Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Geoffrey Idelphonce Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Masasi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. GEOFFREY I. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii kukushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia na kipekee nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema, lakini pia niweze kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali yake ya Chama Cha Mapinduzi ambayo inafanya kazi kubwa kule Masasi kwenye jimbo langu, lakini pia na Tanzania kwa ujumla. Tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu waweze kuwa na afya njema, tuweze kuyafanya mengi kuelekea mwakani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kuunga mkono mapendekezo yaliyoletwa kwetu na Wenyeviti wa Kamati zote mbili; Kamati ya PAC na Kamati ya LAAC. Ni mapendekezo muhimu ambayo tungeomba sana sana Bunge tuyabebe, lakini pia na wenzetu wa Serikali tukishaazimia hapa yakafanyiwe kazi, na isije ikaonekana kwamba wakati wote kazi yetu ni kutoa mapendekezo halafu wanafanya kazi asilimia 40, 42 au 48 na baadaye kusema kwamba utekelezaji unaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nayasema haya kwa sababu kiukweli nchi yetu ni tajiri sana. Tunazo rasilimali fedha, lakini utumiaji wa hizo fedha ndiyo imekuwa ni changamoto.

Mheshimiwa Spika, ukaguzi huu wa ufanisi ambao umefanywa ni sehemu tu ya maeneo mapana ya matumizi ya fedha, na sampuli ya ukaguzi wake haifiki hata asilimia 10.

Waheshimiwa Wabunge, hiki mnachokiona hapa ni maeneo machache sana ambayo yamekaguliwa. Tungekagua nchi nzima kwenye taasisi zote hali ingekuwa ni mbaya zaidi. Natamani ifike wakati hata sisi Kamati ya Bunge ya PAC au Bunge lako, tuweze kufanya tathmini ya kiwango halisi ambacho kimepotea kwa matumizi ambayo hayajaenda vizuri.

Mheshimiwa Spika, napenda kijielekeza kwenye maeneo kadhaa, na nisingependa kueleza kwa undani sana kwa sababu Wenyeviti wamezungumza ila nataka nitoe msisitizo tu kwenye yale mapendekezo ambayo yametolewa na viongozi wetu hasa Wenyeviti wa Kamati, lakini pia na ushauri kwa wenzangu upande wa Serikali.

Mheshimiwa Spika, la kwanza tumeona, tunasema maji ni uhai na kupitia Ilani ya CCM tuna lengo la kupeleka maji kwa wananchi wote. Tumeona hapa kuwa ukaguzi wa ufanisi uliofanywa kwenye uendelezaji na matengenezo ya miradi ya maji una changamoto nyingi. Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati yetu ya PAC amezungumza sana hapa, lakini pia tumekuja kubaini kwamba kuna tatizo kubwa sana la mipango kutokuwa kamilifu. Mipango yetu siyo comprehensive, tunafanya nusu nusu kwa miradi midogo midogo mingi kwneye nchi teyu matokeo yake tunatumia fedha nyingi, lakini pia na usimamizi unakuwa ni shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kusisitiza wenzetu wa Wizara waweze kubeba haya mapendekezo, lakini pia ningependa kutoa ushauri kwao; kwanza, ifanye tathmini ya dhati kabisa juu ya utendaji wa mamlaka hizi ambazo zinasimamia uendelezaji na usambazaji wa maji mijini na vijijini.

Pili, taasisi za Serikali zinadaiwa shilingi bilioni 31.7 hazijalipa bili za maji; hivyo, kuzifanya hizi taasisi ambazo zinasimamia usambazaji wa maji kupata shida kwa sababu bajeti yao sasa inakwazwa kwa sababu taasisi za Serikali ni nyingi na zinatumia pesa nyingi sana. Napenda kumuomba sana Mheshimiwa Aweso, Waziri wa Maji, hebu atuambie hapa ikiwezekana atoe agizo kufikia tarehe 1 Julai, taasisi zote za umma zifungiwe prepaid meters ili kusiwe tena na hili tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la tatu, tumeona tuna miradi mingi ya kutengeneza umeme kwa kutuma maji. Sasa badala ya kuwa na miradi mingi midogo midogo ya kuchimba maji hapa na pale kwa nini tusitumie maji yanayotoka kwenye turbines zinazozalisha umeme na kuelekea baharini kwenda kupotea, kwa nini tusiyatumie yale maji kuya-tap na kuyapeleka kwa wananchi. Tutakuwa na miradi michache, mikubwa ya uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, Bwawa la Mwalimu Nyerere ambalo ni kubwa mno, lile bwawa ukubwa wake ni takribani kilometa 100. Ni bwawa kubwa mno, maji ni mengi, yakishatoka pale, yamezungushwa kwenye turbines na kuzalisha umeme yanaenda baharini, yamepotea.

Mheshimiwa Spika, mimi ninaomba Wizara ya Maji na Wizara ya Nishati wangeweza kufanya kazi pamoja, pale ambapo pana mradi wa maji basi yale maji yakishatumika kwenye kutengeneza umeme, yaweze kuchukuliwa na kupelekwa kwa wananchi. Sisi watu wa Mtwara na Lindi tungetamani sana yale maji ya Rufiji ambayo ni mengi sana, ufanyike usanifu tuweze kupata design ya mradi wa maji ili maji mengine yaelekee upande wa Lindi na Mtwara na mengine waende Dar es Salaam ili kuweza kutatua changamoto, kuliko kujielekeza kwenye miradi midogo midogo ambayo tuko nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tulipata taarifa kutoka kwa CAG juu ya ukaguzi uliofanywa kwenye vituo vya afya vya hiari na binafsi, hizi charitable organizations pamoja na hizi private health facilities. Kwa kweli vituo 518 vilikaguliwa na yalibainika mambo mengi. Kwanza, ni asilimia 18 tu ya vituo ndivyo vilionekana vina vyota tatu kwa kuwa vina facilities za msingi za kumhudumia mwananchi. Pia Baraza la Famasia inaonekana halikufanya mapitio ya miongozo yake kwa sababu kwenye vile vituo kunakuwa na famasi na maabara. Kwa hiyo, zile mbili huwa zinasimamiwa, ili tusipate kesi ambazo tumeziona karibuni hapa kwamba ukienda kwenye maabara za mitaani, lazima uandikiwe UTI, Typhoid, H.Pylori na kila kitu ili utoke pale na dawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukaja kuona kwenye ukaguzi ule kwamba asilimia 32 ya leseni ambazo zilikuwa zinasimamia maabara na famasia zilikwisha muda wake, kwa hiyo, hata kupitia vile vigezo vya msingi vya usajili vilikuwa vimeshapitwa na wakati. Vituo 65 vya maabara vilivyokaguliwa ambavyo ni sawa na asilimia 49 vinaonekana kwamba havina wataalam wa kutosha.

Mheshimiwa Spika, sasa kwangu mimi naona kama haishangazi kuona sasa kila familia kuna mgonjwa wa kansa na kila familia kuna mgonjwa anahitaji matibabu ya figo na hasa hii ambayo juzi Mheshimiwa Naibu Waziri alizungumza hapa kuhusu kusafisha figo (dialysis). Sasa hivi dialysis ni fashion, tunahangaika kununua vifaa, haturudi nyuma kuangalia ni nini kimesababisha sasa magojwa ya figo kuwa ni mengi na magonjwa ya kansa kuongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi ninaomba Serikali mrudi kwenye utafiti, mkafanye very scientific research kwamba sababu ambazo zinatumika kwa sasa kuelezea hoja za kuongezeka kwa tatizo la kansa na figo ni nini. Mimi naona ni utumikaji wa madawa kiholela. Ningeweza kuwashauri sana Wizara, wenzetu kule Ujerumani, hizi health facilities zote pamoja na famasi zote zimeunganishwa kwenye Mfumo wa Afya wa Serikali. Ukienda hospitali labda Nzuguni kuna clinic pale, utakapomuona daktari akakuandikia anakwandikia kwenye system ya Serikali. Ukitaka kwenda kuchukua dawa famasi mjini pale, sijui Nanenane au wapi; pale kwenye famasi wanaangalia jina lako kwenye system kwa sababu wao wenyewe wapo wanakuona kwamba ni daktari fulani alikuhudumia kule ndiyo wanakupa dawa, lakini huku sasa unapitia tu famasi, unapata dawa unakunywa haijalishi unaumwa, umepimwa wala hujijui. Kwa hiyo, kwa kweli tulilinde Taifa letu na tuwajibike upande na kuhakikisha lwamba wananchi wetu tunaokoa maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine dogo ambalo ninataka niliseme ni kuhusiana na uondoshaji wa magari ya Serikali, amelizungumza sana Mheshimiwa Simon Songe, Mjumbe mwenzangu wa Kamati ya PAC pale. Kwa kweli inaumiza, ukiacha mapendekezo ya Kamati, mimi nina ushauri kwa Serikali na hasa kwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha, ni vizuri kupitia GAMIS tutengeneze either mfumo mwingine au tutengeneze module ndani ya GAMIS ili magari yote ya Serikali tuyaweke ndani ya mfumo halafu tu-calculate formula ya salvage value ili kila gari inapoanza kutumika barabarani i-calculate salvage value mpaka mwisho wa matumizi ya gari. Kama ni miaka mitano au labda, kilometa 200,000 na baada ya hapo gharama yake inajulikana na disposition inatakiwa ifanyike ndani ya siku 30 au 60 gari itoke tuweze kuokoa fedha ya umma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii na naunga mkono hoja kwa mara nyingine. (Makofi)