Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Morogoro Kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hoja iliyopo mbele yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nitumie nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi na kibali cha kuingia katika mwaka mpya.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nitumie nafasi hii kumpongeza Mwenyekiti wetu wa Kamati kwa kazi kubwa ambayo ameifanya katika kuiongoza kamati, hatimaye kuweza kuleta taarifa hii mbele ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kutiririsha fedha nyingi kwenye taasisi ambazo tunaziongoza. Kuna mahali tumeona wakati tunapitia taarifa za kazi, tumefika mahali ndani ya kipindi hiki cha robo mwaka wamefika zaidi ya asilimia 70. Tuna haja ya kumpongeza katika hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizo, nami nitumie nafasi hii ku-declare kwamba mimi ni mjumbe katika Kamati ya Miundombinu na nianze kuchangia kwenye suala la TPA. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bandari ndiyo lango la uchumi katika nchi hii, na ni imani yangu kwamba Mwenyezi Mungu sisi kama Watanzania ametupa baraka kupitia Bahari ya Hindi kuweza kufanya Taifa letu liwe na uchumi mkubwa. Katika kufuatilia nikwambie, Bandari ya Dar es Salaam ni Bandari ambayo ina sifa zote. Ina bandari ya uwezo wa kushusha na kupakia mizigo. Kwa hiyo, kiuhalisia kwenye meli na kwenye mizigo wanaweza kuitumia bandari hii na tukaweza kupata mapato makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wajumbe wenzangu wamesema nami niendelee kusema, Kamati imeomba kupitia wharfage walau TPA waachie asilimia 30, lakini mimi naenda mbali zaidi. Duniani kote kwenye Bandari wharfage inabakia ndani ya bandari yenyewe kwa ajili ya maboresho ya miundombinu ya bandari ili iweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tulichukua fedha hiyo ikaenda kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Ombi langu na niombe Bunge, niwashawishi Wabunge wenzangu, tusiende kwenye asilimia 30, fedha ya wharfage irudi kwenye maboresho ya bandari zetu. Kwa nini nasema hivyo? Kazi ya TRA ni kukusanya kodi. Tumezungumza na wenzetu wa TPA, wametuambia gati moja kwa mwaka inaweza kuleta kodi kwenye Serikali kiasi cha shilingi bilioni 600. Wenzetu wa TPA wanataka kutengeneza magati mawili mpaka matano. Tukiwaachia hii fedha ya wharfage ambayo ni shilingi bilioni 50 wanapata kwa mwezi, kwa mwaka wanatakuwa wanapata shilingi trilioni 1.1. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tumekwenda mbali kuwauliza gati moja linatumia shilingi ngapi kwa matengenezo yake, wametuambia gati moja linatumia bilioni 130, nini maana yake? Ukiweza kuwaachia fedha hii hata pengine kwa miaka miwili tu watakuwa na uwezo wa kutengeneza zaidi ya magati 10. Wakitengeneza idadi ya magati 10 kama alivyosema Ndugu yangu Manjira tukaenda mpaka kule Kigamboni, kwa mwaka tutakuwa na uwezo wa kukusanya kodi trilioni sita. Trilioni sita itakuwa ni mapato makubwa kwenye Serikali na ikiingia kwenye mzunguko wa fedha itafanya mambo makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe kupitia Bunge lako tusipepese maneno tuielekeze Serikali kwamba fedha hii irudi na ibakie TPA ili iweze kufanya mambo hayo na kukamilisha. Mimi namwanini sana Mheshimiwa Waziri Mbarawa na msaidizi wake lakini tunamwamini kabisa Mtendaji wa TPA, Mdogo wangu Mbossa, wanafanya kazi nzuri. Shida inayowachanganya ni kwamba hawajapata fedha na kuweza kufanikisha katika hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika hili mimi naomba tuende sambamba na kwenye TAA. Kuna kitu kinaitwa passenger service levy; passenger service levy, kazi yake ni kuboresha viwanja wa ndege, Serikali imekusanya imechukuwa imeingiza kwenye Mfuko Mkuu. Wanapotaka kufanya maboresho yoyote kwenye wwanja wa ndege lazima wakaombe Serikali hii siyo jambo jema, siyo jambo la kheri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe Serikali kupitia Bunge lako tuiambie waache fedha za service levy ambazo zinakatwa kupitia viwanja vyetu vya ndege ili tuendelee kuboresha viwanja vya ndege. Kupitia fedha hizo tungeweza kufanya maboresho makubwa kwenye viwanja vyetu vya ndege na kuweza kusaidia usafiri wa anga ukawa mzuri katika nchi yetu (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la tatu ambalo ningependa kusema na mimi niende kwenye TANROADS; ninaimani kubwa na wajina wangu, Waziri Bashungwa Innocent lakini nina Imani kubwa na Watendaji wa TANROADS. TANROADS inaweza na inaweza kufanya mambo makubwa katika Nchi hii tatizo ni fedha. Sisi kama Kamati tumegundua na tumeona, tunahitaji hardly trilioni tano kwa mwaka kuweza kufanikisha mambo yetu yote yafanyike.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini angalia bajeti ya mwaka jana, TANROADS imetengewa trilioni 1.3 na visenti kidogo ambavyo havitoshelezi. Juzi tulimwita Waziri wa Fedha, tulimwita Waziri wa Ujenzi katika Bunge tulilomaliza, wamejipangaje katika bajeti iliyokwisha? Wametupa matumaini. Lakini niombe kupitia Bunge hili, tuiambia Serikali tunakwenda kwenye uchaguzi mwakani lakini wakati tunakwenda kwenye uchaguzi mwakani Mvua za El Nino zimefanya uharibifu mkubwa katika Nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano barabara ya Bigwa–Kisaki imekatika zaidi ya mara saba kuna mapungufu, kuna shida kubwa katika usafiri wa wananchi. vilevile tunakwenda kwenye uchaguzi, kuna miradi ambayo tumeiahidi kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. Mama Samia Suluhu Hassan amefanya mambo katika nchi hii, tuangalie tusiende tukampunguzia kura zake za Urais. Sasa niombe kupitia Bunge hili tuiambie Serikali tunataka:-
Mheshimiwa Naibu Spika, cha kwanza, miradi 13 ambayo tayari imeshapata wakandarasi inasubiri uwekezaji, mmojawapo ukiwa Barabara ya Bigwa – Kisaki kilometa 78; Barabara ya Ubena Zomozi – Ngerengere kilometa 11 itengewe fedha twende zikasainiwe ili kusudi tuone hayo mafanikio makubwa ambayo Serikali imefanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa zaidi niipongeze Serikali na nimpongeze Mama Samia Suluhu Hassan kwa nafasi yake ambaye ameiona. Juzi tarehe 21 Mwezi wa Kumi na Mbili kulikuwepo na Mkutano Mkubwa wa Wakandarasi pamoja na Serikali ambayo alikuwepo Waziri wa Fedha, alikuwepo na Waziri wa Ujenzi. Mama anataka wakandarasi wazalendo wajengewe uwezo na wafanye miradi mikubwa ili fedha ibaki Nchini, napongeza jitihada hizo. Sasa ndani ya kikao kile Mawaziri walijulishwa na Wakandarasi kwa sababu bahati nzuri na mimi na declare interest ni Mkandarasi, kuna suala ambalo Serikali imetueleza kwamba inatengeneza kiliometa 50, 50 miradi kama minne wapewe Wakandarasi wazawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Serikali; moja, tutengeneze JV ya wakandarasi wazawa kuanzia class one mpaka class five ili waweze kujenga miradi hiyo. Vilevile, hawa wakandarasi wakubwa wawajengee uwezo makandarasi wadogo. Niiombe Serikali kupitia miradi hiyo wawatafutie washauri wa miradi ili miradi hiyo ikamilike kwa muda na wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la mwisho kuna suala la withholding tax ndani ya miradi kuna asilimia tano inayochukuliwa withholding tax inawaumiza wafanyabiashara na hasa wakandarasi wazawa. Tunaomba, tulipendekeza kuna kati ya asilimia mbili ibakie, ichukuliwe asilimia tatu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba kuunga mkono hoja zote za Kamati na niliombe Bunge tusipepese macho kama…
NAIBU SPIKA: Ahsante.