Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana nami kupata fursa hii ya kuchangia taarifa za Kamati zetu hizi mbili.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa jinsi ambavyo ameendelea kumimina fedha nyingi kwenye Majimbo yetu ili kutekeleza miradi mbalimbali ambayo inawagusa wananchi wetu moja kwa moja.

Mheshimiwa Spika, pili, nampongeza Mheshimiwa Rais, kwa jinsi ambavyo aliipokea Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, mwaka jana 2023 mwezi wa Tatu. Alionesha sura ya uchungu kulingana na mambo ambayo yalikuwa yameonekana ndani ya ripoti ile. Alitoa maelekezo ambayo mengi yamesaidia Serikali kufanya marekebisho mengi ya hapa na pale ambayo yamesaidia sana kuboresha maeneo mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze GAG kwa taarifa ambayo ameendelea kuifanyia kazi kwa mujibu wa Ibara ya 143 na Ibara ya 144 ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania; na amekuwa anatoa ushauri, maoni, mapendekezo ambayo yamekuwa yakisaidia sana nchi hii kuweza kuthibiti maeneo mengi tu ya matumizi na kuboresha utendaji Serikalini.

Mheshimiwa Spika, tatizo kubwa ambalo tunalo katika nchi yetu ni kwa watendaji kuwa na mwendokasi mdogo sana katika kutekeleza mapendekezo, maoni na ushauri wa CAG. Tukirekebisha hapo mambo mengi yatakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, miongoni mwa taarifa za ukaguzi ambazo tulizijadili kwenye Kamati ni pamoja na ukaguzi wa ufanisi katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu SDGs. Tumepitia Taarifa ya CAG na kwa kweli katika taarifa ile unaweza ukaona kwamba ufanisi wetu katika kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu bado ni mdogo; na hautuhakikishii kwamba ifikapo mwaka 2030 tutafikia malengo ya maendeleo endelevu kama ilivyopitishwa na Umoja wa Mataifa.

Mheshimiwa Spika, nasema hivyo kwa sababu gani? Miongoni mwa sababu ambazo zinaonesha kwamba tuna kasi ndogo katika kuelekea kuyafikia malengo ya maendeleo endelevu ni pamoja na sisi wenyewe ndani hapa kama nchi kushindwa kukusanya mapato ya ndani ambayo tulikuwa tumeyabainisha wenyewe kwamba haya tutayakusanya.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2016 katika mikakati yetu tulikubaliana kwamba tutaanzisha vyanzo vipya vya mapato ambavyo ni dhamana za manispaa au municipal bounds, dhamana za uraia na uhamiaji, dhamana za hifadhi za mazingira, udhamini wa msongamano au cloud financing, miradi ya mfuko wa fedha, mifuko ya maliasili na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, hadi sasa Serikali haijajipanga namna ya kukusanya vyanzo hivi vya ndani ili viweze kutuongezea mapato ambayo yatasaidia kwenye utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu. Sasa kama hatuna rasilimali fedha hii inatishia uwezo wetu wa kufikia malengo ya maendeleo endelevu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni kuwa hatujawasaidia wananchi wetu kikamilifu ili katika juhudi zao za kujiletea maendeleo na katika juhudi zao za kupambana na umasikini waweze kujikwamua na kulisaidia Taifa. Hivi ninavyozungumza wananchi wanashukuru sana. Tuliwapatia mbolea ya ruzuku kama sehemu ya mkakati lakini nakuhakikishia kwenye jimbo langu zaidi ya asilimia 60 ya mbolea iliyowekwa ardhini imeoshwa na maji ya mafuriko. Hatujawa na mkakati wa kuwasaidia wananchi namna gani sasa watajikwamua ili waweze kupata mazao ya chakula mwaka huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, wakulima wa tumbaku wamelima tumbaku mpaka nyuma ya nyumba. Maeneo mengi wamelima tumbaku kwa sababu wamevutiwa na bei ya tumbaku nzuri ya mwaka jana. Lakini mvua hizi za mafuriko zimesababisha tumbaku nyingi sasa imeharibika katika mashamba. Hatujawa na mkakati wa namna ya kuwasaidia wananchi wetu kujikwamua na tatizo hilo.

Mheshimiwa Spika, lakini la tatu, asilimia 60 ya mabanda ya kukaushia tumbaku yameangushwa na mafuriko. Hatujawa na mkakati wa kuwasaidia wananchi namna gani wanajikwamua na tatizo hilo, na hii ni hasara inayotokana na kwamba hatuna bima ya wakulima, yaani Tanzania hatujawa na bima ya wakulima (bima kwenye kilimo) kwa hiyo, akipata hasara anapata hasara mazima. Kwa hiyo jambo hili hatuwezi kupata maendeleo endelevu kama hatuna mikakati ya namna ya kuwasaidia wananchi wetu wajikwamue na matatizo ya natural hazards ambayo yanakuja kuwasababishia hasara kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nilitaka niliseme katika ukaguzi huu wa ufanisi wa maendeleo endelevu ni eneo la takwimu. Ili nchi iweze kujipima, lazima tuwe na mkakati mzuri wa kuratibu uzalishaji wa takwimu, uchakataji na upelekaji wa takwimu kuanzia ngazi za chini mpaka ngazi za juu. Tuna aina mbili ya takwimu hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, aina ya kwanza ya takwimu ni takwimu za sensa na utafiti. Hizi zinakusanywa na NBS (Ofisi ya Takwimu ya Taifa), lakini aina ya pili ya takwimu ambayo ndiyo kubwa zaidi ni takwimu za kiutawala. Zinakusanywa na Ofisi za Vijiji, Kata, halmashauri mpaka inakuja Serikali kuu.

Mheshimiwa Spika, takwimu za sensa na utafiti ni asilimia 39 tu ya takwimu zote; na takwimu wa kiutawala ni asilimia 91. Tatizo kubwa ambalo lipo hapa nchini ni kwamba takwimu za utawala ambazo zimekuwa zinachakatwa, zinazalishwa na kuchakatwa na kuletwa huku juu ni asilimia 28 tu takwimu zote hizo asilimia 61. Kwa hiyo, ina maana kuna zaidi ya asilimia 30 ya takwimu ambazo hazikusanywi wala kuchakatwa. Hili linamfanya Mtakwimu Mkuu wa Serikali akose namna nzuri ya kuweza kuchakata takwimu zote za kitaifa ili aweze kushawishi vizuri Serikali mipango ya maendeleo. Namna hii hatuwezi kuratibu vizuri namna ya kuyafikia maendeleo endelevu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukaguzi mwingine wa ufanisi ambao ningependa kuujadili hapa ni ukaguzi wa ufanisi katika ujenzi wa barabara za lami nchini. Ukaguzi huu umeonesha kuna ufanisi mdogo katika usimamizi wa mikataba ya ujenzi wa barabara na ndiyo maana barabara nyingi zimekuwa zinaharibika ndani ya muda mfupi.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya consortium kubwa ya kimataifa ya tathimini za ujenzi wa barabara duniani ambayo inaitwa DC Parking Lot International, barabara ya Asphalt yaani hiyo lami aina Asphalt, iliyojengwa vizuri inatakiwa kudumu kwa muda wa miaka 25 bila matatizo makubwa. Katika miaka mitano ya kwanza inatakiwa isiwe na matatizo kabisa. Katika miaka 5 hadi 7 ndiyo kunaweza kukaanza mipasuko midogo midogo inaweza kuzibwa kwa urahisi. Katika miaka 7 hadi 15 mipasuko na vishimo vidogo vinavyoweza kuzibwa kwa urahisi vinaweza vikatokea. Lakini miaka 15-25 ndiyo utahitajika ukarabati wa gharama kubwa.

Mheshimiwa Spika, sasa hapa Tanzania barabara zipo nyingi tu na mifano ipo ambayo inaonekana kabisa kwamba ndani ya miaka mitano barabara inahitaji ukarabati mkubwa ambao tungehitaji baada ya miaka 15-25. Mfano wa barabara ya Manyoni - Tabora tayari ina mashimo makubwa, ina maana tayari inahitaji ukarabati mkubwa lakini haina miaka minne.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hili jambo linahitaji kuangaliwa kwa ukaribu sana ili tuendelee kuhakikisha nchi yetu inapata maendeleo makubwa ambayo tunatarajia. Kwa hiyo, ni lazima maafisa Masuhuli wazingatie ufanisi…

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: …sheria ya ununuzi, wawe wazalendo na mimi katika hili…

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa muda wako umekwisha.

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: …ningependa kusisitiza kabisa kwamba uzalendo ni kitu cha muhimu sana kuliko kusema tu tumetekeleza tumefanya hivi.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)