Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza kabisa nawapongeza Wenyeviti wetu wa Kamati ya LAAC na PAC kwa ripoti nzuri ambayo wametuletea hapa. Nitaunga mkono Maazimio yote kwa kweli, ni mazuri yaweze kufanyiwa kazi. Mimi ni Mjumbe wa PAC na nitazungumzia moja kati ya maazimio ambayo tumeyaweka ya uondoaji wa magari ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, CAG alikuja ndani ya Kamati yetu na tukaita Maafisa Masuuli kuhusiana na ukaguzi wa ufanisi wa uondoaji wa magari ya Serikali aidha kwa kuyauza kwa njia ya mnada au kuwakopesha watumishi wa umma au kuwauzia watumishi wa umma. Kuna upungufu mwingi ambao uliainishwa na kuoneshwa na CAG, madhalani kuegesha magari kwa muda mrefu bila kutengenezwa au kuondolewa kwa maana ya kuuzwa.

Mheshimiwa Spika, kwa ripoti ya CAG ilionesha magari 547 yaliweza kuegeshwa na katika hayo magari 547, asilimia 43 yalikuwa yamewekwa TEMESA, asilimia 53 yalikuwa kwenye hizi taasisi mbalimbali ambazo ni katika taasisi 10 tu ambazo alizitembelea, nje ya taasisi zote ambazo zipo katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika hayo magari yaliyoneshwa kuegeshwa zaidi ya miaka mitatu. Hii inasababisha athari mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, mfano mojawapo, ukiyaegesha muda mrefu bila kuyaendesha yanachakaa na kupungua thamani. Hata ile value for money maana yake unakuta umeagiza gari kwa ajili ya matumizi fulani lakini unaliacha linalipaki kwa muda mrefu, nitolee mfano, mimi natoka Mara, gari lilikuwa katika Halmashauri ya Rorya, limeingizwa likiwa na zero kilometer, likafanya kazi wa muda wa miaka mitatu tu, lakini likaegeshwa kwa miaka 10 kwa hitilafu ndogo tu ndani ya gear box, baadaye likaja likauzwa kwa shilingi milioni nane, gari la zaidi ya shilingi milioni 130. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni upungufu ambao unaweza kuuona kwa magari yote 540 kwa hii sample ndogo tu ya taasisi 10 uweze ku-assume kwa magari ya taasisi zote ndani ya Serikali ni kiasi gani? Mabilioni ya fedha kiasi gani ya Watanzania yanapotea?

Mheshimiwa Spika, lingine, CAG aliweza kubainisha dosari katika uthaminishaji wa magari hayo wakati wanataka kuyauza ambapo katika taasisi ambazo alipitia alichukua sample ya magari 500 tu. Katika hayo magari 500, magari matano yalikuwa overvalued kati ya 1% na 36%. Magari matatu ndiyo yalianza kuuzwa kwa thamani halisi, lakini magari 492 yalikuwa undervalued. Yaani magari 310 yalikuwa undervalued kati ya 10% na 100%. Magari 148 yakawa undervalued kati ya 101% mpaka 200%, magari 34 yakawa undervalued katika 200% mpka 836%. Yaani kama gari ameliuza shiling milioni 10, kiuhalisia kama ni 836% imekuwa undervalued ilitakiwa liuzwe shilingi milioni 83.6 na hii ndiyo maana CAG akaainisha ikasababisha hasara ya shilingi bilioni 2.7.

Mheshimiwa Spika, hii ni sample ndogo sana kwenye hayo magari unapata hasara ya shilingi bilioni 2.7 wana-undervalue magari haya bei zake. Wanauziana, baadaye wanaenda kuyauza kwa bei ya juu zaidi, unakuta wamepoteza fedha za Watanzania masikini walipa kodi, na sote tunajua kwamba magari ya Serikali yanayonunuliwa mengi ni zaidi ya shilingi milioni 100 kwenda juu, lakini wanakuja wanaya-undervalue wanauza shilingi milioni tano, shilingi milioni mbili, shilingi milioni 10, shilingi milioni 20. Hii haikubaliki.

Mheshimiwa Spika, hizi fedha zingeweza kupelekwa na hata zikajenga mabweni, hosteli za watoto wetu wakawa wanasoma kwenye shule za kata tukapunguza mimba za utotoni, lakini zinapotea hivi hivi. Hosteli tu inaweza ikajengwa kwa shilingi milioni 150. Mathalani hizi tu ndogo za 2.7 billion zingeenda kujenga hosteli zaidi ya 18 watoto wetu wakasoma na tukaokoa mimba za utotoni ambazo zimekithiri hapa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine, ripoti iliweza kuainisha kwamba wakati wa uingizaji wa magari, maana yake hapa Wizara inayohusika ni Wizar aya Fedha, Wizara ya Ujenzi, na pia walikuja watu wa Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Uthaminishaji wa magari wakati wa ununuzi, tumeona gharama wanazoziweka siyo halisia. Yaani wanachukua tu CF value wakati imefika bandarini, wanaacha gharama nyingine ambazo zina-count kwa asilimia 53 kwa bei halisi kama zingeweza kuwekwa. Wanaacha vitu kama VAT, tunajua lazima ziwekwe hata kama zitakuwa zina exemption, kodi ya ushuru wa bidhaa, kodi ya ushuru wa forodha, kodi ya maendeleo ya reli na mengine mengi. Unakuta wanayaacha na usajili wa namba husika. Kwa hiyo, unakuta wana-undervalue.

Mheshimiwa Spika, ripoti ya CAG imeonesha kwamba walipitia magari 27 tu wakaona kulikuwa kuna undervalue kwa zaidi ya 83% ya hayo magari 27 ambayo ilisababisha hasara ya shilingi milioni 957 za Kitanzania kwa magari 27 tu. Sasa ukichukua sample ya magari yote Tanzania, ni mabilioni ya hela ambayo yanapotea ambayo yangeweza kufanya kitu kingine, lakini unakuta yanapotea kwa uzembe tu mdogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kitu kingine kwenye uondoshaji wa magari, tumeweza kuona kwamba kumekuwepo na ucheleweshaji wa vibali. Kama nilivyosema mwanzo, unakuta kama magari yanataka kuondolewa, kwa mfano Wizara ya Fedha, imeoneshwa kwamba wanatumia kati ya siku 57 mpaka siku 2,226, yaani kuweza kutoa go ahead ya gari kuweza kuondolewa inatumia miaka sita na mwezi mmoja kuweza kuidhinisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii kama nilivyosema ndiyo inasababisha gari kukaa zaidi ya miaka 10, miaka mitatu na kuendelea kuchakaa zaidi. Pia, hata Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imeainisha pia na wenyewe wanachukua kati ya siku nne mpaka siku 2,050 (miaka mitano) kuweza kuidhinisha uondoaji wa magari haya ili yaweze kuondolewa na kuweza kuuzwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haya yote yanaweza kuonekana kama dosari. Walipokuja tuliweza kuwahoji wakakiri kwamba moja ni Mwongozo kupitwa na wakati kwamba wanatakiwa wauhuishe. Sasa unaweza ukajiuliza, mwongozo ambao umekaa muda mrefu tangu mwaka 1988, unauacha mpaka jicho la CAG lipite ndiyo uje kwenye Kamati na kukiri kwamba ni dhaifu ambalo unataka kufanya.

Mheshimiwa Spika, kingine walikiri kwamba ni kutumia mfumo ambao ni manual, hawaendi kwa kutumia mfumo wa kisasa wa TEHAMA. Tunajua kwamba kupitia GAMIS mbayo imeanzishwa 2018, Afisa Masuhuli wa Wizara ya Fedha akakiri kabisa mbele ya Kamati kwamba pamoja kuwepo kwa mfumo huu wa GAMIS, lakini hakujaweza kuwekwa module ya uondoaji wa magari yaa Serikali. Kwa hiyo, kuanzia 2018 mpaka sasa hivi wanaendelea kufanya vitu manually, business as usual, pesa za Watanzania zinapotea.
Mheshimiwa Spika, ndiyo maana maazimio yetu yamekuja hapo na ndiyo maana tunasema lazima yatiliwe mkazo kabisa. Huwezi kuwa una system ambayo ina-account assets nyingine za Serikali, unaacha hiki ambacho kinatumia fedha nyingi za Watanzania, unasema kwamba bado hamjaweka hiyo module. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, dosari nyingine ambayo ilionekana ni uwazi wa uondoaji wa haya magari ndani ya taasisi zetu. CAG aliweza kubainisha kwamba katika taasisi nane ambazo alitembelea, ni taasisi tatu tu ambazo ziliweza kutoa tangazo pale unapotaka kuondoa haya magari kwenye taasisi husika. Taasisi tano hazikuweza kutoa matangazo haya ikiwepo Wizara ya Fedha, Mahakama ya Tanzania, Jiji la Tanga, Halmashauri ya Mpwapwa na Wakala wa Barabara.

Mheshimiwa Spika, kutokuwepo na uwazi kunasababisha madhara haya. Kwanza, inanyima fursa watumishi wengine kuweza kujua kama kuna gari ambalo linataka kuwa disposed ili na wenyewe waweze kuomba. Pili, inatoa mwanya kwa baadhi ya Watumishi wa Umma kuweza kujinunulia. Tukienda tena mwakani kama gari inauzwa, anachukua huyo huyo, yaani unakuta ni wale wachache kwenye cycle wanachukua hayo magari.

Mheshimiwa Spika, kingine ilionesha kwamba ni mwongozo ambao haupo, ambao umepitwa na wakati, haujamtaka Afisa Masuuli kuweza kutoa tangazo pale ambapo anataka ku-dispose haya magari, kuwatangazia watumishi wa umma na kuweka uwazi zaidi. Sasa katika kwenda katika maazimo haya ya Kamati, tunaitaka Serikali iainishe mwongozo ambao uta-incorporate mambo yote ambayo ni kama udhaifu, lazima aweze kuonesha thamani halisi ya magari haya, ni muda gani yanatakiwa kuwa disposed; mfano, yakifikisha miaka mitano, yakipata ajali, ikiwa yamechakaa yanataka kutengenezwa, yaani ni lazima waainishe haya yote.

Mheshimiwa Spika, pia je, ni kwa baada ya muda gani? Kwa mfano, mimi Esther Matiko nimekopeshwa gari, ni baada ya muda gani tena naruhusiwa kukopa gari katika taasisi husika? Haya yote yataweka uwazi mkubwa.

Mheshimwia Spika, mwisho kabisa, iwepo sheria; ije Sheria ya Chief Valuer awe anafanya uthamini wa mali zote za Serikali pamoja na haya magari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)