Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Anne Kilango Malecela

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Same Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, mimi ni Mjumbe wa Kamati hii, kwa hiyo, nimeiangalia vizuri naomba kuchangia kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kutoa pole kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwamba, imejenga barabara nchi nzima lakini tumepata El Nino ambayo imevuruga barabara pamoja na mengi makubwa lakini lazima tujue kwamba, sisi tunapanga Mwenyezi Mungu ndiye anayepanga vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kuchangia upande wa TANROADS. Kama Mheshimiwa Mwenyekiti alivyosoma taarifa ya Kamati, utaona kwamba changamoto kubwa waliyonayo TANROADS ni fedha za ujenzi na matengenezo ya barabara na madaraja, ukiangalia bajeti ya 2023/2024 TANROADS amepewa pesa trilioni 1.4 tu kwa kujenga barabara, madaraja na matengenezo ya barabara ambazo zilikwishajengwa kwa nchi nzima, sasa naomba nitoe picha ya changamoto ya kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba, TANROADS ina mzigo mkubwa wa barabara zilizoisha muda wa matumizi. Mfano wa barabara hizo ni kama Barabara ya Dodoma – Iringa, Barabara ya Dodoma – Mwanza, Dar es Salaam - Mtwara na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, TANROADS ina tatizo kubwa la barabara ambazo zimekwisha muda wa matumizi. Nikisema zimekwisha muda wa matumizi ni kwamba, barabara hizi zinakuwa zimejengwa zitumike mfano kwa miaka 20 lakini miaka 20 imefika barabara hazifanyiwi matengenezo. Barabara hizo ziko 71. Barabara 71 ambazo gharama yake ni 3,026,007,076,000. Naomba kurudia, barabara ambazo zimekwisha muda wake ni barabara 71 ambazo zilibidi zitengenezwe kwenye bajeti ya 2023/2024 na barabara hizo zina gharama ya 3,026,007,076,000. Urefu wa barabara hizo 71 zina urefu wa kilometa 2840.68. Barabara hizi 71 hazina hali nzuri kabisa kimatumizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipengele kingine ambacho kinaikwaza sana TANROADS ni ucheleweshaji wa malipo ya wakandarasi na wahandisi. Miradi 94 imekamilka, wakandarasi wanadai shilingi bilioni 386.608. Pili, miradi ya barabara inayoendelea ipo 69 yenye urefu wa kilometa 4291.61 gharama ni bilioni 392.68. Kwa haya niliyoyazungumza na bajeti iliyotolewa ya trilioni 1.4 ni dhahiri kabisa kwamba TANROADS wanashindwa kufanyakazi inavyostahili. Kwa hivyo basi, Kamati na kama alivyoongea Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali kwa unyenyekevu mkubwa muone umuhimu wa kuifanya TANROADS ifanye kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba kama ingeweza kupewa trilioni tano ambazo trilioni tatu ziende kwenye ujenzi wa barabara na trilioni mbili ziende kwenye matengenezo ya barabara hasa tukiona ni jinsi gani ambavyo mvua za El-Nino zimeharibu barabara za nchi nzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulijitahidi tukamwita mpaka Mheshimiwa Waziri wa Fedha ndani ya kikao chetu, tukamweleza vya kutosha ili aone umuhimu wa kuiangalia TANROADS. Ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nakuja upande wa TPA. Upande wa TPA napo kuna matatizo. Tuchukue mfano wa TPA ni kama ng’ombe ambaye anatoa maziwa mengi sana, hata hivyo, ng’ombe anayetoa maziwa mengi anahitaji apewe chakula cha kutosha, anahitaji apewe virutubisho ili ng’ombe yule aweze kutoa maziwa ya kutosha. TPA inachangia asilimia 15 ya pato ghafi kila mwezi kwenye Pato la Taifa, TPA inachangia asilimia 70 ya faida yake kwa mwaka kwenye Pato la Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nirudi kwenye utendaji kazi wa TPA, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita 2020/2021, 2021/2022, 2022/2023; idadi ya meli zilizohudumiwa zimekuwa zikiongezeka kwa asilimia 15.8. Aidha, katika mwaka wa fedha 2022/2023 idadi ya meli zilizopokelewa ni sawa na asilimia 118.1 ya lengo la mwaka. Tuende kwenye mapato ya TPA. Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita 2020/2021, 2021/2022 na 2022/2023 mapato ya TPA yameongezeka kwa wastani wa asilimia 24.72 kwa mwaka kutoka shilingi bilioni 896.952 zilizopatikana kwa mwaka wa fedha 2020/2021 hadi trilioni 1.390 kwa mwaka wa fedha 2022/2023 hayo ni mapato.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vema sasa Serikali ikaona kwamba, TPA, kweli ni kama ng’ombe anayetoa maziwa, anapeleka asilimia 15 na asilimia 70 ya ziada yake kwa mwaka kwenye Mfuko wa Serikali, Ofisi ya Msajili wa Hazina. Sasa ni vema Serikali ikaona kwamba, huyu ng’ombe anayetoa maziwa akikamuliwa moja kwa moja bila kupewa majani ya kutosha na virutubisho, atakufa na hataisaidia hii Serikali. Sisi tunapendekeza hivi, Serikali ione umuhimu wa kumpa TPA bilioni 35 kila mwezi kwa ajili ya kujenga na kuboresha miundombinu ya Bandari za Tanzania, ahsante sana. (Makofi)