Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Prof. Norman Adamson Sigalla King

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. PROF. NORMAN A. SIGALLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii.
Kwanza kabisa napende kumpongeza Mheshimiwa Sospeter Muhongo na msaidizi wake na timu yake nzima kwa kazi kubwa ambayo wanalifanyia Taifa hili kuhakikisha kwamba nishati ya umeme inapatikana. Sambamba na hilo, napongeza kwa sababu ni ukweli ulio bayana kwamba kwa sasa Tanzania ni moja ya nchi ambazo zinafanya vizuri zaidi Afrika, kwa maana ya coverage, yaani kwenda kwa kasi katika kusambaza umeme. Hongera sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua uwezo wako na weledi wako, lakini nimesikitika sana ulipokuwa unawasilisha bajeti yako, hasa baada ya kuona Mto Lumakali ambao uko Makete ambao study yake ya kwanza imekamilika mwaka 1998 ikionesha kwamba tuna uwezo wa kuzalisha umeme megawatts 222; ikarudiwa tena mwaka 2002, ikaonesha kwamba tuna uwezo wa kuzalisha megawatts 340.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni mto pekee ambao study kwa miaka 60 inaonesha kwamba maji yake hayapungui. Ninatambua changamoto tuliyonayo kwenye mito mingi iliyoko Tanzania, ni kupungua kwa maji. Ndiyo maana wakati nachangia Mpango wa Serikali nilisema Mheshimiwa Sospeter Muhongo anaonekana ana ugonjwa wa gesi; bila shaka nilimtania, lakini najaribu kusema kwamba upo umuhimu mkubwa wa kupeleka nguvu kubwa kwenye mradi wa maji wa Mto Lumakali unaopatikana Makete, ni muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu unajumuisha kuweka kingo za bwawa. TANESCO wameshafika mara nyingi kule, makampuni ya Afrika Kusini, China yamefika kule, yameshawaweka tumbo joto wananchi wangu wa Makete kwamba mpaka hapa tutakuwa na bwawa. Wameendelea kusubiri toka mwaka 1998 bwawa hilo halitokei.
Naomba sana Waziri mhusika aone umuhimu wa kipekee sana kupeleka bwawa hili. Bwawa hili pamoja na uzalishaji wa umeme litakuwa muhimu kwa uchumi wa Nyanda za Juu Kusini na Tanzania kwa ujumla. Utakuwa umepanda zao jipya la samaki kuvunwa katika bwawa hili la Lumakali pamoja na Mto wenyewe wa Lumakali. Kwa hiyo, ni muhimu sana jambo hili likatekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tena Wizara ione umuhimu wa kupeleka maeneo yaliyosalia umeme wa REA na hasa Kata za Lupila, Mbalache, Ukwama, Mang‟oto, Kipagalo, baadhi sehemu za vijiji vya Tarafa ya Magoma, Tarafa ya Ikuo, Tarafa ya Matamba na Tarafa ya Lupalilo. Ni jambo la msingi sana ili wananchi wa Makete wapate kuleta maendeleo kwenye nchi yetu. Kwa bahati nzuri unatambua, wananchi wa Makete kwa asili ni wachapakazi, kwa hiyo, nishati ya umeme kwao ni nguzo pekee ya muhimu itakayowezesha tukimbizane na maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie kidogo eneo la madini. Sheria ya Madini ni muhimu sana ikafanyiwa marekebisho. Utaratibu uliopo sasa wa kupata leseni Makao Makuu na kupewa eneo Makao Makuu bila ushiriki wa Halmashauri husika, hautendi haki. Ni muhimu sana tutengeneze mahusiano kati ya Mamlaka ya kutoa leseni na Halmashauri mama yenye kumiliki ardhi ambayo inaangukia kwenye eneo hilo ili kuondoa migongano isiyo na sababu lakini pia ili kuwapa faida wananchi ambao maeneo haya kimsingi ni ya kwao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie EWURA. Wenzangu wallyotangulia walikuwa wanasema kwamba wana interest na maeneo hayo; nami kwenye madini pamoja na mafuta nina-declare interest.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Makete pale mjini ina vituo vinne vya mafuta. Wamekwenda Maafisa wetu wa EWURA kufunga vituo vyote. Makete hakuna transit, kwa maana ya malori yanayobeba mafuta kupita Makete. Mafuta haya yanatwaliwa Dar es Salaam kwenye depot. Ni muhimu sana Maafisa wetu wa EWURA wajikite kwenye ku-control quality Dar es Salaam yanakotoka mafuta. Wajikite kwenye kufanya mahusiano stahiki na mamlaka nyingine zinazohakikisha kwamba mafuta yanayokwenda nchi jirani yanakuwa monitored ili kwamba mafuta hayo yasipelekwe mitaani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo sahihi hata kidogo, inaonekana kama ni uonevu hivi kidogo, pale ambapo mafuta yanatoka Dar es Salaam, muuzaji wa mafuta yuko Makete, kilometa 900 kutoka Dar es Salaam, hakuna barabara inayopita kule kwenda nchi jirani, barabara yenyewe ni mbovu, halafu wafanyabiashara hawa wanafungiwa vituo vyao kwa sababu tu ya maafisa wetu wa EWURA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa labda nimwombe Mheshimiwa Waziri, ninaamini sana katika competence based recruitment, ninaamini Sheria ya EWURA ni nzuri, kwenye hili, tatizo ni la watu. Tusioneane haya kwenye hili. Tatizo ni la maafisa wetu. Ni muhimu sana, maafisa wetu, sheria hata ingekuwa nzuri, kama an official ni corrupt ata-jeopardize the entire system.
Kwa hiyo, ni muhimu sana maafisa wetu hawa waangaliwe ili wanapofanya maamuzi, basi waone madhara ya uchumi pia. Tukisema hivi, hatumaanishi kwamba sasa watu waendelee kuvunja sheria, hapana. Tunachojaribu kusema ni kwamba mafuta yanakotoka yanajulikana, ni Bandari ya Dar es Salaam pekee inayoingiza mafuta Tanzania. Kwa hiyo, eneo la ku-control linajulikana. Inaumiza sana kuona watu wa Makete nao wanafungiwa vituo vyao kwa sababu tu ya maafisa hawa wanaoshindwa kuzingatia umuhimu wa kuzingatia mafuta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nisisitize kusema kwamba Tanzania kwa sasa ninafahamu, tunakoelekea ni kuzuri, tena kuzuri sana na kazi hii kwa vyovyote vile nitakuwa nimekosa nidhamu kutokumsifia Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa maamuzi yake ya kuongeza bajeti ya jumla ya maendeleo kufikia asilimia 40. Leo Waziri mwenye dhamana anatuambia, asilimia 94 ya bajeti yake inakwenda kwenye maendeleo. Mungu aibariki sana Tanzania na Mungu aibariki sana Serikali ya CCM kwa jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, Mungu awabariki sana. Ahsante.