Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Halima James Mdee

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. HALIMA J. MDEE - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, nami niwashukuru Wabunge wote waliochangia, jumla ya Wajumbe waliochangia ni 11, Mheshimiwa Munde T. Abdallah, Mheshimiwa Twaha A. Mpembenwe, Mheshimiwa Venant D. Protas, Mheshimiwa Ally J. Makoa, Mheshimiwa Michael C. Mwakamo, Mheshimiwa Ester A. Bulaya, Mheshimiwa Suma I. Fyandomo, Mheshimiwa Jacqueline N. Msongozi, Mheshimiwa Esther N. Matiko, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu L. Nchemba, Mheshimiwa Deogratius Ndejembi na Mheshimiwa Innocent L. Bashungwa japokuwa kwangu aligusiagusia kiujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitaanza kwa kujibu hoja kadhaa kisha nitaliomba Bunge likubali mapendekezo ya Kamati yetu kwa sababu hakuna mabadiliko yoyote ambayo yameletwa mbele ya Meza yako.

Mheshimiwa Spika, kwanza niseme hivi, kwamba ni kweli Mheshimiwa Rais anapenda na pamoja na timu yake kuelekeza fedha huko chini, humu kuna lugha hapa inatumika kwamba Mheshimiwa Rais ameshusha fedha, ni kweli kabisa jana wakati Kamati ya Bunge ya Bajeti inapitisha taarifa yake hapa ilituambia kwamba Deni la Serikali ni trilioni 87.4, wakasema ongezeko la deni limetokana na ukopaji kwa ajili ya kugharamia miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, viwanja vya ndege, elimu, afya, kilimo, mifugo na nishati ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, taarifa yetu LAAC ilijikita kwenye eneo la elimu, eneo la afya, miundombinu inayofanania hivyo. Sasa tunachozungumza hapa ni kweli fedha inaweza ikatafutwa lakini fedha ikishatafutwa ikishuka huko chini inaenda kusimamiwa kwa ufanisi? Kama fedha haisimamiwi kwa ufanisi wa kuwajibika hapa ni nani? Yupo sahihi kabisa! Rais ni mtu mmoja lakini Rais si ana miguu, ana mikono ana vidole, sasa ninyi Wasaidizi wa Rais ndiyo inatakiwa mmsaidie Rais. Sasa si Wasaidizi wa Rais wanakuja hapa wanatumia mgongo wa kumpamba Rais wakati wao hawatekelezi wajibu wao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilisema hapa, hii ni mikopo kwa sababu kila mmoja anajua bajeti yetu haijawahi kujitosheleza, kama tutaweza kujitosheleza tutalipa mishahara, tutalipa Deni la Taifa, ikiisha hivyo hatuna pesa abishe Mheshimiwa Mwigulu hapa. Sisi tunachozungumza ni nini? Kwamba kunapokuwa kuna Mawaziri, kunapokuwa kuna Wakuu wa Mikoa, kunapokuwa kuna RAS kunapokuwa kuna ma-DAS, kunapokuwa kuna Wakuu wa Wilaya kunapokuwa kuna Wakurugenzi wanalipwa mishahara kuna wataalam wanafanya kazi gani? Simple mathematics. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunachozungumza hapa ni kila mmoja atekeleze wajibu wake kwa nafasi yake, kila mmoja awajibishwe kwa nafasi yake lakini asionewe, awajibishwe baada ya kuchunguza na kujiridhisha ndipo tutatengeneza uwajibikaji kwenye Taifa hili, hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili suala la idadi ya wataalam amezungumza hapa ndugu yangu Mheshimiwa Ndejembi amesema wameajiri Wahandisi 362, sasa nisaidie tu Mheshimiwa Ndejembi nijibu pia na Mheshimiwa Mwigulu, sisi tunapofanya kazi yetu huwezi kutuambia ni ripoti ya miaka miwili mitatu iliyopita, utaratibu wa Kamati za oversight za Bunge ni kweli taarifa inatoka ya mwaka fulani lakini wakati wanakuja kukutana na Kamati ya Bunge kwa kipindi kile, wameenda kwenda kurudia tena hivi Serikali hapa mlikuwa mmekosea hapa, hapa na hebu tupeni majibu mpaka sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunapozungumza wakati hili ni Bunge la mwezi wa pili si ndiyo? Bunge la mwezi wa pili, wakati tuko kwenye Kamati Januari Wakaguzi walikutana na Serikali. Kwa hiyo Taarifa hizi tunazozizungumza hapa za upungufu wa watumishi ni upungufu si wa miaka miwili iliyopita, hii ni taarifa current. Sasa basi tu-assume ni taarifa ya zamani, imesema mmeajiri Wahandisi 362, mmepeleka kila Halmashauri Mhandisi mmoja mmoja. Kilwa kwa mfano, tumesema ilikuwa na Wahandisi wanne mkadiraji majenzi mmoja, miradi 157 ya force account, tufanye mmempeleka watano, sasa Wahandisi watano ndiyo wasimamie miradi 157 ndiyo akili hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Nzega kulikuwa kuna Mhandisi mmoja, tu-assume alichokisema ndugu yangu ni correct haya wakadiriaji ujenzi, Mhandisi mmoja, Nzega akapelekwa mwingine wa pili, haya Wahandisi wawili ndiyo wanaweza kusimamia miradi ya force account 115? Haiwezekani! Ndiyo maana watu walioleta hii force account ukisoma muongozo wa PPRA uko-clear, yaani huu muongozo una vipengele 36 ungefuatwa kwa ufanisi wake wala tusingekuwa tunatoana mapovu hapa, kwa sababu kila kitu kingeenda smooth. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa mwongozo unasema general conditions for the use of force account, general conditions! Inasema lazima taasisi nunuzi au procuring entity iwe na qualified personnel ambao wanatambulika na relevant professional bodies to carry out and supervise the required works. Yaani muwe na watu ambao wanakidhi vigezo, wana taaluma ile inayotakiwa na wanatambuliwa na vyombo vya kitaaluma kuweza kufanyiwa kazi, sasa hivi nurse amewahi kuwa, daktari amewahi kuwa, Mwalimu amewahi kuwa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hayo mambo tunayazungumza kwa nia njema, hatutaki mje hapa mjitetee kwa sababu idadi ya wataalam ni pungufu ndiyo maana tunasema tugawane kazi. Ndiyo maana leo Kamati yetu ukiona hiyo miradi midogomidogo sijui milioni 50, milioni 20, milioni kumi, haina shida kwa sababu ni miradi basic, na tunaposema makandarasi hapa kwamba hatusemi wa nje, hivi kweli hatuna Watanzania wanaoweza kufanya kazi za hiyo thamani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii kwenye force account, risk ni kwa Serikali, hatu-shift reliability kwenda kwa mtu mwingine, mnatengeneza hamna wataalam, mnajenga vitu vya hovyo, vikiharibika huna mtu wa kumfanya awe accountable! We should use simple common sense, hakuna mtu anayetafuta mchawi hapa, tunataka kama mnampenda Rais kama mnavyosema, ninyi si ndiyo wasaidizi wake, msaidieni basi, halafu mkishamsaidia hamtahitaji kujieleza yeye mwenyewe ataona hawa wamenisaidia, hilo la pili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu, Mheshimiwa Msongozi nashukuru kwa mifano yako uliyoizungumza hapo, ndiyo yanayosemwa, kuwe na ukomo wa gharama, uliyozungumza Mheshimiwa Msongozi umezungumza katika lugha ya kidiplomasia lakini inasemekana pesa wala hazitoshi kwa sababu pesa zikienda zina mikono mingi! Hiyo ndiyo ilivyo, kwamba zikienda zina mikono mingi, kazungumza Mheshimiwa Bulaya, kazungumza Mheshimiwa Msongozi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tunasema, tutasema mpaka mfanyeje? kuwe na ukomo. Mheshimiwa Mwigulu ninashukuru hukuleta lile pendekezo lako kwa sababu sisi tumesema hivi, kwenye moja kati ya mapendekezo yetu, kuwe na ukomo wa gharama za mradi wa force account. Sasa wewe ukituzungumzia kwa sababu Sheria ya Manunuzi tunayoipitisha ilikupa-room ya kutengeza Kanuni.

Mheshimiwa Spika, hakuna popote kwenye Sheria ya Manunuzi ambako tumezungumza hili jambo, ndiyo maana tukasema kwenye Kanuni mtakazozitengeneza Bunge liazimie ukomo uwepo. Sasa kama wewe umeshatengeneza Kanuni zako ulitakiwa useme hapa kwamba tumetengeneza Kanuni. Kanuni mpaka ifikie Kamati ya Sheria Ndogo ndiyo itakuwa imefikia Bunge, sasa hiki unachozungumza ni kitu ambacho unacho wewe sisi hatukijui, it is well and good kama umefanya hivyo then Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo italetewa tutaona kwamba kwenye hili eneo kuna ukomo ili wapewe fedha ambao wana uwezo wa kuifanyia kazi. Hilo ni jambo la tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, fedha zitolewe kutokana na jiografia ya eneo, imeshazungumzwa vizuri. Nizungumze hoja nyingine ilizungumzwa na Mheshimiwa Ndejembi kama sikosei, wakitaka kuhalalisha milioni 800 na kadhaa ambazo tulizungumzia kuhusiana na Nzega. Kwanza nimsahihishe alitakiwa ajue lakini nataka nimsahihishe, kwamba Nzega ilitumia hela katika mazingira mawili. Mazingira ya kwanza ni hiyo milioni 470 ambayo ilishushwa lakini kulikuwa kuna fedha nyingine milioni 379. Hii milioni 379 siyo fedha ya ndani ya Nzega. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mapato ya Nzega DC hawana ubavu wa kuwa na hii pesa kwenda kupeleka kwenye mradi mmoja, ubavu huo hawana. Hii pesa iliingia Halmashauri katika mwaka wa fedha 2018/2019 kwa ajili ya elimu bure ikawa imekula pause pale, watu walikuwa wanailia timing isishtukiwe hilo wanajua wenyewe. Mwaka 2021/2022 Halmashauri ya Nzega iliomba kibali cha kutumia shilingi milioni 379 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Kata ya Nzega. Kwa hiyo, kwanza nilitaka ajue siyo fedha ya ndani ni fedha ambayo ilikuwa kwenye Halmashauri, kwa ajili ya elimu bure, elimu bure haikufanyika, ikasubiri huko imetulia 2021/2022 wakaomba.

Mheshimiwa Spika, sasa swali linakuja, hivi labda niwarudie ili kuwaelimisha hiyo milioni 470 ilikuwa katika muktadha wa ujenzi wa vyumba nane vya madarasa, maabara za sayansi tatu, jengo moja la utawala, maktaba moja, chumba cha ICT kimoja, vyoo 20 vya wanafunzi yaani wavulana 10 na wasichana 10, matenki mawili ya maji kila moja lita 10,000 na nguzo ya kuweka tanki husika na miundombinu ya kawaida kwa ajili ya maji, ndiyo ilikuwa 470.

Mheshimiwa Spika, wenzetu wa Nzega wakatumia shilingi milioni 849, tunaambiwa walijenga ghorofa. Sasa sisi tuliokuwa kwenye Kamati ambao tuna taarifa hizi kwa mapana, hizi idadi za majengo ambayo yamezungumzwa hapa kama nilivyoyataja, ndiyo exactly idadi ya majengo ambayo Nzega wamejenga. Sasa tukajiuliza, halafu wamejenga ghorofa moja, hivi ghorofa ukijenga ile floor moja ile, yaani kale kanaitwa kasakafu eeh! Ile sakafu ambayo inatenganisha nyumba ya chini na nyumba ya juu ndiyo shilingi milioni zaidi ya 200 inayokaribia 300! Hivi huu msingi ambao sasa, maana na ninyi si mnajenga maghorofa yenu kwenu jamani, si ndio!

Mheshimiwa Spika, huu msingi ambao ndiyo unashindiliwa zaidi ili kuweza kubeba hivyo vyumba vingine vinne vya madarasa huko juu, ndio una justify milioni karibia 300 na nyongeza? Hapana. Kuna Halmashauri ya Arumeru nadhani, wao wamejenga ghorofa mbili, siyo haka kaghorofa kamoja ka Nzega, ghorofa mbili, haijafikisha hata shilingi milioni 700, kitu kimetulia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunachojaribu kuzungumza hapa ni nini? Hatutaki muwe watetezi pale ambapo hamna taarifa sahihi zilizofanyiwa uchunguzi za haya mambo. Mkigeuka watetezi, ndiyo maana hii nchi inakuwa ngumu kuibadilisha. Huwezi kubadilisha nchi pale ambapo mtu ambaye tunafikiria atakuwa msaada wa Rais katika kusimamia jambo, anakuwa ndio mtetezi. Mimi nilidhani angesema tumekuwa, tukafanyie kazi.

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana sisi kwenye maazimio yetu tumewaambia, kwa sababu mwongozo wa Serikali umeeleza categorically kwamba uhai wa majengo yenu yanatakiwa yaweje? Miaka 50, miaka 75, wengine kwenye madaraja huko miaka 100. Tumewaambia nendeni mkafanye ukokotoo, mkakokotoe ili mjiridhishe kwamba je, kwenye hayo majengo yaliyojengwa, yamejengwa kwenye thamani inayotakiwa. Sasa badala mkafanye hiyo kazi halafu mje na findings, Waziri anasimama hapa anatetea nyongeza ya shilingi milioni 300 kwa sababu eti kuna ka-floor kamoja kalichotenganisha juu na chini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, halafu tulisema hapa, hakuna mtu anayebisha kwamba practically kilichoandaliwa na TAMISEMI kama baseline huku Makao Makuu kutokana na tafiti ambayo labda wamefanya kwenye maeneo fulani hakiwezi kuongezeka. Hakuna aliyebisha. Hata sisi kama Kamati hatujakataa kwamba kutoka shilingi milioni 470 inaweza ikaongezeka hadi shilingi milioni 500, hatujakataa, inaweza ikaongezeka hadi shilingi milioni 550, hatujakataa, lakini tunataka nyongeza iweze kuwa justified. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hawa jamaa zetu tuliokuja kuhojiana nao, amezungumza Mheshimiwa mmoja hapa, unawaambia okay, sawa mmeongeza ngapi? Tuambie shilingi ngapi? Wakati huo wameshakaa na CAG mpaka wiki tatu zilizopita wameshindwa kuafikana, sisi tunawaambia okay tunawapa benefit of doubt. Tulitakiwa tusiwasikilize kwa sababu jicho letu mmeshindwa kulisaidia, wala kulipa kulipa majibu, tunawasikiliza basi. Kama wataweza kueleza sana, ataenda shilingi milioni 10, atapiga 20 halafu akifika 30 anaona maneno yanaisha. Anaanza kusema, Mheshimiwa sina maelezo ya ziada.

Mheshimiwa Spika, ukimwambia okay, naomba BOQ, yaani BOQ kuipata kwa wale jamaa ni vita. Sasa unajiuliza, kama ninyi ni wasafi na wanyoofu kama mnavyosema, kwa nini kunakuwa kuna mapambano makali pale Kamati ya Bunge inapotaka BOQ kutoka kwenu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sisi tunawaomba tu ndugu zetu hawa wajue kwamba hatuna nia mbaya. Tunakaa mpaka saa sita usiku Kamati yako, nawashukuru Wajumbe wangu kwa uvumilivu, kwa ajili ya kufanyia kazi mambo haya ambayo kimsingi yalitakiwa yafanywe na mabwana na mabibi au ndugu zetu hapa pamoja na ile mikono na miguu ya Rais, ili Bunge lako likija kusikiliza mambo haya, tunakutana na vitu ambavyo vimefanyiwa kazi na watu ambao wana akili zao timamu, na watu ambao wameajiriwa kwa ajili ya kufanya kazi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, baada ya maelezo hayo, kwa sababu tumekubaliana in principle kwamba tatizo lipo, na kwamba kuna usimamizi hafifu wa miradi, hatuna wataalam, value for money haipo. Kwa hiyo, tunaomba yale maazimio ambayo Kamati yako ya Bunge iliomba Bunge lako liazimie, tunaomba kuweka msisitizo kwenye mapendekezo ambayo Kamati imeyatoa.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mapendekezo haya hayajafanyiwa mabadiliko na mtu yeyote, tunaomba Bunge hili Tukufu liweze kuyaazimia mapendezo yote na Serikali iyatekeleze kikamilifu ili kuondoa upungufu wote uliyobainika kwa manufaa na ustawi wa nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi