Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, naomba na mimi nitumie fursa hii katika kuchangia kusema machache. Kwanza niwapongeze watoa hoja kwa taarifa nzuri ambazo wamezileta mezani.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema jana, moja ya mambo ambayo sisi Serikali hatubishani kabisa na Bunge ni masuala ya usimamizi wa fedha za walipa kodi wa nchi hii. Haya ni mambo ambayo hayana pande mbili, sisi na Wabunge tunaongea jambo moja.

Mheshimiwa Spika, nimekuwa hapa Bungeni awamu ya tatu sasa na nimekuwa Serikalini awamu zote hizi tatu tangia nilipoingia hapa Bungeni. Moja ya Serikali ambayo inasikiliza tena kwa wakati hoja zinazotolewa na Bunge ni Serikali ya Awamu ya Sita, inasikiliza mara moja yanapokuwepo masuala na inachukua hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, taarifa hizi ambazo zimefanyiwa kazi na Kamati za Bunge ni taarifa za mwaka juzi na siyo taarifa za mwaka huu. Ni taarifa za CAG za mwaka juzi na sio taarifa za mwaka jana. Matatizo haya ambayo yanabainishwa yalishasemwa kwenye taarifa zilizopita.
Mheshimiwa Spika, baada ya kuwa yamesemwa Serikali ilichukua hatua, tumeongea sana hili jambo la Force Account, na kwa nini Wabunge walikuwa wanalisemea sana, siyo tu kwenye taarifa hii, ilisemwa mwaka jana na ilisemwa na mwaka juzi. Ilikuwa inasemwa hivyo kwa sababu hakukuwepo na ukomo wala hakukuwepo na utaratibu unaoratibu jambo hili na ndio maana kwenye taarifa yamejitokeza haya.

Mheshimiwa Spika, mwaka jana Tarehe 8 tumepitisha Sheria mpya na Tarehe 29, Septemba Mheshimiwa Rais alisaini Sheria tuliyopitisha hapa Bungeni. Kwa hiyo tunapoongea hapa ile Sheria ambayo Bunge lako lilipitisha ina miezi minne ndio unaenda mwezi wa tano, maana yake nini haya makosa ambayoyamebainishwa tayari Serikali lishachukua hatua na imefanyia kazi tena kwa kusaini Sheria mpya, kwa hiyo, tunatarajia baada ya Sheria hii kuanza kufanya kazi haya hayatajitokeza.

Mheshimiwa Spika, Sheria ile tuliyopitisha tuliweka mambo gani yaliyowekwa na Bunge:-

(i) Tulisema kwenye Sheria mpya Na. 76(1)(a) tulisema kazi za ujenzi ambazo ni ndogo zimetawanyika sana. Tulisema zile kazi zilizotawanyika sana, kujenga choo kwenye shule shikizi, hauwezi kusubiri kutangaza tender, unatafuta mafundi pale watengeneze choo;

(ii) Kazi za ujenzi ambazo zinatakiwa kutekelezwa kwa uharaka, daraja limekatika huwezi ukasubiri kutangaza tender, utafanya utaratibu wa haraka na utatekeleza kwa uharaka. Haya ni mambo ya msingi ambayo tunakubaliana;

(iii) Tukaweka masharti mengine kwamba matengenezo hayo yatakuwa ni sehemu ya shughuli za kawaida za kila siku;

(iv) Tukaweka tena masharti kwamba lazima pawe na watu wenye utaalam wa kuweza kusimamia jambo hili. Haya sio mambo ya kubishana wote tunakubaliana na haya Wabunge ambayo walikuwa wanayasema hata sisi wenzenu tulioko huku yametupata pia. Mimi ilitokea katika shule yangu moja pale Lulumba, katika mwaka ule shule ilikuwa kwenye tano bora za kitaifa, halafu ikatokea kwenye ujenzi headmaster hakusimamia vizuri wakataka wamtoe, mimi mwenyewe niliandamana kwenda kwa Waziri nasema Shule ya Iramba kabisa kule inaongoza kwenye PCB halafu yule Mwalimu Mkuu mnataka mmtoe kwa sababu ya ujenzi nikasema hapana huyu tulimleta ili wanafunzi wafaulu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, haya mnayoyasema, wote tunaongea lugha moja na ndio maana mlipoongea mwaka juzi na mwaka jana Serikali ilifanya haraka sana na tumeshabadilisha Sheria na kwenye ukomo tumeweka kiwango chochote kinachozidi milioni 100 hakitatekelezwa kwa force aacount except kwenye maeneo yenye udharura ambayo tunaweza kupeleka vyombo mahsusi vyenye ufundi maalum vikaenda kutengeneza. Mfano kama pale niliposema daraja limekatika, hayo ni maeneo ambayo wala hatubishani na wala hatuhitaji kubishana. Sisi Serikali tumekubaliana na Wabunge na Sheria imepitishwa tena kwa msaada wa Bunge tumepata hoja nyingi sana za msingi na kwenye kanuni tumezingatia mambo hayo.

Mheshimiwa Spika, lakini kuna mambo ambayo kama nchi ni lazima tukubaliane; jambo la kwanza; Lazima Wakandarasi wetu wakue, wasing’ang’anie kujenga vyoo kwenye shule shikizi, wajenge miradi mikubwa. Tumepitisha kwenye Sheria kwamba wakandarasi wetu wanatakiwa wagombanie ile miradi mikubwa, Nchi yetu imekuwa bomba la kupitisha fedha. Tunatafuta fedha kule hata tukikopa ni fedha ambazo tutalipa kwa kodi zetu, wakandarasi wetu hawa wanang’ang’ania sub contract, sub contract, sub contract mpaka lini? Kujenga vyoo vya shule shikizi mpaka lini, kujenga Zahanati ya Kijiji ya milioni 12 mpaka lini? Darasa, darasa wajenge mafundi. Tugawe fedha zibaki kule kwenye maeneo yetu.

Mheshimiwa Spika, tumesema Wakandarasi Wakubwa wafanye miradi mikubwa na wale wa kutoka nje hatakama watachukua na wenyewe wana mataifa yao na wenyewe waombe kazi kwa wenyeji wa nchi hii ili wananchi wetu wa nchi hii wajijue kwamba wako kwenye Taifa lenye uhuru kwa zaidi ya miaka 60.

Mheshimiwa Spika, sasa leo hii tukisema mafundi wasifanye kazi, hizi kazi za shule shikizi ndio zifanywe na wakandarasi, choo cha shule shikizi kitangaziwe tender, tutakuwa tunasahau kumbukumbu ambazo tuliwahi kuzisema kwa ubaya sana haya mambo ya kuchelewesha hata kazi ndogo kwa ajili ya kusubiri kazi zifanywe kwa kutumia utaratibu wa tender.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunakubaliana kuhusu uboro, ni jambo ambalo hatuna compromise. Tunakubaliana kuhusu udhibiti wa fedha, ni jambo ambalo halina compromise na hata hivi sasa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mwaka mmoja tu baada ya kusikiliza hoja za Wabunge akaleta Sheria tumeshaipitisha, alishasaini na sasa kanuni ziko tayari tumeweka ukomo na tumeweka na utaratibu wa namna ya kuzingatia ubora. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naamini hili jambo hata tusiliweke kwenye maazimio kwa sababu Bunge lilishatunga Sheria na Kanuni ziko tayari, wanasema tuweke utaratibu tumeshaweka, anasema tuweke ukomo tumeshaweka. Sasa tukubaliane tu kwamba labda Sheria ambayo tumeitunga mwaka jana hata haijaanza kufanya kazi kwamba haifai tuifute. Kama tunataka kufuta Sheria kwamba haifai hilo ni jambo lingine tunatakiwa twende kwenye Sheria, lakini kwa mujibu wa Sheria tuliyopitisha, tutakuwa na miradi ambayo itakuwa inafanywa kwa force account.

Mheshimiwa Spika, daraja limekatika hatutangazi tender, tutafanya kwa utaratibu wa haraka. Vyoo vya Shule shikizi hatutangazi tender, zahanati moja, darasa la milioni 12 hatutangazi. Tutatumia utaratibu wa mafundi walioko pale lakini tumeweka mwongozo ambao utawasimamia.

Mheshimiwa Spika, nimekwishaliongelea hili na sheria imetungwa na tumezingatia kanuni, na haya maoni yaliyotolewa na nyongeza ambazo tumezipata tutaboresha, na kwa bahati nzuri sana tuna muda wa kufanya hivyo kwenye kanuni.

Mheshimiwa Spika, haya mengine yameongelewa kwenye upande wa magari; haya pia siyo mambo tunayobishana nayo. Moja ya kitu ambacho Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anakipatia umhimu mkubwa sana ni usimamizi wa fedha za umma. Ndiyo maana tumekuwa tukiongeza fedha kwa CAG ili akague haya yote.

Mheshimiwa Spika, kwenye hili la magari mmpendekeza yale magari yote ambayo ni mabovu mabovu, lakini sisi mtazamo wa Serikali tunataka twende zaidi ya hapo. Mtakumbuka kwenye Hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali, tulitaka siyo tu kuondoa mabovu, Serikali tulitaka kuondoa magari. Bado linajadiliwa, limetengenezewa utaratibu ndani ya Serikali ili lijadiliwe na liweze kufanya vizuri, kuwe na utaratibu, hatuwezi tukawa na magari mengi yamezagaa na mengine hatujui yalipo, tunatumia gharama kubwa halafu tunafanya kama vile kufanya kazi ya kuwatumikia watu ni lazima upewe incentive. Hizi incentive zilikuwa zinatolewa wakati watumishi wa umma hawapo, yaani ukienda mtaani hivi hauwapati. Sasa hivi unaweza ukapanga hata safu nne, hata tano, yaani unabadilisha hii unaleta nyingine, unabadilisha hii unaleta nyingine, unabadilisha hii unaleta nyingine. Kwa hiyo, lazima watu wote waone ni heshima kuwatumikia wenzao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo haya yote ambayo yanafanyika hivi, yote yanatengenezewa mwongozo na haya ambayo Waheshimiwa Wabunge mmeyaweka hapa, sisi ndani ya Wizara tumeyapokea na kwa ajili ya muda ninaweza nisiweze kupitia moja baada ya lingine, lakini yote tumeyapitia, tutayafanyia kazi kwa haraka na usimamizi wake tutaufanyia kazi ili tuweze kuhakikisha kwamba rasilimali hizi zinafanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwenye hili pia alitupia jicho, na si hili tu, ninyi mmeongelea magari ambayo yanakwenda sehemu tofauti tofauti, kuna maeneo mengine kwa upana wake ambao tunayafanyia kazi. Vifaa ambavyo viko kwenye Balozi zetu navyo kumekuwepo na ucheleweshaji wa aina hiyo hiyo. Yote na yenyewe aliunda Kamati ifanye kazi na wenyewe mmeona Kamati ile iliwasilisha juzi juzi hivi, na kila eneo ambalo lina dosari, Mheshimiwa Dkt. Samia amelitengenezea utaratibu wa kupata jawabu. Haya mambo tumpe heshima yake kwa kuchukua hatua, kwa sababu yangekuwa yanachukuliwa hatua, yeye ni Rais wa Sita asingeyakuta, angalau tumpe yeye kila jambo ambalo Bunge limesema kuna tatizo, amechukua hatua na hatua yenyewe inakwenda kwenye sheria ili kuweza kumaliza tatizo hilo.

Mheshimiwa Spika, kwa ajili ya muda niwaambie Waheshimiwa Wabunge kwamba tumeyapokea, tunayafanyia kazi yale ambayo bado hatujayafanyia kazi kama Serikali na yale mengine ambayo yanahitaji tuyafanyie kazi zaidi, tutaendelea kuyafanyia kazi kwa utaratibu ule wa kiserikali. Serikali haijalala iko kazini, na haya ni mambo ambayo tunayafanyia kazi. Tunalihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba Serikali itahakikisha fedha zote za walipa kodi zinazopatikana zinafanya kazi kama ilivyokusudiwa na kama kuna mchwa hatutaacha hata chembe ya nyayo zake alizopitia kwenda kuharibu fedha za umma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja (Makofi)