Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Stella Simon Fiyao

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia katika Kamati hii ya Miundombinu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naanza kwa kuchangia kwenye eneo la TANROADS hasa kwa kuwa ninatambua umuhimu mkubwa wa miundombinu ya barabara ndani ya Taifa letu katika kuchangia Pato la Taifa na kipato cha mtu mmoja mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na changamoto sana katika miradi ya barabara. Laiti kama kila Mbunge angesimama hapa, hata tukianza kumuuliza Mbunge mmoja mmoja hapa, kila mmoja atazungumza changamoto ya barabara kwenye eneo lake, kwa sababu hii imekuwa ni changamoto ya nchi nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi ya asilimia 80 ya mizigo na abiria ndani ya nchi yetu wanatumia barabara. Hivyo, tunajua barabara ina mchango mkubwa katika kuchangia Pato la Taifa letu. Kama walivyozungumza Wajumbe wengine wa Kamati, kumekuwa na changamoto kubwa sana ya fedha za miradi ya maendeleo ndani ya TANROADS. Changamoto hii imesababisha miradi mingi kutokukamilika kwa wakati, na miradi mingi haijatekelezwa kabisa kutokana na changamoto ya uhaba wa fedha ndani ya TANROADS. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto hii ya uhaba wa bajeti ya miradi ya maendeleo ndani ya TANROADS, imeleta athari kubwa. Athari hizi zinaonekana na tumeendelea kushauri kila tunaposimama kwenye Bunge hili. Athari kubwa ambazo tunaziona ni kuongezeka kwa gharama kubwa ya miradi. Miradi imekuwa ikiongezeka gharama kila kunapoitwa leo kutokana na ufinyu wa bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2023, madeni ya wakandarasi na wahandisi washauri yalikuwa ni shilingi bilioni 701, lakini mpaka sasa ninavyozungumza madeni ya wakandarasi na Wahandisi Washauri ni shilingi bilioni 889. Yaani kila kunapoitwa leo, figure inaendelea kuongezeka, gharama ya miradi inaendelea kukua na mwisho wa siku tunatekeleza miradi kwa gharama kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hizi fedha ni kodi za Watanzania. Mimi nadhani hata Watanzania wanahuzunika wanaposikia hizi taarifa huko nje. Hali siyo nzuri. Kuna wakati lazima tujifunze hata kwa mataifa mengine, wanafanyaje katika kutekeleza hii miradi ya barabara? Mbona kuna maeneo gharama haziongezeki lakini sisi kwenye nchi yetu gharama zinazidi kuwa kubwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunazungumza mwaka huu 2024, hii ni Februari, tusishangae kufika Desemba hii figure ikawa imeongezeka kutoka kwenye shilingi bilioni 889 huko tutaenda kwenye matrilioni. Hii hali ni mbaya mno! Kwa asilimia kubwa miradi inakwama, lakini ukiangalia kwenye uhalisia, baadhi ya maeneo kuna miradi inaendelea kutekelezeka. Kama kuna miradi inaendelea kutekelezeka na mingine imeshatekelezwa, hii ina maana bado tuna tatizo kubwa kwenye suala la madeni ya wakandarasi na wahandisi washauri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima kama Serikali tujipange, ni namna gani tunakabiliana na hii changamoto? Kwa sababu hakijawa kilio cha leo, kila tunaposimama; mimi nina kumbukumbu kwenye michango yangu, kila ninaposimama nazungumzia suala la wakandarasi. Madeni ya wakandarasi yamekuwa ni tishio kwa Taifa letu. Ni lazima Serikali tuone ni namna gani tunakabiliana na hii changamoto ikiwa ni pamoja na kutenga bajeti ya kutosheleza kwenye TANROADS ili tuweze kuziepuka hizi changamoto, kwa sababu mwisho wa siku tunaenda kuua uchumi wa Taifa letu kwa mikono yetu wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuzungumza kwenye changamoto ya bajeti kwenye suala la TANROADS. Tumeendelea kusema hapa, katika bajeti ya mwaka 2023/2024 tumepitisha shilingi trilioni 1.4 kwenye miradi ya maendeleo. Hali siyo shwari. Nimesema kila mtu akisimama hapa ataelezea uhalisia kwenye mkoa wake. Barabara zinakatika, madaraja yanabomoka, hali ni mbaya, mawasiliano yanakatika hasa ukizingatia hali ya mvua tuliyonayo sasa hivi. Hali inazidi kuwa mbaya kwenye maeneo ya barabara na fedha hatuna. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ili tuweze kuvuka na kutoka salama hapa, ni lazima tutenge shilingi trilioni tano ili shilingi trilioni tatu iende kwenye miradi ya maendeleo ya barabara na shilingi trilioni mbili iende kwenye ukarabati. Hali ni mbaya! Barabara zimetengenezwa kwa gharama kubwa na fedha nyingi, lakini zinaendelea kuharibika kwa sababu hata fedha ya ukarabati haipo. Ni lazima tuliangalie hilo, hali ni mbaya sana kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuzungumza jambo la pili kuhusu suala la fidia kwa wananchi ambao wamepitiwa na miradi hii ya barabara. Ukitoka Tunduma ukapita kwenda Rukwa pale, ni miaka ya 2000 huko wananchi walishachorewa ‘X’ za kijani na wakaambiwa Serikali inakuja kuwalipa fedha. Wananchi hao wamekaa wakisubiri Serikali ije iwalipe fedha, hawawezi kuendeleza maeneo hayo, hawawezi kufanya chochote kwenye hayo maeneo, hawawezi kuendeleza shughui zozote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukizungumzia miaka ya 2000 ni umri wa mtu sasa hivi, mtu mzima. Huyo ameolewa sasa hivi ana watoto. Hii hali ni mbaya, hebu Serikali mtuambie kama mna uwezo kweli wa kulipa gharama za fidia kwa wananchi hawa ili ikiwezekana kama Serikali mtashindwa, wananchi mwape ruhusa ya kuyaendeleza maeneo yao. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani, kwa sababu mwisho wa siku tunaangalia tu gharama za ulipaji wa fidia ndani ya nchi nzima ni shilingi trilioni 7.5. Hebu Serikali tuambieni, mna uhakika wa kukifanya hiki? Je, hao wananchi mliowachorea ‘X’ za kijani mna uhakika wa kwenda kuwalipa? Kama uhakika haupo, waambieni wananchi wayaendeleze yale maeneo. Tusiwakwamishe wananchi wetu. Hali siyo nzuri, wananchi wanalia huko, hawana tumaini kabisa kwamba Serikali je, itakuja? Mwisho wa siku isije ikatokea Serikali mnawaambia hao wananchi endelezeni maeneo yenu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi miaka 20 umemchelewesha mwananchi hajafanya chochote, utamlipa fidia? Waambieni wananchi ukweli. Kama Serikali hamna uwezo wa kuwalipa fidia, wayaendeleze maeneo yao kwa kufanya shughuli zao kama kawaida, kuliko kuendelea kuweka ‘X’ zenu za kijani pale na hakuna kinachoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii hali inawaumiza sana wananchi wetu, kwa sababu mwisho wa siku wanabaki wanayatazama tu maeneo, hawawezi kufanya chochote. Hii siyo sawa. Ili tukomeshe haya, tunaomba sana bajeti ya Wizara ya Ujenzi iongezeke sasa hivi ili tuweze kuona matokeo yaliyo mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. (Makofi)