Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Ally Mohamed Kassinge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilwa Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ya kuchangia hotuba ya bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Naanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi ambazo anazifanya. Pia nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Mawaziri wote na Manaibu katika ofisi yake kwa namna ambavyo wanachapa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, utakubaliana nami kwamba kutokana na mabadiliko ya tabianchi, maeneo yetu mengi nchini yameathirika na mvua za El-Nino ambazo bado zinaendelea. Kutokana mvua hizo, siyo tu miundombinu ya barabara na miundombinu mingine iliyoharibika, bali pia imeleta athari na madhara kwa makazi pamoja na maisha ya watu nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kwa upekee wake kuwapa pole Watanzania kwa ujumla wao, pia kipekee wananchi wa Kilwa ambao wameathirika na mvua hizi katika maeneo yafuatayo kwa muhtasari; Somanga, Kinjumbi, Njinjo, Kipindindi, Miguruwe, Chumo, Nanjirinji, Kiranjeranje, Kikole, Mirumba, Makangaga, Mbwemkuru. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hatua ambazo Serikali imekuwa ikizichukua, ikiwa ni pamoja na kufika katika maeneo haya na kwenda kushughulika na miundombinu ya barabara iliyoathirika, lakini kwa upekee wake naomba Ofisi ya Waziri Mkuu, Kitengo cha Maafa, kitembelee maeneo haya ya Wilaya ya Kilwa ambayo nimeyataja kwa muhtasari wake ili wakafanye tathmini ya athari iliyopatikana na kwa kweli wananchi hawa wanahitaji msaada wa kibinadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo, naipongeza Wizara ya Ujenzi, kwani baada ya madhara haya, walipata fursa ya kuja katika Mkoa wa Lindi na wametembelea katika maeneo machache ambayo yalikuwa yameathirika. Naomba kupitia Bajeti hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwamba, Kilwa nayo ni sehemu ambayo imepata madhara makubwa na imeharibu miundombinu mikubwa ya barabara. Barabara za kutoka Njia Nne mpaka Kipatimu, Nangurukuru mpaka Liwale, Nangurukuru mpaka Kiranjeranje na barabara kutoka Kiranjeranje mpaka Nanjilinji kupitia Makangaga hizi zimeathirika kwa kiwango kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Wizara ya Ujenzi, to see is to believe (kuona ndiyo kuamini). Wafike katika maeneo haya wajionee ili hatua za haraka zichukuliwe kama ilivyokuwa katika maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije katika eneo la barabara ya Nangurukuru - Masoko. Barabara hii nimekuwa nikiizungumzia mara kadhaa katika Bunge lako Tukufu kwamba, ndiyo lango la kupitia kuelekea bandari ya uvuvi ambayo inaendelea kujengwa pale Kilwa Masoko. Vile vile uthamini na usanifu wa barabara hii ulikuwa ni wa muda mrefu, mpaka sasa Serikali bado haijatoa fedha kwa ajili ya kukarabati na kuboresha barabara hii ambayo kiukweli kutokana na shughuli za ujenzi wa bandari zinazoendelea, barabara hii sasa inapitisha mizigo mizito ya mchanga, mawe na material nyingine kwa ajili ya ujenzi wa bandari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kabla bandari haijakamilika mwakani, kwa ahadi ya Serikali, barabara hii ndani ya bajeti hii ifanyiwe utaratibu wa kutengewa fedha kwa ajili ya kuiboresha na kipande chake cha kutoka Nangurukuru mpaka Masaninga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije katika sekta ya miundombinu kwa upekee wake, viwanja vya ndege. Katika Bunge lako hili Tukufu tulipitisha Mpango wa Miaka Mitano wa Kuboresha Viwanja 12 vya Ndege kikiwemo Kiwanja cha Ndege cha Kilwa Masoko. Kiwanja hiki hakipo katika kiwango kinachotakiwa, na tulipitisha katika Mpango, lakini mpaka ninapozungumza hapa, bado Serikali haijatoa fedha za kutosha kwa ajili ya kuboresha kiwanja hiki katika kiwango kinachohitajika. Ulifanyika uthamini mwaka 2013 ambapo wananchi 144 walioathirika, walikuwa bado hawajalipwa. Ukafanyika uthamini wa pili mwezi Juni, 2023, wananchi wameongezeka kutoka 144 mpaka 447, bado hawajalipwa fidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Kilwa wanaathirika. Maeneo hayo ni katika Vitongoji vya Mchomoro na hususan Maeneo ya Mnazi Mmoja, Sanga, Utabiri pamoja na Kisangi. Wamekuwa wakiwasilisha hoja yao hii kila wanapopata fursa ikiwa ni pamoja na kunituma Mbunge wao kulieleza suala hili hapa Bungeni, nami nimelizungumza mara kadhaa ikiwa ni pamoja na Mkutano wa Kumi na Moja wa Bunge la Bajeti. Nirudie, kutokana na athari ambayo wananchi hawa 447 wameendelea kuipata na kutolipwa fidia kwa muda mrefu, wamebaki wakiwa na makazi ambayo hayana hadhi, na wameshindwa kuyaendeleza kwa sababu tayari yapo katika utaratibu wa kulipwa fidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mheshimiwa Zainab Telack katika utaratibu wake wa kusikiliza kero za wananchi, alifika Kilwa Masoko. Moja ya hoja alizowasilishiwa ni pamoja na hii. Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa akasema, “ninaichukua kwa lengo la kuwasiliana na wenzangu katika Serikali ili wananchi hawa waweze kulipwa fidia.” (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kwa msisitizo, Serikali ipo hapa Bungeni, walisikilize hili na wananchi wangu hawa walipwe fidia ndani ya muda mfupi ujao kabla hatujamaliza Bunge hili la Bajeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)