Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Husna Juma Sekiboko

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nashukuru sana kwa kupata fursa ya kuchangia kwenye Wizara hii muhimu kuhusu Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Naanza moja kwa moja kwa kuchangia upande wa utawala bora. Wote tutakuwa mashahidi namna ambavyo Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameleta mapinduzi makubwa katika utawala bora katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mzuri ni ile philosophy ya 4R za Mheshimiwa Rais; Reconciliation, Resilience, Reform na Rebuild. Mheshimiwa Rais amekuja na falsafa ya kuhakikisha kwamba kwanza panakuwa na maridhiano kwenye nchi yetu. Pili, resilience kwa maana kunakuwa na umadhubuti na kuvumiliana. Vilevile, kunakuwa na mageuzi makubwa katika maeneo yenye uhitaji, na pia kunakuwa na kujenga upya yale maeneo yanayohitaji kujengwa upya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa natoa mfano mmoja. Wakati Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anaingia madarakani, vyama vya siasa vilikuwa vimezuiwa kufanya mikutano, lakini baada ya muda mfupi Mheshimiwa Rais alikubali watu kufanya mikutano, vyama vyote vilianza kufanya mikutano, hata wale ambao wanapenda kuandamana wanapoomba kuandamana Mheshimiwa Rais amewaruhusu na wanafanya maandamano, japokuwa, muda mwingine wanashindwa hata kufanya maandamano yenyewe kutokana na kazi nzuri anayoifanya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Hii inaonesha ni namna gani Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa katika kuhakikisha kwamba anasimamia utawala bora katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ambalo napenda kuchangia ni kuhusu utumishi wa Umma kwa ujumla. Hapa, naanza kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Ilani ya Uchaguzi ya 2025 inatamka dhahiri kwamba Chama Cha Mapinduzi kimewaahidi wananchi kuhakikisha kwamba kitatetea, kitalinda na kujenga mtaji watu (human resource/human capital). (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa namnukuu mwanafalsafa mmoja anaitwa Claudia Goldin wa Havard University anasema; “Human capital consists of knowledge, skills and health,” kwamba, mtajiwatu una vitu vitatu. Cha kwanza ni elimu, cha pili ni ujuzi, na cha tatu ni afya. Hapa nataka kueleza kwa namna hii, kwanza kwa nini knowledge? Kwa sababu tunahitaji mafunzo kwa watumishi waliopo makazini. Kuajiri mtumishi ni jambo moja, hata kama amefanyiwa interview namna gani, lakini muda unakwenda, mambo yanabadilika, mambo yanakwenda, yanakua.

Mheshimiwa Naibu Spika, mtumishi huyu anapaswa kupewa elimu na ujuzi kuhakikisha kwamba anandelea kuenenda kulingana na uhitaji. Ujuzi wake unasaidia kuleta mabadiliko katika eneo ambalo anafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali, kwenye eneo hili tuhimize mafunzo kazini. Juzi wakati nachangia Ofisi ya Rais, TAMISEMI, nilieleza hapa kwamba tunahitaji kuhakikisha hata wale ambao tunategemea kuwaajiri; kwa sababu, kwa mfano kwa sekta ya elimu, walimu tunaohitaji ni wengi kuliko walimu ambao wamehitimu, walioko mtaani. Sasa wakiendelea kuwa kwenye eneo ambalo ama wana-practice, wanajifunza au wanapewa knowledge ya namna fulani, tunakuwa na uhakika wa kupata watumishi ambao watakwenda kuleta tija inayokusudiwa kwenye Taifa letu. Pia wale ambao wameajiriwa, wanahitaji kupewa elimu (knowledge) ili waweze kufanya vema na waweze kuleta tija ambayo inakusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo hilo hilo, kwanini tunahitaji health kwa watumishi? Tunahitaji maslahi kwa watumishi ili angalau aweze kumudu maisha yake, aweze kusaidia familia yake, aweze kuwa na utulivu wa akili (settled mind) na utulivu wa mwili na nafsi ili aweze kutekeleza vizuri majukumu yake. Sasa hapa pamoja na kwamba Serikali imefanya vizuri katika kima cha chini cha mshahara, bado zipo kada ambazo kusema kweli ukiziangalia, ukiwalinganisha, wengine wanafanya kazi moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, Polisi na Magereza; Polisi ana nafuu wanavyodai kwamba mshahara wake kidogo ana nafuu, lakini Askari Magereza ni kama amesahaulika kabisa. Sasa tuangalie namna ya kuoanisha kuleta usawa kidogo kwenye maslahi ya watumishi ili kuwatengenezea afya (health) na amani waweze ku-settle kwa ajili ya kutekeleza vizuri majukumu yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapo hapo kuna suala ambalo kadiri muda unavyozidi kwenda naona linazidi kuwa baya na pengine mwisho wa siku likatuletea athari kubwa zaidi kama Taifa. Uhamisho; ni kweli yapo maeneo ambayo tunafanya msawazo, maeneo mengine yana watumishi wachache mengine yana watumishi wengi. Lazima tufanye hivyo, lakini dunia na nchi yetu kwa sasa tuna janga kubwa la mmomonyoko wa maadili.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya sehemu ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa ni watoto ama kulelewa na mzazi mmoja au kulelewa na ndugu. Kukosa malezi ya pande zote mbili au wazazi wote wawili ni hali ambayo inaathiri sana watoto katika ukuaji wao na maadili yao na hata namna ambavyo wanaweza kukua na kwenda kujitegemea baadaye. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ushauri wangu kwenye eneo hili ni kwamba, kwa kuwa watumishi wetu na wenza wao, wanalazimika kuishi pamoja ili kuendeleza familia zilizo bora kwa ajili ya kutengeneza Taifa la kesho. Tusizuie uhamisho wa watumishi ambao wanawafuata wenza wao. Kumfuata mwenza iwe ni sehemu muhimu ya kuhakikisha kwamba mtumishi analindwa kwa lengo la kwenda kukisaidia kizazi kijacho kuwa na Taifa lililo bora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nilikuwa mtumishi, tena wa ngazi ya chini kabisa, lakini nataka kukwambia, nimeanza kuishi na mume wangu baada ya kuchaguliwa kuwa Mbunge. Utumishi wangu wote zaidi ya miaka kumi mimi naishi Nachingwea, naishi Korogwe, na kadhalika, mwanaume yuko Dar es Salaam. Imagine, tulikuwa tunajenga familia ya namna gani? Kwa hiyo, hii haijanitokea mimi peke yangu, inawatokea watumishi wengi Tanzania. Watumishi wengi wanalea watoto wao ama na mzazi mmoja au na ndugu. Muda mwingine inafika mahali wanawatupia boarding, watoto wanaishi kwenye mazingira ambayo hata hawana mahusiano mazuri na wazazi wao. (Makofi)

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Husna, kuna Taarifa.

TAARIFA

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mchango mzuri wa Mheshimiwa Husna, lakini suala la uhamisho basi liwe pande zote mbili, kwamba pia wakati mwingine mwanaume naye ahame kumfuata mke wake. Ilivyo sasa ni wake tu wanahama kuwafuata wanaume. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Husna, taarifa hiyo unaipokea?

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa naipokea na wakati mwingine hata mimi mume wangu angekuwa tayari kunifuata Nachingwea ningefurahi na ningeendelea na maisha Nachingwea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni suala la…

MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Taya, Taarifa.

TAARIFA

MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kufahamu, kwa sasa mume wa Mheshimiwa Mbunge amehamia hapa Dodoma na wewe au yuko Dar es Salaam? (Makofi/Kicheko)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Husna, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kuhusu TASAF.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Husna mbona unacheka sana? (Kicheko)

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu TASAF.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Husna endelea. Mheshimiwa Waitara kaa chini unachukua muda wake.

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, niliwahi kuzungumza na Naibu Waziri, Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete, nikamweleza kuhusu hali mbaya ya upatikanaji wa wanufaika wa TASAF kwenye Mkoa wa Tanga hususan kwenye Wilaya ya Korogwe. Nikamwonesha mpaka picha ya wazee wa zaidi ya miaka 90 ambao kwa bahati mbaya wale wazee hawakuwahi kuwa na watoto kabisa, lakini ndugu zao wote wameshatangulia mbele ya haki.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)