Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Joseph Michael Mkundi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ukerewe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii. Kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema, niweze kutoa mchango wangu kwenye hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Natumia nafasi hii kwanza kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya kutuletea maendeleo kama Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Makamu wa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri ambayo imesheheni mambo mengi na kuonesha dira ya Taifa letu na namna gani mambo mbalimbali ikiwemo miradi ya maendeleo namna ilivyotekelezwa. Nawapongeza Waheshimiwa Mawaziri wote kwenye Wizara hii na watendaji wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua Mheshimiwa Jenista na wasaidizi wake namna gani wanafanya kazi kubwa, na Ukerewe ni moja kati ya maeneo yaliyonufaika na miradi mikubwa ya maendeleo ambayo Mheshimiwa Rais ameweza kutusaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu utakuwa kwenye maeneo kama mawili na muda ukiruhusu basi nitaongeza eneo la tatu. La kwanza, ni eneo la kilimo. Tanzania tumebahatika kuwa na eneo kubwa lenye sifa ya kuweza kutumika kwa ajili ya uzalishaji wa mazao mbalimbali. Kwa kuangalia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kuanzia aya ya 46, inaonesha namna gani kupitia mradi wa ASDP II ulivyotunufaisha ingawa pamoja na mafanikio tuliyoyapata kwa sababu kwa mujibu wa hotuba mpaka sasa tumefanikiwa kwa asilimia 66 na mradi wenyewe unaenda mpaka mwaka 2027/2028.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaamini kupitia Sekta ya Kilimo tunaweza tukafanya mambo makubwa sana kupitia hii ASDP II, tunaweza tukafanya vizuri sana na tukitumia maeneo tuliyonayo yenye rutuba na uwezo wa kuzalisha mazao, tukawa na uchumi mkubwa na endelevu kwenye Taifa hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado kuna maeneo mengi hatujaweza kuyafanyia kazi pamoja na dhamira ya Serikali kuweza kuongeza uzalishaji kwenye maeneo yetu mpaka kufikia hekta zaidi ya 1,200,000, lakini bado kuna maeneo mengi na hasa rasilimali maji hatujaweza kuitumia vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua jitihada za Serikali kutengeneza mabwawa na kuimarisha kilimo cha umwagiliaji, lakini bado hatujaweza kufanya vizuri. Nikitoa mfano, mimi natoka Jimbo la Ukerewe ambapo tumezungukwa na maji. Katika eneo tulilonalo, zaidi ya kilometa 6,400, asilimia 90 ni maji. Inasikitisha kwamba pamoja na eneo tulilonalo ambalo tuna hekta karibu 31,000, lakini kwa sababu hatufanyi kilimo cha kisasa ambacho kinaweza kuleta tija kila mwaka katika maeneo tuliyonayo, tunaona mahitaji ya chakula ni tani 151,000, lakini uwezo wa kuzalisha chakula ni tani 104,000 pekee.

Mheshimiwa Naibu Spika, matokeo yake, pamoja na kwamba kitaifa tuna ziada ya chakula karibu tani 400,000 lakini bado Ukerewe kila mwaka tunakuwa na upungufu wa chakula karibu tani 40,000. Naomba kwamba, pamoja na jitihada kubwa ambazo zinafanyika kwenye kuimarisha kilimo, maeneo yenye rasilimali kama Ukerewe ambayo ina rasilimali maji, basi itumike kwa ufanisi ili angalau tuweze kuzalisha chakula kwa wingi na eneo husika vile vile liweze kujikidhi kwa mahitaji yake ya chakula.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni aibu kwenye eneo lililo na maji kwa kiasi kile kila mwaka kuendelea kuwa na upungufu wa chakula, kuwa na shida ya usambazaji wa maji safi na salama. Wakati Wakerewe wanaona wamezungukwa na maji, ukiwaambia tuna shida ya maji, watu hawawezi kuelewa. Kwa hiyo, naomba Ofisi ya Waziri Mkuu na Serikali kwa ujumla wake ione namna, na haja ya kutumia rasilimali tulizonazo kwa ajili ya uzalishaji na kuondokana na changamoto zinazotukabili kama nilivyotoa mfano kwenye eneo la Ukerewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa uwekezaji kwenye Sekta ya Uvuvi. Ni kweli siku chache zilizopita katika uwekezaji uliofanyika wa zaidi ya shilingi bilioni 13 kwenye kununua boti, lakini na ufugaji kwa kutumia njia ya vizimba, sisi Ukerewe ni wanufaika wa mradi ule. Nashauri kwamba, pamoja na jitihada zote hizi, kama ilivyofanyika kwenye eneo la kilimo kuanzisha BBT, lifanyike BBT vilevile kwenye eneo la uvuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri hivi kwa sababu Ukerewe tuna visiwa karibu 38 na vyote vinafanya shughuli za uvuvi, kwa hiyo, kinaweza kutengwa hata kisiwa kimoja kikatumika kama eneo la kutengeneza mradi wa BBT ili tuone matokeo yake yanakuwaje, kwa sababu zaidi ya asilimia 90 ya wakazi wa Ukerewe wanategemea Sekta ya Uvuvi. Kupitia BBT sasa inaweza kuwa njia ya kuonesha wananchi wa Ukerewe namna gani uvuvi kwa kutumia vifaa vya kisasa unaweza kuwatoa kwenye shida waliyonayo na kuweza kupata mafanikio ya kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ambalo nilitamani kuchangia ni eneo la nishati. Kupitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu aya ya 73 mpaka 75, amelezea namna gani tulivyo na changamoto kwenye eneo la nishati, lakini nafarijika kwa sababu Serikali imeonesha jitihada zinazofanyika kuimarisha Sekta ya Nishati.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli mpaka sasa kama Taifa tuna umeme kidogo, tunazalisha Megawatt chache pamoja na kwamba kupitia Bwawa la Mwalimu Nyerere tunategemea zaidi ya Megawatt 2,000 kuongezeka kwenye Grid ya Taifa, lakini bado tunahitaji kuzalisha zaidi nishati ya umeme, kwa sababu umeme kama nishati, ni kichocheo cha maendeleo ya eneo lolote lile.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Ukerewe ni kweli kwamba karibu vijiji vyote vimefikiwa na nishati ya umeme, lakini bado maeneo ya visiwa yana changamoto kubwa. Natambua jitihada za Wizara kuweka mradi wa kutoa umeme kwenye kisiwa kikubwa cha Ukerewe kwenda kwenye visiwa, kwa mfano kama Ukara, lakini bado kuna changamoto kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali, pamoja na jitihada inazozifanya, bado kuna umuhimu wa kuhakikisha kwamba vitongoji vyote vinapatiwa nishati hii ya umeme ili wananchi sasa waweze kutumia nishati hii kujiletea maendeleo kupitia uanzishaji wa shughuli mbalimbli za uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo, natambua harakati zinazoendelea kufanya Bwawa la Mwalimu Nyerere lianze kutoa uzalishaji katika uwezo wake wa juu, lakini pamoja na jitihada zinazofanyika, kuna changamoto ninayoiona katika miaka michache ijayo inaweza kukwamisha jitihada zote hizi. Tumewekeza pesa nyingi sana kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere, lakini tunatambua vyanzo vya maji yanayoenda Bwawa la Mwalimu Nyerere ni kuanzia Morogoro, Iringa na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kosa moja linalofanyika, tumeruhusu mifugo mingi sana kuwepo kwenye eneo la Morogoro, jambo ambalo miaka michache ijayo itaathiri mazingira kwenye eneo lile na vyanzo vya maji vinavyotiririsha maji kuelekea kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere kuathirika. Sasa matokeo yake ni kwamba jitihada na rasilimali kubwa zinazowekezwa na Taifa hazitakuwa na tija kwenye miaka michache ijayo, jambo ambalo itakuwa ni hasara na tutakuwa hatujawatendea haki wananchi wa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Serikali ichukue hatua madhubuti kudhibiti uwepo wa mifugo mingi sana kwenye eneo la Morogoro ili sasa maji na vyanzo vya maji vinavyotiririsha maji kuelekea kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere visiathirike na kufanya rasilimali nyingi na pesa nyingi tunazozitumia kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere zisiwe na faida tena hapo baadaye. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua tuna changamoto kubwa ya miundombinu kutokana na mvua kubwa zilizonyesha. Eneo la Ukerewe ni moja kati ya maeneo yaliyoathirika sana kwenye miundombinu yake. Barabara nyingi zimeathirika kutokana na mvua kubwa iliyonyesha. Natambua kwamba Serikali iliahidi kutenga pesa kwenye kila jimbo ili kuweza kurekebisha miundombinu hii. Naomba sasa vile vile Ukerewe iangaliwe kwenye eneo hili, kwani barabara zetu zimeathirika sana. Kwa hiyo, Serikali iangalie namna ya kutusaidia pesa ili barabara zinazotengenezwa kwenye maeneo haya ziweze kuwa imara.

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua kwamba Serikali tayari imepata mkandarasi kwa ajili ya barabara ya kutoka Kisorya kuja Nansio, ninashukuru, lakini bado kuna umuhimu wa kuimarisha barabara ya kutoka Nansio kuelekea Ilangala ambako ndiko lango la uchumi wa Ukerewe liko, ambako kuna uzalishaji mkubwa wa samaki. Naomba Serikali ione umuhimu wa kutengeneza barabara hii ili wananchi wa Ukerewe waweze kunufaika na rasilimali zinazozalishwa kwenye eneo hili, hasa mazao ya uvuvi. Natambua kazi kubwa wanaifanya, lakini naomba sana hili jambo liweze kutiliwa nguvu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ni juu ya ugawaji wa majimbo.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili, Mheshimiwa Mkundi, ahsante. Mheshimiwa Raymond, atafuatiwa na Mheshimiwa Nashon William Bidya.

MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Nashukuru sana. (Makofi)