Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Deogratius John Ndejembi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chamwino

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii kushukuru kwa nafasi hii ya kuchangia taarifa ya Kamati hizi mbili ambazo zimewasilishwa siku hii ya leo. Pia, nichukue nafasi hii kupongeza Kamati hizi mbili kwa kazi nzuri ambayo wamekuwa wakifanya.

Mheshimiwa Spika, mchango wangu utajikita katika Kamati ya LAAC ambapo pia nachukua nafasi hii kumpongeza Mwenyekiti wa Kamati hii Mheshimiwa Halima James Mdee, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hii Mheshimiwa Stanslaus Mabula na Wajumbe wa Kamati hii ya LAAC kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tuko tayari kupokea miongozo, maelekezo na maazimio ya Bunge lako Tukufu yatakayo toka hapa na tutakwenda kutekeleza kama vile ambavyo Kamati na Bunge lako Tukufu litaazimia hapa mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumesikia hapa Waheshimiwa Wabunge wengi wakichangia hoja juu ya Force Account, jambo hili ni zuri kwa maana nilinaokoa gharama kubwa. Ndio, kuna changamoto nyingi juu ya usimamizi wa miradi kupitia Force Account, na katika utatuzi wa changamoto hizi tayari Serikali imeajiri Wahandisi zaidi ya 362 kote nchini na katika hao kila halmashauri nchini walau ilipata mhandisi mmoja. Mwaka jana wa fedha Serikali iliajiri ma-quantity Surveyor 100 kwa ajili ya kuhakikisha kwamba mfumo mzima wa Force Account unafanya kazi bila kuwa na changamoto yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Force Account, natoa mfano; katika majengo yanayojengwa sasa ya shule za mikoa kuna mikoa ambayo ilitekeleza Force Account to the T kama ilivyotakiwa kwa mujibu wa sheria na wamefanikiwa vizuri sana na mpaka sasa shule hizo zimefika zidi ya asilimia 90 ya ujenzi wake katika zile shilingi bilioni tatu ambazo zilikuwa zimepelekwa. Hapo hapo kuna wengine ambao Mikoa mingine ilitangaza tender kupata wakandarasi na BOQ za Wakandarasi zilikuwa mara mbili ya gharama ile ambayo ilikuwa imepelekwa na Serikali katika Mikoa hiyo, kwa hiyo utaona ni namna gani ambavyo Force Account inaokoa fedha nyingi ya Serikali katika ujenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa cha kusimamia ni ubora wa kile ambacho kinapatikana kama ambavyo kamati imewasilisha mbele ya Bunge lako. Nirejee tena kusema tuko tayari kwa ajili ya utekelezaji wa maelekezo ya Kamati yaliyotolewa na maazimio ya Bunge yatakayotolewa.

Mheshimiwa Spika, vilevile kuna michango ilikuja kwa ajili ya shule zile ambazo zilipelekewa shilingi milioni 470, tayari tathmini inafanyika na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuona ni wapi ambapo kuna mapungufu ili fedha iweze kutafutwa kujazilizia lakini wakati huo huo kuna ambao waliomba vibali maalum baada ya kupokea shilingi milioni 470 kuweza kujenga majengo ya ghorofa. Mfano, Tunduma TC walipopokea shilingi milioni 470 walikuwa na uhaba wa maeneo waliomba kibali cha kujenga ghorofa kwa kuongeza na mapato yao ya ndani, thamani nzima ya majengo yale itakuwa ni shilingi milioni 800. Liwiti, Shule ya Sekondari Liwiti, Halmashauri ya Manispaa ya Ilala waliomba kibali cha shilingi milioni 470 waweze kujenga ghorofa na wanaongeza kwenye mapato yao ya ndani, vilevile Nzega waliomba kibali kwa ajili ya kuweza kujenga ghorofa kwa mapato yao ya ndani.

Mheshimiwa Spika, tutaendelea kusimamia changamoto, narudia tena hatutamvumilia yeyote, kama ambavyo Kamati imependekeza, hatutamvumilia yeyote ambaye atazembea katika usimamizi wa fedha ya umma na tutachukua hatua mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tayari Serikali hii ya Awamu ya Sita imeanza kuchukua hatua kali dhidi ya wale wote ambao wameonekana kuzembea usimamizi wa miradi ya Serikali. Kuna wakurugenzi ambao wamepoteza teuzi zao kwa kutenguliwa, kuna wakuu wa idara za ujenzi ambao wametenguliwa teuzi zao, kuna wale wasimamizi wa miradi hii tayari wamechukuliwa hatua mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, nirejee tena nchi hii ni yetu sote na hapa mapendekezo ambayo yanatolewa ni kwa ajili ya kuboresha, katika kuhakikisha tunapata value for money katika fedha ya Serikali na Ofisi ya Rais, TAMISEMI italisimamia hilo chini ya uongozi mahili wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa na kwa msaada mkubwa wa Kamati hii ya LAAC ambayo inatupa mapendekezo mazuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba niseme naunga mkono hoja ya Kamati zote mbili zilizokuwa mbele yetu. (Makofi)