Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kondoa Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
3
Ministries
nil
MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi nami nichangie katika hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu. Pia naipongeza Serikali kwa kazi kubwa inayofanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa napitia hotuba hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu, nimeona namna Serikali ilivyopeleka fedha mfano kwenye hili Fungu 65, walipangiwa kwenye miradi ya maendeleo shilingi bilioni 14.7 na zimeenda shilingi bilioni 10 mpaka Februari, 2024. Ni jambo la kuipongeza Serikali, lakini ni vema pia Serikali ikaangalia sana hapa katika hili Fungu 65 kwamba, fedha hizi ziende kwenye programu za kusaidia vijana katika kuwapatia ujuzi na programu za kukuza kazi za staha kwa vijana kwa malengo yale yale ya kuwasaidia kuweza kujiajiri na kupata maendeleo yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu hiyo basi, nilikuwa napitia hotuba hii nikaona kuna hii programu ambayo ilianzishwa ya kazi za staha ambayo asilimia 100 inategemea fedha kutoka kwa wafadhili. Kwa maana hiyo, walihitajika wapate shilingi bilioni 1.3 mpaka Februari, 2024, walipata shilingi milioni 310 peke yake. Jambo hili limesababisha programu yenyewe kutokuwa na tija na mwaka wenyewe wa fedha ndiyo huu unaisha, na ukiangalia hata hiyo shilingi milioni 300 imetumika kwenye kuboresha Sera ya Taifa ya Vijana, Hifadhi ya Jamii ikiwemo na fedha ya watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia programu hii, iko katika hatua za chini sana, lakini uhitaji kwa vijana katika mitaji na vitu kama hivyo ni mkubwa kwa ajili ya kutengeneza ajira. Kwa hiyo, ninaunga mkono ushauri wa Kamati ya kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu ijikite zaidi kwenye kuwajengea uwezo na kuwapa ujuzi vijana pamoja na kujikita kwenye hiyo programu hasa ya kuwagusa wale vijana wenyewe kwenye hiyo project.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto nilizoziona kwenye bajeti hii ya Wizara na nilivyopitia hotuba ya Kamati, inaonekana kwamba, bado tija haijaonekana juu ya hizi programu mbili ambazo ziliwalenga vijana. Kwa maana hiyo, sasa Serikali ijikite moja kwa moja kuhakikisha hizi project zinaleta tija kwa vijana.
Mheshimiwa Naibu Spika, yako mambo mengi na changamoto nyingi ambazo zinawa-face vijana na watu wenye ulemavu. Kwa maana hiyo, Serikali inatakiwa sasa iongezwe nguvu na juhudi kubwa katika kuhakikisha miundombinu inajengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano mmoja, mimi niko Jimbo la Mjini Kondoa lenye Kata nane na mitaa 36. Vijana wa mjini wanatarajia wawekewe miundombinu mizuri kwa ajili ya kuendesha maisha yao. Mfano, miundombinu ya umeme bado utekelezaji wake upo chini sana. Kwa sisi ambao tupo kwenye Majimbo ya Mijini, umeme ni ajira kwa vijana, na umeme unawasaidia vijana kuweza kujitegemea katika shughuli mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukikuta mitaa ya mjini haina umeme halafu tunataka vijana waweze kujiajiri, haitawezekana. Maana yake mjini hatuna mashamba, tunatarajia tupate umeme na miundimbinu iliyoboreshwa ndiyo vijana waweze kujiajiri. Hata huo ufundi ambapo tunakwenda kuwapa hizi project za kuwaongezea ujuzi vijana, kama miundombinu haijakaa vizuri kwenye majimbo yetu, basi moja kwa moja hatutafikia malengo. Tunawapeleka watoto kwenye vyuo vya ufundi, wakija mitaani wanakutana na miundombinu hafifu ambapo wanashindwa kujiendeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiongelea vijana wa Jimbo la Kondoa Mjini mathalani, kuna mitaa zaidi ya 10 hata nguzo ya umeme hakuna. Sasa utawapelekaje vijana hawa kwenda kujifunza kuchomelea au kujifunza saluni na vitu vingine kama hivyo? Watawezaje kutumia ujuzi wao hali ya kuwa miundombinu hiyo haitoshelezi? Kwa maana hiyo, naomba, kwa kuwa hii ni Ofisi ya Waziri Mkuu, ndiyo ina Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Naibu Waziri Mkuu yupo dada yetu Mheshimiwa Judith Kapinga ambaye nilimweleza masuala haya ya umeme, naye ameyachukulia serious, na ninadhani kupitia Bunge lako, Mheshimiwa Kapinga aliniahidi kwamba weekend hii atakwenda kutembelea jimboni kuona hali halisi ya miundombinu ya umeme ilivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mitaa haina nguzo ya umeme na haina umeme. Kwa maana hiyo, hata ukipeleka ujuzi kwa vijana kule, hawawezi kutekeleza majukumu yao kwa sababu hawana miundombinu ya kusaidia kuwafikisha pale wanapotaka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kupitia Bunge lako, nakuomba mambo mawili. Kwanza, naomba Naibu Waziri atekeleze ahadi yake ile ya weekend kwenda kutembelea Jimbo la Kondoa Mjini tukaone hali ya mitaa ambayo haina umeme, lakini cha ajabu unakuta kuna Jimbo lina vijiji 84 na vijiji vyote vina umeme, ila mitaa 36 haina umeme.
Mheshimwa Naibu Spika, vijana wa mjini hawana mashamba, wanatarajia wachomelee, wafungue saluni, wauze maduka ya vinywaji, lakini hakuna umeme, watafanyaje? Kwa maana hiyo, hilo nilikuwa naomba lifanyiwe kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili katika kuwajengea uwezo vijana ili kuwasaidia kupata miundombinu, tujikita hapo hapo kwenye umeme, iko mitaa yangu ambayo ilipata bahati ya project za umeme wa REA, ni muda umeenda sana, karibu mwaka wa pili huu, ila kwenye hiyo Kata ya Suruke miundombinu imekamilika, lakini mkandarasi hajawasha umeme. Kwa maana hiyo, ujio wa Naibu Waziri unaweza ukamsukuma mkandarasi kwenda kuwasha umeme ili wale vijana waweze kupata miundombinu ya kujipatia kipato kwa kufungua biashara ambazo zinaendana na masuala ya umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili kuna mtaa ambao umerukwa na nguzo za umeme zipo, zimekaa pale, hazina kazi. Nimeulizia, nikaambiwa kwamba zitaondolewa pale na kupelekwa jimbo lingine la vijijini. Sasa kama mji unakosa umeme halafu nguzo zimepelekwa mtaani, kesho zinanyanyuliwa zinahamishwa kupelekwa sehemu nyingine za vijiji, tunaona hapa kuna haja ya kuliangalia hili vizuri. Ukienda kukuza vijiji ukaacha miji ikabaki haina umeme, bado itakuwa hatujaitendea haki hii miji, na tutakuwa hatujafanya vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Bunge lako pia liweke msisitizo juu ya jambo hili kwamba nguzo zile zilizopo pale zibaki zihudumie mitaa. Hata kama ni za mkandarasi, lakini kwa sababu najua Naibu Waziri Mkuu yuko hapa, anaweza akaelekeza nguzo zile zikabaki zifanye kazi kwenye Mitaa ya Guruma na Chemchem. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haraka tu nikutajie. Mpaka leo kwenye mitaa 36 hakuna hata nguzo na ni Halmashauri ya Mji. Kuna Mtaa wa Chemchem, Mtaa wa Kwa Mtwara, Tampori, Hachwi, Kutumo, Chora, Mongoroma, Chandimo, Guruma, Chavai, Choi, Gongo na Kereri. Maeneo haya yana wakazi wengi na makazi mengi lakini hakuna umeme. Kwa hiyo, ili kuwasaidia watu wale na jamii zile za mjini, na kwa sababu hatuna mashamba mijini, naomba Ofisi ya Waziri Mkuu iweze kusaidia mitaa hii kupata umeme ili ile sera na project ya Serikali ya kuweza kuwasaidia vijana kujiajiri iweze kufanikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)