika eneo moja la mahoteli na facilities nyingine kuwa karibu na convention center. Suala hili ndiyo ambalo AICC pia wanataka kulifanya pale Arusha kwenye convention center, wanataka kuijenga kubwa, lakini kuna shida kwenye kiwanja hicho. Mojawapo ni kwamba, kimekuwa encroached na watu na upande mwingine, kimemegwa. Sasa hili ni wazo zuri sana ambalo AICC inataka kulitekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kikwazo kingine cha kutolipwa fedha zao na taasisi zinazofanya mikutano katika ukumbi wao. Kwa hiyo, nacho ni kikwazo kikubwa ambacho kitawachelewesha hili. Ila wazo hili ni zuri sana, naamini kabisa Serikali italifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru sana Mheshimiwa Zahor kwa mchango wake wa jumla. Mheshimiwa Waziri amelielezea nalo pia na ameshauri kwa msisitizo sana kwamba fedha zipatikane za kutosha katika Zimamoto na kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Ussi Pondeza ameshauri Ofisi zetu za Ubalozi zijengwe, nadhani tumeshalisema hili na tunalisisitiza na tumesisitiza katika mapendekezo yetu. Tunaomba mtuunge mkono katika maoni na mapendekezo tutakayowasilisha hapa punde.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Balozi Mbarouk ameelezea kuhusu uendelezaji wa viwanja vya Ubalozi. Narudia tena kusema, tunaomba Mkandarasi akanze kazi ili nchi yetu isivunjiwe heshima ya kidiplomasia. Kazi kubwa iliyofanya Kamati yetu kwenda kumwomba Mheshimiwa Rais wa Ethiopia na akatuheshimu na akaturudishia viwanja, kwa hiyo, tunaiomba sana Serikali, huyo Mkandarasi aanze mapema iwezekanavyo. Muda ule umekwisha toka mwezi wa Kumi na Moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi ya AICC ilimwomba CAG kufanya special auditing, tunashukuru sana. Tunachoweza kusisitiza ni kwamba tumeelekeza humu katika maoni yetu kwamba Bunge linaazimia, Wizara zote zinazozisimamiwa na Kamati hii ziwasilishe ufafanuzi kwa sababu ya kutotolewa baadhi ya maazimio sambamba na mpango wa kutatua changamoto zilizobainishwa katika maazimio, lakini pia ziwasilishe kila baada ya miezi mitatu Maazimio ya Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba sana hii Taarifa ya CAG ikishafika, utekelezaji wake uwasilishwe katika Kamati mwezi wa Tatu. Tunaomba sana taarifa hiyo ya utekelezaji iwasilishwe. Pia tunaomba kama tulivyosisitiza katika Taarifa ya Kamati kwamba wale wote watakaobainika kuwa wamehusika, wachukuliwe hatua stahiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Engineer Hamad Masauni tunamshukuru sana kwa mchango wake, tumemwelewa. Kuhusu eneo la upungufu wa msongamano umeuelezea vizuri, nasi tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwanza kwa kuiunda ile Tume ya Haki Jinai ambayo imesaidia sana kwa mapendekezo yake, kazi zimefanywa kwa haraka na leo haki inapatikana na wafungwa wengi na mahabusu waliweza kutoka Gerezani. Kwa hiyo, tunashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mifumo ya safer seat kwamba itatusaidia kudhibiti uendeshaji mbaya wa boda boda pamoja na ulinzi na usalama wa nchi yetu. Tunaiomba sana Serikali, kama tulivyosema katika maoni yetu, mhakikishe kwamba mwaka huu na wewe umesisiza kwamba mtakamilisha mradi huo. Ukamilishwe mradi huo ili tuweze kuwa na miji salama katika nchi yetu na tuweze kuishi kwa amani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Stergomena Tax ameahidi kwamba ataendelea kutekeleza ushauri, tunakushukuru sana. Pia, kuhusu ufinyu wa Bajeti ameuelezea vizuri, tunashukuru sana. Vyombo vya Ulinzi na Usalama vimeendelea kupata fedha za kutosha, amelinganisha kutoka mwaka 2021 mpaka 2023. Mwaka 2021 Wizara ilipata 2.4 trillion shillings na mwaka 2023 ni 2.7 trillion shillings. Tunaishukuru sana Serikali ya Mama Samia na wote ambao wanasimamia upatikanaji wa fedha hizi. Tunaomba tuendelee kuzipata fedha kwa wakati ili majeshi yetu yaweze kuendelea kufanya kazi yake vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kutopelekwa vijana wote JKT Mheshimiwa Waziri ameielezea vizuri, nasi tunasisitiza kwamba Serikali tunaiomba iongeze Bajeti ya JKT ili kujenga miundombinu katika Makambi ya JKT na kuongeza Makambi ya JKT kwa vijana ili tuweze kupata vijana wengi ambao watakaopata Mafunzo haya ya JKT. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kueleza maoni yangu na mapendekezo, sasa naomba kutoa hoja kwamba Bunge likubali Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama pamoja na maoni na mapendekezo yaliyomo katika taarifa hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.