Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibamba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi nichangie taarifa zetu hizi. Kwanza na mimi nikiri kukubaliana kabisa au kuunga hoja mkono taarifa zote mbili za Wenyeviti wetu wa LAAC na PAC, nikiwa natokea kwenye Kamati ya Hesabu za Serikali.
Mheshimiwa Spika, tuliyojadili sana kwenye taarifa zetu kwa kipindi hichi ni taarifa za Ukaguzi wa Kiufanisi. Kuangalia si tu fedha tulizopeleka lakini fedha tulizopeleka zimekuwa na thamani gani au na mchango gani katika miradi ambayo tulikuwa tunaikusudia kama Taifa.
Mheshimiwa Spika, kabla sijaeleza lolote, nitumie nafasi hii nami kumshukuru sana sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuitendea haki sana Halmashauri ya Wilaya ya Ubungo hususan Jimbo la Kibamba. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi sana, jimbo lile lilikuwa linakaribia kuzikwa (niseme). Wananchi wa jimbo lile walikuwa wanatamani hata kuhama, wote tu, lakini leo katika huduma za jamii zote; nikizungumzia shule, shule mpya saba; nikizungumzia eneo la afya, hospitali mpya kaijenga Mheshimiwa Rais Mama Samia, lakini shule ya Mkoa wa Dar es Salaam, ile ya shilingi bilioni 4.1 kaijenda ndani ya Jimbo la Kibamba. Pia juzi nimekabidhi ambulance.
Mheshimiwa Spika, mambo ni mengi, mambo ni mazuri. Yaliyobaki niliwahi kusema hapa, ni machache, lakini mwisho wa siku mambo ni bam bam.
Mheshimiwa Spika, uniruhusu nijielekeze kwenye maeneo machache. Moja, ni eneo la ufanisi wa ukaguzi katika miradi ya maji hasa mijini. Jicho letu CAG amefanya kazi kubwa sana. Pamoja na kazi kubwa ambayo anafanya mwamvuli wetu katika eneo la maji ndugu yangu Mheshimiwa Aweso, lakini ukweli jicho linamwonesha kuna upungufu mkubwa sana katika usimamizi wa miradi hasa miradi mikubwa.
Mheshimiwa Spika, moja, mipango hamna, taratibu hakuna katika ofisi au hizi mamlaka za maji bila usimamizi wa miradi husika. Hata matumizi ya ufanisi kwenye mitambo tunayowekeza, ile mitambo mikubwa ya gharama kubwa uwezo wa kuitumia hawana. Inawezekana hapa sasa kunahitajika kuwa na mafunzo ya hali ya juu kwa wataalamu wetu ili waweze kuitumia.
Mheshimiwa Spika, katika mamlaka nane ambazo jicho limeweza kuangalia au CAG ameweza kuzipitia unaweza kuona kwa kiwango cha chini kabisa Wakala wa Maji wa RUWASA na SUWASA chini ya 22% kuweza kusimamia mitambo iliyowekezwa. Zaidi ya hilo, kutosimamia kule maana yake imesababisha wananchi katika maeneo yale au halmashauri zile wameshindwa kupata maji ilhali uwekezaji ulikuwa unatosha kabisa wananchi wale waweze kupata maji.
Mheshimiwa Spika, nawapongeza sana, angalau katika zile nane, mbili zilizofanya vizuri ni DAWASA na DUWASA, yaani kwa maana ya 100% hapa Dodoma na kwa 78.5% kwa Dar es Salaam. Kwa hiyo, unaweza ukaona angalau kuna mafanikio katika maeneo hayo. Mapungufu haya yote wanatoa sababu wao. Wana sababu kama tano; moja, ni kukatika kwa umeme, wanasema ni moja ya sababu inayowafanya washindwe kufanikisha usimamizi wa maji na kusambaza maji mijini.
Mheshimiwa Spika, lingine ni kupungua kwa nguvu za umeme, low voltage. La tatu ni ubovu wa pampu na uchakavu wa miundombinu. Hii sample ilifanyika kwa miaka mitatu 2019/2020 hadi 2021/2022 miaka mitatu, lakini sasa hivi tunavyozungumza, Dar es Salaam Jimbo la Kibamba wana siku ya 34 changamoto ya maji zaidi ya mwezi mmoja watu hawana maji, lakini sababu ni hizi hizi tena, wataalamu wanatuambia low voltage, miundombinu imechukuliwa na maji na sababu nyingine kama hizi pampu Ruvu Juu pale, ndani ya miaka mitatu labda haijatengenezwa.
Mheshimiwa Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri atoe jicho, aangalie sana, kazi anaifanya kubwa, lakini anaweza kuangushwa na wataalamu wake katika jambo hili. Yaani ninavyozungumza, hatuna maji Dar es Salaam. Jimbo la Kibamba wananchi wa maeneo mengi hawana maji zaidi ya wiki tatu, lakini kuna mmoja alizungumza, Mheshimiwa Mwambe juu ya madeni, baadhi ya taasisi za Serikali kutolipa madeni ya maji. Zaidi ya shilingi bilioni 43.3 ni madeni.
Mheshimiwa Spika, kwanini hawalipi wakati kwenye bajeti zetu tukipitisha hapa tunaweka token kwenye utility? Shida ni nini? Wanatumia katika matumizi mengine au ni nini? Katika hili tumshauri Mheshimiwa Waziri wa Fedha, ni vizuri na kama ananisikia vizuri, wataalamu wake kama wapo, ni vizuri sasa mkali-reinvest fedha kwa ajili ya utility ili moja kwa moja fungu la 21 – Hazina (Treasure) iweze kulipia madeni haya, kwa sababu hawa watu inaonekana tukiwapa wanatumia kwenye matumizi mengine, lakini tukizifunga, zitaenda kutusaidia katika malengo yaliyokusudiwa.
Mheshimiwa Spika, tunaambiwa eti ni taasisi zile nzito nzito. Kwa sababu mimi niliwahi kuhoji kwenye Kamati, sasa kama ni kwenye taasisi zile nzito, kama majeshi na megine na kadhalika, hizi fedha si ndiyo kwanza tunaweza tukaanza kuwapa wao! Tunampelekea nani? Tukimaliza madeni ya Serikali (public dept), mishahara, tunapeleka kwao. Kwa hiyo, wataweza kulipa madeni. Nafikiri, ndiyo maana nakumbuka zamani tuliambiwa kaa, kaa. Ee, maneno mawili, lakini sijui kama tunaendelea nayo yale maneno mawili.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nikitoka katika eneo hilo, kuna jambo la Mradi wa DMDP page ya 114 ya taarifa ya Kamati yetu. Nashukuru sana katika ukaguzi wa ufanisi, katika mradi wa DMDP awamu ya kwanza ulifanya mambo mazuri na makubwa na wananchi wengi wa Dar es Salaam wanajua, na Waheshimiwa Wabunge ambao wanakaa Dar es Salaam Kijichi nimeiona lami inatembea, Temeke nzima, Buza na maeneo machache ya Kinondoni kwa maana ya Sinza mataa mazuri, Mburahati na maeneo mengine yote ni DMDP one, tumefaanya kazi nzuri. Zaidi ya US dollar ya milioni 330.3 na zaidi ya milioni 300 hizi tumepata kutokea Benki ya Dunia. Kwa hiyo, tuwashukuru sana.
Mheshimiwa Spika, upungufu mdogo ambao ninaamini katika nyakati za miradi ambayo inakuja karibuni watafanyia kazi, mfano changamoto ya muda kuongezeka kutoka miezi 15 hadi miezi 26, laini ucheleweshaji wa malipo kwa wakandarasi kutoa siku 33 hadi siku 295 miezi 10 unachelewa kumlipa mkandarasi, lazima hata deni litaongezeka.
Mheshimiwa Spika, ziada ni certificate of completion. Unatoa certification ya kumaliza kazi kabla hata kazi haijaanza. Kwa hiyo, nawaomba sana TARURA kupitia hii DMDP, hii DMDP inayokuja sasa, ambayo sisi Dar es Salaam, nafuu imesomwa hapa, tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, siasa ya Dar es Salaam ni miundombinu. Hatuna siasa nyingine, nilisema asubuhi. Sisi hatuna siasa ya uvuvi, hatuna siasa ya kilimo, siasa yetu ya msingi ni barabara tu ili uchumi wetu uweze kuendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwenye eneo hili anatutendea haki, DMDP ya kwanza ilihusu wilaya tatu; Temeke, Ilala na Kinondoni, sasa hivi ameiongeza Kigamboni na Kibamba au Ubungo ambapo na wananchi wa Kibamba wanaenda kukutana na kilometa 23 hizi vizuri kabisa. Kwa hiyo, niwaambie kabisa, kazi ya Mheshimiwa wenu Issa Jumanne Mtemvu inaendelea kuwasemea Bungeni mliponileta. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia kidogo sana ni eneo la urasimishaji. Kazi imeendelea kufanywa vizuri katika page ya 131 limesemwa jambo la urasimishaji. Namshukuru sana Mheshimiwa Mabula kwa kuendelea kufanya kazi nzuri akiwa Naibu na baadaye Waziri baada ya Mheshimiwa Lukuvi na sasa mdogo wangu Mheshimiwa Jerry William Silaa, Mbunge wa Ukonga anaendelea kufanya kazi vizuri, anatupa ushirikiano mzuri katika eneo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunatambua changamoto unazo sana, zimesemwa kwenye taarifa, sitaki kuzisema. Taarifa imesomwa na Mheshimiwa Mwenyekiti, japo changamoto nyingi ambazo zimesababisha, hamjafikia malengo. Mpaka sasa hivi chini ya 10% ndiyo hati nchini mmezipata. Kwa hiyo, nataka niseme, mmekuja kwenye bajeti ya sasa hii iliyopita ya 2023/2024, mlituambia dola za Kimarekani milioni 150 ambayo ni takribani shilingi bilioni 345, na shilingi bilioni 61 zitakuwa ni kwa ajili ya urasimishaji, naombeni mkazitumie.
Mheshimiwa Spika, najua mmeanza kazi kupitia madawati, mmefanya kazi nzuri sana, mnaanza kwa awamu, nendeni mkaharakishe ili wananchi wapate hati.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi naunga mkono hoja ya Kamati.