Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Munde Abdallah Tambwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuchangia ripoti ya LAAC na PAC. Awali ya yote niwapongeze wajumbe wa kamati zote mbili akiwepo Mwenyekiti wangu wa Kamati ya LAAC, Mheshimiwa Halima Mdee pamoja na Wajumbe wake wote kwa taarifa nzuri aliyoisoma hapa leo Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nitajikita kabisa kwenye taarifa ya LAAC, kwenye upande wa force account lakini kabla ya hapo nimpongeze sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ya kihistoria anayoifanya. Hakuna wakati wowote uliyokuwa na pesa nyingi kwenye Serikali hii ya kwetu ya nchi hii hasa kwenye Halmashauri zetu kama kipindi hiki cha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haya yote tunayoyaongelea force account, ma-engineer wachache wa miradi haisimamiwi ni kwa sababu pesa ni nyingi mno Halmashauri na yote hiyo ni juhudi kubwa zinazofanywa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kuwapongeza Mawaziri wanaohusika TAMISEMI ambao wanahusika sana na wanapambana na mambo ya TARURA kwa kuangalia hali ya hewa iliyopo sasa hivi, wanahangaika kadri ya uwezo wao kuhakikisha mambo yanakwenda, nimpongeze Kaka yangu Mheshimiwa Bashungwa, tunamuona huku na huku kwa kazi za dharura kwa ajili ya mvua anapambana sana sana.

Mheshimiwa Spika, pia ni kwa ukweli lazima tumpongeze Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, kazi aliyonayo si kazi ndogo ni kazi kubwa sana. Sisi kama Wabunge kuongea kukosoa tunaona ni rahisi lakini ukiwekwa pale Wizara ya Fedha ni changamoto kubwa, bajeti ipo kamili unakuta kuna mambo yamejitokeza ya dharura, mvua imenyesha daraja limekatika unaambiwa toa pesa, ukiangalia bajeti haipo sawa, kwa kweli tuendelee kuwaombea viongozi wetu, tumuombee Mheshimiwa Rais lakini na Mawaziri wake wote waendelee kufanyakazi vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kutoa pongezi kwa Wakurugenzi wote wa Halmashauri zetu zote. Mabilioni yote ya fedha yanapelekwa kwenye Halmashauri kama kuna ubadhilifu ni watu wachache sana otherwise miradi isingekuwepo, tuwatie moyo Wakurugenzi wetu wa Halmashauri kama kuna mapungufu ni machache na tuendelee kuyarekebisha, lakini tusiwe tunatamka Wakurugenzi wote ni wezi ni jambo baya sana, tunawavunja moyo na wakati kila siku wanasimamia miradi wao. Miradi yote tunayoiona nchini kwetu Wakurugenzi wanahusika kuisimamia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nirudi kuongea kwenye suala la force account, mimi binafsi sipingi force account ni jambo zuri sana lakini uboreshaji wa force account unatakiwa. Mapungufu yake ni mengi na mapungufu yake ni makubwa sana yanasababisha hasara kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, nimepata bahati ya kufanya ziara kwenye Mikoa tofauti tofauti lakini tumesikia taarifa ya Kamati kwamba wametoa mfano, nitolee mfano kwenye Mkoa wangu wa Tabora, kuna miradi 812 lakini kuna ma-engineer 19 tu. Unaweza ukaona pesa ya Serikali inasimiwaje. Kwa hiyo, ubora wa usimamizi kutafuta value for money unakuwa ni mdogo sana kwa sababu hakuna wasimamizi wa karibu. Watu 19 kwa miradi 800 yaani haiingii akilini wataisimamia vipi na yote hiyo ni juhudi za Serikali kutafuta pesa lakini bado tuangalie jinsi force account itakavyofanya kazi ili iwe na manufaa badala ya kuleta hasara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumekuwa tunawaweka walimu wanasimamia, Madaktari wanasimamia, mpaka Manesi unakuta wanasimamia jengo la Serikali lakini kitakapoharibika kitu Mwalimu huyu ambaye hana qualification yoyote ya usimamizi wa hizi kazi anapelekwa Polisi, anasumbuliwa, anaadhibiwa lakini tunasahau hata kuwapa semina kidogo tu za procurement kuwaonesha kwamba hata kamwanga kidogo hatuwapi, tunawakabidhi kazi ambazo hawajazisomea, tunawakabidhi kazi ambazo akipata tatizo kidogo unampeleka Polisi wakati hana hiyo qualification, tuendelee kuboresha force account ikae vizuri, hatuikatai kwamba ni mbaya lakini iendelee kuboreshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, utakuta hata kwenye ziara zetu sisi Wabunge unakuta ni Daktari anasimamia hospitali ya Wilaya pale kuna technician mmoja Wilaya nzima, Daktari ndiyo anasimamia, unakuta kuna kosa kidogo Mbunge anamfokea Daktari, anatetemeka wakiona Wabunge, anafoka sana badala ya kumuelewesha, siyo qualification yake, siyo qualification yake kwa hiyo nenda naye taratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unamfokea kitu ambacho anasema mimi nimeletewa kila kitu na engineer, mimi nilisimamia tu sijui chochote, yaani mpaka unajisikia saa nyingine kwamba tunakuwa tunawaonea hawa viongozi wengine ambao wapo kule kwenye usimamizi. Kwa kweli, unakuta kazi haijaenda vizuri value for money haieleweki yaani unakuwa unasema jamani hivi hela za Serikali zinapotea kiasi hiki! Lakini cha kushangaza kila Mkoa una Ofisi ya TAMISEMI Mkoa, hawa Ofisi ya TAMISEMI Mkoa wanaenda kule chini kuangalia hizi hali? Hapo ndipo tunabaki tunakuwa tunajiuliza lakini kwa kweli force account inabidi iboreshwe iboreshwe zaidi.

Mheshimiwa Spika, unakuta wilaya moja tulienda wodi ya wazazi, kuna hospitali mbili zina wodi ya wazazi. Wodi moja ya wazazi kwenye Wilaya moja fundi amechukua shilingi milioni 41 kujenga tu, lakini kuna wodi nyingine ya wazazi fundi amechukua shilingi milioni 15 kuijenga tu ile wodi, na ni Wilaya moja. Huyu milioni 41 na huyu milioni 15 hiyo ndiyo force account ambayo bado haijafanyiwa marekebisho na inahitaji marekebisho makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mpaka unajiuliza hivi force account zingine ni za watumishi tu wanaweka mafundi wao? Maana itakuwaje wodi moja imejengwa kwa shilingi milioni 15, wodi nyingine inajengwa kwa shilingi milioni 41. Ukiangalia Kanuni ya PPRA ya 2020 kama alivyosema mwezangu kuna Kamati ya Manunuzi na Kamati ya Mapokezi vitu vingi havifanyi kazi kama inavyotakiwa, kwa hiyo niwaombe Wakurugenzi, Waziri aliopo madarakani na Naibu wake wahakikishe taratibu zinafuatwa. Maana yake unaweza ukajiuliza sasa shida ni nini, kwa nini watu hawa hawafanyi kazi kama kanuni zilivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tulienda kwenye Halmashauri moja tulipofika Mkurugenzi akatuita pembeni akasema miradi yote ya hapa inafanywa na Mwenyekiti wa Halmashauri na Naibu Mwenyekiti sitataja lakini Wajumbe wenzangu wanajua, naombeni mnisaidie hali ni mbaya mtu mwingine akipewa wanagoma kila kitu inabidi uwape wao wafanye kazi. Value for money ni mbaya yaani miradi haieleweki, wameweka mafundi watoto wao wa nyumbani kwao, kwa hiyo hivi vitu kwa kweli inabidi visimamiwe sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mkurugenzi huyo ni msichana mdada tu alikuwa umoja wa vijana, alipambana ikatangazwa kazi ya kujenga hospitali ya Wilaya kwa bajeti ya shilingi milioni 500, akatangaza kwa wakandarasi wakaomba. Lowest aliomba kwa milioni 900, Mwenyekiti wa Halmashauri na Makamu wanaitaka ile kazi, yule Dada akamuita mkandarasi akamwambia umeomba kwa 900 mimi nataka nikupe hii kazi kwa 500 unakubali? Wakafanya negotiations pale, yule Mkandarasi akukubali kujenga ile hospitali ya Wilaya kwa shilingi milioni 500, akaona badala nipeleke force account itaenda zikaharibike value for money haitapatikana na mimi nimeanza kazi juzi tu ni bora nipate lawama za Mwenyekiti wangu wa Halmashauri lakini jambo liwe salama, akampa Mkandarasi kwa shilingi milioni 500.

Mheshimiwa Spika, nataka kusema kwamba ifike sehemu hawa Wakandarasi sometimes aitwe mkae naye mfanye negotiations, akikubali kupunguza bei kwa bajeti yenu mliyonayo basi ni vema achukue hii kazi Mkandarasi kwa sababu, moja atalipa kodi ya Serikali lakini mbili asipofanya value for money mnahaki ya kumshtaki na ana haki ya kurudia ile kazi mara mbili mpaka pale ninyi mtakaporidhika. Kwa hiyo miradi ile mikubwa ni vema waichukue Wakandarasi.

MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ile miradi mikubwa nilisema waichukue wakandarasi wakubwa na miradi ya kawaida hatukatai…

SPIKA: Mheshimiwa Munde kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Charles Kajege.

TAARIFA

MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, nashindwa kumuelewa mzungumzaji mara anasema hiki mara kile, sasa atupe msimamo wake je, anaikubali force account au hapana? (Kicheko)

SPIKA: Mheshimiwa Munde kuna taarifa hiyo iliyokuja kwa sura ya swali unaikubali? (Kicheko)

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, kwanza siipokei taarifa yake kwa sababu hasikilizi Bunge, nadhani ana-chat huko nimesema force account siikatai lakini iboreshwe, ndivyo nilivyoongea aangalie Hansard itamuelewesha. Mnakuja hapa mna-chat halafu mnakuwa mnatupotezea dakika zetu. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

SPIKA: Mheshimiwa Munde, hayo ya ku-chat yaondoe, hayo maneno ya ku-chat, Mbunge alikuwa anasisitiza tu.

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, nimefuta maneno ya ku-chat, Mbunge hakuwa ana-chat humu ndani. (Kicheko/Makofi)

Mheshima Spika, napenda niishauri Serikali Wakandarasi wengi wanatabia ya kupandisha bei mara mbili zaidi lakini atakapopandisha bei ukamuita ukakaa naye ukafanya negotiations kwamba kazi hii bajeti yake shilingi milioni 500 kama atakubali kufanya basi ni vema afanye Mkandarasi kwa pesa iliyopo pale.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo napenda niliongelee ni ramani au BOQ za TAMISEMI. Mimi kwetu nilipozaliwa Baba yangu alijenga nyumba kabla sijazaliwa miaka mitano au sita toka umri wangu huu niliyofikia, nyumba hiyo bado ipo. Nyumba yenyewe inazege pale kwenye madirisha, pale kwenye milango ndiyo imewekewa mkanda siyo mkanda wa kuzunguka nyumba nzima, ile nyumba mpaka leo ipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama ulibahatika kuona BOQ ya zahanati msingi wake unaweza ukajenga ghorofa tatu, yaani nondo ni nyingi unashangaa zahanati ni kijumba cha kawaida tu why pesa zote hizo mnazilundika chini karibia shilingi milioni 10, milioni 20, milioni 30 zinaenda chini kwa nini? Kwa nini zahanati moja unaweza ukatoa zahanati moja na nusu, msingi wake unakuwa strong ambao unaweza kujenga gorofa tatu, mimi sioni faida yoyote kama nyumba ya kawaida tu inaweza ikaishi miaka 70 hiyo nyumba ambayo ni ya kitaalam ikiishi miaka 150 si inatosha? Kwa hiyo naomba TAMISEMI waziangalie upya BOQ zao. BOQ ukiiangalia ya zahanati unaweza ukacheka sana, unaweza ukashangaa kwa nini wanafanya namna hiyo. Nondo ni nyingi mno ambazo zinasababisha unaweza ukajenga gorofa tatu kwenda juu.

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa kengele ya pili tayari.

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)