Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Venant Daud Protas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igalula

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwanza na mimi nianze kwa kuunga mkono hoja za Kamati zote mbili, naunga mkono hoja ya Mwenyekiti wangu wa Kamati ya PAC, Mama yangu amewasilisha hoja vizuri na sisi kama Wajumbe tulikubaliana hiyo hoja kwa niaba ya Bunge zima, kwa hiyo naamini yale tuliyoyashauri kwenye upande wa Serikali yatafanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme jambo moja, Serikali ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kipindi hiki hakuna Serikali ambayo iliwahi kushusha fedha kama Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, hakuna anayebisha mpaka mtoto mdogo ameguswa na fedha ya Serikali yetu ya Mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, fedha hii pamoja na kushushwa kwa wingi Mama kazi yake ameimaliza, imebaki sasa sisi ambao tumepewa dhamana ya kwenda kusimamia ibadilishwe kuleta matokeo ili mwananchi wa kawaida aweze kuona matunda na yale tunayosema fedha zimeletwa za Mama Samia, aweze kuona matokeo mazuri. Ninayasema haya kwa sababu gani?

Mheshimiwa Spika, leo tuna miradi ya REA kwenye maeneo yetu, Mheshimiwa Rais ameelekeza vijiji vyote vifikiwe na nishati ya umeme, hilo nampongeza na mimi nilikuwa katika Jimbo langu la Igalula katika vijiji 58 nilipokuwa naingia 2020 vilikuwa havina nishati ya umeme vijiji 46 na leo niwaambie vijiji vyote vimepelekewa miundombinu ya nishati ya umeme, hiyo ni kazi kubwa ambayo imefanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na kupelekewa nishati ya umeme bado kuna changamoto. changamoto mojawapo iliyopo lengo na madhumuni ya Mheshimiwa Rais ni kuona matokeo yanatokea lakini ukiangalia tunapeleka mabilioni ya fedha kwenye miradi hii haiwezi kwenda kuonekana kwa uhalisia kwa sababu aidha wataalam wetu walisinzia wakatoa ushauri mbaya na leo tunakwenda kufanya mradi uleule tunakwenda kuingiza Taifa hasara kwa kupeleka kazi kufanyika mara mbilimbili, kwa sababu gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo tunapeleka umeme kwenye vijiji, kijiji ambacho kilitakiwa kifungwe transformer ya KV kuanzia 200 tunakwenda kupeleka KV 50 wateja wanaohitajika kuonganishwa zaidi ya 300 kwenye kijiji kimoja mnaweka limit ya wateja waunganishwe chini ya 20 kwa transformer moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa mimi najiuliza huyu mtaalam alikuwa anapiga hesabu alifika huko au aliandikia kwenye ofisi? Kama aliandikia kwenye ofisi hawa watu wa TANESCO waliopo huko kwa nini hawajashauri? Leo miradi ya REA yote sasa hivi wamekaa Wakandarasi wanasubiri muda wao uishe, mzigo utupiwe TANESCO, TANESCO wakipewa tu wanaanza kufyatua tena katoa transformer hii kaipeleka chumbani, kaleta transformer nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama tungeweza kutatua mapema haya mambo ya kufanya kazi mara mbilimbili yasingeweza kutokea. Kwa hiyo, mimi niombe tunakwenda kuweka umeme kwenye vitongoji kwenye bajeti ijayo, mfanye tathimini na uhalisia wa maeneo husika. Kwa mfano, mimi hapa kwenye Wilaya yetu ya Uyui walitakiwa waunganishwe wateja 6,120 mpaka leo tumeunganisha wateja 1,357. Sasa ukiangalia huyu Mkandarasi mkataba wake uliisha mwezi wa Disemba, 2022 na sasa hivi tumemuongezea muda sijui unaisha mwezi Juni, amebakiza miezi minne aondoke. Mtamuona TANESCO kaja na magari ya Serikali anaanza kubadilisha tena, kwa hiyo tuombe hayo mambo yawekwe sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuchangia hiyo lakini na mimi nirudi kwenye fedha zinazokwenda hasa kwenye force account. Mimi hapa nilikuwa nataka nishauri jambo moja, force account imetusaidia sana wananchi na hasa sisi Wabunge ambao tunatoka vijijini imetusaidia sana, lakini force account inatakiwa ikafanyiwe assessment nyingine tujue kwenye force account wangapi wamekufa kwa sababu ya force account, wangapi wameugua presha kwa sababu ya force account, nasema haya kwa sababu gani?

Mheshimiwa Spika, tumepeleka miradi huko leo Daktari kawa engineer wa majengo, Mwalimu kawa engineer wa majengo, mtu amesoma baiolojia, amesoma auguze watu sasa hivi anashinda madukani kununua cement na nondo, hiyo kazi haikumpeleka kule, lakini leo mtu badala ya kutibu wagonjwa au kufundisha anakazana kulinda pale msumari na cement zisiibiwe kwa sababu zikiibiwa anakuja kushughulikiwa yeye. Kwa hiyo, tunatakiwa tufanye modality nzuri ili hawa watumishi wetu tuwasaidie waweze kufanya kazi zao. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo tunasema tumesaidia kuleta force account lakini tumeleta majanga kwa baadhi ya watu. Leo watumishi wanaandika barua ya kwenda kusoma hata kabla ya muda kwa sababu wakimbie hizi adha. Kwa hiyo, mimi nataka nishauri Serikali kama tunaisaidia kweli Serikali, force account ni nzuri tuiwekee utaratibu mzuri ili iweze kusaidia namna gani ya kutekeleza majukumu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii force account hizi BOQ zinazokuja kutoka TAMISEMI, hivi BOQ inakwambia ufunge beam tatu kutoka chini, katikati, uende kwenye madirisha na uende mwisho. Hivi kule kuna matetemeko ya ardhi? Hawa wataalam wamesomea wapi? Leo tumejenga madarasa ambayo tungeweza kujenga shule mbili kwa shule moja, tunakwenda kulaza tofali la nchi sita tofali tunalaza, kuanzia chini mpaka juu. Sasa hebu tujiulize tulishapata matetemeko madarasa yakaanguka? Je, kwa nini kwenye shule ‘A’ tunalaza, shule ‘B’ hatulazi, kule hakuna watoto? Hivyo, wataalam wetu watusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa napata maajabu, hii force account kuna watu hapa wameshaanza kuiga force account hata kwenye Wizara zingine. Leo Wizara ya Mifungo tena imekuja na yenyewe na force account kujenga kwenye majosho. Sasa force account ya kwao bora hii ya TAMISEMI, wao sasa anayelipa anakaa Dodoma sijui Dar es Salaam Makao Makuu, fundi yupo kijijini, anaandika invoice hajui hata anampelekea nani, na yule pale anampelekea watu wa Wilayani nae anasema nimetuma kule kwa wakubwa. Huyu mkubwa ni nani? (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaomba Waziri wangu wa Mifugo, force account imekushinda rudisha hela kwenye Halmashauri, kuna watu wanakudai mpaka saa hizi nikutajie majina na uwalipe. Kwanza, kuna huyu mtu mmoja anaitwa Gita Dotto Malema anadai shilingi 1,400,000 fundi huyo ambaye tulitakiwa tumsaidie, halafu kuna mwingine Noel Jumanne anadai shilingi zaidi ya shilingi milioni moja tangu mwaka 2022 hajalipa kisa force account, naye sijui alikuja hajafanya utafiti wa force account ikaletwa hivyo.

Mheshimiwa Spika, sasa baada ya kumkera zaidi nikamtumia meseji nikamwambia Mheshimiwa Waziri, hebu nisaidie hawa watu wanadai kwa muda mrefu wamekopa huko fedha ili waweze kulipwa, Waziri akamtumia mtaalam wake Wizarani jibu alilokuja kumrudishia akamwambi Mheshimiwa Waziri hilo deni kweli lipo Wilaya ya Uyui na huyo Ndugu Noel tumelifuatilia kwa ukaribu sana lakini wakati tunataka kulipa badala tumlipe Noel wa Uyui, tukamlipa Noel wa shamba gani sijui wapi huko, akalipwa mtu mwingine. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, sasa ukija kuangalia, hao akina Noeli pamoja na kuwa labda majina yamefanana, walikuwa na amount sawa? Hawa Wahasibu huko Wizarani wanafanya kazi gani? Noeli sawa, majina yamefanana, hatukatai; na amount zimefanana? Haya huyo mwananchi amekuja kuniambia mimi. Nimeweza kufuatilia, nimekutana na kisanga hicho. Yule ambaye hana connection fedha yake inakwenda wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii Force Account ichunguzwe na yenyewe. Leo tunaletewa Force Account inakuja BOQ, inakwambia kabisa nenda ukanunue bati namba fulani kwa fulani. Kumbe kule sijui wameshaweka ten percent! Wanatuambia mabati tukanunue ALAF, tena na namba wanakupa kabisa, wanakupiga pin, namba fulani. Zikaanza kupita harambee huko, changisha kama mabakuli, wewe peleka huko utakuta mgao wako umechelewa. Wakalundika fedha yote ALAF. ALAF mwenyewe akakosa kuzalisha, miradi ikachelewa. Kwa hiyo, lazima tuweke strategy ya kusaidia. Fedha zimekuja, lakini inakuwa ni kero. Mheshimiwa Rais, anataka aone matokeo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naunga mkono Kamati zote mbili, Force Account ni nzuri, lakini sisi kama Wawakilishi wa wananchi tuweze kuisaidia Serikali ili azma ya Mheshimiwa Rais ilete matokeo kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)