Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Justin Lazaro Nyamoga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilolo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa uhai na nafasi hii niliyoipata ya kuweza kuchangia hoja hii. Pili, kwa niaba ya wananchi wa Kilolo namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya ya miradi mingi ambayo inatekelezwa katika Jimbo la Kilolo. Miradi ni mingi, siwezi kuitaja yote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa zaidi, barabara ya kutoka Iringa Mjini hadi Kilolo kwa sasa inajengwa, mkandarasi yupo site na tunashukuru sana. Pamoja na Barabara, pia ipo miradi mingine mingi sana ambayo yote kwa ujumla wake tunaishukuru Serikali kwa kazi nzuri inayofanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, napenda kuipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Mawaziri wote kwa kazi nzuri wanayoifanya na kwa utekelezaji wa mambo mengi. Tunaona kazi zao, na kwa kweli tunawapongeza. Nawapongeza Mawaziri wote na Waziri Senior, dada yangu Mheshimiwa Jenista kwa kazi nzuri na Manaibu wake tunampongeza na tunamshukuru kwa kazi nzuri sana ambayo anaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kuzungumza mambo mawili muhimu ambayo nadhani yanaweza kusaidia ustawi wa Taifa letu na pia kwa maeneo yetu. Jambo la kwanza ambalo napenda kuzungumzia ni suala zima la upelekaji wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara kwa TARURA na kwa TANROADS. Kwenye miaka ya nyuma tulikuwa na utaratibu mzuri ambapo barabara hizi zinatangazwa mapema, ikifika mwezi Januari au mwezi wa Pili, basi barabara zinatangazwa. Hii ilitokana na kwamba maeneo yenye mvua kama Jimbo la Kilolo, Mufindi na maeneo mengine, barabara zinatakiwa zianze kutengeneza mwezi wa Saba halafu ikifika mwezi wa Kumi mvua zinaanza. Kwa hiyo, tutakuwa tumekamilisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana, 2023 jambo hili halikufanyika kwa sababu kulikuwa na kitu kinaitwa NEST, ambao ni mfumo wa manunuzi, ulikuwa unabadilishwa. Kwa hiyo, ukavuruga utaratibu wote na barabara hazikutangazwa mapema. Kilichotokea ndicho hiki tunachokiona sasa, barabara nyingi zimeharibika kwa sababu hazikutengenezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu ni kwamba, mwaka huu Serikali ijiridhishe kama barabara zimekwisha kutangazwa tayari kwa ajili ya kuanza kujengwa mwezi wa Saba kama ambavyo tumekuwa tukifanya miaka mingine. Hii imesababisha barabara nyingi sana kuharibika. Nikitoa tu mfano kwenye jimbo langu, barabara karibu zote, nyingi zimeharibika. Barabara ambayo nimeitaja hata asubuhi ya kutoka Idete – Kidabaga – Kilolo haipitiki, imefungwa. Barabara ya kutoka eneo la Ukwega, kata nzima imejifunga na haipitiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna baadhi ya maeneo ya Kata ya Ukumbi, barabara zote zimejifunga. Ukitaka kupita kutoka Kilolo kwenda Pomerini kwenda Mwatasi, zote zimejifunga. Sasa hii imetokana na kuchewelesha kutangaza, halafu wakandarasi wapo, lakini hawawezi kupeleka vifaa kwa sababu mvua zinanyesha. Jambo hili naomba sana, muda wowote ambapo mtalijadili, fedha za barabara zipelekwe mapema, na kibali cha kuzitangaza kitolewe sasa hivi ili wakati tutakapomaliza kupitisha bajeti, ile asilimia inayotakiwa kwenda mapema, iende na barabara zijengwe mapema.

Mheshimiwa Naibu Spika, izingatiwe kwamba haya ni maeneo yenye mvua na kwa hiyo, yanahitaji fedha mapema ili kuhakikisha kwamba tunakidhi yale tuliyojiwekea na ili kuondoa kero, kwa sababu barabara ni kero kubwa na ndiyo inayozuia uchumi kwa kiwango kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mifano ipo mingi kwa Uchumi, kwa mfano uchumi wa misitu, badala ya kuuza mti kwa shilingi 15,000/= hadi shilingi 20,000/=, barabara ikiwa mbovu mwananchi anauza kwa shilingi 2,500/= ili mtu aweze kuvuna, achane mbao na hii inamrudisha nyuma sana kimaendeleo. Kwa hiyo, tunapoomba sana, kwamba hata hiyo fedha kidogo iliyopo ipelekwe mapema, tunataka uchumi wa haya maeneo uweze kukua na wananchi waweze kufaidi, na vile vile kuondoa kero nyingi ambazo sasa hivi tunazipata kwenye maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo napenda kulizungumzia na ambalo nadhani hatujali-exploit vizuri na labda Mheshimiwa Waziri wa Mipango anaweza akalichukua na kuliangalia ni kuhusu biashara ya carbon. Sasa maeneo mengi ya Tanzania ina misitu takribani hekta milioni 48. Nataka nitoe mfano mmoja tu wa Wilaya ya Tanganyika, vijiji vinane mwaka 2023 vimepata shilingi bilioni nane. Halmashauri nyingi zinapata shilingi bilioni mbili, shilingi bilioni tatu. Vijiji vinane kwa kufanya biashara ya carbon vimepata shilingi bilioni nane. Mwaka huu wanatarajia shilingi bilioni 14 kwa vijiji vinane.

Mheshimiwa Naibu Spika, kiasi kikubwa cha misitu Tanzania ikiwemo misitu ya Kilolo haivunwi carbon wala hatuuzi carbon ambayo ingeweza kuipunguzia Serikali gharama kubwa ya kupeleka fedha kwenye halmashauri. Tatizo lipo kwanza kwenye utaalamu kwa sababu tunahitaji wataalamu. Pale TAMISEMI amewekwa mtu mmoja kwa ajili ya biashara ya carbon, na huyo mtu mmoja mwenyewe utaalamu wake ni wa kujifanyia juhudi yeye mwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huwa kunafanyika makongamano ya biashara ya carbon, lakini hawapelekwi wataalamu wowote halafu hata hizo shilingi bilioni nane au shilingi bilioni 14 tunazozipata zinatokana na mtu kati, yaani yule mnunuzi ni wa sita kutoka kwetu sisi, ndiyo tunapata shilingi bilioni 14. Hebu fikiria, ninyi mnafahamu biashara ya watu kati, kama sisi ni wa sita, je kama sisi wenyewe tungeuza tungepata shilingi ngapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii nchi ingeweza kuwa na uchumi mkubwa sana kama Serikali ingetenga kitengo maalamu pale kwenye Wizara ya Mazingira ambapo hawa watu wanaofanya biashara ya carbon wangewekwa, lakini kakiangalie kile kitengo kina watu wangapi? Kuna wataalamu wangapi wa nchi hii wanaoweza kujadili biashara ya carbon, na wanaoweza kuwatafuta wanunuzi halisi wa biashara ya carbon, wakakaa waka-negotiate?
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi jirani zina wanunuzi, na wanunuzi wanafahamika. Mnaenda kwenye makongamano, wanaonekana, halafu wewe unatumia mtu kati wa sita wakati wewe mwenyewe kwenye makongamano unaenda na unawaona na wanajitambulisha, mimi ndiyo mnunuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukirudi huku, tunawauliza, wale watu wa Tanganyika wamekuja wanasema sisi wanunuzi hatuwajui, tunatumia madalali. Kwa nini nchi isiwe na wataalamu wa kuwatafuta watu halisi wa biashara hiyo ya carbon, sisi wenyewe tukajadiliana nao? Mbona kuna nchi jirani wanafanya biashara ya moja kwa moja! Sasa si twende tukajifunze wao wamewapataje? Kwa kuwa wanajulikana, kwa nini hatuoni umuhimu wa kuwekeza kwenye biashara ya carbon? Hii misitu tunayoitunza ni ya nini kama hatuwezi kufanya biashara? Biashara hizi zina msimu, itaenda baada ya muda itaisha, tutakuwa hatuja-exploit hela yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Mipango ituambie, hivi kuna kizuizi gani cha ku-exploit hiyo opportunity ambayo kwa sasa duniani kote wanaizungumzia? Changamoto yake ni nini? Nami nazungumza hivi wa sababu misitu ya Serikali za vijiji peke yake tu, kwa Kilolo ni zaidi ya hekta 54,000, lakini misitu ambayo Kilolo inayo ambayo sasa ingeweza kuingizwa kwenye soko ni zaidi ya hekta 170,000. Hiyo ingeweza kuingiza fedha ambayo ni mara 15 ya hela ambayo wanakusanya. Mama Ntilie wanafukuzwa, sijui watu gani, tusingekuwa na haja ya kuhangaika na hizi hela ndogo na fursa ipo. Opportunity ipo, mifano ya halmashauri zinazopata tunayo, lakini tumekaa tunaangalia fedha kidogo tulizonazo. Kwa nini tusitumie brain tuliyonayo Mungu aliyotuijalia? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunao wataalamu wazuri sana katika hii nchi, kwa nini kisiundwe kikosi kazi kizuri cha wataalamu kitufanyie tathmini? Tunawezaje kunufaika na biashara ya carbon kabla haijaisha, kabla hili soko halijaondoka? Natamani wakati wa majumuisho tupate majibu mazuri ya kuelewa hiki kitu kitafanyika lini kwa sababu nina uhakika kina maslahi mapana kwa Taifa letu, lakini nina uhakika kingewapunguzia mzigo mkubwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hizi hadithi za wafanyakazi wachache, wataalamu wasiokuwepo, na wale waliokuwepo wasipokuwa na commitment kwenda kwenye makongamano na kuzunguka kwenye shopping mall na kurudi hapa wamenunua vitu vichache, tusingependa jambo hilo liendelee. Tunatamani kuona biashara ya carbon inafanikiwa kwenye nchi yetu na sisi tunapata manufaa kama nchi nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, tujifunze kutoka kwenye nchi nyingine kwa sababu biashara ya carbon ni uchumi. Sisi tunaotoka kwenye maeneo ya misitu tunajua tungeweza kunufaika kwa namna kubwa. Kwa kweli hili ni jambo ambalo ningependa lifanyiwe kazi na tuone jinsi gani tunavyoweza kunufaika na biashara ya carbon. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nilitaka nichangie ili nione kama pia leo hamtasikiliza, maana ni mara yangu ya nne kuzungumzia biashara ya carbon, basi nitajua hamtaki wala hamtaki hizo fedha, wala hamtaki ku-exploit hiyo carbon. Machoni kwa Watanzania, ninanawa mikono, tumeshaipigia kelele, sasa ni kazi kwa Serikali, kama wataiacha, waiche, lakini sisi tumezungumza. Ahsante sana. (Makofi)