Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Daimu Iddi Mpakate

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili nami mchana huu nichangie hoja iliyopo Mezani. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu na kutoa mawazo yangu mawili matatu.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumshukuru Rais wetu wa Awamu ya Sita, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea miradi mingi kwenye majimbo yetu pamoja na Jimbo la Tunduru Kusini. Moja ya miradi ambayo inaleta faraja kwa watu wa Jimbo la Tunduru Kusini ni miradi ya afya, elimu, maji pamoja na barabara. Jimbo la Tunduru Kusini lilibahatika kupata vituo vya afya vitatu na zahanati nane. Vituo vya afya viwili vimekamilika lakini hamna watumishi mpaka hivi leo, na hata vifaatiba bado havijaweza kupatikana. Kati ya zahanati nane, zahanati tatu bado hazina watumishi kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona nianzie hapo kwa sababu Bunge lililopita 2021 Waheshimiwa Wabunge tuliongelea sana suala la ajira ya watumishi wa afya na walimu. Hiyo imekuwa ni changamoto kwa upande wa mikoa na majimbo yaliyopo pembezoni mwa nchi. Tunapoajiri wafanyakazi kutoka maeneo mbalimbali kwenda kwenye majimbo yetu hasa ambayo siyo asili ya maeneo yale, matokeo yake baada ya mwaka mmoja watumishi wote wanakuwa wanahama, wanarudi huko walipotoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, mwaka wa fedha uliopita pekee yake, Jimbo la Tunduru Kusini na Halmashauri ya Tunduru wamehama wafanyakazi wa afya 57 na kuacha zahanati nyingi zikiwa na mtumishi mmoja mmoja au wawili na nyingine hazina watumishi kabisa, kwa sababu ya wafanyakazi wote walioajiriwa kwa mwaka 2021 wamepata uhamisho kurudi mahali ambapo wametokea. Mara nyingi inatokea hasa kwa watumishi wa kike, wengi wameajiriwa wakiwa hawajaolewa, lakini baada ya mwaka mmoja wote wanaleta vyeti vya kuolewa na wanaondoka katika maeneo yetu na kuacha wananchi wetu bila huduma yoyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu ni ule ule niliotumia mwaka 2021, tunaomba Serikali iangalie, wakati wanaajiri watumishi hawa, basi waangalie mazingira wanayowapeleka yafanane na yale waliyotoka ili angalau kila jimbo au kila halmashauri ipate watumishi; walimu na watumishi wapya kutoka maeneo yao ili waendelee kukaa katika maeneo yetu, kwa sababu inaonekana sasa imekuwa ni kama mradi, wanachukua ajira kupitia maeneo yetu na baadaye wanafanya mipango, wanarudi kwenye maeneo ambayo wametokea. Hili jambo kwa kweli kwenye maeneo yetu ya upande wa kusini imekuwa ni changamoto kubwa. Ninaomba Serikali waliangalie, wakati wanatoa ajira hizi, basi waangalie watu wanaotoka maeneo ambayo yanafanana ili waendelee kukaa na kutoa huduma kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo napenda niongelee ni suala la barabara. Barabara ya Mtwara Pachani – Nalasi – Tunduru imekuwa ni kilio chetu cha muda mrefu. Tayari barabara hii imeshafanyiwa upembuzi yakinifu tangu mwaka 2020, lakini kila mara, hata asubuhi mwenzangu, Mbunge wa Namtumbo ambaye ana kilometa 200 kwenye barabara hii, nami nina kilometa 100, amelizungumza na kuulizia. Barabara hii iko kwenye Ilani ya Uchaguzi. Upembuzi yakinifu tayari, lakini mpaka leo dalili za kuwa barabara hii inatengenezwa kwa kiwango cha lami, bado hazionekani.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ni muhimu hasa kwa upande wa ulinzi. Jimbo letu la Tunduru Kusini pamoja Namtumbo limepakana na Msumbiji, hali ni mbaya upande wa pili, na askari wetu wanaitumia sana barabara hii kwa ajili ya kufanya patrol na kulinda nchi yetu ili tusiathirike na wale waasi wanaotoka upande wa pili.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaikumbusha Serikali, kwa sababu ya umuhimu wa barabara hii ya ulinzi na uchumi wa Wilaya hizi mbili; Tunduru na Namtumbo, wanategemea katika maeneo haya, basi ni vyema sana Serikali ifanye hima watusaidie kupata kipande cha lami ili barabara ile iweze kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo napenda nilizungumze, ni kwamba Mkoa wa Ruvuma tumepata neema kubwa ya kuwa na makaa ya mawe maeneo ya Ngaka pamoja na Wilaya ya Mbinga na Songea Vijijini. Neema hii imekuwa ni kubwa, na magari yamekuwa ni mengi. Tumekuwa na mpango wa muda mrefu wa kujenga reli ya kusini, lakini kila mwaka tunavyokuja kwenye bajeti hatuoni dalili zozote za kuwa na mpango wa kujenga reli hii. Tumekuwa tunazungumza, na mara nyingi wanasema kuhusu PPP, lakini reli hii itakuwa ni mkombozi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu barabara ya kutoka Songea kwenda Mbinga, Songea kwenda Makambako, Songea – Tunduru – Masasi mpaka Mtwara, kwa sababu siyo chini ya malori 2,000 kwa siku yanapita kwenye barabara hizi, matokeo yake barabara zinachimbika. Dawa pekee ya kuhakikisha barabara hizi zinaendelea kudumu ni ujenzi wa reli ya kusini ambapo upembuzi yakinifu ulishafanyika kwa muda mrefu. Ni reli ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa. Makaa ya mawe huwezi kusafirisha kwa ndege, yakisafirishwa kwa treni itakuwa ni bora zaidi na itaongeza uchumi kwenye kanda zetu za kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana hili jambo pamoja na kwamba bajeti zetu hazisemi, mara kwa mara tunaendelea kutafuta wahisani. Naomba sana, Reli ya Kusini ni muhimu ili barabara zetu ziweze kupona kwa ajili ya mizigo mikubwa ambayo inasafirishwa na malori yale. Pamoja na barabara hiyo kuwa hivyo, barabara ya Songea kwenda Njombe, nayo mwaka jana, 2023 bajeti iliyopita walisema wataanza kujenga kilometa 100, lakini mpaka leo ile barabara bado haijaanza kufanyiwa chochote. Barabara ile sasa hivi ni mbaya kwa wanaopita na magari madogo, kwa kweli naiona adha ile ambayo wanaipitia. Barabara ile ina mashimo mengi sana kutokana na hayo malori ambayo tumeyazungumzia.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningependa sana nilizungumzie ni mgao wa maeneo. Majibu ya Serikali tunayasikia, lakini kuna maeneo hatutendi haki kwa sababu ya ukubwa wa maeneo yaliyokuwepo. Halmashauri ya Tunduru ni miongoni mwa halmashauri ambazo eneo lake ni kubwa ukilinganisha na wilaya nyingine. Wilaya yetu ina kilometer square zaidi ya 18,776, hata watumishi waliopo maeneo haya kuhudumia, Mkuu wa Wilaya imemhitaji atumie zaidi ya mwaka mmoja ili angalau apitie kila kijiji kwenda kufanya mikutano.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba, pamoja na dhamira nzuri ya Serikali kuendelea kuhudumia halmashauri ambazo hazina huduma, tunaomba mgao wa wilaya hii. Ni muhimu sana. Kwa sababu, eneo letu ni kubwa sana ambapo inakuwa ni ngumu kwa watumishi wetu kuhudumia hili eneo. Halmashauri tuna kata 35, kata moja ina watu zaidi 24,000 zingine zina watu zaidi ya 18,000, ni kwa sababu ya wingi wa watu na ukubwa wa eneo. Kwa kweli, tunaomba mtusaidie tupate eneo la utawala, halmashauri inahitajika nyingine ili tuweze kuwahudumia watu wetu vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nilikuwa napenda sana niliongee ni suala la tembo au ndovu. Ndovu kwenye Wilaya ya Tunduru ni kilio kikubwa sana. Mkutano wa Bunge uliopita tulipewa bajeti hapa kwa ajili ya askari wa kufukuza tembo. Tunashukuru tumepata askari wasiopungua wanane, lakini hawatoshi. Sasa hivi ndiyo kipindi cha tembo, na kwenye maeneo yetu wameshaanza kuleta madhara. Watu wawili wameshakufa mpaka sasa. Kwa mwezi wa Pili mwishoni tayari tumeshazika kwa sababu ya majanga ya tembo, lakini bado tayari wameshaanza kushambulia mazao ya wakulima kwenye mashamba yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana jambo la kifuta jasho cha wakulima kwa ajili ya tembo kuharibu mazao yao tukigeuze, badala ya kuwa kifuta jasho, yawe ni majanga. Kwa sababu, mkulima amelima heka mbili au heka tatu, asubuhi ameenda tembo amekula mahindi kwenye shamba lote. Hili ni janga. Huyu mtu atakula nini asubuhi? Kesho atakula nini? Kwa sababu shamba lake lote limeliwa na tembo. Tuweke katika maeneo ya majanga ili mkulima badala ya kusema apewe kifuta jasho, Hapana, liwe janga. Serikali iwafidie wakulima ili waweze kuishi vizuri, kwa sababu tusipofanya hivyo, kila mwaka kilio cha tembo kimekuwa ni kitu cha kawaida. Serikali imeshindwa kudhibiti tembo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sasa, kwa sababu tumeshindwa kuwafanya hao tembo wasiharibu mazao ya wakulima, basi hiyo iwe ni sehemu ya majanga ili inapotokea uharibifu, basi wakulima walipwe fidia na Serikali, badala ya kulipwa kifuta jasho, kwa sababu lile ni janga, ni jambo ambalo hawakukusudia. Mtu ameamka asubuhi, amekuta shamba lake limeliwa na tembo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wakati huu tunapoendelea na zoezi hilo, basi tunaomba tuongezewe askari. Sasa hivi ndiyo wakati mgumu sana kwetu sisi wakulima wa Tunduru kwa sababu tembo ndiyo wanatoka. Sasa wale wanaotoka Msumbiji wanakuja Tanzania pamoja na kujaa mto, lakini wanaogelea, wanakuja Tanzania kwa ajili ya malisho. Wanajua tayari Tunduru ina mazao yameshakuwa tayari, wanakuja kuyatumia kama chakula chao na hao tembo wa Selous ndiyo nao wanataka kutoka Selous, wanapita mbuga zetu za hifadhi za wananchi, wanarudi Tunduru. Kuna maeneo ambayo mpaka jana na juzi nimeongea na Mheshimiwa Naibu Waziri... (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante.

MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naunga mkono hoja.