Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Miraji Jumanne Mtaturu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami nichangie kwenye taarifa ya Kamati yetu ya Miundombinu ambayo tunayo mezani ambayo kimsingi ni taarifa ya Serikali kwa kipindi cha mwaka mmoja. Nami na–declare kwamba ni Mjumbe wa Kamati nasi tulipata taarifa hizi na tulisomewa. Tuliihoji Serikali kwenye Kamati yetu kama ambavyo ulitupata ruhusa ili tuweze kupitia taarifa za kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza katika yote nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuleta fedha nyingi kwenye taasisi zetu ambazo leo zimetoa huduma mbalimbali katika maeneo ya wananchi. Taarifa ambayo imetajwa, pamoja na changamoto lakini kuna fedha zimekwenda za kutekeleza miradi mbalimbali, tunaipongeza Serikali na tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa utayari wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha taarifa nitaanza kwenye eneo la Mamlaka ya Bandari Tanzania. Kama ambavyo wote tunajua Mamlaka ya Bandari ya Tanzania kwa maana ya bandari ndiyo lango kuu la Uchumi, tumekuwa tukitegemea kukusanya fedha nyingi kupitia bandari yetu. Katika kipindi cha taarifa tumejulishwa kwamba tumeweza kuhudumia nyongeza ya tani kwa maana ya asilimia 17.5 kuacha ile ya nyuma ambayo ilikuwepo kwa mwaka uliopita. Tumeweza kuhudumia kutoka tani milioni 5.81 kwenda mpaka tani milioni 6.83. Maana yake ni kwamba pamoja na yote kuna hatua kubwa tumepiga katika kuhudumia shehena katika bandari yetu ya Dar es Salaam. Kama haitoshi, mapato yameongezeka kutoka shilingi bilioni 310.78 hadi bilioni 365.12 katika hiki kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/2024.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na juhudi zote hizi na kwa sababu asilimia 90 ya mzigo wote unaosafirishwa unatoka kwenye Bandari ya Dar es Salaam, maana yake Bandari ya Dar es Salaam ikiboreshwa tutakuwa na uwezo mkubwa wa kuingiza mapato ya Serikali. Kwa hiyo, kama ambavyo Mheshimiwa Mwenyekiti amesoma kwenye taarifa yetu, tumegundua baadhi ya mambo mbalimbali ambayo yanakwamisha suala hili la usafirishaji wa mizigo ikiwemo kuwepo kwa foleni kubwa ya meli katika Bandari yetu ya Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili pamoja na juhudi zote bado tumeona kuna tatizo kubwa la ushushaji wa mizigo kwa kasi. Kwanza, lazima tukubali kwamba Bandari ya Dar es Salaam imekuwa kivutio kikubwa cha ukanda huu wa nchi nane. Ndiyo maana katika kipindi hiki wanakuja wateja wengi, kipindi hiki cha Desemba kuanzia Novemba mpaka Januari kumekuwa na mizigo mingi inapokelewa kwa sababu ya msimu, kwanza ni msimu wa kilimo, nchi yetu imekuwa ikihamasisha wakulima kutumia mbolea katika suala la kilimo. Pili, tumekuwa tukitumia mbegu bora maana yake zikitoka nje ya nchi, kuleta katika nchi yetu zinakuja kwa njia ya meli.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kuona meli nyingi pia ni mafanikio kwa sababu watu wameona destination ya Dar es Salaam ni nzuri katika kushushia mizigo yao, hayo ni mafanikio makubwa sasa lazima yazae changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili tuliposikia taarifa tuliwahoji wenzetu wa TPA wakatuambia kwamba wao wanatakiwa waongeze gati 12 mpaka 15 ili kuoongeza uwezo wa ushushaji wa meli nyingi kwa wakati mmoja, hivyo kazi hii inahitaji uwekezaji. Kama alivyosema mwenzangu aliyetangulia kwamba, kama unataka kumkamua ng’ombe basi lazima umlishe chakula cha kutosha ambacho ni majani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala pia la ushushaji mafuta. Katika gati ile ya mafuta ya KOJ, eneo lile ni dogo na meli za mafuta pia zimekuwa zikisubiri. Utatuzi wake ni kwamba lazima ujenge eneo lingine la kuhifadhia mafuta mbayo ni Single Receiving Terminal ambayo wanaita (SRT). Ukijenga hii Single Receiving Terminal utasaidia kuongeza kasi ya ushushaji wa mafuta lakini pia unaweza ukafanya storage wakati unasubiri wateja ambao wameagiza mafuta hayo kuyapokea, pia itapunguza gharama ya mafuta nchini katika soko la kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nilitaka niseme kama walivyosema wenzangu kwamba, lazima Serikali ione namna ya kuongeza fedha kwa ajili ya kusaidia hii miradi ambayo tumeisema ili TPA waweze kujenga gati za kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama haitoshi tumeomba kwamba wharfage hii ambayo inatajwa, huko nyuma TPA walikuwa wanaachiwa na Serikali. Hii ni kama vile kodi tu ya kufanya packing ya meli katika eneo la bandari na wala haihusiani na mapato ya TRA. Huko nyuma walikuwa wanafanya wenyewe, wanakusanya hizi fedha na wanafanya miradi mbalimbali ya ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, maana yake Serikali inavyokusanya hela yote inapeleka kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali, inaifanya TPA ishindwe hata kutaka kununua chochote mpaka iiombe kwanza Hazina. Kwa hiyo, niombe kama ilivyosemwa kwenye taarifa wharfage irudi waachiwe TPA waweze kukusanya na wakikusanya watakuwa na uwezo wa kuendeleza miundombinu ya bandari na kuvutia zaidi ushushaji wa mizigo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama haitoshi, tuwaachie asilimia 30 ambayo itabaki kwenye bandari ili iwasaidie, kwa sababu hauwezi kuwa na ushindani kama hauna fedha. Kwa hiyo, ninaomba sana jambo hili lizingatiwe ili tuweze kuondokana na changamoto ambayo wanayo wenzetu wa mamlaka ya bandari.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni suala la SGR. SGR itakuwa ni support kubwa ya kuondoa mzigo bandarini, SGR haijakamilika kwa muda mrefu, ninaomba kwamba wakikamilisha SGR watakuwa na uwezo wa kutoa tani zaidi ya milioni 17 kwa wakati mmoja kwa mwaka. Kwa hiyo, watapunguza msongamano wa Dar es Salaam, malori mengi pia hata kuharibu barabara zetu ambazo zinajengwa. Kwa hiyo, ninaomba sana kama inawezekana wenzetu wa SGR waharakishe ili waweze kukamilisha uwezekano wa kuanza kutoa huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ni upande wa TANROADS. Imeelezwa sana hapa kwamba TANROADS wamekuwa wanasaidia sana barabara zetu, kama haitoshi Serikali inategemea sana miundombinu ili iweze kupeleka huduma katika nchi hii. Kama miundombinu siyo imara hakuna kitakachofanyika, watu hawatasafiri, uchumi hautakwenda mbele. Ombi langu ni kwamba tujitahidi sana wenzetu wa TANROADS waongezewe fedha ambazo wanaziomba zitakazosaidia kwenda kuboresha barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara zilizopitishwa na Bunge zimesainiwa kupitia mradi ule au utaratibu wa EPC+F, barabara zenye urefu wa kilometa 2,035 mpaka leo barabara hata moja haijaanza kazi, haijaanza kujengwa na tumebakiza miezi sita ya bajeti hii kukamilika lakini changamoto iliyopo ni kwamba, wenzetu wanahitaji fedha zaidi ya trilioni 3.75 bila VAT ili waweze kuanza miradi hii. Miradi hii ni pamoja na barabara yenye urefu wa kilomita 460 kutoka Singida – Kwa Mtoro kwenda mpaka kule Tanga. Barabara hii ni miongoni mwa barabara saba zilizopitishwa katika kujengwa. Kwa hiyo, naomba sana kwa sababu miundombinu ni uchumi ninaiomba sana Serikali iweke jicho katika kuhakikisha kwamba barabara hizi zinakamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneno haya ninaunga mkono hoja ya Kamati yetu ili iweze kupita katika Bunge hili. Ahsante sana. (Makofi)