Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Vincent Paul Mbogo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwanza naunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nampongeza Mheshimiwa Rais, kwa kazi kubwa anayoifanya kwa kuwaletea wananchi maendeleo katika sekta mbalimbali za afya, elimu, miundombinu pamoja na mawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo Nkasi Kusini lina barabara za kiuchumi ambazo ni barabara ya Wampembe - Kala - Mpasa - Kizumbi. Hizi barabara zimeathirika sana. Kwa hiyo, naiomba Serikali itenge fedha za dharura ili ziweze kwenda kufanya matengenezo ili wananchi waendelee kupata usafiri na huduma za kiuchumi na biashara zao ziendelee, kwa sababu zinaelekea ukanda wa Ziwa Tanganyika. Kwa hiyo, zilipokatika, wananchi wamebaki kwenye kisiwa. Ziwa likichafuka, hawana pa kwenda. Kwa hiyo, wagonjwa wengine wanakufa kwa sababu miundombinu imeharibiwa. Nilikuwa naishauri Serikali itenge fedha kwa haraka iende ikatengeneze hizo barabara za Wampembe - Kizumbi - Kala - Mpasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni umeme. Yapo maeneo ya uzalishaji ya vijiji, ambayo nilikuwa naomba kabla hii miradi ya umeme kwenda, ukafanyike utafiti kwenye yale maeneo ambayo vijana wamejiajiri katika maeneo ya uzalishaji, ndiyo waanzie huko kupeleka umeme. Mfano, Vijiji vya Masamba, Kyela, Mwinza, Izinga Kapumbuli na Kilambo cha Mkolechi. Haya maeneo ni ya uzalishaji ukanda wa Ziwa Tanganyika na yanahitaji umeme. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni suala la fidia. Kuna barabara hizi za TANROADS zilijengwa. Nyumba nyingi zilibomolewa hasa Kijiji cha Chala. Watu hawaelewi kuwa wananchi wanacheleweshewa maendeleo. Naomba wananchi wangu wapatiwe jibu, wanalipwa ama hawalipwi, ili waendelee kufanya shughuli zao za maendeleo na kujenga nyumba bora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Nkasi Kusini, Kata ya Kizumbi na Ninde yapo maeneo mazuri ya kuanzisha uboreshaji wa skimu ya umwagiliaji, lakini katika jimbo zima hakuna skimu hata moja na haya maeneo Kata zilishaandaa. Kwa hiyo, naiomba Wizara ya Kilimo iende kuanzisha skimu za umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Nkasi Kusini pamoja na Mkoa wa Rukwa, kuna Ziwa Rukwa na Ziwa Tanganyika, lakini hatuna Chuo cha Uvuvi. Hawa wananchi hawapati elimu ya uvuvi. Pamoja na kupumzisha ziwa na mikakati mingi, lakini kama wananchi hawana centre, hawana chuo cha kupata elimu ya uvuvi itakuwa ni kazi bure. Hata tukipumzisha ziwa, samaki wakazaliana, uvuvi haramu utaendelea, kwa sababu wanavua kienyeji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Naibu wa Waziri Mheshimiwa Mnyeti, alifika Rukwa na nilimwomba akatuahidi ujenzi wa Chuo cha Uvuvi Kata ya Wampembe kati ya Kata tatu ili wananchi wafike pale wapate elimu. Wananchi wa Ziwa Tanganyika na Ziwa Rukwa wapate elimu waanze uvuvi wa kisasa. Naomba kwenye bajeti uwekwe huo ujenzi wa Chuo cha Uvuvi Kata ya Wampembe, Jimbo la Nkasi Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lipo suala ambalo linachanganya sana. Kwanza niwape pole wananchi wa Wilaya ya Nkasi, Ukanda wa Ziwa Tanganyika. Nimefanya takwimu, ndani ya miaka mitatu, siyo chini ya wananchi 30 wameliwa na mamba ikiwa ni pamoja na wanafunzi, kwa sababu wengi wanafuata huduma ya maji katika Ziwa Tanganyika. Wakienda kule wanakutana na mamba, wengi wameliwa na mamba hasa wanafunzi na watu wazima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wizara hizi tatu; Wizara ya Uvuvi, Mheshimiwa Mnyeti, Naibu Waziri wa Uvuvi, naomba unisikilize Bwana! Hili suala lipo serious, na picha nilimtumia Waziri wa Maliasili watu wanavyoliwa na mamba. Wapo wavuvi ambao unawapumzishia ziwa, wanaliwa na mamba. Kwa hiyo, Wizara ya Uvuvi, Wizara ya Maliasili na Wizara ya Maji wakae pamoja watenge bajeti waende wakaainishe maeneo yaliyo salama kwa kila kijiji ili wananchi wajue kuwa wanapoenda kutafuta huduma ya maji, ni sehemu salama. Kwenye maeneo hatarishi wawekewe mabango, wajue, kwa sababu wanaoliwa ni wanafunzi na wananchi wanaofanya biashara za samaki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Rais, alihamasika sana kutoa ruzuku za mbolea na wananchi wamelazimika kulima, na mwaka huu kuna mavuno mengi sana ya mahindi. Naomba Wizara itenge na iongeze vituo vya ununuaji wa mazao, mwananchi asije akapata gharama ya kusafirisha mazao mbali kutoka eneo analolima. Mfano, Kata ya Kala na Kate kutengwe vituo vitakavyomwezesha mwananchi kutokupata gharama ya kusafirisha kutoka eneo la kununulia mazao.

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo shule chakavu sana hasa sekondari zile kongwe. Mfano, Sekondari ya Chala ni kongwe, iliyojengwa na wazazi, haikujengwa na lenta, imeharibika. Itengwe bajeti ikaboreshwe pamoja na kupatiwa madawati. Kuna shule za msingi zimechoka, mfano, Shule ya Msingi Yondokazi, Liyapinda, Sintali na Ninde. Hizi shule zimechoka, pamoja na Mahakama za Mwanzo. Mfano, Kata ya Kate, mahakama wanayotumia ni godauni, huku wameweka magunia, huku hakimu anaendelea kuendesha kesi; na nyingine ni Mahakama ya Mwanzo Kata ya Chala. Mahakama hizo zimechoka, naomba zitengwe fedha ili ziweze kuboreshwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)