Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Eng. Ezra John Chiwelesa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Biharamulo Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami pia nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika hotuba hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kipekee nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo anaifanya. Tukiangalia Hotuba hii ya Waziri Mkuu, imeelezea maendeleo ya miradi yote mikubwa ya kitaifa na yote iko katika hali nzuri. Sasa, tunapoona Taifa linawekeza fedha nyingi katika miradi hii ya maendeleo especially miundombinu, maana yake ni kwamba hili ni Taifa linalokua, ni Taifa lenye uchumi mzuri na ni Taifa ambalo lina malengo makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata Mataifa yote makubwa, mfano leo uende China au Dubai na kwingineko, zile nchi bado zinajenga kila siku. Wanajenga barabara kila siku, pamoja na kwamba wana barabara nzuri, wanaongeza reli wanafanya na vitu kama hivyo kwa sababu uwekezaji katika miundombinu ndiyo unaonyanyua Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo, pia nampongeza sana sana Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anayoifanya. Tumemwona amekuwa ni msaada mkubwa sana kwa Mheshimiwa Rais kwenye kuisimamia Serikali, na kila anapofanya ziara, anapokanyaga sehemu, Wabunge wote na wananchi wote wa Tanzania ni mashahidi, amekuwa akiacha alama hasa akikemea ubadhirifu na vitu vingine kama hivyo. Kwa hiyo, tumpongeze. Halikadhalika tunampongeza Naibu Waziri Mkuu, na wasaidizi wake wote kwenye ofisi yake wakiongozwa na Mheshimiwa Jenista ambaye yuko hapa. Kwa kweli kazi mnayoifanya ni kubwa na hivyo ni lazima tuwapongeze kwa haya mazuri ambayo mnayafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema haya, ninayo mambo kama mawili ya kuongelea kuhusu jimbo langu, na pia nitaongea na mambo mengine ya Kitaifa. Kwenye masuala ya jimbo langu, kwanza nashukuru kwa miradi mingi sana ya maendeleo. Tumepata fedha nyingi kwenye miradi ya maendeleo kama vile maji, barabara, afya, elimu, umeme na mambo mengine ambayo yanafaa kwa ajili ya wananchi. Wananchi wamefarijika na mambo ambayo yanaendelea kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yako maombi ambayo niliyawasilisha hapa, ni mwaka wa pili sasa. Kwenye maombi ya kimkakati ya Mkoa wa Kagera tuliomba ujenzi wa Stendi ya Biharamulo, tukaambiwa tulete andiko. Tulishaleta andiko la shilingi bilioni 2.7, liko kwenye maombi ya Kimkakati ya Mkoa wa Kagera, sasa ni mwaka wa pili; tumeomba ujenzi wa jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo, sasa ni mwaka wa pili. Tumeleta maombi ya shilingi bilioni 3.4 na tukajibiwa kwamba wanaingiza kwenye bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni aibu Wilaya kongwe kama ya Biharamulo unapokuja unapofika ofisi za halmashauri zimejaa magrili utafikiri maduka ya Mangi. Kwa kweli ni aibu. Hata sisi ifikie hatua tuonwe, na ionekane kwamba tunastahili kuboreshewa hii miradi. Zile conditions ambazo mmeziweka za kupeleka miradi ya maendeleo hasa majengo ya halmashauri kwenye wilaya mpya tu, sioni kama zinafaa kwa sababu zinawaonea hawa wa zamani. Hawa ni wakongwe, na hawakutaka wawe vile. Lazima Serikali iwekeze kote, iangalie hata wa zamani iweze kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba kwenye bajeti hii, hasa kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, mambo haya mawili ni muhimu kwa ajili ya watu wa Biharamulo. Nimeshaomba mara nyingi hata mbele ya Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo, naomba tupate majibu watu wa Biharamulo kwamba ujenzi wa Stendi ya Biharamuro na jengo la halmashauri unaanza lini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tuliomba habari ya kuongezewa maeneo. Biharamulo ni wilaya iliyokua na ninavyoongea leo ndilo jimbo lenye watu wengi kwa Mkoa wa Kagera, likiongoza kwa Mkoa wa Kagera, na ni jimbo namba 20 kwa wingi wa watu Tanzania hii, lakini hatuongezewi maeneo kwa sababu tumezungukwa na hifadhi kila upande. Kwa hiyo, nimeomba haya maeneo mara nyingi, na ninadhani nitaweka vizuri kwenye hotuba ya Wizara ya Maliasili na Utalii, lakini ombi lichukuliwe, tuongezewe maeneo, kwani watu wanaongezeka lakini maeneo ya kufanyia shughuli za uchumi ni machache kwa sababu tumezungukwa na Hifadhi ya Buligi, tumezungukwa na maeneo yote ya TFS, sasa wananchi hawana pa kwenda. Wakichunga ng’ombe wanakamatwa, wakienda kulima wanakamatwa. Kwa hiyo, Serikali ilione hilo na itoe maelekezo maalumu ili watu waweze kuongezewa maeneo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niseme kwa niaba ya wenzangu wote wanaotoka maeneo ya mipakani. Tumelia sana na habari ya NIDA. Wewe najua unatokea Ilala pale, unaweza usiulizwe kuhusu NIDA, lakini sisi tunaotoka mikoa ya pembezoni, NIDA imekuwa kilio kikubwa. Sisi ni Watanzania kama Watanzania wengine, lakini inapokuja kwenye suala la kupewa vitambulisho vya Taifa, imekuwa kama tunaonekana tunatokea sehemu nyingine tumekuja kuvitafuta hapa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaomba Serikali itoe majibu hapa, maana hili jambo niliuliza humu zaidi ya mara mbili tunaambiwa wanashughulikia, lakini imefikia hatua mbaya. Pale kwangu Biharamulo yuko mtumishi mmoja wa Ofisi ya Uhamiaji, watu wanaenda pale kuomba kujaza hata fomu tu, akishamwona tu, anamwambia wewe sio Mtanzania, anamfukuza. Hata kumpa fomu ajaze hampi. Ukitaja jina, anakwambia siwezi kukupa fomu wewe siyo Mtanzania. Sasa Utanzania wa mtu unapimwa kwa majina au kwa kumwangalia sura, au umpe fomu ajaze, baada ya hapo ndipo muanze kufanya vetting, umjue ni Mtanzania au sio Mtanzania!

Mheshimiwa Naibu Spika, huyo mtu anaenda mbali, alienda Mheshimiwa Diwani mmoja akapeleka watu pale, inafikia stage anamwambia mimi si¬-deal na wanasiasa. Hivi kweli hu-deal na wanasiasa, Waziri wako Mheshimiwa Masauni ni nani? Siyo mwanasiasa? Kwa hiyo, tunaomba kwanza hizi dharau za watumishi ziishe. Wanapohudumia Watanzania kule wanatengeneza chuki ya watu dhidi ya Serikali yao kwa majibu ya ovyo kama hayo ambayo hata walioko juu hawayajui. Wananchi wanaenda kule wanarudi wakilalamika tumenyimwa vitambulisho, tumenyimwa hiki. Ukiwaambia mjiandikishe kwenda kupiga kura, wanakwambia kwenye kupiga kura mnatukumbuka, lakini kwenye vitambulisho sisi sio Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunawaomba watumishi wa Serikali kupitia Bunge hili wasikie na wajue wapo kwa ajili ya kuwatumikia Watanzania. Wasiichonganishe Serikali na Watanzania na wasimchonganishe Mheshimiwa Rais na Watanzania. Wafanye kazi yao, wawe na wasemaji. Kama wewe siyo Mtanzania, ujibiwe kwa documents na sio mtu unaenda, anakunyima hata fomu. Umesafiri, umetoa nauli, unafika pale hata fomu tu ya kujaza unanyimwa. That is not fair. Kwa hiyo, tunaomba hilo liangaliwe, lichukuliwe na Wizara ya Mambo ya Ndani, mtumishi huyo afuatiliwe Biharamulo. Hamkutuletea mtu wa kuwa kero, anatakiwa aondoe kero za wananchi kukosa vitambulisho, asiwe kero hata ya kuwanyima fomu ya kujaza. That is not fair. Naomba niliweke wazi hapa ili lichukuliwe na Serikali ilifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikimaliza hayo, wewe ni shahidi na unakumbuka kwenye Bunge la mwezi wa Pili Wabunge tulisimama tukaongea kwa habari ya uharibifu wa barabara na tukajibiwa na Serikali, kweli 20% iliyokuwa imebaki ilitangazwa, baadhi ya barabara zinaendelea. I was very specific, nilisema, kuna barabara ziliongezwa za shilingi bilioni 350 kwa kutumia system ya EP4R, tukaambiwa zitakuja shilingi milioni 500 kila jimbo kwa ajili ya kuanza ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri wa Fedha akaliambia Bunge hapa kwamba zile fedha ameelekeza ziende na zile barabara zitatangazwa, lakini ninavyoongea hapa, nawe ni Mbunge wa jimbo, nina uhakika jimbo lako nalo limo, kama zimeletwa Dar es Salaam kwa watu wa mjini, sawa. Kwetu Biharamulo hizo barabara hazijaletwa...

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ezra jitolee mfano mwenyewe, usiguse kabisa mambo ya Ilala. (Kicheko)

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimepokea, hayo ni maelekezo. Najua sigusi Ilala, lakini ni sehemu ya majimbo. Kwa hiyo, ninachoomba, tunataka tupate majibu. Ahadi aliyoitoa na Mheshimiwa Waziri wa Fedha ndani ya Bunge hapa ilikuwa ni kututuliza Wabunge tuondoke kuelekea majimboni ili ile ajenda tuiache au nini? Kwa sababu tumeondoka hapa tukijua barabara zinatangazwa. Tumefika kule, na tulishawaambia wananchi juu ya ujenzi wa zile Barabara, lakini mpaka leo imebaki miezi mitatu tumalize Bunge hili la Bajeti ilhali hatujui direction ya ile barabara, hatujui nini kinaendelea. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunataka tupate majibu ya Serikali kwamba shilingi milioni 500 ya ile nyongeza ya shilingi bilioni 360 ambayo iliahidiwa humu ndani ya Bunge wakati tunapitisha bajeti hii tunayoendelea nayo, zile barabara zinatangazwa lini? Kwa sababu kama maelekezo yalikuwepo ni lazima tuzione. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia, tumesema nchi hii tunafanya miradi mikubwa sana ya maendeleo lakini iko habari ambayo tumekuwa tunaiona, kwamba ushirikishwaji wa Watanzania kwenye miradi hii mikubwa tunayoisema ni mdogo sana. Ni lazima tuseme, miradi hii yote mikubwa; miradi ya reli, miradi ya ujenzi wa barabara tunayoisikia hapa, ujenzi wa meli na vitu vingine vyote vikubwa haifanywi na wazawa. Miradi hii inafanywa na wageni. Inafanywa na kampuni kubwa sana za kigeni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunaomba, tumeona Serikali imefanya bidii kubwa sana kwenye habari ya Wizara ya Kilimo. Katika miradi ya kilimo riba imeshushwa mpaka single digit, lakini unavyokuja kuangalia, mwajiri mkubwa katika miradi hii mikubwa ya maendeleo ni Serikali. Kwa hiyo, kama ni Serikali na miradi hii inakatiwa bima, ni miradi ambayo hata cash flow yake na sustainability yake ni kubwa, hata benki zinapokopesha zina uhakika wa kulipwa kwa sababu ni miradi inayoonekana, ni miradi ya Serikali. Tunaomba kupitia Bunge hili, Serikali irudi mezani ikaongee na benki, kwani wakandarasi wengi wa Kitanzania wanashindwa kuwa competitive kwenye miradi hii mikubwa, wanaishia kuwa sub-contractors, kwa sababu hawana uwezo wa kukopesheka katika riba nzuri, halikadharika hawezi kushindana kwenye bei wakati wanafanya tender.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa tunaomba hata wakandarasi wa nchi hii kupitia Serikali, kupitia CRB kaeni chini muongee na benki, wakandarasi wakopesheke kwa single digit. Haiwezekani leo mtu anatoka China anakopeshwa kwa asilimia saba kwenye nchi yake, lakini hapa ukakope kwa asilimia 22 na uweze kuwa competitive. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Haya Bwana China, muda wako umekwisha.

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi. Naunga mkono hoja. (Makofi)