Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Momba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Kwanza niseme naunga mkono hoja ya Kamati zote ambazo zimewasilishwa Mezani. Niseme kwamba ufanisi wa Kamati zetu, LAAC pamoja na PAC umetokana pia na umahiri wako kwa namna ambavyo umeendelea kutupa ushirikiano sisi Wanakamati, kututia moyo na kutuomba tuhakikishe tunalitendea haki Bunge lako. Kwa hiyo, matunda ya ubora wa taarifa nzuri ambazo zimewasilishwa hapo Mezani yanatokana na ubora wako. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kipekee kabisa niishukuru Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa namna ambavyo imepeleka pesa nyingi sana kwenye Majimbo yetu. Serikali ya Chama cha Mapinduzi imepeleka pesa za kutosha ni jambo ambalo halifichiki, nasi wote tukiwa hapa ndani tumekiri, na kwa namna tofauti kila mtu amemzungumzia vizuri sana Mama kwa namna ambavyo ameonesha moyo wake wa upendo kwa Watanzania wenzake na kudhihirisha kwamba kweli yeye ni Mama yamkini tofauti na watu walivyokusudia.
Mheshimiwa Spika, jicho letu la Bunge ambaye ni CAG anajaribu kuonesha namna ambavyo pesa hizi nyingi ambazo zimetafutwa na Mwanamama huyu shupavu na Mwanamama huyu mwenye huruma kuna mahali imeenda hazijatumika kikamilifu. Kwa hiyo, inawezekana mafanikio ambayo tunayaongea sasa na muda huu yalipaswa kuwa maradufu, maradufu, maradufu.
Mheshimiwa Spika, yamkini hata bajeti ya TARURA ambayo tunaiongelea sasa ilibidi sasa hivi ingekuwa imeshafikia hata shilingi trilioni mbili kutokana na pesa nyingi ambazo zilikuwa zimetafutwa na Mheshimiwa Rais, zingeweza kusimamiwa kikamilifu zingeweza kufanya kazi ambayo imekusudiwa.
Mheshimiwa Spika, pia kumekuwa kuna kasumba moja, mimi nimfananishe Mheshimiwa Rais ni kama mzazi ambaye umemtafutia mtoto wako shule nzuri sana, ukamlipia na ukampa gharama yote ya kila kitu ambacho anakitaka, jukumu la mtoto. Jukumu la mtoto kufanya vizuri sio la mzazi tena ni la mtoto mwenyewe, hakuna namna ambavyo mzazi huyu atatoka pamoja na kumpenda mtoto wake ataenda kumfanyia mtihani ili aweze kufaulu awe kama mzazi wake, hapana.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Rais ametekeleza vizuri majukumu yake kikamilifu, changamoto wako baadhi ya watu wachache wasio kuwa waaminifu, wasio kuwa wazalendo ndio ambao wanafanya mwaka jana tumesoma taarifa hii tunarudi kuongea mambo hayo hayo, CAG amebaini kitu hawataki kujirekebisha, halafu kwa bahati mbaya wamekuwa wakikimbilia kujificha kwenye kichaka cha Mheshimiwa Rais. Makosa wafanye wao na CAG amewabainisha kabisa, vitabu viko wazi vinawataja kama ni taasisi hii nani watendaji hawa wanatajwa, lakini unakuta oh, Serikali! Serikali? Mheshimiwa Rais hapa anaingiaje? Wewe kama ni mbadhirifu ni mbadhirifu tu na CAG amekuainisha. Wamtofautishe Mheshimiwa Rais na wizi na ubadhirifu ambao wao wanafanya wasimuunganishe kwenye hayo matukio. Yeye ni kama mzazi ambaye ametafuta shule nzuri kwa mtoto, jukumu la mtoto kufanya mtihani vizuri ni mtoto mwenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kabla sijaendelea na mchango wangu, kwenye ufanisi ambako CAG alitupitisha sisi kama Kamati na tukaja na maoni. Nataka angalau nirejelee kidogo ziara ya Mwenezi wetu wa Taifa Mheshimiwa Makonda.
Mheshimiwa Spika, nilijaribu kufuatilia kidogo kuona ziara ambazo alikuwa anafanya Mheshimiwa Makonda, nilikuwa naangalia labda clip moja kwenye kila mkoa nikaanza kuongeza clip mbili, nikaanza kuongeza clip tatu. Nilichokigundua, wananchi hawa inawezekana wamesikilizwa lakini changamoto zao hazijatatuliwa, na wakati mwingine kusababisha hata chama chetu kuonekana hakifanya majukumu yake ilihali kuna watu wachache ambao wamepewa dhamana wamekasimishwa madaraka yao hawajataka kutendea kazi majukumu ambayo wamepewa ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais ana kipande kikubwa sana cha nchi hii hawezi kafanya kila kitu na ndio maana aling’amua madaraka yake akaweka huyu fanya hivi, huyu fanya hivi. Kwa ushauri tu, mimi niziombe baadhi ya wizara, mfano Wizara ya Katiba na Sheria, tunaomba ifike kule chini kusikiliza kero za wananchi. Yale mambo yote ambayo wananchi walikuwa wanalalamika, wao ndio wanasimamia Katiba na Sheria mahali ambapo panaonekana wananchi hawajatendewa haki, si wafike wawasikilize? Lakini Wizara ya Ardhi, ipo baadhi ya migogoro unaona kabisa, kwa mfano tuchukulie Waziri mwenye dhamana, Naibu Waziri, Katibu kwenye hii Wizara, Kamishana wa Ardhi wangekubali kuzunguka walau majimbo karibu 200 wangekutana na hayo matatizo ambayo hayakupaswa hata Mwenezi yeye awe anaendelea kuyatatua.
Mheshimiwa Spika, lakini na wizara zingine ambazo zinahusika na maisha ya wananchi moja kwa moja kwa mfano, tunaomba TAMISEMI wapite kwenye majimbo yetu, inawezekana mambo hayo hayo Wabunge wameshaongea hapa Bungeni lakini wakati mwingine walichukuliwa tofauti lakini Mwenezi amepita huko kwenye maeneo wananchi wameendelea kuyalalamikia hayo. Hayo mambo mengine sio ya Mheshimiwa Rais hata kidogo, Mama Dkt. Samia amekaimisha madaraka kwa watu wamsaidie.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu hiyo hiyo, wakati mwingine kwanza nirejee jukumu la Kamati yetu. Shughuli ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya PAC, kushughulikia maeneo yenye matumizi mabaya ya fedha za umma katika Wizara, Idara, Wakala na Mashirika ya umma.
Mheshimiwa Spika, wakati mwingine kumekuwepo na mianya ambayo inapelekea fedha zinapoingia zinatoboka na kutokwenda mahali ambako hakustahili. CAG katika ufanisi wa ukaguzi wake anaonesha kwamba kuwa na mifumo duni ya TEHAMA wakati mwingine inaweza ikasababisha kuwa na uvujivu wa pesa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali Mtandao, eGA ambaye yeye amepewa majukumu ya kusimamia miundo yote na mifumo yote ya TEHAMA hapa nchini. Yeye mwenyewe kuna mahali CAG anamzungumzia na kumkagua kuona kwamba yapo maeneo ambayop yeye hakutekeleza majukumu yake vizuri. Katika hili Serikali mtandao yeye mwenyewe pia ni chombo ambacho kinapaswa kuwezeshwa. Kijengwe vizuri atumie mifumo ambayo ni high technology ili aweze, yeye hawezi kusimamia mifumo yote kwenye taasisi mbalimbali ikiwa yeye mwenyewe anatumia mifumo ambayo sio high technology.
Mheshimiwa Spika, mfano mzuri ni CAG alitupitisha kwenye mifumo yake. Kiukweli kwa watu ambao wamesoma mambo ya TEHAMA ukiangalia namna ambavyo anafanya shughuli zake, anavyokagua mambo yake ya ki-TEHAMA unathibitisha kabisa uwezo wake kwamba anaweza aka-penetrate kwenye maovu yote na akaja na kitu ambacho ni cha maana.
Mheshimiwa Spika, CAG anasema kwamba kuwepo na mifumo duni katika taasisi zetu inasababisha vitu ambavyo vimesababisha, cha kwanza ni kuwa na sera ambayo imepitwa na wakati. Sera ambayo Serikali mtandao inatumia ni sera ambayo imeshapitwa na wakati ni ya miaka mitano huko kutoka 2017 mpaka 2022, hivyo kuwepo na sera hiyo mbovu inawafanya watu hawa washindwe klutekeleza majukumu yao vizuri na kikamilifu.
Mheshimiwa Spika, wakati mwingine kumekuwa na changamoto ambayo inawafanya hao watu wa eGA wanaposhindwa kwenda kusimamia mifumo mbalimbali ambayo iko kwenye taasisi mbalimbali ilisababisha hasara kubwa ambayo Serikali yetu ya Tanzania ilipata kutokana na changamoto hizo ambazo hazitendewi haki kikamilifu.
Mheshimiwa Spika, CAG anasema kwa mujibu wa ripoti ya usalama wa mitandao ya Tanzania mwaka 2017, Tanzania ilikadiriwa kupoteza Dola za Kimarekani, milioni 99 kwa kila mwaka kutokana na mashambulizi ya kimtandao, hii ni sawasawa na shilingi 268, 650,000,000.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Kengele imeshagonga Mheshimiwa.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine ambao CAG ameeleza…
SPIKA: Kengele imeshagonga Mheshimiwa.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, la mwisho, jambo lingine ambalo CAG anaeleza, mifumo yetu mingi haisomani taasisi kwa taasisi, haisomani na haielewani, hivyo inasababisha kutokuwa na ufanisi mzuri katika kutekeleza majukumu ya ki-TEHAMA. (Makofi)
SPIKA: Ahsante sana.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, kwa ushauri Serikali iwekeze kwenye mambo ya Ki-TEHAMA kwa sababu dunia iliyoko sasa hivi iko kwenye kiwango kikubwa cha kutumia matumizi ya kompyuta ili tusiendelee kuibiwa, ahsante. (Makofi)