Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisesa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa nafasi uliyonipa ili niweze kuchangia hii hotuba muhimu sana ya Ofisi ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambapo kwa kweli ndiyo engine ya utekelezaji wa shughuli zote za Serikali na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, naungana na wenzangu wote ambao wamewapongeza sana watumishi wa umma wa nchi hii kwa kazi nzuri sana wanayoifanya wakiongozwa na mtumishi namba moja, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo anaendelea na shughuli za umma usiku na mchana. Pamoja na changamoto zote wanazozipata, tunawaombea na tunawatakia kila la heri katika majukumu ya kuliongoza Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna changamoto nyingi katika mifumo ya utekelezaji wa shughuli za umma na dhana ya utawala bora. Ukisoma Ilani ya Uchaguzi ile sura ya sita halafu ukaangalia na utekelezaji wa shughuli za Serikali zinavyoenda, utaridhika na utabaini kabisa kwamba matukio haya yote yanathibitisha nchi yetu tayari ilishaacha utekelezaji na uzingatiaji wa dhana ya utawala bora. Kwa sababu gani? Unaweza kuona kabisa matukio mengi ya uvunjaji wa katiba wa moja kwa moja na uvunjaji wa sera na kanuni na kutokuzingatia haki za binadamu unafanyika kwa uwazi kabisa halafu kila kitu kinaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaona kwamba kama Taifa ni lazima tuitafakari upya mifumo yetu ya kiutumishi wa umma na utekelezaji na uzingatiaji wa utawala bora ili tuweze kuona kwamba tuko wapi. Kwa kweli tusikubali hali hii ikaendelea kwa sababu kama itaendelea, nchi yetu hii ambayo inastawi vizuri, itaenda kuanguka na itakuwa failed state.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni vita. Mwalimu Nyerere wakati anatangaza vita ya kumng’oa Nduli Idi Amin alisema maneno haya; “Tunayo kazi moja tu sasa Watanzania, ni kumpiga Nduli Idi Amin. Uwezo wa kumpiga tunao, sababu za kumpiga tunazo na nia ya kumpiga tunayo. Tunataka dunia ituelewe hivyo kwamba hatuna kazi nyingine na tunawaomba marafiki zetu wanaotuambia maneno ya suluhu waache maneno hayo.”
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi katika kuirekebisha nchi yetu na kuiweka kwenye misingi ya utawala bora, ni vita ambayo ni lazima tuipigane sasa. Hatuwezi kuendelea kuruhusu dhuluma, wizi, ufisadi na rushwa hizo vikaendelea kufanyika. Dhuluma na uonevu wa baadhi ya sekta ambao unafanywa hapa nchini hauwezi ukavumilika. Watanzania wenzetu wanauawa na kuteswa halafu maisha yanaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkanganyiko wa mifumo ya utumishi wa umma, kuna mkanganyiko mkubwa sana wa mifumo ya utumishi wa umma. Hivi sasa, kwanza kuwepo kwa parallel system kunafanya kila mtu kuwa ni mkubwa na hivyo kunakosekana hata nani amwagize mwenzake. Kuna mwingiliano mkubwa sana wa madaraka katika utekelezaji. Hakuna clear separation of power ya watu, hatimaye watumishi wetu wanalumbana tu kule, hakuna mkubwa. DC analumbana na Mkurugenzi, Mkurugenzi analumbana na Mbunge, Mbunge analumbana na Mkuu wa Mkoa, Mawaziri na Makatibu Wakuu hivyo hivyo. Hatimaye tunakuwa na mfumo ambao ni tatizo kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia teuzi na baadhi ya ajira kutolewa bila kufanyika kwa ushindani, inatufanya kupata viongozi na watendaji dhaifu ambao wanashindwa kutekeleza majukumu yao na kumpa kazi kubwa Mheshimiwa Rais kila leo kutengua na kuteua. Ni kazi kubwa kusoma CV za watu ilhali kazi hizi zingeweza kutangazwa, Watanzania wenye uwezo wakapata hizo kazi. Kwa nini Waziri ateuliwe? Kwa nini asishindane tu kwenye interview? Kwa nini Makatibu Wakuu, Wakurugenzi, Wakuu wa Wilaya, na Wakuu wa Mikoa nao wasishindanishwe? Mwisho wa siku tungeweza kupata viongozi wazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata huu mfumo wa vetting hau-guarantee kuwapata Watanzania wote milioni 60. Huwezi ku-guarantee vetting unampata wapi? Unapendekeza huyu awe DC au Mkuu wa Wilaya, umempata wapi? Nani ameanzisha maombi? Yamepatikanaje kwa Mheshimiwa Rais maombi hayo? Kwa hiyo, tunajenga taifa ambalo hatuwezi kupata viongozi wazuri. Pia, mpaka sasa watu wamepewa nafasi, mfano nafasi ya ukurugenzi, baadaye anakuja kutenguliwa...
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
MHE. LUHAGA J. MPINA: ...mshahara unabaki ule ule.
NAIBU SPIKA: Taarifa.
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Naibu Spika, haya mambo yanatupa tabu sana, lakini mfumo huu wa utumishi...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mpina kuna Taarifa.
MHE. LUHAGA J. MPINA: ...umetufanya pia hata kupata watumishi ambao siyo raia wa Tanzania.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mpina Kiti kikizungumza wewe unakaa kimya. Kuna Taarifa.
TAARIFA
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mchango mzuri wa Mheshimiwa Luhaga Mpina pamoja na mambo mengine amegusia kwamba Mawaziri, Makatibu Wakuu na Wakuu wa Wilaya wanateuliwa teuliwa tu. Nataka nimpe taarifa kwamba Mamlaka ya Uteuzi kwa nafasi ambazo anataja ambazo naye amewahi kuteuliwa ni za Kikatiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna tofauti kati ya kuhoji Katiba na kuhoji matendo, anachokihoji ni Katiba. Namtaarifu tu kwamba mamlaka hayo ambayo anayazungumzia kwa Mheshimiwa Rais ni mamlaka ya Kikatiba, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Naibu Spika,...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mpina si mpaka nikuite? Mheshimiwa Mpina taarifa hiyo unaipokea? (Kicheko)
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu tu ya muda, kwanza taarifa yake siikubali. Mimi nachangia hapa naye akipata nafasi ya kuchangia, atazungumza yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mfumo wa utumishi ambao unaruhusu mpaka watumishi ambao siyo raia wa Tanzania, mpaka viongozi ambao siyo raia wa Tanzania. Taarifa hii imeshatolewa na vyombo vyetu vya dola, na Jenerali Jacob John Mkunda Mkuu wa Majeshi ameshatoa taarifa hii, lakini Waziri wa Utumishi na Utawala Bora kwake hajaona kama hii ni changamoto wala hata hajazungumza. Suluhisho la tatizo hili ni nini? Hawa waliotajwa kuajiriwa na kuteuliwa na siyo raia wa Tanzania ni akina nani?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa changamoto ya muda, nizungumzie kuhusu kupuuzwa kwa maagizo ya viongozi. Viongozi wetu sasa hivi wanapuuzwa. Viongozi walioko juu wanaweza kuagizwa na kiongozi yeyote na wakapuuza maagizo yake. Mfano mzuri Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa aliwahi kuagiza hapa maelekezo 12 katika Bunge hili kwa watendaji wa Serikali hasa wale wa uhifadhi. Mpaka nikaja hapa Bungeni na vielelezo ikathibitishwa kwamba maelekezo ya Waziri Mkuu yamepuuzwa, lakini yale niliyoyakataa na yale ambayo hata Ofisi ya Spika ilithibitisha kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu inapuuzwa yanaendelea mpaka sasa hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitegemea kwamba baada ya kupuuzwa kwa maelekezo haya ya Waziri Mkuu, moja, walioyapuuza wangekuwa wamefukuzwa au Waziri Mkuu mwenyewe angekuwa ameshajiuzulu kwa sababu huwezi ukawa Waziri Mkuu halafu maelekezo yako yanapuuzwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wa Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Esther Matiko na Mheshimiwa Emmanuel yule Mbunge wa Ngorongoro kweli mliongea kwa hisia kubwa sana na mchango wenu ulibubujisha machozi hapa Bungeni. Hongereni sana na Mwenyezi Mungu awabariki.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kuhusu kutokuwiana kwa taarifa ya uchunguzi na taarifa ya ukaguzi. Kumekuwa na shida kubwa PCCB, DCI na DPP wana taarifa zao na wakaguzi wana taarifa zao. Wakaguzi wanakagua na kubaini kila aina ya dalili ya wizi katika maeneo husika. Unaenda kwenye taarifa ya PCCB hakuna hizo taarifa za wizi. Hazijafanyiwa kazi mahali popote na hawasemi kama ni wizi au nini kilitokea.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2023 hapa, tuliona maeneo mengi ambayo yalikuwa yana ishara kubwa sana za ufisadi na rushwa kubwa kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere na hata IPTL, zaidi ya shilingi trilioni 1.4; tuliona kwenye SGR zaidi ya shilingi trilioni 3.4; tuliona kwenye deni la Taifa mikopo inachukuliwa bila ya kufuata sheria, zaidi ya shilingi trilioni 2.5; tuliona kwenye mikataba mingine ambayo fedha za umma zimetumika na mamilioni ya fedha yamepotea na wahusika wote wanajulikana. Ukienda kusoma taarifa ya PCCB, hakuna taarifa hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma malalamiko yanayowasilishwa na taarifa ambayo PCCB wanaifanyia kazi, ni kama asilimia sita tu ya malalamiko yaliyowasilishwa. Sasa hapo utazungumzia utawala bora! Hapo utazungumzia ushughulikiwaji wa rushwa? Kama kwa mwaka unapokea malalamiko halafu unashughulikia kati ya 6.7% mpaka 23%, utazungumzia utawala bora pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, kesi tunazoshindwa mahakamani ni wastani wa 43% yaani kesi ambayo imechunguzwa, ina Ushahidi, PCCB wakajiridhisha, DPP akaidhinisha kwamba ni kweli tuna madai ya halali, mnaendaje kushindwa kesi mahakamani? Mpaka 43% ya kesi tunapoteza Mahakamani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kumeendelea kuwepo na mikataba ya siri, mikataba ya siri inafungwa hapa nchini, zaidi tuliambiwa hapa kuna mikataba ya rasilimali 43 ambayo ilifungwa hapa, lakini Watanzania hatujaelezwa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)