Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hotuba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kwanza kumpongeza sana Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu pia nawapongeza sana Wajumbe wote wa Kamati ya Miundombinu kwa taarifa yao na ripoti yao nzuri ambayo wameiwasilisha hapa sasa hivi na sisi tunaweza kuiongozea nyama kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza pia Mawaziri wote waliopo katika sekta hii ya miundombinu na Manaibu Mawaziri na Watendaji wote wa Wizara zote ambazo zinaguswa na hii Kamati ya Miundombinu. Vilevile, naomba pia nimpongeze Spika na nikupongeze Naibu Spika kwa kazi nzuri inayofanyika katika Bunge letu hili la Muungano. Naendelea pia kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu na Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri sana ambayo amekuwa akiifanya pamoja na kuhakikisha kwamba pesa nyingi sana zinakwenda katika sekta hii ya miundombinu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na sekta ya barabara na nianze kuchangia kuhusiana na barabara za kiuchumi zilizopo katika nchi yetu. Naiomba Serikali iangalie na iweke kipaumbele kikubwa kuhakikisha kwamba bajeti kubwa inawekwa kuhakikisha kwamba barabara za kiuchumi zinapitika wakati wote na hasa wakati huu wa mvua hizi za masika. Tunaona barabara nyingi sana wakati wa masika hazipiti na ni za kiuchumi na zinasababisha sasa uchumi kudorora au kupunguza uchumi katika nchi yetu. Kwa hiyo, naomba uwepo mkakati wa kuhakikisha kwamba barabara zote zinapitika wakati wote, na kwa sababu kuna baadhi ya barabara nyingine unakuta kwamba kuna eneo tu dogo ambalo linasababisha barabara ile isipitike. Kwa hiyo, hiyo barabara kama itatengenezwa vizuri basi unaona kwamba zinaweza zikapitika wakati wote na malori yanaweza yakapita.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe mfano wa baadhi ya barabara ambazo hata katika Mkoa wetu wa Iringa zimekuwa za kiuchumi lakini hazipitiki. Kule Mafinga unakuta kuna Barabara ya Kinyanambo ‘C’ - Mapanda - Mlimba hii inakwenda mpaka Morogoro ni muhimu sana ikawa inapitika wakati wote. Pia kuna barabara ya Nyololo – Mtwango hii ni ya kilomita 40, unaona kwamba hii barabara ni muhimu sana katika uchumi wa nchi hii. Tunayo pia barabara kwa mfano ya Ilula – Wotalisoli – Mlafu - Mkalanga na Kising’a hii inakwenda mpaka kwenye Makao Makuu ya Wilaya ya Kilolo lakini unakuta watu badala ya kupita hii, maana yake kuna Kilolo ya Chini na Juu badala ya kukatiza kupita mpaka kule Wilayani wanalazimisha sasa kupita mpaka Iringa Mjini ili waende Kilolo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni muhimu barabara kama hizi zikaangaliwa zina umuhimu wake ili kupunguza hata wananchi kuweza kufanya shughuli zao kwa wakati. vilevile, kuna hii barabara yetu ya Mlima Kitonga, hii barabara ni ya kiuchumi tena wa Kimataifa. Unakuta magari yanakwama hata siku mbili au siku tatu, barabara haipitiki kabisa lakini tunashukuru sasa hivi Serikali imeanza kweli tunashukuru Waziri alikuja katika ile barabara na tunaona sasa matengenezo yameanza ya upanuzi wa ile barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba iwepo barabara mbadala kwa sababu bado matengenezo yake hayatachukua leo au kesho yatachukua muda mrefu sana, sasa tunaomba wakati hii barabara inafanyiwa matengenezo basi inapanuliwa basi ile barabara mbadala ya kutoka Mahenge kupitia Udekwa kutokea Ilula, hii barabara ingepewa kipaumbele ili kusiwepo na mkwamo wa magari kwa sababu hata wakati huu wa matengenezo magari yanakuwa hayapoiti kwa wakati, kwa hiyo hii ni muhimu sana Serikali ikaangalia barabara hizo za kiuchumi ziweze kupitika kwa wakati wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, nami niendelee pia kuzungumzia kuhusiana na viwanja vya ndege. Mjumbe aliyepita amechangia vizuri sana kwamba tuna viwanja vingi sana vya ndege na vimekuwa vikipewa pesa kidokidogo kwa ajili ya kuhakikisha kwamba vinajengwa. Vingeangaliwa pengine hata vingefanyiwa hata upembuzi yakinifu kweli ili vile viwanja vingine ambavyo karibu vinamalizikia, kwa mfano kwenye Mkoa wetu wa Iringa tuna Kiwanja cha Ndege cha Iringa, hiki kiwanja kimechukua muda mrefu sana kukamilika ilikuwa kikamilike tangu mwaka juzi na mwaka jana tunaongezewa tu muda, hiki kiwanja sasa hivi kwa uchumi wa Iringa ni muhimu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna kilimo cha parachichi, tuna kilimo cha maua na tuna kilimo ambacho tunajua kwamba kama kiwanja hiki kingekamilika kingeweza kusaidia uchumi mkubwa sana wa Nyanda za Juu Kusini pamoja na kusafirisha mazao yake. Pia, zingetoa ajira nyingi sana kwa wananchi wa Iringana Mikoa ya jirani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba kwa kweli hiki kiwanja kimalizike sasa mana yake kila siku tunauliza mpaka tumechoka na naungana na mwenzangu kwamba ilikuwepo ndege ya ATCL inatua pale. Sasa tatizo lake ni nini kwa sababu barabara zile zimeshakuwa ziko tayari na tunaona viwanja vingine wakati vinaendelea kujengwa kuna ndege zinatua za ATCL ili kupunguza ile adha, tuna wagonjwa tuna nini kiasi kwamba ingeweza kusaidia. Kwa hiyo tunaomba basi wakati matengenezo kama yanachukua muda mrefu basi barabara zikikamilika basi ndege zile za ATCL zitue ili wananchi waweze kuwa na uhakika wa usafiri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine, zamani zile kale wanasema hapo zamani za kale tulikuwa tunaweza kusafiri kwenda kuangalia miradi ya nchi nyingine nilikuwa Kamati ya Miundombinu tuliweza kusafiri kwenda Malaysia kuna mambo ambayo tulijifunza pengine Serikali pia ingeangalia. Kwanza kabisa tuliona wale wenzetu hii miradi mikubwa ya barabara kunakuwepo ile miradi ya PPP (Private Sector Partnership) ndiyo inayochukua. Inasaidia kwamba pesa za ndani zinatumika kwenye barabara ambazo zinazunguka katika nchi. Pengine hata Serikali sasa hivi ingeangalia iwepo hii miradi ya private sector kusaidia hii miradi mikubwa ya barabara. Pia, tuliona wenzetu wakandarasi wakubwa wanapokuja kwenye nchi yao hawaruhusiwi kufanya ile miradi mikubwa mpaka waingie ubia na wakandarasi wa ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ingesaidia pia kuwajengea uwezo wakandarasi wetu wa ndani na vilevile hata wakiondoka vifaa vingi vinabaki kwenye nchi yetu. Kwa hiyo, pia hili lingeangaliwa kwamba iwekwe sheria itakayosababisha hawa wakandarasi wanaotoka nje basi waingie ubia na wakandarasi wetu wa ndani ili kuwajengea uwezo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunaomba wakandarasi wetu walipwe basi kwa wakati, kwa sababu tumeona wakandarasi wengi miradi inachelewa kuisha kwa sababu na gharama inakuwa kubwa kama ripoti ilivyosema kwa sababu hawalipwi kwa wakati na hiyo inasababisha kabisa wanashindwa kufanya kazi yao kwa wakati na gharama zinaongezeka kwa kiasi kikubwa sana. Baada ya hapo nakushukuru na namshukuru Mwenyezi Mungu pia, ahsante sana. (Makofi)