Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ili nami nitoe mchango wangu wa mawazo ya namna ya kuendeleza Sekta hii ya Utumishi na Utawala Bora. Kwanza, nianze kutoa pongezi nyingi kwa Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo anaendeleza amani, utulivu, mshikamano, umoja, uhusiano wa kimataifa pamoja na kuendeleza miradi mikubwa na miradi midogo katika nchi hii. Majimbo yetu yote yana ahueni kubwa, na sekta zote Mheshimiwa Rais anazigusa.

Mheshimiwa Naibu Spika, umahiri wa Mheshimiwa Dkt. Samia katika uongozi ni wa kupigiwa mfano siyo katika nchi ya Tanzania tu, bali duniani. Ndiyo maana siku ya tarehe 10/10/2023 katika Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru cha India kilimtunukia Mheshimiwa Rais Samia Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Falsafa kwa kutambua mchango wake katika maendeleo ya Tanzania. Huyu alikuwa ni kiongozi wetu wa pili kupewa heshima hiyo baada ya Rais Dkt. Julius Kambarage Nyerere mwaka 1995.

Mheshimiwa Naibu Spika, jana tarehe 18/04/2024 katika Chuo Kikuu cha Ankara Uturuki, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alitunukiwa Ph.D ya heshima kwa kutambua jitihada zake katika kuendeleza mageuzi ya kijamii, kisiasa na kiuchumi kupitia zile 4R zake, zimetambulika Kimataifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, unaweza ukashangaa kwamba kuna baadhi ya watu hapa hapa nchini wanaweza wakawa hawatambui umuhimu wa uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, lakini dunia inatambua. Kuna watu hapa Tanzania walikuwa hawapumui kisiasa. Sasa hivi wanapumua, wanafanya mikutano na kila kitu, na wamekiri hadharani. Kwa hiyo, tuna kila sababu ya kumpongeza Rais wetu kwa namna ambavyo anatimiza majukumu yake vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake na timu yote ya Wizara hii kwa namna ambavyo wanaendeleza weledi, umakini, uadilifu na uaminifu kwa Rais pamoja na nchi yetu. Hongereni sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina ushauri katika maeneo machache. Eneo la kwanza ni kwenye Serikali mtandao. Katika Serikali mtandao nimkumbushe Mheshimiwa Waziri na Serikali kwamba, mwaka 2003 Serikali ilipitisha secular kwamba watumishi wote wa Serikali lazima wawe na anuani ya barua pepe ya internet kwa ajili ya mawasiliano ya Serikalini ili kutunza siri za Serikali hasa wanapo-share documents.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo hilo bado tumeonesha udhaifu mkubwa. Watumishi wengi wa Serikali bado wanatumia anuani za Gmail na Yahoo kwa ajili ya matumizi ya ofisi. Ni jambo ambalo Serikali inatakiwa ifanye tathmini kuona ni kwa nini nchi nyingine zimeweza na kwa nini sisi tumeshindwa kudhibiti hali hiyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo nataka nilizungumze kuhusiana na Serikali Mtandao ni mifumo ya kuratibu utendaji Serikalini. Kuna wakati hata Mheshimiwa Rais aliagiza ipunguzwe, lakini bado ipo mingi. Mfano, mifumo ya ununuzi, mifumo ya mapato, mifumo ya ufuatiliaji na tathmini na mifumo ya kupeana taarifa. Iko mingi sana, kila sekta ina mifumo yake tena ni mingi, ndani ya sekta mifumo mingi. Mratibu wa suala hili ni Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora. Sasa mifumo hii itapunguzwa lini na isomane? Hili ni jambo ambalo naamini Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha atatueleza mikakati iliyopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ambalo ambalo napenda nichangie ni kuhusu utumishi wa umma. Kwenye eneo la ajira, kwa jinsi tunavyoajiri wale wanaoomba ajira Serikalini na kwenye vyombo vyetu vya umma, kuna tatizo ambalo linatakiwa lifanyiwe kazi. Kidogo wale wanaoomba ajira wanalalamika kwamba uwazi ni mdogo, ndiyo maana mpaka Wabunge wamelalamikiwa kwamba Mbunge fulani hajanisaidia mimi kupata kazi. Ni kwa sababu uwazi ni mdogo, wanahisi kwamba Mbunge anaweza akamwambia Waziri, bwana, kijana wangu huyu mpe kazi akapata kazi. Kumbe siyo hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, eneo hili la ajira naomba, licha ya juhudi mbalimbali ambazo zimefanyika lifanyiwe mapitio makubwa ili kuongeza uwazi katika eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kuhusu mikataba ya utendaji wa kazi, OPRAS. Wakati wa kuanzisha OPRAS ilipigiwa debe sana na ilikuwa nzuri sana. Wakurugenzi walikuwa wanasaini na watumishi wao na Makatibu Wakuu walikuwa wanasaini na Wakurugenzi. Ilifikia wakati mpaka Mawaziri walitaka kusaini hiyo mikataba ya kazi. Sasa OPRAS baada ya miaka mingi, je, ni ni lini ilifanyiwa tathmini kubwa? Je, imekuwa na tija na ufanisi gani katika utendaji wa kazi? Ni jambo ambalo natoa wito Serikalini wafanye mapitio makubwa ili kuhakikisha kwamba hii mikataba ya kazi inakuwa na tija. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la tatu ambalo napenda kushauri ni kusimamia maadili ya utumishi wa umma. Tunayo Sekretarieti ya Maadili, hivi kazi yake ni kutusimamia tu sisi kujaza fomu za maadili? Kwa hiyo, tukishajaza fomu za maadili, basi! Kwa nini wasiende mpaka kwenye sehemu za kazi wakaangalia, hivi maadili yanaendeleaje kwenye sehemu ya kazi? Nadhani lazime kuwe na mfumo wa ufuatiliaji na tathmini ambao utahakikisha kwamba mambo haya yanakuwa yanasimamiwa kwa maadili tangu ujaze fomu na jinsi unavyofanya kazi za kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili kuhusiana na suala la maadili ni TAKUKURU. Kupitia sheria TAKUKURU tuliwapa meno makubwa sana, lakini kadiri siku zinavyoenda wale watu wetu wa TAKUKURU ni kama vile wanapotea potea hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, anaonekana Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Kitaifa, lakini Mkuu wa TAKUKURU wa Wilaya na Mkuu wa TAKUKURU wa Mkoa ni kama vile wanapotea hivi kiasi ambacho inakuja kuonekana kwamba kunapokuwa na issue imetokea unakuta amekuja Waziri Mkuu, ndiye anayeibua mambo, lakini TAKUKURU wapo. Anakuja CAG ndiye anayeibua mambo, lakini TAKUKURU wapo. Zinakuja Mbio za Mwenge ndizo zinaibua mambo ilhali TAKUKURU wapo. Je, kwa nini wanapotea? Ni jambo ambalo inatakiwa Mheshimiwa Waziri aliangalie ili kama wanahitaji msaada, basi waweze kusaidiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la nne ni TASAF. Bila kupepesa macho, hata Waheshimiwa Wabunge wengi walilizungumzia wakati wa kuchangia kwenye hotuba ya Waziri Mkuu kwamba kwenye eneo hili la TASAF kuna malalamiko mengi sana. Watu wengi wanaolalamika ukiwakuta, ni kweli walistahili kuwemo kwenye mpango wa TASAF.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukichunguza kwa undani, unakuta kweli kuna watu wengi ambao hawakustahili kuwemo kwenye mpango wa TASAF lakini wamo. Kwa hiyo, ni jambo ambalo naomba Serikali isitishe mpango wa TASAF mpaka wafanye mapitio makubwa nchi nzima ili kuangalia nani alistahili na nani hakustahili, kisha waweke utaratibu mpya ambao utaondoa hayo malalamiko.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ni kuhusu usimamizi wa uwiano wa watumishi katika maeneo yetu mpaka leo...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo ni kengele ya kwanza. (Makofi/Vicheko)

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka leo kuna baadhi ya mikoa ina ziada ya watumishi na kuna baadhi ya mikoa ina upungufu mkubwa wa watumishi. Kuna baadhi ya halmashauri zina ziada ya watumishi, kwa mfano walimu. Hivi ni nani anasimamia uwiano wa watumishi hapa Tanzania? Ni Wizara hii! Naomba ifanywe study kubwa kuangalia mtawanyiko wa watumishi katika nchi yetu ili baadaye wapendekeze namna ya kuweka balance.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kabisa, huko nyuma kulikuwa na mipango mikakati (Strategic Plans) na mabingwa wa strategic plan walikuwa wanatoka Ofisi ya Rais, Utumishi. Wanasimamia strategic plan kila Wizara, halmashauri na mkoa, lakini sasa hivi ni kama vile wamepotea, kama hawapo. Naomba, kwa sababu jambo hilo ni zuri katika tija ya utendaji kazi Serikalini, ni muhimu nalo lirudiwe kama lilivyokuwa zamani ili mambo yetu yaende kuwa mazuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Nashukuru sana. (Makofi)