Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Mohamed Lujuo Monni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chemba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii muhimu ya watumishi wetu wa Tanzania. Kwanza kabisa nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia afya njema, amenijalia uhai na nimepata fursa ya kuchangia hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama wenzangu waliotangulia kusema kwamba tuna kila sababu za kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Mama yetu kwa mema ambayo anayafanya kwa Watanzania. Kipekee kabisa nimshukuru pia kaka yangu Mheshimiwa Simbachawene, Waziri na Naibu Waziri wake kwa kazi kubwa wanayoifanya kwenye ofisi hii. Niwashukuru na kuwapongeza pia watendaji wa ofisi hii kwa kazi wanazozifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa miaka mitatu Wilaya yetu ya Chemba imepata watumishi zaidi ya 550, kati ya hao 300 ni wa elimu, 250 ni wa kada zingine. Nachukua nafasi hii kuishukuru Serikali, nakumbuka mwaka 2021 nilisimama hapa kueleza namna Chemba ambavyo ilikuwa na upungufu wa watumishi, kwa hiyo nichukue nafasi hii kuwashukuru kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kuhakikisha wanatutendea wema Chemba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuletewa watumishi wa kutosha hawa, bado changamoto ni kubwa sana Chemba, mahitaji ni zaidi ya 3,052, lakini waliopo ni 1,700, maana yake kitakwimu zaidi ya 43% ni upungufu. Katika mazingira hayo unaweza ukaona ni namna gani watumishi wa Chemba wanavyolazimika kufanya kazi za watu wengine. Nimwombe Mheshimiwa Waziri Kaka yangu Simbachawene aendelee kuiangalia Chemba kwa namna ya kipekee ili walau tuwe na watumishi wa kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu nifafanue kidogo kwa mfano kwenye afya. Tunao upungufu wa zaidi ya 70% kwenye afya, kwa hakika ni takwimu za kutisha kidogo pengine kwenye Mkoa wa Dodoma au na wenzangu wengi, kwenye kada ya afya mimi ndiyo nina kiwango kidogo cha watumishi. Kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Utumishi aangalie namna ambavyo anaweza akatusaidia na mwezi Juni tunaenda kufungua zahanati nne ambazo nina hakika hatutakuwa na watumishi. Kwa hiyo, naomba katika watumishi hawa ambao wanaenda kuajiriwa tuiangalie kipekee Chemba.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika elimu tunayo changamoto zaidi kwenye elimu ya msingi na wenzangu wamesema. Kwangu pia watumishi waliopo ni 52% tu, 48% ni upungufu. Hali hii inaweza ikachangia pia matokeo mabaya, matokeo hasi. Wakati mwingine tunaweza kukaa tukalaumiana amesema ndugu yangu Mheshimiwa Mtenga, hizi shule zetu za vijijini mnaweza mkakaa mnalaumiana kwamba watoto hawafaulu, lakini je, tumewahi kuangalia uwiano uliopo wa wanafunzi ulioko kule na walimu? Ukweli ni kwamba kuna upungufu mkubwa sana wa walimu na waliopo wanafanya kazi kubwa, wanajitahidi lakini ukweli unabaki palepale na matokeo hayo yanakuwa hivyo kwa sababu ya upungufu huo wa walimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kumwomba Mheshimiwa Simbachawene, kaka yangu aangalie pia kwenye sekta hiyo ya elimu ya msingi. Nashukuru sekondari kidogo hali imetengamaa, kuna upungufu lakini ni upungufu ambao unakubalika wa 20%, lakini huku kwenye primary school, nawaomba sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niongelee kuhusu watendaji wa kata. Wenzangu hapa watakubaliana kwamba majimbo ya vijijini au wilaya za vijijini kwangu kote ni vijijini, watendaji wa kata na vijiji ni watu muhimu sana, si tu wanafanya kazi za majukumu yao waliyopewa, lakini wanafanya kazi nyingi, wanafanya kazi nje na zile ambazo wamepangiwa. Wanafanya kazi za kukusanya mapato, wanafanya kazi za kusimamia miradi ya Serikali, wanafanya kazi ya kuchangisha michango kwa ajili ya miradi ya Serikali. Kwa hiyo wanafanya kazi nyingi sana, ndiyo wasuluhishi wa migogoro, ndiyo mahakama, kwa hiyo katika mazingira hayo tunaweza tukaona watendaji wa kata walivyo muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwangu kuna kata 26, lakini watendaji waliopo ni wa kata 19 tu, mnaweza mkaona kuna kata saba hazina watendaji. Nina vijiji 113, watendaji waliopo ni wa vijiji 85 tu, kwa hiyo tuna vijiji zaidi ya 28 ambavyo havina watendaji. Kwa hiyo nakuomba sana pia ndugu yangu, kaka yangu Mheshimiwa Simbachawene, tuangalie ni namna gani tunaweza kuwasaidia hawa, kwa sababu ukweli ni kwamba makusanyo yote ya vijijini huko yanafanywa na watendaji wa vijiji, yanafanywa na watendaji wa kata. Maana yake ni kwamba kama kijiji hakina mtendaji tafsiri yake ni kwamba, hata mapato ya Serikali hayawezi kukusanywa, hakuna chochote kinachoweza kukusanywa na hivyo inapelekea upungufu mkubwa wa makusanyo ya mapato. Kwa hiyo niwaombe sana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nawashukuru sana watumishi wa Wilaya ya Chemba, nawashukuru kwa sababu moja tu, upungufu mkubwa huu, lakini kwa Mkoa wa Dodoma Chemba tunaongoza kwa kukusanya mapato vizuri, nafikiri ndugu zangu wa Mkoa wa Dodoma wanafahamu. Kwa hiyo nimshukuru sana Mkurugenzi wetu Ndugu Siwema Hamoud Jumaa kwa kazi kubwa anayofanya pamoja na upungufu mkubwa huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu mara kadhaa tumekuwa tukijadili ni namna gani tutafanya shule zetu zifanye vizuri, lakini mara kadhaa amekuwa akihangaika kufikiri namna gani anaweza akaweka vizuri ikama ya walimu. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri ndugu yetu aangalie namna ambavyo anaweza kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba niseme jambo la mwisho ambalo ni muhimu sana kuhusu pikipiki za watendaji. Tulikubaliana hapa kwamba watendaji wote wa kata wawe na pikipiki. Jografia ya Chemba ni complex, kipo kijiji ambacho kitongoji chake kiko kilometa 50. Ili mtu atoke kwenye kitongoji aje apate saini ya Mtendaji wa Kijiji lazima asafiri na alale huko. Sasa tunaweza kuangalia hali halisi ilivyo. Mtendaji wa Kata hana usafiri. Mnaweza kuangalia namna gani wanaweza kufanya kazi. Ni kazi ngumu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, zililetwa pikipiki nane wakati watendaji wapo 26. Unaweza ukaona zaidi ya watendaji 18 hawana pikipiki na hawana usafiri nao ndio wanaofanya kazi zote na jiografia ni mbaya. Kwa hiyo, nawaomba sana kwenye hiyo bajeti ambayo imewekwa kwa ajili ya vifaa, naomba na Chemba walau tununuliwe pikipiki kwa ajili ya watendaji wetu ili nao wafanye kazi ya Serikali vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, nachukua nafasi hii kuwashukuru sana kwa nafasi. Naunga mkono hoja. (Makofi)