Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Twaha Ally Mpembenwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibiti

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi kuwa mchangiaji wa kwanza katika taarifa zetu mbili ambazo ziko mezani. Awali ya yote niseme tu kwamba naunga mkono hoja. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya LAAC. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla sijaanza mchango wangu sina bundi kutoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaendelea kuifanya. Dunia inajua, Afrika inajua na sisi Watanzania tunamwelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni historia ambayo imewekwa Tanzania, kwa mara ya kwanza hakuna wilaya hata moja ambayo haijawahi kuguswa na mkono wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sekta zote zile za kimaendeleo; iwe sehemu ya afya, iwe katika Sekta ya Elimu au iwe katika Sekta ya Barabara zile ambazo ziko chini ya TARURA. Katika hili sina budi kumpongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo naipongeza vilevile Ofisi ya TAMISEMI kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wanaendelea kuifanya katika kuweza kuhakikisha kwamba ni kweli ile tafsiri ya kusema kwamba Wizara hii ni Wizara ya wananchi sasa tunaanza kuiona. Kwa namna ya kipekee kabisa naomba vilevile nichukue fursa hii kumpongeze mchumi mbobezi, ndugu yangu Mheshimiwa Lameck Mwigulu Nchemba kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuweza kusukuma fedha katika halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, historia imeweza kutengenezwa hapa Tanzania, mathalani katika Jimbo la Kibiti, tuna kata 16; hakuna hata kata moja ambayo fedha haijaenda katika miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, niko hapa kuweza kujadili na kuchangia hii Taarifa ya Kamati ya LAAC na mimi nitagusa kipengele kimoja tu cha force account. Baada ya hapo nitakwenda kidogo pale jimboni, kuna mambo mawili matatu ya kuyaweka sawa.

Mheshimiwa Spika, kwanza naipongeza Serikali, hapa tulipofika tumefika kwa sababu ya force account. Wote mliopo humu ndani ni mashahidi mnajua, shughuli zote za ukandarasi zilikuwa zinafanywa na wakandarasi. Ujenzi wa namna yoyote ulikuwa unafanywa na wakandarasi, lakini tunajua athari kubwa sana iliyokuwa imepatikana na ndiyo maana force account ikawa introduced.

Kwa hiyo, kwanza kabisa nawapongeza Wakurugenzi na watendaji kwa jitihada kubwa ambazo wanajitahidi kuzifanya pamoja na mapungufu mengi ambayo tumeyaona na ni kazi yetu sasa kama Wabunge kuweza kuishauri Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye hii force account kuna masharti ambayo yamewekwa ya kutumia force account. Mimi katika mjadala wangu nitaongelea sharti moja tu. Sharti hili lililokuwa limewekwa linasema kwamba force account itumike kwenye kazi ndogo ndogo zitakazoweza kufanyika katika maeneo ambayo yako mbali kidogo na eneo la mjini kule ambako wakandarasi kwa namna moja ama nyingine wakiwa wanatupa quotation zitakuwa ni ari ya juu sana, mapungufu ndiyo yanaanzia hapa.

Mheshimiwa Spika, Serikali haijaweka wazi, tunapozungumza miradi midogo midogo, ni miradi gani hiyo? Je, ni ujenzi wa matundu ya vyoo, ujenzi wa madarasa au ujenzi wa ofisi za halmashauri? Hiyo miradi ni miradi gani? Kwa hiyo, pamoja na mapungufu yaliyopo ndani ya force account. Naomba niseme tu, ni msingi sasa Serikali iweze kuhakikisha inakwenda kuchanganua kwa mapana yake ili kuanza kuweka tafsiri sahihi kama vile Kamati ilivyokuwa imeshauri. Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye Kamati tulikuwa tumeshauri kuhusiana na suala zima la fedha ambazo zinaweza kutumika katika miradi ya force account, lakini kwa bahati mbaya zaidi Serikali walichoweza kukisema katika masharti ambayo yalikuwa yameoneshwa hapa, tumeambiwa kwamba miradi midogo midogo ndiko force account inakoweza ikatumika.

Mheshimiwa Spika, inasikitisha, tunashindwa kupata tafsiri halisia, wanapozungumza miradi midogo midogo ni nini? Tukiwa tunakwenda kwenye Kamati kukagua miradi, unakuta kwamba mradi unatengenezwa kwa kupitia force account una thamani ya shilingi bilioni tano au shilingi bilioni sita; je, hii ndiyo miradi midogo midogo? Sasa hapa ndiyo shida inapoanza. Kwa hiyo, kuna shida ya msingi ambayo lazima sasa Serikali waweze kukaa kitako na kuweza ku-address hizi issues ili sasa tuweze kuona force account kwa madhumuni yake iliyokuwa imeanzishwa kweli inakwenda kuleta tija ili sasa wananchi waweze kunufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na mapungufu haya yaliyokuwa yameelezwa ya shughuli ya miradi midogo midogo, lakini kuna mapungufu kadha wa kadha ambayo vilevile kwenye Kamati tumeweza kuyaainisha. Miongoni mwa mapungufu ambayo tumeweza kuyaanisha kwenye Kamati, kuna shida kubwa sana ya wataalamu na inashangaza, katika halmashauri unaweza kukuta kwamba Head of the Department yeye ni QS. Sasa unaambiwa sijui mimi siyo engineer, mimi niambie mambo ya namba, debits and credits, lakini unashangaa QS huyo yeye ndiyo anakuwa mtaalamu wa kwenda kukagua majengo. Sasa unapata shida, QS na engineering hivi vitu vinafanana? Ninyi mliokuwa wataalamu katika fani hii mnaweza mkatuambia.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali ifike wakati sasa muweze kuangalia ili miradi ya force account iweze kuwa na tija, lazima muweze kuajiri watumishi wenye sifa ambao kwa namna moja ama nyingine wanaweza wakaisimamia miradi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa kuna shida ya msingi sana, ile accountability inashindwa kupatikana. Leo unakwenda kumlaumu QS kwamba jengo limejengwa chini ya kiwango, lakini yule si engineer, he is just a normal QS. Sasa unashindwa kum-hold accountable, at the end of the day kinachotokea tunarudi kwa Afisa Masuuli. Tunaanza kumbana Afisa Masuuli tunamwambia jengo ni bovu, jengo lina nyufa, kwa nini iko hivi? Lakini kiuhalisia ni kwamba, hatuna wataalamu wa kutosha ambao wanaweza wakasimamia kazi hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo yote, jambo lingine ambalo ni changamoto kubwa sana, zile taratibu za sheria za manunuzi katika mfumo wa force account zinakuwa hazifuatwi. Hii tumeiona katika Kamati na maeneo mengine wakati tunaenda kukagua miradi. Katika mfumo wa force account kuna ile Kamati ya Manunuzi na kuna Kamati ambayo kazi yake ni kupokea vile vifaa, lakini kuna shida kubwa sana nah ii shida hii inatokana na changamoto ya mambo ya kimaslahi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika ofisi za Afisa Masuuli, utakuta wao ndio wananunua vitu in bulk wanavipeleka kule chini. Wale kule wanaenda kuvipokea tu vile vitu. Wanashindwa kuweza ku-verify quality ya vitu vile, lakini wakati mwingine wanashindwa kufahamu mpaka thamani halisi ya vitu hivyo na ndiyo maana unakuta kuna variation kubwa wakati mwingine zinaweza kupatikana katika mradi unaofanyika katika halmashauri X na mradi unakuwa unafanyika katika halmashauri Y, hili ni tatizo la msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo kuna tatizo lingine ambalo tumeweza ku-identify katika taarifa yetu sisi watu wa Kamati ya LAAC. Kuna shida kubwa sana ya msingi hasa katika suala zima la BOQ ambazo zinakuwa zinatolewa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Leo Ofisi ya Rais, TAMISEMI inapokuwa inatoa BOQ ya kusema kwamba darasa moja linakwenda kutengenezwa kwa shilingi milioni 20, hii kitu haiko sawa sana kwa sababu darasa la shilingi milioni 20 linalokwenda kujengwa kwenye Jimbo la Kibiti kule chini Delta, Mbuchi, Kiongoloni au maeneo mengine au ukienda kule Busekera, ni tofauti kabisa na darasa la shilingi milioni 20 linalokwenda kujengwa Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba niishauri Serikali, ni lazima wakati wanafanya BOQ hizi waweze kuangalia tofauti zilizopo za kijiografia kati ya halmashauri moja na halmashauri nyingine na ndiyo maana katika taarifa yetu kuna tofauti kubwa sana za fedha, tatizo ni kwamba unamuuliza Afisa Masuuli unamuuliza kwa nini jengo hili wenzio katika halmashauri fulani wamepewa shilingi milioni 470 wameweza kukamilisha, wewe unatumia shilingi milioni 560, tofauti ni nini?

Mheshimiwa Spika, Afisa Masuuli anaanza kukwambia tofauti ya jiografia, vifaa vinapatikana mbali. Kwa hiyo, vitu hivi wakati mwingine hao Maafisa Masuuli tunawabebesha mizigo. Ofisi ya Rais, TAMISEMI ni lazima sasa muweze kuangalia, wakati mnaandaa BOQ na wakati mnakwenda kupeleka fedha katika halmashauri husika lazima muweze kuzingatia suala zima la kijiografia… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Haya ahsante sana Mheshimiwa, kengele ya pili imeshagonga.

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, oh really?

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Kicheko/Makofi)