Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Naghenjwa Livingstone Kaboyoka

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI: Mheshimiwa Spika, hitimisho la hoja; kwa mara nyingine tena nikushukuru wewe binafsi kwa kuendelea kutuongoza hapa Bungeni kwa weledi mkubwa. Aidha, naomba niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja ya Kamati ya PAC ikiwa ni pamoja na Mawaziri wetu wanne ambao wote wamechangia katika hoja hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja ya Kamati imechangiwa na jumla ya Waheshimiwa Wabunge tisa nitawataja tu upesi upesi, akiwepo Mheshimiwa Simon Songe Lusengekile, Mheshimiwa Venant D. Protas, Mheshimiwa Joseph G. Kakunda, Mheshimiwa Ester A. Bulaya, Mheshimiwa Geoffrey I. Mwambe Mheshimiwa Jacqueline N. Msongozi, Mheshimiwa Issa J. Mtemvu, Mheshimiwa Esther N. Matiko pamoja na Mheshimiwa Condester M. Sichalwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia michango iliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge, ningependa tu kutoa maelezo ya msisitizo katika maeneo machache yafuatayo, haya maeneo nataka Bunge lako lielewe kwamba sasa hivi tunasisitiza kuangalia mambo ya ufanisi kuliko kuangalia tu mambo ya hesabu. Kwa hiyo, kwa nini naeleza haya? Maana value for money tutaipata pale ambapo tutaona kaguzi za kifanisi au za kiufundi inasemaje? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maana kihesabu unakuta kwamba kweli hela inaonekana zimetumika lakini je, kazi field iko wapi? Ndiyo maana sitajibu hoja zote Waziri amezitoa kwa vile nataka tu nionyeshe kwamba kuanzia sasa na kuendelea kazi yetu kubwa ya PAC itakuwa ruksa ya Mheshimiwa Spika kuangalia zaidi ukaguzi wa ufanisi na ukaguzi wa kiufundi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitoe tu ufafanuzi kidogo maana ya ukaguzi wa ufanisi. Hii ni aina ya ukaguzi uliojikita kuangalia kama uwekevu tija na ufanisi yaani economy efficiency na effectiveness miongoni mwa taasisi za umma katika matumizi ya rasilimali ili kufikia malengo waliyojiwekea. Ukaguzi wa ufanisi huchunguza iwapo shughuli mipango au miradi ya Serikali inayohusisha ukusanyaji wa matumizi ya fedha za umma inafanyika kwa kuzingatia kanuni hizo tatu, yaani uwekevu, ufanisi na tija. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukaguzi wa kiufundi technical audit ni ukaguzi unaojumuisha uchunguzi na tathmini huru juu ya upangaji, usanifu ununuzi na utekelezaji wa miradi ya ujenzi kwa lengo la kutoa matokeo ya usimamizi na utekelezaji wa miradi hiyo. Wahusika juu ya masuala yote yanayoathiri utekelezaji na utendaji wa miradi hiyo.

Mheshimiwa Spika, ukaguzi wa kiufundi ni ukaguzi katika mchakato mzima wa utekelezaji wa mradi kuanzia hatua ya maandalizi ya awali utekelezaji wa mradi, ukamilishaji na makabidhiano ya mradi. Hujikita zaidi katika kutazama kama mradi utetekelezwa kwa wakati ndani ya gharama iliyokusudiwa, kwa ubora uliokusudiwa, na kama malengo ya uanzishwaji wa mradi yametimia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama walivyochangia Waheshimiwa Wabunge nguvu kubwa sasa ya Bunge ni lazima ielekezwe kwenye kupitia na kujadili kaguzi za namna hii kwani zinasaidia sana kuweka uwajibikaji wa fedha za umma badala ya kuangalia kaguzi za hesabu tu yaani financial audit reports peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja ya uondoshaji wa magari imeongelewa kwa kina hasa magari kuuzwa bei ya chini ya soko, kutokuwepo kwa uwazi katika uondoshaji wa magari na kuchelewa kutoa vibali vya uondoshaji wa magari. Pia hoja ya utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu imesisitizwa, umuhimu wa kusimamia ukusanyaji wa mapato kwa vyanzo vya ndani ilivyoainishwa na umuhimu wa takwimu ili kuweza kufanya tathmini ya utekelezaji wa mpango. Pia hoja nyingine ambayo imegusiwa kwa undani hasa na ripoti ya CAG juu ya matengenezo ya miradi ya maji wachangiaji wamesisitiza usimamizi unaofaa wa miradi ya maji ili kuleta tija, pia ulipaji wa madeni ni jambo muhimu katika kuhakikisha kwamba miradi yetu ya maji inakuwa endelevu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo naomba sasa kutoa hoja kwamba Bunge likubali kupokea Taarifa ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kwa mwaka 2023 pamoja na maoni na mapendekezo ya Kamati ili yawe Maazimio ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)