Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Vita Rashid Kawawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Namtumbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii leo ili niwasilishe ushauri wangu katika Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nampongeza Mheshimiwa Rais, kwa juhudi kubwa anazozifanya kwa kushirikiana na wasaidizi wake na hadi leo hii Serikali inaendelea kufanya kazi nzuri sana ya kuboresha uchumi wetu ambao unaendelea kuwa stable kama unavyoendelea. Hongera sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia, hongera sana Makamu wa Rais, hongera sana Waziri Mkuu na hongera sana Mawaziri wote kwa kufanya kazi nzuri hii ya kujenga nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe shukrani pia kwa Serikali kwa kutupatia mbolea ya ruzuku kwenye msimu huu. Msimu huu utaratibu wa pembejeo ulikwenda vizuri sana. Wakulima walipata pembejeo kwa ruzuku na siyo kama msimu uliopita ambapo tulipata shida sana kuzipata mbolea za ruzuku. Hivyo basi, wakulima wamelima vizuri na mazao mazuri yako mashambani, na kwa sisi wakulima wa mahindi, yapo ya kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunakwenda kwenye masoko. Tunaiomba Serikali, sisi dira yetu kwa bei ya zao la mahindi ni NFRA. Kwa hiyo, tunaiomba sana Wizara ya Kilimo itangaze mapema soko la ununuzi wa mahindi, kwani yenyewe ndiyo inachukua dira ya bei kwa zao hili la mahindi. Tutashukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, kule kwetu Namtumbo hatuna stendi yenye hadhi. Tuna njia tu ya kupitishia mabasi na kuondoka. Mwaka 2023 niliomba Serikali katika vipindi vya Bunge hapa kwamba tujengewe na Serikali kwa sababu mapato yetu ni ya chini sana na hatuna uwezo wa kujenga stendi ya mabasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilitujibu kwamba, halmashauri iandike andiko ili iweze kuleta TAMISEMI ndiyo Serikali iweze kuichukua na kuifanyia kazi kutusaidia kujenga stendi yetu. Kwa hiyo, ni lalamiko letu kubwa sana kuwa hatuna stendi. Naikumbusha tena Serikali kuwa andiko letu tumeshaandika, basi tunaomba tujengewe stendi yetu pale Mji wa Namtumbo.

Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu ni wanyama waharibifu hususan tembo. Mwenzangu Mbunge wa Tunduru amezungumza hapa kuhusu tembo. Ni kweli sisi tumepakana na Selous, vijiji vyetu tunapata shida sana ya tembo. Tembo wanaua watu wetu. Juzi mwezi mmoja uliopita walimuua mama mmoja alikuwa anakwenda shambani. Vilevile, siku za nyuma waliua katika Kijiji cha Nambecha, pia waliua katika Kijiji cha Mputa na hii juzi waliua pale katika Likuyuseka. Hata hivyo, tembo wanatamba sana katika mashamba yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wetu ni watu wa hali ya chini, wanategemea uchumi wao kwa kulima ekari zao chache, lakini zote zinaliwa na tembo. Leo hii tembo ndiyo anatuvuruga kabisa kiuchumi katika Wilaya yetu ya Namtumbo pamoja na Tunduru. Kwa hiyo, tunaomba sana Serikali itumie weledi wake kuzia hawa tembo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi babu yangu Mfaume Ali Kawawa, alikuwa Game Officer toka miaka hiyo ya 1919/1920 mpaka baba yangu anazaliwa mwaka 1926, alimzaa akiwa porini wakiwa wanasaka na kuzuia tembo. Yeye alipewa jina la Kawawa kwa sababu ya ufundi…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kawawa, sema vizuri, nani alizaliwa na tembo? (Makofi/Kicheko)

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, babu yangu akiwa anafanya kazi ya kuzuia tembo waharibifu wasiharibu kwenye vijiji miaka ya 1920 na kitu, mwaka 1930 aliteuliwa kuwa Game Officer wa Selous, akapelekwa Liwale. Wakati huo hawakuwa na magari, walitembea kwa miguu. Waliweza kudhibiti tembo wakati huo na walikuwa tembo wengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii tuna wasomi wengi wanasomea behavior za wanyama hawa, tuna teknolojia na tuna magari, tunashindwaje kuwazuia tembo kufanya uharibifu? Kwa hiyo, tunaomba sana Serikali itumie weledi wake ili kuzuia hawa tembo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, historia niliyokuwa nayo, tembo wakienda kwenye kijiji wakifanya vurugu, babu yangu alikuwa anakwenda anakaa kuwa-study siku tatu tu, halafu anampiga tembo huyu mmoja, wote wanaondoka pale na hawarudi tena. Leo hii tunazuia, ndiyo; kuna Sheria mbalimbali za kuzuia kuwapiga tembo, lakini lazima tuwapunguze wale waharibifu na kidogo kidogo hawatarudi tena. Tembo hawa wanaua, wanaharibu vyakula na kadhalika. Kwa hiyo, tunaomba sana kwenye eneo hili la tembo Serikali ilichukue kwa sababu ina weledi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni miradi viporo katika halmashauri zetu. Halmashauri yetu ya Namtumbo tuna miradi mingi ya nyuma ambayo ni viporo. Tunaishukuru sana Serikali imefanya kazi nzuri sana ya kutujengea madarasa na vituo vya afya. Kwangu tumejenga vituo vitatu vya afya na madarasa 86. Pia, tumejenga na kuongeza madarasa katika shule za msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna shida ya miradi viporo ya nyuma ambayo haijakamilika. Sasa haiwezi kuendelea kukaa kama maboma. Tunaiomba na kuishauri Serikali itenge fedha za kukamilisha miradi hii viporo ili twende kama ilivyokusudiwa. Miradi hii ilijengwa kwa nguvu za wananchi na Serikali ilisema itakuja kumalizia kwa vifaa vya viwandani, lakini mpaka leo ipo haijajengwa. Wakati ni huu, tunaomba sasa tuweze kujenga na kukamilisha miradi viporo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kule kwetu tuna mradi wa Urani. Nchi yetu tunahitaji fedha na tunahitaji kupunguza gharama za uendeshaji kwa kupata mapato. Mradi wa Urani ni moja ya mradi ambao utatusaidia sana katika kuingiza mapato. Leo nilikuwa naangalia hapa katika hotuba ya Waziri wa Fedha aliyoitoa kwenye Bunge, alizungumzia mikopo aliyokopa karibu shilingi trilioni 2.7. shilingi trilioni 1.7 tumelipia hati fungani, lakini shilingi trilioni moja tumelipia miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ili kupunguza mikopo hii maana yake lazima tuwe na miradi ya uzalishaji. Sasa sisi tunao mradi wa Urani ambapo kuna urasimu na hatuelewi. Wanasema mara inafanyika strategic environment assessment, sijui inafanyika lini? Mradi ule hauanzi mpaka leo na urani imepanda bei. Leo ile wakia moja ni dola 72. Duniani sasa hivi kuna viwanda au vinu 57 vinajengwa kwa ajili ya kutaka kuzalisha umeme hasa nchi za Ulaya. Kwa hiyo, kwetu sisi urani ni soko mojawapo kubwa sana. Kwa hiyo, tunaiomba sana Serikali imalize urasimu ili ule mradi wa urani uweze kuanza kule Mkuju wilayani Namtumbo.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mwisho ni tumbaku. Tumbaku inalimwa kwa mkataba na mkataba wenyewe ni kwa dola. Sasa Serikali katika uboreshaji wa biashara, tumepata mikataba ya kuzalisha tani nyingi sana za tumbaku, lakini tuna changamoto ya pembejeo kuwa ghali sana kwenye uzalishaji. Tunaomba Serikali itupatie ruzuku kwenye zao la tumbaku. Kwa sababu kwanza inauzwa kwa dola, nasi tuna shida ya dola, lakini tuna mkataba wa kuzalisha tani nyingi sana za tumbaku.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakulima wanashindwa kulima mashamba mengi au ekari nyingi kwa sababu hawana uwezo wa kununua mbolea ya NPK ambayo haina ruzuku. Kwa hiyo, sisi tunaomba tumbaku ipate mbolea ya ruzuku. Leo wenzetu wa korosho wanapata ruzuku au pembejeo yao bure. Sisi tumbaku tunanunua bila ruzuku. Tunaomba Serikali isitugawe, sote tunazalisha kwa ajili ya wananchi na nchi hii. Tunaomba tumbaku nayo ipate ruzuku katika uzalishaji wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii. (Makofi)