Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia kwenye Taarifa za Kamati zetu mbili. Kipekee kabisa niwapongeze Wenyeviti wa Kamati kwa taarifa zao nzuri, na Bunge kazi yetu kuamua Kamati zimefanya kazi, zimeleta, zimepika, wengine LAAC tunakaa mpaka saa sita usiku tuje tulete maoni ya kusaidia Taifa letu kwa sababu tuna nchi moja tu Tanzania ya kuishi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye suala la Force Account. Kabla ya kuanzisha wazo la Force Account kulikuwa na misingi, taratibu, kanuni na miongozo mbalimbali, lakini pia kulikuwa na malengo ambayo tulikuwa tunatarajia tuyafikie kutokana na Force Account. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, moja ya malengo ni kuwe na miradi yenye ubora, kupunguza gharama, kumaliza miradi kwa wakati. Waheshimiwa Wabunge lazima tujiulize kwa hali ilivyo na ripoti ya Kamati tuliyowaletea ambayo ni sample tu ya baadhi ya halmashauri, tumefikia malengo tuliyojiwekea? Kama hatujafikia tunahitaji tufanye nini kuokoa mabilioni ya shilingi yanayoenda kwenye halmashauri na mwisho wa siku hatupati matokeo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, moja ya eneo la msingi ukienda kwenye miongozo ya TAMISEMI yenyewe, miongozo ya Force Account, ukienda kwenye Sheria ya PPRA moja ya issue ya msingi ambayo imesisitizwa kwenye Force Account lazima tuwe na wataalam wa kutosha kwa lengo la kuleta ufanisi na ubora wa majengo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa GAG naye alifanya ukaguzi wa ufanisi kwenye miradi ya Force Account na ametuambia kwamba wataalamu waliopo kwenye eneo la ujenzi, wahandisi, wasanifu majengo wapo 213. Wanaohitajika ni 859. Hivi kweli kwa idadi hii na mabilioni ya shilingi yanayoenda kwa wataalamu hawa wenye kusimamia miradi ya mabilioni ya shilingi, kutakuwa na ufanisi kweli? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baadhi ya wajumbe wamechangia hapa. Wametoa mfano, Namtumbo wahandisi wawili, wakadiriaji majengo mmoja, msanifu majengo mmoja. Idadi ya miradi ni 143. Kilwa, wahandisi ni wanne, mkadiriaji majengo mmoja, wasanifu majengo sifuri, miradi 157. Nzega - DC, mhandisi mmoja, mkadiriaji majengo mmoja, wasanifu majengo wawili, miradi 115. Mtwara - DC, wahandisi wawili, mkadiriaji majengo mmoja, wasanifu majengo sifuri, miradi 103. Force account, mabilioni ya shilingi, idadi ndogo namna hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna mwongozo wa mwaka 2019 unaoleza ni namna gani majengo ya Serikali yaweze kuishi muda mrefu. Sasa kwa idadi hii ya wataalamu tumepita kwenye majengo ya bilioni za shilingi, shule inaisha, haijaanza kutumika kuta zina nyufa. Darasa limemalizika halijaanza kutumika, ukitembea na high heels unatoboa sakafu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeambiwa hapa kwenye mwongozo wa Wizara ya Fedha maana huku nako kuna kitengo cha mali za Serikali. Wanasema; “Ukijenga nyumba ya makazi inatakiwa iishi kwa miaka 50.” Tujiulize Waheshimiwa Wabunge, kwa mradi huu wa force account kuna nyumba itakayoishi hapa miaka 50? (Makofi)

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Taarifa inatokea wapi? Mheshimiwa Esther Bulaya kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Stella Fiyao.

TAARIFA

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nilitaka kumpa mzungumzaji taarifa kuwa kiukweli hii hali inatuletea hasara kubwa sana kwenye halmashauri zetu. Mfano mzuri ni kule Momba, shule imejengwa ina mwaka mmoja lakini imeshachanika nyufa kutoka kwenye msingi mpaka juu. Kwa hiyo, hali ni mbaya sana, hii kitu inatuletea hasara sana kwenye halmashauri zetu.

SPIKA: Mheshimiwa Esther Bulaya unapokea taarifa hiyo.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, naipokea. Tumeambiwa kwenye nyumba za makazi tunajenga nyumba za waalimu, imekamilika imenyesha mvua paa linaondoka, kuna nyumba ya kukaa miaka 50? Tunaambiwa shule ikae miaka 75 kwa shule ambazo zinajengwa na fundi mchundo, kuna shule ya kukaa hapa miaka 75? Tunaambiwa hospitali ikae miaka 60, hakuna engineer, hakuna fundi mchundo. Kuna hospitali hapa ya kukaa miaka 60? Tunapeleka mabilioni ya shilingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini tunasema lengo hapa ni upunguza gharama, kuna pesa hapa zimeenda. Ukiona Mtama ijengwe pale shule miliioni 470 wenyewe wameongeza milioni 56 si lengo kupunguza gharama Force Account. Milioni 56 wanahitaji kukamilisha milioni 129 jumla ya mradi utagharimu milioni 655. Haya ukienda Nachingwea, 470 wameongeza 46 wanahitaji milioni 191 shule itagharimu milioni 718. Waheshimiwa Wabunge hatupingi ongezeko la gharama, lakini lazima liendane na hali halisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile hawa wakurugenzi wamekuja kwenye Kamati, tumekutana na mambo wenzenu, unamwambia tuambie ongezeko la nini? Hana justification ya ongezeko la gharama. Force Account, ndiyo maana tunasema, na ndiyo maana kuna mambo yanasemwa kuna cheni ya ulaji kutoka Wizara ya Fedha, kutoka TAMISEMI na kuja kwenye halmashauri. Ukimuomba mkurugenzi nipe BOQ mwingine hakupi mpaka umtishie kumfukuza kwenye Kamati. Force Account. Miradi mikubwa yote ni mibovu lakini ukienda kwenye ukarabati wa darasa unakuta hauna shida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lazima tujipange, lazima tuone tulipoanguka. Tuwe na uchungu na fedha za walipa kodi. Nilikuwa naangalia hapa, Kamati ya PAC ni aibu, hivi magari kweli yanaweza yakawa dampo? TAMESA magari 547 na Serikali hii inapenda mashangingi, inapenda VX, inapenda Land cruiser zile hard top. Hivi nani anaweza akaacha gari yake gereji miaka miwili? Tunaona pesa hazina wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hizi pesa ambazo zimekaa kule TEMESA, magari 547 is not fair, ni nchi ni moja tu. Halafu kila siku wanaongeza idadi kule, halmashauri wanaomba hawana magari, kuna gari zimekaa pale kweli? Ndugu zangu tuna nchi moja tu inaitwa Tanzania, nzuri ya kuishi. Tunahitaji maamuzi, tunahitaji tuone huruma na fedha za walipakodi, wakati tunawaongezea kodi hizi pesa wanazozitoa ziende zikalete tija kwenye halmashauri zetu. Lazima tutimize wajibu wetu, tuwe na uchungu wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante, nakushukuru. naunga mkono hoja. (Makofi)