Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi nami pia nichangie siku ya leo. Awali ya yote napenda kumshukuru Mungu kwa kunipatia nafasi nami kuweza kuchangia. Namshukuru sana Waziri Mkuu kwa hotuba yake ya jana ambayo ni nzuri sana na iliyosheheni mambo mengi sana ambayo kwa kweli yanaonesha kwamba nchi yetu tunakwenda mbele sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo naomba nichukue nafasi hii kumshukuru sana Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika suala la sekta ya afya. Nitajikita katika sekta ya afya kwa sababu taarifa nyingi sana za masuala ya afya haziwafikii wananchi, na zinapowafikia pia, zinafika kwa malalamiko. Nakupongeza sana dada yangu na Naibu Waziri, mnafanya kazi kubwa sana katika masuala ya afya, na kwa kweli tumesogea mbele sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu nijikite leo kuelezea mambo ambayo Serikali inayafanya ambayo wananchi wengi hawayajui au wanapata taarifa ambazo siyo sahihi. Nianze kwa kusema tu kwamba, Tanzania katika miaka hii mitatu ya Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imefanya kazi kubwa sana katika kuongeza wigo wa masuala ya afya. Watu wengi walikuwa wanakwenda nje kwa ajili ya afya, lakini sasa hivi tumepunguza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze tu kwa haraka haraka kusema kwamba, huduma za ubobezi zimeongezeka sana katika nchi ya Tanzania. Kwa mfano, suala la ugonjwa wa figo lilikuwa ni gonjwa ambalo likipatikana, watu walikuwa wanaona labda ni suala gumu, lakini sasa hivi katika nchi yetu katika mwaka 2020 mpaka 2023, teknolojia imeongezeka sana kiasi cha kuweza kutengeneza figo kwa kutumia matundu madogo na kuweza kuweka figo kwa wananchi wetu. Kwa hiyo, hayo ni mafanikio makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia jambo la pili ni katika upandikizaji wa uroto. Uroto ilikuwa ni changamoto kubwa sana na ndiyo unaotengeneza white blood cells katika mwili. Uroto ukikosekana, basi mtu hawezi kuishi, lakini Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu amefanya kila njia, na kuanzia mwaka 2021 tumekuwa na wagonjwa 11 wameanza kupandikizwa uroto na wanaishi kwa matumaini. Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa sana pamoja na Naibu Mawaziri, tunawapongeza sana kwa kazi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, isitoshe katika sehemu hii ya afya kulikuwa na tatizo kubwa la kuondoa uvimbe kwenye ubongo. Ilikuwa mtu akipata trauma au tatizo la ubongo, ilikuwa ni shida. Ilikuwa mara nyingi huyu mtu kuishi siyo rahisi, lakini kwa muda mfupi sana Rais ameweza kufanya hili jambo na tunaweza sasa kupitia matundu ya kwenye pua, wagonjwa sita wamefanyiwa operation ya ubongo. Kwa kweli ni mafanikio makubwa kwa muda wa miaka mitatu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Mheshimiwa Rais pamoja na Mawaziri na wafanyakazi wote wa Wizara wameweza kuvunja mawe kwenye mfumo wa mkojo kwa kutumia mionzi bila upasuaji. Hili jambo lilikuwa siyo la kawaida. Tuna wagonjwa 510 ambao ni wengi, lakini kwa muda wa miaka mitatu wameweza kupatiwa matibabu hayo. Sasa hivi hata likitokea tatizo lolote la mawe katika mfumo wa mkojo mtu anaweza akaenda kupata matibabu katika hospitali zetu. Kwa hiyo, ni mafanikio makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni upasuaji wa saratani ya utumbo mpana kwa njia ya haja kubwa. Kwa kweli pia lilikuwa ni changamoto. Ilikuwa mtu akipata saratani, inaonekana ni ugonjwa mkubwa sana na wengi walikuwa wanakufa. Miaka mitatu ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu, na miaka mitatu ya Waziri Ummy Mwalimu pamoja na Naibu wake na Mawaziri wengine, wagonjwa 410 wameweza kufanyiwa hii huduma na kwa kweli ni mafanikio makubwa sana. Sasa hivi hata mtu akiwa na tatizo hilo la saratani ya utumbo siyo issue tena ya kufikiria kufa. Kwa hiyo, ni mafanikio makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niendelee kusema tu kwamba, kumekuwa na ubobezi katika masuala ya uzazi. Saratani ya uzazi ilikuwa ni changamoto sana. Mwanamke alikuwa akipata matatizo ya saratani alikuwa anajiona labda huenda ni mtu wa kufa, lakini kuanzia Julai, 2020 muda mfupi sana watu 92 wamepata hii huduma. Hivi tusema nini? Kwa kweli afya imeboreshwa sana katika hii miaka mitatu. Tunampongeza sana Rais wetu, tunaipongeza sana Serikali pamoja na Mawaziri wote ambao mmefanya hii kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kuna upasuaji wa ubobezi wa kupandikiza nyonga na magoti kuanzia mwaka 2022. Februari tu mpaka leo watu 135 tumeokoa shilingi ngapi za Watanzania? Kwa kweli, tuwe wakweli, tuseme Rais amefanya kazi kubwa sana. Nimeenda leo kwa data ili kuonesha kwamba sekta ya afya imefanikiwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kuna upasuaji wa matundu madogo ambayo yanaitwa endoscopy procedures, watu 24 wamefanyiwa upasuaji na umefanikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme hivi, afya ndiyo kila kitu. Mtaji wa binadamu ni afya. Tunakwenda sasa kuboresha bima kwa wote, tutafanikiwa. Kwa namna tulivyokwenda, hakuna jinsi, tutafanikiwa. Hakuna mahali ambapo, hata mkuyu ulianza tu kama mchicha, tutafanikiwa. Kwa hali ilivyo sasa hivi, wagonjwa wana matumaini. Tumetoka huko kwenye ma-paracetamol tumekwenda huku kwenye upasuaji mkubwa, wala watu hawafikirii kwenda nje. Nampongeza sana Rais kwa kazi anayofanya na vilevile nawapongeza sana madaktari ambao wamejitolea. Hii sasa inawajengea vijana wetu ari ya kuona kwamba, kumbe haya yanawezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vijana wengi sana waliokuwa wanafikiria wakimaliza tu mtihani, japo walikuwa wanapenda sana kupata Division One, walijua hawawezi kuajirika Tanzania, lakini hawa wanaofanya hizi kazi ni Watanzania na ukienda hata Mloganzila ni Watanzania. Mheshimiwa Dkt. Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya, mimi nakuita Doctor, hongera sana pamoja na Naibu wako.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile salamu nyingi ziende kwa Rais wetu, amefanya kazi kubwa. Afya ya wananchi inapoimarika, basi kazi zitafanyika. Najua mengi ni muhimu, barabara ni muhimu, na kila kitu ni muhimu, lakini ndugu zangu mtu kama huna afya, utatumia hivyo vitu?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa haya matibabu sasa hivi yanapatikana nchini, naomba nitumie fursa hii kuwaambia, tusinung’unike, jambo likitokea kama uvimbe na kadhalika, tujitokeze, huduma zipo, na zinapatikana. Kwa kweli Rais anafanya kazi kubwa, naomba salamu hizi zimfikie na kwa kweli, Mungu ambariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi. (Makofi)