Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru nami kupata nafasi ya kuchangia katika wizara hii. Nitajikita zaidi katika eneo la kilimo. Tunafahamu kabisa nyanda za juu kusini, mikoa mitano inalisha takribani Taifa zima. Kinachoshangaza, Benki ya Kilimo ambayo kimsingi tunafahamu kwamba yenyewe ndiyo inatakiwa kusaidia wakulima wadogo wadogo, bado wakulima hao wapo kwenye matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Benki ya Kilimo kwenye bajeti hii inasema imetoa takribani shilingi bilioni 160 kwa wakulima, lakini ukipiga hesabu ya wakulima hawa, hawazidi asilimia 10 ya wakulima ambao ndio wengi katika Taifa hili. Tunaomba Benki ya Kilimo ijikite kusaidia wakulima wadogo wadogo wapunguze masharti ili wakulima hawa waweze kupewa mikopo hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia kilimo, kuna mazao ya kimkakati. Tunafahamu zao la chai ni zao muhimu sana, na zao la chai katika soko la dunia bado linahitajika. Hata kama wataalamu na wadau wanadai vita ya Ukrain imesababisha bei hii kushuka, lakini bado chai katika biashara ya ndani inanyweka, hata katika East Africa pia chai inanyweka. Chai hii inapatikana sana Wilaya ya Rungwe na kwa inapatikana kwa ndugu zetu wa Njombe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakulima wa chai ni watumwa katika Taifa lao. Leo hii tuna wawekezaji, kwa mfano nikichukulia kwa Mkoa wa Mbeya, tuna viwanda viwili; Kiwanda cha Katumba na Kiwanda cha Busokelo. Mwekezaji ameamua kuuza kiwanda kile bila kuwashirikisha wakulima wadogo wadogo. Baada ya kuleta malalamiko, anasema kwamba, anawapa AMCOS ndiyo wawe wananunua. Naomba katika wizara hii, msimamie mwekezaji huyu kama kweli hiyo chai anawapa AMCOS, tunaomba mfuatilie lakini wakulima walinunua shares, leo ni zaidi ya miaka 15 katika zile share walizonunua hawajawahi kupata faida na wala kile walichokipanda hawajakivuna bado. Naomba Serikali msimamie hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la bei, tumelia sana na bei. Wakati tunaanza kulalamika hapa, bei ilikuwa ni shilingi 132 kwa kilo, angalau mmepandisha mpaka shilingi 366. Kwa hilo nawapongeza, lakini bado chai inahitajika kuwa na bei kubwa kwa sababu wanunuzi wake wanauza nje kwa bei kubwa zaidi. Kwa nini mkulima anyonywe wakati pembejeo ni za kwake, anaishughulikia yeye, anakuja kupata shilingi 360? Tunaomba chai iongezeke bei ifike shilingi 700 angalau ili mkulima aweze kujikwamua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumzia habari ya parachichi, kule nyanda za juu kusini. Parachichi tunaita ni zao au dhahabu ya kijani, kwa maana leo hii parachichi inalika kama dawa, ni chakula, na ina soko dunia nzima, lakini mzalishaji wa zao hili pesa anayopata ni ndogo. Leo kilo ni shilingi 1,600 au 1,500, lakini ukienda Uingereza kwa soko la leo, parachichi moja ni pound saba. Tunamsaidiaje mkulima wa kawaida? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kibaya zaidi ndugu zetu majirani, East Africa wanakuja wananunua parachichi hizi wanapeleka nchini kwao, wanazi-brand kwa majina yao wakati sisi tupo. Naomba Serikali msimamie hilo. Wizara ya Viwanda na Biashara hakikisheni mnatoa mafunzo kwa wakulima tuweze na sisi ku-export na tupate faida kama Wanarungwe kama Wanambeya, na kama Watanzania na Wananjombe pia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, ninazungumzia suala la TAZARA, Reli ya TAZARA miaka ya 1974 na kuendelea. Rais wa Kwanza alifanya vizuri sana na reli hii ilikuwa inasaidia sana kutoka Dar es Salaam mpaka Zambia, Kapiri Mposhi. Leo hii mzigo mkubwa upo kwa Tanzania. Wenzetu wa Zambia wamekuwa wakisuasua, hawachangii mchango wanaotakiwa kuchanga, deni kubwa limebaki kwa Tanzania. Watanzania kwenye TAZARA wanadai madeni mengi sana hasa ya wafanyakazi. Tunaomba msimamie hilo, wafanyakazi wapate haki yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie madeni. Wakandarasi wengi sana wanadai, lakini kibaya zaidi, mikataba ya ukandarasi tunayoingia inaongeza riba kwa sababu hawalipi kwa wakati. Leo hii Serikali inadaiwa takribani shilingi trilioni moja, tunawezaje kuweka madeni haya? Mzigo huu ni mzigo kwa Mtanzania anayelipa kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna watu wamepisha ujenzi wa barabara au miradi yoyote katika nchi nzima, na wanadai shilingi trilioni saba. Serikali hamwatendei haki Watanzania. Tunaomba fedha hizi zilipwe. Watu hawaendelezi majengo, hawafanyi maendeleo, wanadai fedha. Tunaomba mwalipe. Tunaomba sana sana, tusimamie haki ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba kujua, kuna suala ambalo sasa linaendelea, Serikali ikisimama hapa itueleze kuhusu mitandao ya kijamii. Tunaomba nchi yetu iende kidigitali. Tumeomba kwa muda mrefu na tumeingia huko. Nimepata taarifa, na ninaiomba Serikali itupe taarifa rasmi kuhusu ulipaji wa WhatsApp, kwamba makundi ya whatsApp yalipiwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi sijafahamu, naomba nielekezwe ndani ya Bunge lako Tukufu, makundi haya yapo ya kifamilia, ya kiukoo, ya kijiji na mikataba mbalimbali. Kama ni kweli yanayosemwa kwenye mitandao, tunaomba myaingilie tuweze kuwa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni unyanyasaji wa kijinsia kupitia hiyo mitandao. Wasichana wengi wamesemwa vibaya na kusingiziwa kwenye mitandao, hata wanasiasa pia. Tunaomba Serikali isimamie. Tunajua wanaoandika na kutuma kwenye mitandao hii ni rahisi kuwapata kwa kuwa TCRA ipo. Tunaomba msimamie haki ya watu wanaozushiwa uongo kwenye mitandao. Wanaozusha uongo wowote, wachukuliwe hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niliyoyasema yafanyiwe kazi. Mwisho wa siku nitaangalia kama naunga mkono au siungi mkono. Ahsante, naomba kuwasilisha. (Makofi)