Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Innocent Lugha Bashungwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Karagwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia hoja za Kamati mbili na mimi niwapongeze Waheshimiwa Wenyeviti wote wawili wa Kamati hizi kwa hoja walizowasilisha.

Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, nchi yetu imekuwa na checks and balances ili kuweza kupata haya. Sisi kwa upande wa Serikali tunatekeleza na Bunge lina monitor, ku-evaluate na kutupatia ushauri. Kwa hiyo, ushauri wa Kamati tumeuchukua na tutaufanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi naomba nitumie nafasi hii kutoa ufafanuzi wa baadhi ya mambo ambayo yamejitokeza wakati wa mjadala na nianze na hoja ambayo imesemwa na Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, Waziri wa Fedha, baada ya Bunge letu kupitisha sheria ya kutoa wigo wa kusaidia wakandarasi wazawa kwa threshold kutoka bilioni 10 kwenda bilioni 50, tulikaa na Wizara ya Fedha na sisi Wizara ya Ujenzi tukaandaa local content strategy ya ku-support sheria hii.

Mheshimiwa Spika, wakati wa Bunge la Bajeti au kwa maelekezo yako, ningependa tuwaoneshe Bunge letu namna ambavyo tumejipanga ili kanuni ambayo Mheshimiwa Waziri wa Fedha ataisaini ya kuongeza wigo ili wakandarasi wa ndani waweze kushiriki zaidi katika ujenzi wa nchi yetu, tukisema tuondoe force account tutakuwa huku tunatoa ustawi, lakini kwa mkono mwingine tunawaondolewa ustawi wakandarasi wetu wazawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo ningependa suala la force account tulipe muda, lakini pia muangalie ni kwa namna gani upande wa Serikali tumejipanga kwa hii sheria ambayo tumeipitisha ya kuongeza threshold ya ushiriki wa wakandarasi wa ndani kutoka bilioni 10 kwenda bilioni 50. Sisi Wizara ya Ujenzi kwenye hii local content strategy tunayo mambo mengi mazuri ambayo kupitia mfumo huu wa force account utasaidia sana wakandarasi wazawa.

Mheshimiwa Spika, vilevile hata hili ambalo limezungumzwa na Kamati ya LAAC kwa upande wa halmashauri zetu, wasanifu majenzi, wakadiriaji wa gharama za ujenzi, engineers, tunao vijana wetu graduate engineers wengi ambao wanatafuta fursa za ajira, lakini kupitia force account baada ya hoja hizi za Kamati hizi mbili, kwa upande wa Serikali tutakaa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili tuangalie vijana wengi ambao wangependa kwenda field na kupata uzoefu ni namna gani wanaweza wakaenda kwenye halmashauri zetu kwa kupitia programu ambayo tunayo chini ya ERB (Msajili wa Engineers pamoja na Msajili wa Wakandarasi).

Mheshimiwa Spika, kupitia hii programu ya vijana graduate engineers ambao wanapitia programu ile, tutakaa na TAMISEMI tuangalie namna ambayo vijana hawa wanaweza wakaenda kwenye halmashauri wakashiriki katika kusimamia miradi, huku wanapata ujuzi lakini huku tunatatua changamoto ambayo imesemwa na Kamati zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa kufanya haya tunaona ni jinsi gani kwenye upande wa force account tukilipatia muda na tukashirikiana, bado mfumo huu unaweza ukatusaidia kusimamia miradi huko kwenye halmashauri.

Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, jambo lingine ambalo ningependa kulitolea ufafanuzi na dada yangu Mheshimiwa Msongozi amekuja hapa tumeelewana vizuri, ni lile la madeni versus riba, zile bilioni 701 hata taarifa ya Mwenyekiti wa PAC ameitaja hapa kama ilivyo ni bilioni 701 ni madeni na siyo riba.

Mheshimiwa Spika, katika deni hilo nilitaja bilioni 68, baada ya ku-check na wataalamu wangu, kwa sababu ya Hansard, as of December, 2023 ni bilioni 61. Kwa hiyo, naomba niweke rekodi sahihi. Kwa hiyo, bilioni 701 ni malimbikizo ya madeni na siyo riba.

Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, jambo lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni hili suala la premature failure; yaani barabara zinaharibika kabla ya ule muda uliopangwa au uliokadiliwa. Tumebainisha changamoto ambazo zinapelekea hili na niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, kwa miezi ambayo nimekaa kwenye Wizara tayari nimekwishakaa na wataalamu. Changamoto ambazo zimejitokeza na ambazo zilikuwa zinasababisha haya ni value chain nzima kuanzia kubainisha miradi, hatua za manunuzi, usimamizi wa mikataba lakini na suala la baadhi ya watumishi kutokuwa waaminifu ku-connive na consultants pamoja na contractors. Haya yote tumekwisha yabainisha, na ndiyo maana nimesema kuna checks and balances. Tutajipanga kuhakikisha hii hali tunaikomesha kwenye sekta ya ujenzi.

Mheshimiwa Spika pamoja na Waheshimiwa Wabunge, mmeona hata kwenye ziara zetu, nilipokwenda kule Kyela tukakuta mkandarasi ambaye amepewa kazi hana uwezo, amepewa kilometa 32, yuko nje ya muda, mitambo haijafika site, key staff hawajafika, lakini mkandarasi huyo huyo kule Sengerema Nyehunge amepewa kilometa 54. Tumechukua hatua na Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ametusaidia, tunachukua hatua za kimkataba kumshughulikia huyo mkandarasi bila kuvunja sheria za nchi. Hata hivyo, wakandarasi wa aina hii tumeanza kuchukua hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile, nikiwa natembelea barabara ya kule Mbinga (Amani Makolo – Luanda) tulikuta consultant ambaye ni mzembe, tulimsimamisha kazi lakini hapo hapo nikawambia wasaidizi wangu, inakuwaje miaka yote hii tunatumia consultant kutoka nje na bado tunakuwa na changamoto hizi hizi?

Mheshimiwa Spika, sasa hivi kupitia hii local content strategy, tumeanza kuwajengea uwezo consultant wa ndani ili with time usimamizi wa barabara zetu usitegemee tu wakandarasi wa nje kwa sababu wakandarasi wa nje pamoja na consultant wa nje, changamoto hizi tumekuwa nazo wakiwa wanatusaidia kusimamia hii miradi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama nilivyosema kwa ujumla hoja zote za Kamati mbili tumezichukua, Serikali tunafanya kazi kwa kushirikiana, tunakwenda kujipanga lakini tumeanza kuchukua hatua.

Mheshimiwa Spika, kwenye hoja ya usimamizi usiorizisha wa barabara, pipo changamoto upande wa consultants hao niliowataja. Pia barabara nyingi kubwa unakuta ni hao wanaotoka nje. Tunawachukulia hatua za kimikataba.

Mheshimiwa Spika, vilevile, kwenye usimamizi wa hizi barabara, Regional Managers wa TANROADS nimegundua kumekuwa na changamoto, huku kuna ratiba labda ya Waziri fulani au kiongozi fulani kwenye Mkoa, Regional Manager anatakiwa kuwa kwenye kusimamia mradi wa barabara, lakini wakati huo huo kuna ziara za viongozi inabidi ashiriki. Kwa hiyo, wakati yuko kwenye ziara za viongozi, muda wa kwenda kusimamia barabara hana.

Mheshimiwa Spika, nimetoa maelekezo kwamba katika miradi yote lazima kuwe kuna project engineers. Kwa hiyo, tayari kila mradi ndani ya nchi yetu uwe mdogo au mkubwa, tumeweka utaratibu wa kuwa na project engineers ambao wanakuwa site muda wote ili kuwasimamia wakandarasi. Kwa hiyo, kwa kufanya hivi ninaamini kwamba tutatatua changamoto hizi ambazo zimetajwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, kulikuwa kuna suala la variations; yaani gharama kwenye mkataba unapokwenda kujenga, mkandarasi anakuja kuomba hela ya ziada ili kukamilisha ujenzi wa barabara. Kumekuwa na changamoto mbalimbali nyingine ikiwepo usanifu wa kina unapofanyika tunachelewa kuanza ujenzi wa barabara, inaweza ikachukua miaka mitano, miaka kumi, lakini kule mawandani unakuta hali imebadilika, eneo ambalo halikuwa na makazi unakuta watu wamekwishahamia au mvua za El Nino zimeharibu eneo husika. Kwa hiyo, unapokwenda kwenye ujenzi unakuta gharama halisi imekuwa kubwa kuliko usanifu uliofanywa miaka mitano au miaka kumi iliyopita.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimeelekeza TANROADS kwamba kabla hatujaanza taratibu za manunuzi, kuhakikisha barabara zote ambazo tumezisanifu tunazi-review ili mikataba tunayoingia na gharama za kujenga hizo barabara iwe na uhalisia ili kuepuka haya masuala ya variation, maana kukiwa na variations, hujalipa hiyo additional cost, unaweza ukajenga hizi barabara ili mradi iishe na baadaye mnapata hizi changamoto za premature failure.

Mheshimiwa Spika pamoja na Waheshimiwa Wabunge, kama nilivyosema Serikali hii ambayo inaongozwa na Jemedari wetu Mheshimiwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni Serikali sikivu, inaheshimu mchango na usimamizi wa Bunge kwa Serikali anayoiongoza. Sisi wasaidizi wake hatutakuwa kikwazo kwa hii dhamira ya Mheshimiwa Rais na 4R ambazo anazisimamia ikiwemo suala hili la checks and balances. Masuala ambayo Bunge mnatuagiza, tutakuwa tayari kuyatekeleza na kuleta mrejesho kama ulivyo utaratibu wa Bunge letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)