Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Emmanuel Adamson Mwakasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi hii uliyonipa ya kuchangia Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nianze kwa kuipongeza Serikali chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na viongozi wote akiwemo Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Naibu Waziri Mkuu na Viongozi wote wa Serikali kwa jinsi wanavyofanya kazi nzuri sana ya maendeleo katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na Sensa ya Watu. Sensa iliyopita inaonesha kwamba nchi yetu idadi yetu imeongezeka sana. Ni zaidi ya miaka 10 tulikuwa hatujafanya sensa, lakini nilikuwa na hoja katika eneo hilo kwamba baada ya sensa tumekuwa tuna maswali mengi humu hasa ya kuongeza maeneo ya utawala. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mahali popote kama kuna watu wameongezeka hata kwenye familia zetu lazima kuna vitu vitabadilika tu, lakini baada ya sensa hii ukiangalia maeneo ya utawala, kwa mfano, kata zetu ni zile zile hata baada ya sensa hii, mitaa ni ile ile na vitongoji ni vile vile. Suala la utoaji huduma baada ya watu kuwa wameongezeka kwa kweli inakuwa ni shida.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali iangalie upya suala la namna ya kugawa maeneo na kutenga bajeti ambapo itasaidia wananchi kupata huduma kwa urahisi baada ya sensa hii ya kuongezeka kwa watu, kwa sababu bado sehemu za utawala ni zile zile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali hasa kwenye suala la umeme. Upatikanaji wa umeme ulikuwa ni mgumu sana katika kipindi kilichopita, lakini kwa sasa kuna unafuu mkubwa. Naipongeza sana Serikali chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo ameweza kushughulikia kwa kiwango kikubwa hili tatizo la umeme. Umeme ni uchumi na bila umeme shughuli nyingi zinasimama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi hizo, bado kuna tatizo. Hata juzi hapa tumeona tatizo la kukatika kwa umeme karibu nchi nzima, na moja ya sababu ambayo imetolewa ni kwamba maji sasa yamezidi, sijui mvua zimezidi, sasa maji yanakwenda kwenye mitambo, yanaharibu mitambo. Naishauri Serikali, wakati inanunua vitu hivi, nilitegemea kwamba suala hilo wangekuwa wameliona.

Mheshimiwa Naibu Spika, unapotegemea kwamba mvua zitakuja katika kiwango kidogo, au unasikia kuna mafuriko na vitu kama hivyo, nilitegemea Serikali ingekuwa imechukua tahadhari kwamba maji hata yakizidi, basi mitambo isizimwe kwa sababu maji yamezidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, niliona kwenye taarifa moja kwamba, hata mitambo ya Bwawa la Mwalimu Nyerere ilizimwa kwa sababu hiyo ya kwamba maji yalizidi yakawa yanaingia kwenye mitambo. Kwa hiyo, naomba Serikali iweze kuliangalia hilo kwa sababu kwa kweli halijakaa sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza pia Ofisi ya Waziri Mkuu kwa namna walivyoshughulikia suala la utwaaji wa maeneo, na hasa maeno yanayolizunguka Bunge. Niliangalia ile Taarifa ya Kamati ya Bajeti ukurasa wa 4 – 5, Serikali ilikuwa imetoa fidia ya shilingi bilioni 12.2 kwa ajili ya wale wakazi ambao wanazunguka maeneo ya Bunge, kwa maana ya taasisi mbalimbali. Wengine wameshaanza kuhama na wameshaondoka, lakini kuna baadhi bado wapo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna taasisi kama GPSA bado wapo, pia NFRA bado wapo na Bodi ya Nafaka, pengine na taasisi chache. Naomba Serikali kwa sababu tayari imeshatoa fidia na hawa waliobaki waweze kuondoka ili sasa maeneo yaweze kufanyiwa shughuli ambazo Bunge imepanga kuzifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuchukue mfano wa wenzetu wa Kenya au Zambia, sisi hata wakija wageni wetu humu tunakutana nao canteen; wakija wananchi wetu, tunakutana nao canteen au nje ya Bunge, lakini pia hata magari ya Waheshimiwa Wabunge mengi yanakaa nje na mengine mbali kabisa, kitu ambacho pia ni hatari, hakiko salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu wa hizi nchi nilizozitaja na nyingine, nadhani ni pamoja na Rwanda, maeneo ya Bunge ndiyo kuna Ofisi za Wabunge humo humo ambazo wanaweza kukutana na wapigakura wao maeneo ya Bunge. Hata vifaa vyao vya usafiri vinakuwa ndani ya maeneo ya Bunge. Kwa usalama, pia ni muhimu kwa maeneo hayo kuchukuliwa haraka ili yaweze kufanyiwa kazi ambayo ilikuwa imepangwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nizungumzie suala la mbolea ya ruzuku na hasa mwaka jana, 2023. Mwaka jana Serikali kweli ilifanya kitu kizuri kutoa mbolea kwa wananchi katika sehemu nyingi. Hata hivyo, nikichukulia kilichotokea Tabora, maeneo mengi hasa kwenye jimbo langu la Tabora Mjini, mbolea ya ruzuku ilikuja lakini utaratibu wake wa kugawa ulikuwa hauko sawasawa kabisa. Wananchi wengi walipanga foleni hata siku mbili bila kupata mbolea, lakini na wengine waliishia kutokupata kabisa na usumbufu ulikuwa ni mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mliona mpaka kwenye vyombo vya habari wengine mpaka walikuwa wanalalamika kwamba walipata majeraha mbalimbali kwa ajili ya kugombania mbolea. Kwa hiyo, naishauri Serikali kwamba, inapotoa tena mbolea ya ruzuku kama ilivyotokea mwaka jana, 2023 na siku nyingine basi utaratibu upangwe, uwe mzuri, ambao hautakuwa usumbufu kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, niliona nichangie hayo maeneo machache. Naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)