Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Simon Songe Lusengekile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami nichangine taarifa za Kamati zetu mbili. Nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anazofanya kwa kuhakikisha kwamba Serikali yetu inapata fedha na zinaenda kwenye majimbo yetu. Pia kipekee nawapongeza Sana Wenyeviti wetu wa Kamati, Kamati yetu ya LAAC pamoja na Kamati ya PAC na Makamu Wenyeviti kwa kazi kubwa wanazofanya na kutuongoza katika Kamati na kuhakikisha kwamba tunaleta taarifa ambayo ni nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nataka nichangie eneo moja tu leo na nataka nichangie usimamizi wa uondoshwaji wa magari Serikalini.
Mheshimiwa Spika, katika eneo ambalo ni pasua kichwa, hili eneo ni mojawapo ya eneo ambalo ni pasua kichwa. Kwa nini nasema hivyo; CAG alifanya ukaguzi wa taasisi nane na kubaini magari zaidi ya 547 yameegeshwa kwa muda wa zaidi ya miaka mitatu. Maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba magari haya tunayaegesha bila mpango wowote.

Mheshimiwa Spika, alivyokwenda TEMESA akakuta magari yote yaliyoegeshwa pale, yaliyopelekwa kwa ajili ya kuegeshwa lakini pia yaliyopelekwa kwa ajili ya matengenezo na mengine yakiwa yanasubiri vibali, asilimia 43 ya magari yote yaliyokuwa TEMESA yamekaa zaidi ya miaka mitatu; sasa yalipelekwa kufanyaje pale? Kwa sababu kama limepelekwa kutengenezwa, linakaa miaka mitatu halijatengenezwa nini maana yake? Kama lilipelekwa kwa ajili ya kusubiri kibali kutoka Wizara ya Fedha, kibali hakijatoka miaka mitatu, nini maana yake? Hapa kuna tatizo kubwa. Ni lazima sasa Serikali ije na mpango, ije na mwongozo wa muda gani utakuwa kwa ajili ya kuegesha magari. Kama ni muda wa wiki mbili, kama ni muda wa miezi miwili gari limeegeshwa, iwe na sababu za msingi kwa nini bado liko pale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna story moja is very interesting; Mkaguzi alienda kukagua Morogoro nafikiri halmashauri mbili, Halmashauri ya Morogoro DC pamoja na Kilosa. Alivyowaambia pale Morogoro DC magari yenu yako wapi, wakasema yako gereji binafsi. CAG akasema nipelekeni, wakampeleka, wakaanza kusema hili la kwetu, hili la kwetu, hili la kwetu. Baadaye kwenye ile gereji binafsi CAG akaona bado kuna gari limeandikwa STK liko pale halina mwenyewe, akashtuka.

Mheshimiwa Spika, alivyoenda Kilosa, Kilosa nao wakasema hatulijui, wakiwa gereji anauliza, hili gari nani alilileta hapa? Yeye anasema hajui. Sasa hii maana yake nini?

Mheshimiwa Spika, CAG alivyoenda Wizara ya Fedha, wakaliangalia kwenye Mfumo wa GAMIS wakagundua lile gari ni la Kilosa, wakati huyo wa Kilosa alikataa gari si la kwake na liko gereji ya mtu binafsi zaidi ya miaka mitano. Implication yake ni nini? Implication yake ni kwamba magari haya tunaya-dump ili baadaye waje wauziane watu kwa bei ambayo ni bei chee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lazima sasa Wizara ya Fedha ije na mpango, i-set muda, ni muda gani, ni wakati gani magari yanatakiwa yaegeshwe na baada ya huo muda yatolewe maelezo kwa nini bado yameegeshwa. Eneo hili la magari kuna baadhi ya taasisi zinauziana magari kwa watumishi, kitu ambacho ni sawa, sina tatizo na hilo; lakini hakuna uwazi, hakuna tangazo linalotolewa kwa watumishi ili waweze kununua gari, unashtukia tu tayari watu wameshauziana na mtu anamiliki gari. Hamna tangazo, hamna chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lazima sasa Wizara ya Fedha ije na mpango, izielekeze taasisi zetu, izielekeze Wizara, izielekeze halmashuri kuwa na uwazi wakati wanataka kuwauzia watumishi magari. (Makofi)

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Lusengekile, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Musukuma.

TAARIFA

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nimpe taarifa mzungumzaji, anachangia vizuri. Ni siku tano tu Halmashauri ya Geita DC walinyang’anywa gari barabarani na mnunuzi aliyeuziwa gari ya Udhibiti Ubora wa Elimu, ikachukuliwa barabarani, watumishi wakashushwa. Ile gari ameuziwa Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora kwa shilingi 1,900,000. Baada ya mimi kuamsha moto kwa Mheshimiwa Mkenda hapa, wameletewa gari bovu la kutengeneza shilingi milioni tano ndiyo liende Geita, nakushukuru mzungumzaji. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Lusengekile, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa anasema na ana uhakika nayo, mimi niipokee, kwa sababu ni sehemu ya maeneo ambayo nilikuwa nataka kuchangia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo hilo ambalo tumeliona kutokuwa na uwazi katika kuuziana magari, CAG amekagua taasisi nane na katika taasisi nane; sita zote hazikuwa na uwazi katika kuuziana magari. Hili ni tatizo kubwa, lazima Wizara ya Fedha ije na mkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni eneo la uthamini wa zile gari wanapokuwa wanaenda kuziuza kwa watumishi. Unakuwa ni wa bei ya chini kama alivyosema sasa hivi Mheshimiwa Musukuma. Unakuta gari ya shilingi milioni 50, ya shilingi milioni 100 inauzwa kwa shilingi 1,500,000, haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati sijawa Mbunge nikiwa nafanya kazi huko Shirati, kuna gari moja nilikuwa naiona pale Halmashauri ya Rorya, gari imekuja mpya, imenunuliwa zaidi ya shilingi milioni 128, imefanya kazi miaka mitatu ikaharibika kidogo tu Wakai-park. Sasa kila siku nikienda pale naikuta, nikaanza kuwaza, what is the problem? Baadaye miaka 10, ile gari imeenda kuchukuliwa, imeenda kuuzwa shilingi milioni nane. V8! Shilingi milioni nane na huyo aliyeenda kutengeneza ametengeneza sijui kwa shilingi milioni tatu au nne. Unajikuta mtu anamiliki V8 ya zaidi ya shilingi milioni 120 kwa shilingi milioni 10. Haiwezekani, ni lazima sasa Wizara ya Fedha waje na mpango, ni kwa namna gani uthaminishwaji wa magari unafuata market value iliyopo kwenye soko, la sivyo tutakuwa tunayarundika magari, yanaharibika kidogo tunayaweka, watu hawayajali, halafu mwisho wa siku Wizara ya Ujenzi inayachukua halafu inaenda kuyauza kwa watumishi kwa bei ambayo si sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mkaguzi alikagua magari 500 na akabaini, katika magari 500 magari nane ndiyo yaliyouzwa kwa bei ambayo iko sawa na soko. Magari 492 yaliuzwa kwa bei chini ya soko na kusababisha hasara kwa Serikali. Ni lazima sasa Wizara ya Fedha ije na mwongozo wa namna gani uthaminishwaji wa magari unafanyika ili kuendana na soko lililopo kwenye soko letu la magari husika, la sivyo haitakuwa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho eneo hili ni ucheleweshwaji wa vibali kutoka Wizara ya Fedha; Taasisi zimeomba vibali vya kuondoshwa magari, lakini wanaomba kuanzia siku 57 – 2,226 bila kibali kutolewa. Sasa unaona kama wao walichelewa kuomba kibali mwaka mmoja au miwili, wanapeleka Wizara ya Fedha nao wanakaa miaka mitano hawajatoa kibali, maana yake lile gari litakaa zaidi ya miaka saba linasubiri kibali. Tunasababisha value for money ya haya magari kukosekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama gari lilinunuliwa lifanye kazi kwa miaka mitano, linafanya kazi kwa miaka mitatu, linaharibika kitu kidogo, wanali-dump miaka 10, halifanyiwi services na hatimaye linakuja kuuzwa kwa bei ndogo halafu muhusika anaenda kutengeneza kwa bei ndogo na inakuwa gari lake. Shilingi milioni 10 anamiliki V8. Hii haiwezekani.

Mheshimiwa Spika, hivyo niishauri sana Wizara ya Fedha, katika Sheria ya Uthaminishaji nafikiri ni sheria Na. 61 kama sikosei, ni lazima sasa waiboreshe, wamhusishe hata Mthamini Mkuu wa Serikali, kwa sababu kinachofanyika saa hizi ni Wizara ya Ujenzi pekee yake, ikishasema hili gari tuliuze kwa shilingi milioni tano sawa, Mthaminishaji Mkuu wa Serikali hausishwi. Kwa hiyo kwenye kuthaminisha magari tunaomba pia Mthaminishaji Mkuu wa Serikali ahusishwe ili tupate value for money ya gari husika ili iweze kuleta tija kwa Watanzania na kwa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. (Makofi)