Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana nami kuweza kuwa mmoja kati ya wanaochangia katika Wizara hii. Nitazungumzia sana suala la ajira za Watanzania. Ninafahamu kabisa Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri ninyi ndio mawakili namba moja wa kutetea haki za wafanyakazi. Mheshimiwa Waziri changamoto kubwa sana katika ajira ni shida kubwa ya walimu. Tumejenga shule, zahanati na hospitali, lakini bado tuna shida kubwa sana katika ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna vijana tunaowazalisha katika vyuo vikuu vya nchi hii ambao wengi hatujawaingiza katika soko la ajira. Ninafahamu kwa zaidi ya miaka mitano iliyopita huko nyuma ajira zilipungua kidogo, lakini tunashukuru kwamba mmeanza japo speed ni ndogo. Kuna shida kubwa sana ya ajira na bado nafasi za kazi zimekuwa chache.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu mwalimu anao wastani wa kufundisha watoto kiasi kadhaa katika darasa, lakini inafika mahali mwalimu ambaye anatakiwa afundishe watoto 25 anafundisha mpaka watoto 200 kwenye baadhi ya madarasa. Wenzangu wamezungumza hapa, wamesema kuna uwiano tofauti ambao haueleweki mmeupangaje, ipo mikoa mingine ina ziada ya walimu, ukienda maeneo ya mijini unakuta walimu wamezidi, lakini vijijini hawapo. Mheshimiwa Waziri tunaomba sana ulisimamie hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, wapo walimu pamoja na wafanyakazi wa kada ya afya ambao wanajitolea kwa muda mrefu, yaani miaka miwili, mitatu mpaka mitano kwa sehemu nyingine. Tumewahi kuuliza swali hapa Bungeni kwamba, inakuwaje mtu anayejitolea kwa miaka minne au miaka mitano mnapoajiri ajira mpya yeye mfumo unamkataa? Tukatoa mawazo kwamba, ni lazima mtengeneze mifumo yenu. Kwa yule aliyejitolea, ajira inapokuja awe wa kwanza kuwa considered kwa sababu, kama angekuwa hafanyi vizuri, basi asingejitolea katika shule hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nina mfano katika shule moja Wilayani Rungwe. Shule ya Ikuti, kuna walimu zaidi ya watano wanajitolea, wana mwaka wa nne sasa hadi watano. Tunaomba inapokuja ajira mpya mwafikirie kwa sababu tayari Afisa Elimu anawafahamu, Mkuu wa Shule anawafahamu, na wazazi tunawafahamu. Tunaomba mwapatie ajira hiyo waendelee kuliko anakuja mtu ambaye amesoma nyuma yake anapata, yeye mnamwacha.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

TAARIFA

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kumwongezea Taarifa mchangiaji kwamba, walimu hawa wengi ambao wamekuwa wakijitolea kwa asilimia zaidi ya 90 ndiyo ambao masomo yao yamekuwa yakifanya vizuri kufaulisha kuliko walimu ambao wako kwenye ajira rasmi. Kwa hiyo, ni kundi la kutazamwa kwa ajili ya kukuza uzalendo. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Sophia.

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaipokea taarifa hiyo kwa kuwa ndiyo maisha halisi tuliyonayo katika vijiji vyetu, majimbo yetu na maeneo tunayotoka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusu malimbikizo ya madeni kwa walimu, maaskari na watu wengine wote ambao wanahusika katika mambo ya ajira. Mheshimiwa Waziri, tunaomba mtu anayekuwa amefanya kazi, amehamishwa au amepandishwa daraja, alipwe sawasawa na stahiki yake anayostahili. Kuna watu toka 2013 wamepandishwa madaraja, wanaenda daraja la pili, wanaenda mpaka daraja la tatu, bado wanapata mshahara ule wa daraja walilokuwa mara ya kwanza. Tunaomba sana hili lifanyiwe kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumelalamikia suala la upandishaji wa madaraja, mmeanza kupandisha madaraja. Basi ongezeni stahiki zao. Pia wanapokwenda likizo, kuna wakati mwingine mnawakopa, mnasema tutawalipa, inaenda mwaka wa kwanza, wa pili mpaka wa tatu. Hii siyo sawa kabisa. Tunaomba lisimamiwe hilo na watu hawa wapate stahiki zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni suala la uhamisho. Leo hii imekuwa shida sana kwa wanandoa. Mwanandoa mmoja anaweza akawa yuko Dodoma, lakini familia yake kaiacha Kigoma. Tunapinga UKIMWI, tunapinga magonjwa ya kuambukiza, basi tunaomba watu wapewe nafasi ya kuungana na familia zao, waweze kutunza watoto. Maadili yanaharibika kwa sababu ya kutunzwa na familia upande mmoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba uhamisho uwe wa haki maadamu tu documents zinaonesha na vigezo vyote vinasimamiwa. Leo hii kupata uhamisho imekuwa ni shida sana. Inaonekana kama ni makosa. Ajira ni baraka na wala siyo laana. Tunaomba mwapatie watu hawa uhamisho, waungane na familia zao waweze kuendeleza Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii Watanzania wengi wanalalamika kuhusu suala la kikokotoo. Japokuwa ni sisi tulipitisha hili suala la kikokotoo humu ndani, lakini leo hii lawama inakuja kwako Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri. Tunaomba mlitazame upya kwa sababu mwisho wa siku wananchi hawa hawa ndiyo ambao wanatupigia kura na ndio ambao wanaongeza uchumi wa Taifa hili. Basi mtoke kule mlikozidisha kwenye 33 angalau basi turudi kwenye 50 hawa watu waweze kupata haki yao kwa sababu tuliwahifadhia tukimaanisha kwamba mwisho wa siku hawa watu watakuja kupata uzeeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi leo hii nikistaafu nilipwe hela yangu, maisha yangu nitayajua mwenyewe, lakini ukiniambia utakuwa na maisha magumu baadaye, huko ni kuwafanya Watanzania hawawezi kujisimamia wenyewe. Tunaomba kikokotoo kirekebishwe, mkitengeneze kiwasaidie wanaotakiwa kupata hiyo stahiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, utendaji kazi wa zamani, mtu alikuwa anafanya kazi anahamishwa baada ya muda fulani, lakini sasa hivi mtu anazoea anakaa miaka 20 sehemu moja ya kazi, anajijengea ufalme, anafanya mambo yasiyofaa kwa ajili ya mazoea. Tunaomba zile Sheria na Kanuni mlizokuwa mkizitumia zamani zirudi ili hawa watu wasizoee. Sijui ni kwa sababu ya kuogopa kuwalipa, lakini mwisho wa siku ufanisi unakuwa mbovu kwa sababu ni kijiwe, mtu anakuwa amekaa kwa muda mrefu sana. Tunaomba tafadhali sana msimamie hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, nitaunga mkono pale ambapo nitapata majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri na Waziri. Kama yataniridhisha nitaunga mkono, yasiponiridhisha nitashika shilingi. (Makofi)