Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Karagwe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia Hoja ya Kamati ya Miundombinu kuhusu utendaji wa Serikali. Naanza kwa kukushukuru na kukupongeza kwa kazi nzuri unayoifanya katika majukumu yako ya Unaibu Spika. Pia nakupongeza kwa kazi nzuri unayoifanya ya uwakilishi wa wananchi wako wa Jimbo la Ilala. Hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu, Mwenyekiti wetu Mheshimiwa Kakoso kwa wasilisho zuri la hoja ya Kamati. Pia, nampongeza Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati, Mama yetu, Mheshimiwa Anne Kilango pamoja na Wajumbe wa Kamati kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kushauri Wizara ya Ujenzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu na timu yote ya Wizara na taasisi zake, tunaahidi kuendelea kuwapa ushirikiano. Pia tunawashukuru sana kwa ushirikiano mnaotupatia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nawashukuru Waheshimiwa Wabunge ambao wamepata fursa ya kuchangia hoja hii zikiwemo hoja zinazohusu Wizara ya Ujenzi. Naomba kutumia muda niliopewa kutoa ufafanuzi kwa baadhi ya masuala ambayo yamejitokeza mara nyingi kutoka kwenye hoja za Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mchango wa Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati, mama yangu Mheshimiwa Anne Kilango, pamoja na Waheshimiwa Wabunge mmetoa pongezi kubwa…
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wamepongeza Serikali na Mheshimiwa Rais wetu, mpendwa wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kazi kubwa inafanyika ya kujenga miundombinu nchini ikiwemo miundombinu ya barabara pamoja na madaraja, na wakasema mvua za El-Nino zimeleta dosari kubwa ya kazi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, concern ya Waheshimiwa Wabunge, wote tunakubaliana kwamba miundombinu imara inajenga uchumi imara na Serikali inatambua hilo. Ndiyo maana pamoja na changamoto zinazojitokeza kipindi hiki ambacho tunapata Mvua za El-Nino mkakati wa Serikali ni mara moja baada ya miundombinu kuharibika ni kufanya kila linalowezekana kurudisha mawasiliano kama emergency response huku tukiangalia namna ya kuboresha miundombinu hii kwa maana ya mkakati wa medium to long term.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama Waheshimiwa Wabunge walivyochangia, Serikali katika bajeti hii tunayoandaa na bajeti zijazo, yale masuala ambayo yameleta dosari kubwa ambayo yanahitaji bajeti kubwa, tutayazingatia katika bajeti hii tunayoandaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, concern ya Waheshimiwa Wabunge kwamba Mvua za El-Nino na barabara nyingi kufikia muda wake kwa maana ya matumizi ya barabara, umeleta hitaji kubwa la bajeti, limetajwa hitaji la shilingi trilioni tano.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nawaondoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge, pamoja na mahitaji haya kwa upande wa Serikali na nature ya ujenzi wa barabara na madaraja mahitaji huwa hayatekelezwi kwa wakati mmoja yaani hatuwezi kusema tutapata shilingi trilioni tano leo hii tutimize mahitaji yote; lakini incrementally kwa phases wote tukishakubalina kama hapa tulivyochangia basi hata kwenye uzingatiaji wa bajeti na bahati nzuri Mheshimiwa Waziri wa Fedha yuko hapa,
Mheshimiwa Waziri wa Uwekezaji na Mipango Profesa Mkumbo yuko hapa. Wiki hii nakutana na timu yake ili kuangalia kwenye miaka 25 inayokuja ya Development Plan ya nchi, masuala haya pia tuyaangalie ikiwemo suala la kujenga barabara za kutumia PPP na Mheshimiwa Rais pamoja na Waheshimiwa Wabunge, jambo hili mmelijadili na kuona sasa katika kujenga miundombinu, lazima tuwe wabunifu na tutumie kila aina ya njia ikiwemo njia ya PPP kuboresho miundombinu nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Profesa Mkumbo na timu yangu ya Wizara pamoja na timu yake, wiki hii tunakaa kuangalia Development Plan inayoisha mwakani, ile ya 2025 kwenda 2050, maeneo mahususi ya kimkakati yanayohusu ujenzi wa barabara pamoja na madaraja zikiwemo Barabara za Trunk Road ambazo zimetajwa na Kamati, kupitia mchango wa Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti. Barabara 71 ambazo zimeisha muda wake, pia tunaangalia kupitia huo Mpango wa miaka 25 tunayoiandaa, baadhi ya barabara tuangalie namna ya kujenga kwa njia ya PPP. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tayari kwa mfano Barabara ya kutoka Dar es Salaam kuja hapa Morogoro, kuja Dodoma hapa kupitia Morogoro tayari tunazungumza na wabia ambao tunaweza tukaingia nao kujenga Express Way kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma, Makao Makuu ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo ambalo ningependa kulisema, barabara ambazo tutajenga kwa njia ya PPP, hatutaathiri barabara zilizopo ili mwananchi yeyote ambaye anataka kuendelea kutumia barabara zilizopo, maisha yaendelee. Pia ku-support uchumi wa nchi kwa kujenga barabara ambazo iwe ni mizigo, malori na watu ambao wanahitaji kwenda kwenye shughuli mbalimbali za uzalishaji uchumi, basi awe na option kutumia barabara iliyopo au barabara kwa njia ya express. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, yote haya Waheshimiwa Wabunge tunayachukua lakini tayari tumeanza kuyafanyia kazi. Kuhusu Wakandarasi wazawa, limezungumziwa suala la madeni kuchelewa kulipwa. Katika hili, Mheshimiwa Rais tunamshukuru, maelekezo yake Wizara ya Ujenzi kukaa na Wizara ya Fedha, tayari tumeshajiwekea utaratibu wa kupunguza madeni ya wakandarasi wazawa kila mwezi na deni la wakandarasi wazawa mpaka hivi sasa tumelipunguza mpaka Disemba, mwaka jana.
Mheshimiwa Naibu Spika, deni ambalo limebaki mwezi huu wa Februari, kupitia Wizara ya Fedha, wametuahidi tutaendelea kutoa commitment ya kulipa shilingi bilioni 50 kila mwezi ili takribani shilingi bilioni 115 ambayo imebaki kwa wakandarasi wazawa, kufika mwezi Aprili, tuwe tumekamilisha ina maana tutakuwa tuna certificate mpya za kuanzia Januari na kuendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili, tunamshukuru Mheshimiwa Rais, kwa maelekezo yake na kupitia Wizara ya Fedha, tunaendelea kulifanyia kazi; lakini hatujaishia hapo kwenye wakandarasi wazawa, ni dhamira ya Mheshimiwa Rais kuona uchumi wa nchi kwa kadri inavyowezekana, tunakuwa tuna mikakati endelevu ya kuwezesha wakandarasi wazawa. Kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais wakati ananiapisha kuja kwenye Wizara ya Ujenzi, niliunda Kamati ya kuchambua mapungufu yaliyopo ya wakandarasi wazawa yakiwemo masuala ya mitaji, mitambo, uwezo wa kusimamia miradi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati hii imeshakamilisha tunachokiita local content strategy ya wakandarasi wazawa. Ninaamini kupitia Ofisi yako, wakati wa Bunge la Bajeti, tukipata nafasi ya kuwasilisha kwa Bunge local content strategy tuliyoiandaa kwa ajili ya wakandarasi wazawa, tutapata ushauri ili Mkakati huu sasa ukawe ndiyo Master Plan ya kuwasaidia Wakandarasi Wazawa. Yamo masuala ya kulegeza vigezo ambavyo vilikuwa …
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri, malizia.
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, katika kumalizia, namalizia na suala la miradi ya EPC + F. Niwaondoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge, Wakandarasi saba ambao wamepata miradi hii, wanafanya mapitio ya design ambazo zilifanywa na TANROADS mwaka 2017 ili waweze kuwa na taarifa sahihi kuhusu majenzi ya barabara hizi na jambo hili liko hatua za mwisho, kwa hiyo, miradi yote saba tutaitekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, suala la fidia, zimesemwa takribani shilingi trilioni 7.5. tunaendelea kufanya uchambuzi ndani ya Serikali ili kuona namna bora ya kuendelea kufidia maana siku zote barabara tumezijenga kwa utaratibu wa kufidia wananchi ili tuweze kujenga Miundombinu ya Barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa sababu suala la fidia limekuwa accumulative na la muda mrefu, tunafanya uchambuzi wa kina ili maeneo mengine ambayo yatasaidia kuokoa usumbufu upande wa wananchi lakini pia kupunguza gharama hizi tuweze kuyatumia, barabara tuzijenge lakini pia na wananchi wetu waweze kupata fidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)